Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na Balozi
wa Tanzania, nchini Misri, Balozi Mohammed Hamza, wakati wakitoka kwenye
Boti baada ya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Mfereji mpya wa Suez
Canal, kwa ajili ya meli za mizigo. Hafla hiyo ilifanyika jana Agosti 6,
2015 jijini Ismailia. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na Balozi
wa Tanzania, nchini Misri, Balozi Mohammed Hamza, wakati wakitoka kwenye
Boti baada ya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Mfereji mpya wa Suez
Canal, kwa ajili ya meli za mizigo. Hafla hiyo ilifanyika jana Agosti 6,
2015 jijini Ismailia. Picha na OMR
ISIMAILIA AGOSTI 06, 2015
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal jana ameiwakilisha
Tanzania katika uzinduzi wa mfereji mpya wa Suez unaounganisha mabara ya
Ulaya, Afrika na Asia. Mfereji huu mpya ambao Misri inauita “zawadi
mpya kwa Dunia” unalenga kukuza uchumi katika usafiri wa maji na
utarahisisha usafirishaji wa mizigo kwa mabara haya matatu, huku Misri
ambayo kijiografia iko jangwani ikitegemea kukuza uchumi wake kutokana
na meli zitakazopita katika mfereji huo.
Mradi wa ujenzi wa Mfereji huu
mpya umejengwa kwa mwaka mmoja licha ya kupangwa kukamilika baada ya
miaka mitatu na umetumia kiasi cha dola za Marekani Bilioni Nane ambazo
zimechangwa kwa njia ya Hisa na wananchi wa Misri kwa kipindi
kisichozidi siku tisa. Mfereji huu ambao umezinduliwa jana, unatoa fursa
kwa Meli kupita bila usumbufu tofauti na zamani ambapo ilipaswa Meli
kusimama ili kupishana lakini sasa kila upande wa Meli utapita bila
kuathiri upande mwingine.
Sherehe hizo za aina yake
zimehudhuriwa na viongozi kadhaa wa nchi mbalimbali na kupata kuripotiwa
na vyombo vyote vikubwa duniani na hivyo kutoa picha ya kuwa Afrika
inapiga hatua katika kukuza uchumi wake pamoja na kuonesha dunia kuwa
fursa mpya za maendeleo zipo Afrika.
Sherehe hizo za aina yake
zilipambwa na maonesho ya ndege za kivita zilizotanda anga la Mfereji
mpya wa Suez huku zingine zikiruka kwa kasi na kutoa moshi ulioakisi
bendera ya Misri, zingine zikipeperusha bendera ya nchi hiyo.
Katika tukio hilo la kuathimisha
tukio hilo la kihistoria serikali ya Misri ilitangaza kuwa siku hiyo
ni ya mapumziko huku ulinzi mkali ukiimarishwa katika miji yote mikuu ya
nchi hiyo huku jiji la Cairo walipofikia viongozi mbalimbali wa
kimataifa likiwa chini ya uangalizi wa kijeshi kwenye maoneo yote
muhimu. Barabara ya kwenda eneo la Islamelia zilikofanyika sherehe hizo
ilifungwa kwa siku nzima, walioruhusiwa kupita ni viongiozi na wageni
mbalimbali waalikwa waliotakiwa kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
Rais wa Misri Abdel Fatah Sisi
alisema kufunguliwa kwa Mfereji ni uthibitisho kwamba Misri inaweza na
kueleza kwamba njia hiyo itaimarisha zaidi shughuli za usafirisha na
kufungua fursa zaidi kwa mataifa duniani.
Katika moja ya matukio ya
uzinduzi huo Rais Fatah na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe
hizo walisafiri katika meli za kifahari huku kiongozi huyo wa Misri
akivalia mavazi maalumu ya kijeshi akiwa juu ya sehemu ya uwazi wa meli
hiyo pamoja na kijana mdogo mwanafunzi wa miaka tisa aliyevalia kijeshi
na kupeperusha bendera ya Misri kama ishara ya kufunguliwa rasmi kwa
mfereji huo.
Shughuli ilimazika usiku kwa
maonesho mbalimbali ya sanaa na utamaduni wa Misri na kuhudhuriwa na
viongozi na wageni wote waalikwa.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Cairo Misri Agosti 7, 2015