UVCCM YAPONGEZA MIRADI YA AFYA TABORA

January 01, 2018
Na Mwandishi wetu,Tabora 

Umoja wa Vijana wa CCM umesema umeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya afya inayotokana na ahadi katika ilani ya uchaguzi katika halmshauri za wilaya mji  wa Nzega na Nzega vijijini mkoani Tabora. 

Pia Umoja huo umeeleza kikubwa kasi hiyo inatokana na kuwepo kwa mashirikiano makubwa kati ya viongozi wa chama,halmashauri za wilaya na serikali kuu. 

Matamshi hayo yametamkwa jana na Mwenyekiti  wa Taifa wa UVCCM Kheri Denise james mara baada ya kumaliza kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Kazogolo katika halmashauri ya mji wa Nzege .

Kheri alisema kitendo cha serikali ya awamu ya tano kupeleka jumla ya shilingi milioni mia tano toka serikali kuu oktoba mwaka huu  kwa ajali ya ujenzi wa kituo hicho ni kielelezo kuwa serikali inajali maisha ya wetu wake .

"UVCCM tumeridhishwa na ujenzi wa miradi ya afya katika halmashauri za mji wa Nzega na halmashauri ya nzega vijijini.Ilani ya uchaguzi ya chama imetekelezwa kwa vitendo. Hii ndiyo tafsiri halisi ya hapa kazi "Alisems Kheir .

Aidha alisema kazi ya kuwatumikia wananchi haina mjadala badala yake inamhitaji kila kiongozi dhamana kuwa nafasi yake kuwajibika na kuwatumikia wananchi. 

"Kuimarika kwa huduma za jamii na watu kupata huduma bora ndiyo malengo ya kisera yanayotakiwa kufanikishwa. Tuna wajibu kila mmoja kwa nafasi yake kumsaidia Rais na serikali yale "Alisisitiza 

Kheri akiwa mkoani Tabora ametembelea mradi mkubwa wa usambazaji maji toka
ziwa Victoria mkoani  mwanza kupitia shinyanga hadi Tabora,kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya kazogolo na kuzumgumza na wananchi katika halmashsuri ya mji wa nzega na nzega vijiijini. 



Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James akipokelewa na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi  Nzega- mkoa wa  Tabora  akiwa anaelekea Mwanza kwa ajili ya mapokezi yake baada ya kuchaguliwa na mkutano mkuu wa 9 wa UVCCM kuwa mwenyekiti mpya wa UVCCM 2017-2022. 

 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James wa tatu toka Kushoto  akivikwa Skafu mara baada ya kuwasili katika Ofisi za CCM Wilayani Nzega.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James akikagua kikundi cha ngoma mara baada ya kupokelewa.
 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James akisaini Kitabu cha Mauzulio ya Wageni.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Bi Tabia Maulid Mwita Akizungum,za na Wanachama wa Chaa cha Mapinduzi Wilayani Nzenga.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James akizungumza na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake Wilayani nzega mkoa wa Tabora.
 Wanachama Wilayani Nzega Wakimsikiliza
 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice Jameswa tatu toka kushoto akizungumza jambo na M..mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shillingi billioni 600 utakaotokea Ziwa Victoria na kunufaisha wananchi wapatao milioni 1.1 wa mikoa ya Shinyanga (vijiji 39) na zaidi Tabora (vijiji 89).
 Baadhi ya Vifaa vya Ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shillingi billioni 600 utakaotokea Ziwa Victoria na kunufaisha wananchi wapatao milioni 1.1 wa mikoa ya Shinyanga (vijiji 39) na zaidi Tabora (vijiji 89).
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James akitunza fedha katika kikundi cha ngoma ya Asili alipowasili Wilaya ya Nzega Vijijini kuzungumza na Viongozi mbali mbali wa chama.
 Viongozi wamsikiliza
 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James akipata maelezo toka kwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Nzega Ndugu Amos Kanuda na Mkuu wa wilaya ya Nzega Ndugu Godfrey William Ngupula,alipotembelea kituo cha afya cha Zogolo kilichopo Halmashauri ya mji wa Nzega kinachotegemewa zaidi kuhudumia wananchi wa mji wa Nzega yenye watu wasiopungua laki mmoja. Ujenzi unaolenga kuboresha utoaji wa huduma katika kituo hiki ulikadiriwa kugharimu shillingi milioni 500 ukiwa ni ufadhili wa mfuko wa World Bank.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Kheri Denice James akipokelewa na Wanachama wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Shinyanga akitokea Tabora kuelekea mwanza.(PICHA ZOTE NA FAHADI SIRAJI)

