Madaktari Bingwa kutoka nchini Ujerumani kuwasili Tanga Julai 13 mwaka huu

July 11, 2023


Na Oscar Assenga,TANGA

MADAKTARI Bingwa kutoka Nchini Ujerumani wanatarajiwa kuwasili Mkoani Tanga Julai 13 mwaka huu ambao wanakuja kwa ajili ya kutoa huduma za Kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga –Bombo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Tanga leo,Mratibu wa Kambi ya Upasuaji wa Kurekebisha Maumbile (Plastic Surgery) kwenye Hospitali hiyo Dkt Wallace Karata alisema madaktari hao watakuwepo hadi Julai 28 mwaka huu na siku inayofuatia wataondoka nchini.

Dkt Karata alisema kwamba madaktari hao wanakuja kutoa huduma kwa watanzania ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu lakini pia kwa fani yao ya upasuaji na kurekebisha maumbile ambayo haipatikani vya kutosha nchini na hivyo wanakuja kutoa bure kama msaada kwa watanzania.

Alisema hadi sasa wagonjwa 200 wamekwisha kujiandikisha na wakiwa tayari kwa ajili ya kusubiri huduma na Julai 10 ilikuwa ni mwisho kujiandikisha na wageni hao watakapoingia Julai 14 watafanya uchunguzi wa awali na kuweza kupanga ratiba za upasuaji.

Dkt Karata alisema operesheni zitaanza Julai 17 hadi Julai 28 kabla ya wageni hawajaondoka nchini hivyo waliojiandikisha wasishaua tarehe waliozopewa ili kuepukana na usumbufu wa kupanga ratiba zao.

“NIMEFARIJIKA " DKT. MLIMUKA

July 11, 2023

 NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID

MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka ametembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye viwanja vya Julius Nyerere barabara ya Kilwa na kusema amefarijika kuona Wanachama na Wastaafu wakitoka kwenye banda hilo wakiwa na nyuso za furaha.

Ameyasema hayo Julai 9, 2023 wakati akitoa tathmini yake baada ya kutembelea banda namba 13 la Ushirikiano wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF ili kujionea jinsi Wanachama na Wananchi kwa ujumla wanavyohudumiwa.

“Nimefurahishwa kuona huduma zinavyotolewa na wafanyakazi wetu, huduma zote zinazotolewa ofisini zinapatikana hapa,” alisema.

Alisema amefarijika zaidi kuona Wanachama wanaondoka katika banda hilo na nyuso zenye tabasamu na wenye furaha.

Alisema Mfuko umepita katika changamoto lakini sasa PSSSF iko katika hatua za mafanikio.

“hali hii imechagizwa zaidi na hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa non cash bond, ya trilioni 2.1, fedha hizi zimesaidia sana kuuwezesha Mfuko kuwa katika hali nzuri na hivyo kuweza kulipa Mafao kwa Wastaafu kwa wakati.” Alifafanua Dkt. Mlimuka.

Aliwataka watumishi wa Umma kuendelea kuchapa kazi kwani serikali inajali maslahi yao na iko tayari kutatua changamoto zinazowakabili.

“Tunawahakikishia hakuna haja ya kubabaika, Mafao yenu yanatunzwa vizuri na yako salama, Bodi ya Wadhamini tunafanya kazi kwa umakini mkubwa, jukumu tulilokabidhiwa na serikali yetu tunalitekeleza kwa uaminifu mkubwa na uadilifu mkubwa msiwe na wasi wasi wowote.” Alisisitiza Dkt. Mlimuka.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF Bw. Mbarouk Magawa alisema Mfuko ulipoanza miaka mitano baada ya kuunganishwa kwa Mifuko ya PSPF, PPF, GEPF na LAPF, kazi kubwa iliyokuwa ikifanyika ni kuunganisha mifumo ili iweze kusomana.

“Kingine tulichokuwa tunafanya ni kuweza kuwatambua Wanachama wetu, na tuweze kuwaeleza wanachama wajitambue kuwa sasa wao ni wanachama wa PSSSF (culture change) , hilo tumelifanikisha kwa asilimia kubwa sana na sasa Mfuko umeanza kwenda mbele na niwahakikishie wanachama wetu kuwa Mfuko uko imara, Mfuko unaendelea kufanya vizuri na kuimarika zaidi.” Alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi alisema PSSSF imejiimarisha kuhakikisha Mwanachama akiwa amekamilisha nyaraka zake zinazohitajika analipwa Mafao yake kwa wakati ndani ya siku 60 kama sheria inavyoelekeza.

Ingawa Mfuko umejiwekea malengo endapo Mwanachama atakuwa amekamilisha nyaraka zake zote analipwa ndani ya siku 30, anasema Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe.

