WABUNGE, WAKUU WA MIKOA -FANYENI SUALA LA UCHANGIA DAMU NI AGENDA YENU KWA JAMII

July 12, 2023

 

MKUU wa Idara ya Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga  Sinde Mtobu

Na Oscar Assenga,TANGA.


MKUU wa Idara ya Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga  Sinde Mtobu amewaomba viongozi mbalimbali wa kijamii wakiwemo Wakuu wa Mikoa,Wabunge na Madiwani kuhamasishaji wananchi kuchangia damu na kuifanya  kama sehemu ya agenda yao wanapokuwa katika matukio mbalimbali ya kijamii.

Pia amewasihi viongozi wa dini kutumia maeneo yao ya ibada kuhamasisha waumini kuchangia damu ikiwemo kuandaa matukio mbalimbali ya uchangiaji damu kwa sababu wananchi wanawaamini sana viongozi wao na hivyo itakuwa ni njia rahisi watoa huduma kupata damu ya kutosha kuwahudumia wahitaji.

Hatua hiyo inaweza kusaidia kwa asilimia kubwa wananchi kuwa na mwamko wa kuchangia damu na hivyo kuwezesha benki za damu kuwa na utoshelevu ambao utasaidia wahitaji wanapojitokeza.

Mtobu aliyasema hayo wakati akizungumza  kuhusu umuhimu wa wananchi kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watanzania wengine ambapo alisema viongozi hao iwapo wakiitumia vizuri agenda hiyo ya kuandaa na kuwahamasisha katika mikutano na mikusanyiko mbalimbali wanayoifanya kwenye maeneo yao itasaidia jamii kuwa na mwamko wa kuchangia damu

Alisema wanawaomba viongozi wa dini wawasaidie maana wao wana watu wa kutosha wanaowaamini wakisimama kwenye maeneo yao na kuhamasisha wananchi kuchangia na wakati kuratibu matukio ya yatakayohusisha uchanguaji wa damu.

“Katika hili niwaombe viongozi wetu wa Kijamii, Serikali za Mitaa, Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa, Wabunge, Wakuu wa Wilaya na Mikoa kufanya matukio ya uchangiaji damu kuwa agenda yao ya jamii wanapokuwa na matukio ya watu kwa kuhamasisha  jamii katika kuchangia damu.” Pia aliongeza kuwa, jamii ina hofu juu ya ushiriki wa kuchangia damu, hivyo viongozi wetu wa kijamii wakiwa katika msitari wa mbele wa kuchangia kwa vitendo na kuhamasisha, hakika mwitikio na hamasa kubwa itakuwepo toka kwa wananchi, alisema ndugu Mtobu.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Idara alivitaka pia vyombo vya habari kuhamaisha na kuwaita wataalamu ambao watasaidia kutoa elimu ya umuhimu wa kuchangia damu kwa kuhamasisha jamii kuchangia damu kwa hiari mara nyingi iwezakanavyo.

“Ndugu zangu tendo la kuchangia damu ni la imani na thawabu mbinguni maana unakuwa umeokoa uhai wa mtu ni suala la kiimani hivyo niwaase wananchi wenzangu tuwe na mwamko wa kuchangia damu kuokoa maisha ya wenzetu wahitaji walau mara tatu kwa wanawake na mara nne kwa wanaume kwa mwaka” Alisema. 

Aidha pia aliitaka Jamii kuwa na mwamko wa kuchangia damu ili kuwa sehemu ya kuokoa uhai wa wengine ambao ni wahitaji

Mtobu alisema katika Hospitali hiyo, wanatoa huduma za kitabibu zinazohitaji matibabu tofauti tofauti kwa mfano huduma ya damu ni moja ya tiba muhimu kwa wagonjwa wenye uhitaji wa damu kama ilivyo tiba ya dawa.

Alisema hospitali ya Rufaa kwa mwezi inatumia damu wastani wa chupa 500 mpaka 600 za damu lakini uwezo wa kuchangisha damu kutoka kwa wananchi kwa hiari mara nyingi chupa 200 mpaka 300. Mtobu alisema upungufu huo unahitaji wananchi kujitokeza kwa wingi waweze kupata damu ya kutosha. Aliiasa jamii kuona umuhimu wa kuchangia damu. mara kwa mara kwa kuwa matumizi ya tiba damu yapo wakati wote katika kuwahudumia wagonjwa. 