MWANJELWA AWATAKA WANANCHI MBEYA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS MAGUFULI KWA VITENDO

January 01, 2018
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akiwasihi waumini kumuunga mkono na kumuombea Rais Magufuli wakati akitoa salamu kwenye ibada ya Siku ya Wazee iliyofanyika katika kanisa La Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) lililopo Katika Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga Jijini Mbeya, Leo 1 Januari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akimlisha chakula mmoja ya wazee waliohudhuria ibada ya Siku ya Wazee iliyofanyika katika kanisa La Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) lililopo Katika Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga Jijini Mbeya, Leo 1 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa pamoja na Viongozi wengine wakiongoza maombi wakati wa ibada ya Siku ya Wazee iliyofanyika katika kanisa La Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) lililopo Katika Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga Jijini Mbeya, Leo 1 Januari 2018.
 Miongoni mwa wazee waliohudhuria ibada ya Siku ya Wazee iliyofanyika katika kanisa La Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) lililopo Katika Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga Jijini Mbeya, Leo 1 Januari 2018.
 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akifanyiwa maombi na viongozi wa dini wakati wa ibada ya Siku ya Wazee iliyofanyika katika kanisa La Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) lililopo Katika Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga Jijini Mbeya, Leo 1 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akishiriki chakula cha mchana na wazee waliohudhuria ibada ya Siku ya Wazee iliyofanyika katika kanisa La Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) lililopo Katika Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga Jijini Mbeya, Leo 1 Januari 2018.

Na Mathias Canal, Mbeya

Wananchi Mkoani Mbeya wametakiwa kuunga mkono kwa vitendo juhudi za uwajibikaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli.

Mwito huo umetolewa Leo 1 Januari 2018 na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa wakati akitoa salamu kwenye ibada ya Siku ya Wazee iliyofanyika katika kanisa La Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) lililopo Katika Mtaa wa Sinde B, Kata ya Manga Jijini Mbeya.

Alisema kuwa Rais Magufuli na serikali anayoingoza anawathamini kwa kiasi kikubwa wazee kote nchini kwani kwa umri wao ni sehemu ya turufu muhimu kimawazo na busara katika utendaji ndio maana Mke wake Mhe Mama Janeth Magufuli hushirikiana na wazee waliopo katika makundi mbalimbali katika huduma za kijamii.

Alisema kuwa serikali hii ya awamu ya Tano inayochagizwa na kauli mbiu isemayo "HAPA KAZI TU" inawakumbusha na kuwahamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuinua haraka uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Katika ibada Hiyo Mhe Mwanjelwa ameshiriki chakula cha mchana na wazee waliohudhuria ibada Hiyo ya siku ya wazee kutoka Kata ya Manga na Sinde ikiwa ni ishara ya mapokezi mema ya Mwaka Mpya 2018. 

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo aliongoza waumini wa kanisa la Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) kumuombea Rais Magufuli sambamba na serikali kwa ujumla ili wananchi waendelea kujivunia matunda ya Rais Magufuli ambaye Duniani kote anasifika kwa umakini na ushupavu.

Alisema kuwa zoezi hilo linapaswa kuwa endelevu kwa kanisa hilo kushirikiana kwa Karibu na wazee huku akisema kuwa litakuwa jambo zuri na muhimu zaidi endapo litafanyika kwa ajili ya wazee wa Mkoa mzima wa Mbeya.