“Biashara yote tunayofanya mwisho wa siku ni kuhakikisha kwamba Mafao yanalipwa, na Mafao yatalipwa kwa kuhakikisha kwamba kanuni za uandaaji wa hesabu, kanuni za utunzaji wa fedha ziko sahihi, ukaguzi unafanyika kwa kutumia taratibu sahihi,hivyo kupelekea kiasi ambacho kinatarajiwa wakati wowote wanachama wanapostaafu waweze kupata Mafao yao.” Alibainisha Mkurugenzi huyo wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi.

Alisema baada ya kukamilisha mchakato wa kuunganisha Mifuko kwa mafanikio ambapo kazi kubwa ya kuhakikisha wanaweka hesabu sahihi na hesabu zinazoweza kuaminika na umma, kazi iliyopo sasa ni kuwahudumia Wanachama kwa Viwango vya juu vinavyoendana na sheria na kanuni.

“Kwa miaka yote minne na sasa….. tunaelekea mitano,   Mfuko umepata hati safi kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG,  vile vile tumepata hati ya kutambuliwa uandaaji bora wa hesabu kutoka Bodi ya Hesabu na Ukaguzi (NBAA) kwa miaka minne mfululizo.” Alifafanua.

Kwa upande wao Wanachama wa PSSSF wameonyesha kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa na Mfuko.

“Pensheni yangu naipata kwa wakati muafaka, zile tarehe nilizoambiwa nitakuwa napata Pensheni ndio hizo hizo napata,” anasema Abdallah Mandwanga ambaye ni Mstaafu.

Bw. Mandwanga alisema “Wakati nafuatilia Mafao yangu ya kustaafu nilishughulikiwa vizuri mno,  ninaomba waendelee hivyo hivyo.” Alifafanua Bw. Mandwanga.

“Nayasema haya kutoka moyoni, na sio kuwafurahisha wahudumu hapa, nayasema haya kutoka moyoni na nimeridhishwa sana na huduma zao kwakweli nawapa hongera kubwa.” Alisema Bw. Mandwanga.

Aidha Mstaafu mwingine Bw. Dominic Chanchu alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa nyuma ya mabadiliko haya.

“Sisi tunaona ubora umeongezeka, mama Samia ameboresha hali, sisi tunakula vizuri na tunasema Alhamdullillah, Pensheni inaingia kwa wakati, wastaafu hakuna kulia lia siku hizi labda tu iwe vurugu zetu.” Alibainisha Bw. Chanchu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka (kushoto) akiongozwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ili kujionea utoaji huduma na elimu kwa Wanachama na Wananchi.
Dkt. Mlimuka (wapili kulia) akiongozwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe akijionea utoaji huduma kwa Wanachama na Wananchi wanaotembeela banda la PSSSF. 
MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka (katikti) akiwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe (kulia) wakati akiangalia bidhaa za ngozi zinazozalishwa na kiwanda cha Kilimanjaro Leather International Company Limited, (KLIC) alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ili kujionea utoaji huduma na elimu kwa Wanachama na Wananchi. Kiwanda hicho ambacho kiko mkoani Kilimanjaro, kinamilikiwa kwa ubia kati ya PSSSF na Jeshi la Magereza
Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa (kulia) akizungumza jambo na Mwanachama wa PSSSF aliyejawa na  furaha
Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi (katikati) akishuhudia jinsi Mwanachama wa Mfuko huo (kushoto) akijihakiki kwa kutumia mashine ya Biometric.
Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi , akimzawadia Mwanachama wa PSSSF aliyetembelea banda la Mfuko huo.
Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bi. Suzan Mkangwa (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Uhusiano Mwandamizi PSSSF, Bi. Fatma Elhady alipotembelea banda la PSSSF.

CCM TANGA YAZICHANGA KARATA KUELEKEA KWENYE UCHAGUZI WA 2024/2025

July 11, 2023

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurhamani akizungumza katika moja ya mikutano yake 


NA Oscar Assenga,TANGA

NDIVYO tunavyosema kusema ili uweze kufanikiwa jambo lolote lile za kisiasa au lingine ni lazima uweke mazingira mazuri mapema kabla ya kulifanya.

Hata wafanyabiashara ambao wanataka kuanzisha shughuli zao lazima wanakwenda kuangalia namna zinafanyika ili baadae wajipange kufungua za kwao tayari wakiwa na uelewa wa kutosha namna ya kuzifanya.

Hali kadhalika katika suala la siasa kila mtu anapoongoza chama Fulani anakuwa na mipango yake dira na muelekeo ambao utampa mafanikio siku za mbeleni kwa kuweka mikakati madhubuti.

Rajabu Abdurhamani ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa viongozi wenye maono makubwa ndani ya chama hicho ambapo baada ya kuchaguliwa Novemba mwaka jana ameanza kufanya kazi kubwa ya kukiimarisha kuanzia ngazi ya vijiji,vitongoji,Mitaa ,Kata na Ngazi ya wilaya.

Katika uimarishaji huo hasa ukizingatia mwakani utafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla ya ule wa mwaka 2025 ambao utawachagua Rais,Wabunge na Madiwani .