Alisema watumiaji wa tiba damu wapo wa makundi mbalimbali  yakiwemo makundi ya akina mama wajawazito (kabla, wakati na baada ya kujifungua), kundi la majeruhi wa ajali mbalimbali, kundi la watoto, kundi la wagonjwa wa upasuaji na kundi la wagonjwa wa magonjwa wa kudumu kama vile seli mundo (sickle cell disease)  na kansa mbalimbali hasa kansa ya damu. Makundi haya ni moja ya makundi ya wagonjwa wanaotumia tiba damu kwa kiwango kikubwa, hivyo uwepo wa damu muda wote katika benki zetu za damu ni suala la lazima ili kuimarisha afya na kulinda uhai wa maisha yao.

“Hivyo niiase jamii ione umuhimu wa kuchangia damu mara kwa mara, kwa kuwa na moyo wa kufanya hivyo kutawezesha benki zetu za damu kuwa na damu ya kutosha kuwahudumia wahitaji wanapojitokeza wakati wowote ili kuepuka kupambana na changamoto za utafutaji wa damu kwa dharura katika kuwahudumia wagonjwa wahitaji wa tiba damu wakati wote” Alisema ndugu Mtobu.

WAZIRI PROFESA MKENDA ASIFU UBUNIFU UNAOFANYWA NA TAASISI YA TOIO

July 12, 2023



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiendesha moja ya baiskeli ya magurudumu matatu iliyotengenezwa na kubuniwa na Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organization (TOIO) wakati wa ziara yake


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiendesha moja ya baiskeli ya magurudumu matatu iliyotengenezwa na  kubuniwa  na Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organization (TOIO) wakati wa ziara yake  kushoto ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organization (TOIO) Shaukatali Hussein 

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kushoto akiteta jambo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organization (TOIO) Shaukatali Hussein  kulia wakati wa ziara yake

Na Oscar Assenga,Tanga

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesifu ubunifu unaofanywa na Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organization (TOIO) ya kubuni vifaa mbalimbali vya umeme ikiwemo Baiskeli na Pikipiki huku akihaidi kuunga mkono juhudi hizo.

Profesa Mkenda aliyasema hayo wakati alipoitembelea Taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea Mradi wa pikipiki za umeme,baiskeli ambazo zinazoziunda wenye shule ya Sekondari Tanga Ufundi.

Akiwa katika eneo hilo Waziri Profesa Mkenda alizitaka taasisi zinazojihusisha na teknolojia na ubunifu kuwasaidia wabunifu nchini kuweza kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Alisema kwamba kupitia ubunifu ambao unafanywa na taasisi kama TOIO wanaweza kuona namna ya kupata bajeti ambayo wanaitumia kuweza kuitumia kwa ajili ya kununua hivi vitu ili kuwaunga mkono watanzania ambao wanabuni vitu mbalimbali vyenye manufaa.

“Kupitia bajeti hiyo tutaitumia kununua hivi vitu vinavyotengenezwa hapa kitu kimoja tutangeneza mfumo wa kuvifabrikate kwa scale ya haraka”Alisema

Waziri Mkenda alisema kwamba vipaumbele vyao kwa bajeti iliyopo ya serikali ni kuona namna ya kuwasaidia wabunifu hao kununua hivi vitu tayari na serikali itanunua.

Awali akizungumza Mwakilishi wa Botna Foundation  Dkt Hassan Mshinda alisema wao walipata ufadhii wa kujenga ujuzi huo sio kwa wanafunzi tu bali na jamii ya nje.

Alisema  wanachofikiria ile integration kwenye mafunzo kama hayo ni fursa nyengine nzuri wanaweza kuona namna ya kupatna pamoja

Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organization (TOIO) Shaukatali Hussein alisema  wamekuwa wakitoa ujuzi jinsi ya kutengeneza na kurekebisha vifaa mbalimbali ikiwemo pikipiki za umeme na baiskeli nia ikiwa na ya kuwa mjasiriamali anaweza kutengeneza pia

BOMBO WAIKABIDHI TAASISI YA TADENE JENGO LA CLIF KWA AJILI YA KUFANYA UKARABATI MDOGO

July 12, 2023
Kamati ya Ujenzi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo 





UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga –Bombo leo umewakabidhi Taasisi ya Tadene ambao wanafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kufanyia ukarabati mdogo wa sehemu ya eneo la Jengo la Clif ambalo baadhi ya sehemu ya nguzo zake zimeanguka.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo,Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga –Bombo Dkt Juma Ramadhani alisema kwamba wamewakabidhi jengo hilo ili waweze kufanya ukarabati mdogo.

Dkt Juma alisema kwamba wanatarajia waanze kufanya kazi yao hivi karibuni mara masuala la msamaha wa kodi yatakapokamilika ingawa wanatarajia baadhi ya shughuli zianze kwa sasa.

Alisema wanatarajia shughuli ndogo ndogo za ukarabati huo zianze kabla ya kuanza kupata msamaha wa kodi.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Taasisi ya Tadene Dkt Ally Fungo alisema kwamba taasisi hiyo kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo wamemkabidhi mkandarasi kutoka kampuni ya Ray Build jengo linalofanyiwa ukarabati ambalo ni la kihistoria lililojengwa 1890.

Alisema jengo hilo lilikuwa likitumika kama sehemu ya mwanzo wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo hata kwa ukanda wa Afrika Mashariki wakati huo walikuwa wakitegemea Hospitali hiyo.

“Jengo hili kwa muda mrefu limekuwa likiporomoka kutokana na kutokutumika sawasawa na kutokupata matunzo na mwaka 2011 Desemba kona ya nguzo moja iliporomoka hatua inayotishia jengo zima kuporomoka”Alisema

Dkt Fungo alisema hivyo wanafanya jitihaza za kuhakikisha kona hiyo inakaa sawasawa nguzo nzima inyooke mpaka juu ili iweze kulishikilia jengo wakati wanatafuta msaada wa kulikarabati jengo nzima .














SERIKALI YAENDELEA NA UJENZI WA VYUO 65 VYA UFUNDI STANDI VETA UTAKAOGHARIMU BILIONI 54

July 12, 2023
Waziri wa Elimu Sayansi na Teklonojia Profesa Adolf Mkenda

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu, Mafunzo ya Ufundi Stadi Veta Anthon Mzee Kasore



Na Mashaka Mhando Tanga

SERIKALI imesema inaendelea na ujenzi wa vyuo 65 vya ufundi stadi Veta utakaohharimu kiasi cha shilingi bilioni 54 katika Mikoa na Wilaya hapa nchini, ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha inatoa elimu ya Amali itakayokidhi matakwa ya mabadiliko ya sera ya elimu. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teklonojia Profesa Adolf Mkenda alisema hayo jana alipotembelea chuo cha ufundi stadi Veta Jijini Tanga ili kujionea namna kinavyotoa mafunzo ya Ufundi Stadi lakini pia kuhakikisha wanatoa huduma zinazostahiki kwa jamii. 

Waziri Mkenda amesema kuwa kati ya vyuo 65 vinavyojengwa Nchini, Vyuo 64 ni za Wilaya na Chuo Kimoja cha Mkoa ambapo hadi sasa tayari imetoa kiasi cha shilingi bilioni 37 huku matumaini yakiwa makubwa katika kila maeneo yanayojengwa vyuo hivyo ambavyo ni mkakati wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. 

"Tukiwa bungeni swali kubwa ambalo limekuwa likiulizwa mara nyingi kuliko maswali mengine yote katika wizara ya elimu sayansi na teknolojia ni kuhusu veta kila mmoja anauliza ni lini veta itajengwa kwake watu wanamatarajio makubwa sana kwenye veta kwa maana hiyo sisi tuna kazi ya kuhakikisha tunakidhi matarajio yao kwa kutoa elimu ya amali ambayo ni bora na ambayo itakidhi matakwa ya vijana, "alisema Waziri Mkenda. 

Prof Mkenda amesema zipo namna mbili za kuendelea kuwapima wahitimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Veta ambapo moja ya njia ni kuangalia wahitimu wanafanya wapi kazi mara baada ya kuhitimu mafunzo yao na kuwahoji waliowaajiri namna walivyoridhika na utendaji kazi wao. 