Tayari Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga chini ya Komred Rajabu Abdurhamani kimeanza kimeanza mikakati kabambe ya kuelekea kwenye chaguzi hizo kwa lengo la kuibuka kidedea.

Rajab ambaye awali kabla ya kugombea nafasi hiyo alikuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Pangani ambako nako amefanya mambo makubwa ya kukijenga chama hicho na kusambaratisha upinzania ambapo anaweka bayana kwamba atakitumika chama hicho kwa moyo wake wote kila kujali itikadi za vyama na hilo kwake ndio lilikuwa deni kubwa.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari,Rajabu anasema analo deni kubwa kwa wana CCM na wananchi wa Mkoa wa Tanga na vitongoji vyake hasa katika swala zima la kuwaletea maendeleo na kuisimamia Serikali.

Anasema ili kuweza kufikia malengo lazima kujengwe umoja na mshikamano kwa wananchi bila ya kuangalia itikadi za vyama vyao na kuacha malumbano ya kisiasa ambayo hayatakuwa na tija ya kusukuma maendeleo katika Mkoa na wilaya zake.

Anaeleza kwamba Tanga inahitaji maendeleo na kurudisha hadhi yake ya kuwa kitovu cha ajira katika sekta ya viwanda,kilimo na uvuvi na ili kufanikisha azma hiyo Rajabu alisema milango ipo wazi ya kupokea maoni toka kada mbalimbali ili kufanikisha malengo hayo.

Rajabu anasema wakati umefika wa kufanya kazi za chama na kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero zinazowakabili kwa kuzitafutia njia sahihi za ufumbuzi wa haraka ili kutekeleza majukumu ya chama hicho kuwasaidia wananchi.

Anasema miongini mwa mambo ambayo wameanza kuyatekeleza ni pamoja na kuanza kufanya ziara ya Mkoa mzima ambapo kuna Wilaya 9, kata 245 na Vijiji zaidi ya elfu kumi sambamba na vitongoji vyake dhamira kubwa kuwafikia wananchi katika maeneo yote na kupata fursa ya kuzungumza nao na kusikiliza kero zao.

Mwenyekiti huyo anasema tayari ameanza kufanya ziara katika Wilaya za Kilindi,Handeni,Pangani na Tanga Mjini ziara iliyojikita hasa kwenye kukiimarisha Chama,kuangalia kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo pia anatoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali wanaosimamia miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali katika Wilaya hizo na kuwaagiza kusimamia miradi hiyo inamalizika kwa wakati na iendane na thamani ya fedha zilizotengwa.

Anasema CCM inawajibu wa kuwasimamia viongozi wa Serikali juu ya utekelezaji wa majukumu yao kwa wananchi na namna wanavyotatua kero kwa mujibu wa kanuni za kazi zao na kufanya hivyo kunaweza kupunguza malalamiko kwa wananchi hao dhidi ya Serikali yao.

“Tuna kazi ya kufanya kwa wananchi wetu na ili kupunguza malalamiko dhidi ya Serikali yao lazima tuwajibike na kuhakikisha tunawatendea haki bila ya kuangalia itikadi za vyama vyao “Anasema Rajabu.

Rajabu anasema si jambo la kawaida kuyafikia maeneo yote ndani ya Mkoa wa Tanga na ni lazima kufanya hivyo ili kubaini changamoto zilizopo na viongozi wa chama wanatakiwa watambue hilo ndilo jukumu la kufanya ziara za mara kwa mara ili kurudisha imani kwa wananchi ambao labda wengi wao walianza kukata tamaa.

Anasema ziara hizo zina tija kwa wananchi hasa wale waishio Vijijini ambapo baadhi ya watumishi wa Serikali wamekuwa na tabia ya kufanya wanavyojisikia katika maeneo yao na badala yake tabia hiyo hupelekea kudumaa kwa maendeleo jambo ambalo katika uongozi wake halitakubalika.

“Mimi na viongozo wenzangu hatutakubali kuona wananchi wanakosa huduma za msingi au miradi ya maendeleo inazorota kutokana na uzembe wa baadhi ya watumishi lazima tuchukue hatua”Anasema Rajabu.

Anasema maendeleo ni mkakati na lazima itengenezewe njia sahihi nya utekelezaji wa maendeleo hayo ambapo Serikali ya ccm imejipambanua kuhakikisha inafikisha huduma zote za kijamii kwa wananchi katika maeneo yao.

Anasema swala sio kufikisha maendeleo katika maeno yote lakini lazima uwepo usimamizi wa kutosha na kuhakikisha miradi na huduma za kijamii zinazotolewa na watumishi wa Serikali vyote kwa pamoja vinafanyika ipasavyo.

Rajabu anasema uwajibikaji na uwadilifu makazini ndio lengo la Serikali ya chama cha mapinguzi na ndio turufu ya ushindi katika chaguzi zijazo jambo ambalo linahitaji kusimamiwa ili chama hicho kiweze kufikia malengo ya kunyakua nafasi zote katika chaguzi zijazo.