Pia Waziri Profesa Mkenda aliwaagiza viongozi wa Veta kuhakikisha wanaandaa bajeti na kuiwasilisha wizarani itakayoomba fedha kwa ajili ya kununulia zana bora zinazokidhi teklonojia ya sasa katika karakana za Ufundi wa magari ili vyuo hivyo vya Veta viweze kuingia sokoni kutengeneza magari ya serikali, mashirika na watu binafsi.

Mkurugenzi wa Veta kanda ya Kaskazini Monica Mbele, alisema wamepokea maagizo hayo ambayo pindi wakipata nyenzo na zana bora za kisasa wataweza kuwa na utayari wa kutengeneza magari lakini pia kuongeza walimu wenye ujuzi wa teklonojia ya kisasa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Antony Mzee Kasore alisema watahakikisha wanakwenda kutekeleza maagizo ya Waziri ya utoaji wa mafunzo bora na kuhakikisha wanatoa mafunzo yanayohitajika na yanayozingatia ubora unahitajika. 

"Kama tulivyosikia kuna vyuo vinavyojengwa 65 katika wilaya mbalimbali na Mkoa na chenyewe pia tunakwenda kusimamia kama maelekezo aliyotoa ya kuhakikisha tunasimamia ujenzi huo uweze kufanyika tukiamini tutakuwa tumekwenda kutekeleza yale yote yaliyoanishwa, "alisema 

Mwisho.

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA PROJECT INSIRE MCHAKATO WA UJENZI WA KITUO KIKUBWA CHA SAYANSI NA TEKNOLOJIA DODOMA

July 12, 2023





 Na Mashaka Mhando, Tanga

SERIKALI kwa kushirikiana na Project Inspire ipo kwenye mchakato wa kujenga kituo kikubwa cha Sayansi na teknolojia Mkoani Dodoma.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teklonojia Profesa Adolf Mkenda alisema jana kwamba kituo hicho kitatumiwa  na viongozi wengine wa serikali kama mfano utakaosaidia vituo vya aina hiyo kujengwa maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wanafunzi kusoma na kupenda masomo ya sayansi. 


Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea kituo cha sayansi cha Stem Park kilichopo jijini Tanga, na kwamba mpango huo utasaidia kumaliza tatizo la wanafunzi kutopenda masomo ya sayansi wanapokuwa shuleni.


Waziri Mkenda alisema kituo hicho kitajengwa mjini Dodoma kitakuwa kama kituo cha mfano ambacho wabunge na viongozi wengine wa serikali watakitembelea ili kuona umuhimu wa kuwa na vituo vya aina hiyo kwenye maeneo yao. 


"Dodoma ni katikati ya nchi yetu halafu pale wabunge,  mawaziri wenzangu na watu mbalimbali wakuu wa mikoa nitapenda watembelee waone nini kinaweza kufanyika vituo hivi vinapaswa kujengwa kila mkoa najua haitafikia wanafunzi wote vitu vyote hivi ni matumda ambayo yanapatikana kirahisi, "alisema Waziri Mkenda. 


"Kwahiyo mimi mwenyewe nitasapoti kwanza tutafute eneo jijini Dodoma litupe eneo na majengo waje pale na tusiwatoze hata thumni kwasababu wenyewe hawawatozi wanafunzi wanaokuja kufanya mafunzo hapa hawalipishwi chochote,"alisisitiza Prof Mkenda. 


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Project inspire Lwidiko Edward alisema kituo hicho kinawatengeneza wanafunzi kwenye masomo ya sayansi kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kujifunza kwa miradi na kuandaa mazingira yanayotoa hamasa ya kusoma. 


Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Amos Nungu alisema kituo hicho kitasaidia kujenga mapenzi ya watoto kupenda masomo ya sayansi tokea wakiwa katika umri mdogo. 


Mpango wa ujenzi wa vituo hivyo unakuja wakati kukiwa na ari ndogo ya wanafunzi wanaopenda masomo ya sayansi ambao wengi wamekuwa wakikimbilia masomo ya sanaa kutokana na mazingira duni ya kujifunza masomo hayo. 


Mwisho.