"Wazee ni Tunu, kuwa Mzee ni Baraka kwani hata vijana ni wazee wajao, Lakini niwasihi kuendelea kuwatumia wazee kwa ushauri wa kijamii pia kidini lakini zaidi Mwaka Mpya 2018 uwe Mwaka wa Mafanikio kwetu sote:" Alikaririwa Mhe Mwanjelwa

Mhe Mwanjelwa Alisifu uongozi wa kanisa hilo kwa kumualika kushiriki nao katika ibada hiyo huku akiwapongeza kwa kufanya ibada ya kiroho lakini pia ibada ya kimwili kwa ushirikishaji wa jamii.

Naye Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Huduma ya Maombezi na Uponyaji (Jesus Healing Centre T. Ministry) Mchungaji Capson Masimbani alimpongeza Mhe Mwanjelwa na kusema kuwa ni kiongozi mwenye kujali wananchi pasina kubagua itikadi za dini zao.

Alisema kuwa ni Viongozi wachache nchini ambao wana unyenyekevu kama yeye huku akimsihi kuendelea na busara na hekima Hiyo.

Sambamba na hayo Mhe Naibu Waziri wa Kilimo aliunga mkono juhudi za kanisa hilo kwa kuandaa sherehe hiyo ya siku ya wazee kwa kuwapatia mifuko 66 ya sukari wazee hao.

WAZIRI MKUU ATOA KADI ZA CHF KWA WAZEE 4,000

WAZIRI MKUU ATOA KADI ZA CHF KWA WAZEE 4,000

January 01, 2018

PMO_4152
*Ahimiza wakazi wa Ruangwa wajiunge na bima hiyo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Ruangwa wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kumudu gharama za matibabu bila kulazimika kuwa fedha taslimu. 
 Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Ruangwa na vijiji vya jirani katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CWT, mjini Ruangwa, mkoani Lindi.
 “Leo hii nimetoa kadi za CHF kwa wazee 4,000 wa wilaya hii. Ninaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kutenga fedha na kuwalipia wazee hawa ili wanufaike na bima hii ya afya kama ambavyo imeelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.”
 “Ninatoa wito kwa wananchi wengine walipie sh. 15,000 kwa mwaka ili wapatiwe kadi kwa ajili ya watu sita wa familia zao; yaani mhusika, mwenza wake na watoto wanne. Bima hii inasaidia kwa vile unapata matibabu hata kama huna fedha taslimu,” alisema.
 Waziri Mkuu alikabidhi kadi kwa Mzee Issa Juma Ngalapa, mkazi wa kata ya Nachingwea pamoja na Mzee Suleiman Stola Lihepa wa kijiji cha Kilimahewa, kata ya Nachingwea kwa niaba ya wazee wote waliotakiwa kupatiwa kadi hizo.
 Akitoa ufafanuzi juu ya mpango huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Andrea Chezue alisema mpango wa kutoa kadi za bima ya afya kwa wazee wameuita ‘CHF Endelevu’ kwa sababu walifanya tathmini na kubaini kuwa matibabu yao yana gharama, na yasipolipiwa, dawa zitaisha au wazee hao hawataweza kupatiwa huduma.
 “Katika Halmashauri tulifanya utambuzi wa wazee wa kuanzia miaka 60 na kuendelea kwenye vijiji vyote na kubaini kuwa kuna wazee 4,000. Tukaamua Halmashauri iwalipie sh. 15,000 kwa kila wazee sita kama ilivyo katika kaya ili tuweze kuchangia gharama za matibabu yao,” alisema.
 “Mzee akipatiwa kadi hii, inakuwa ni ya kudumu, anaitumia miaka yote. Si ya kulipia kila mwaka kama zilivyo zile nyingine. Hadi sasa tumeshatoa kadi kwa wazee 2,700 na tunaendelea kutengeza kadi hadi tukamilishe zote. Tumepanga kuwa kila mwaka, tutafanya utambuzi wa wazee katika vijiji vyote ili wale wanaofikisha umri huo, nao pia waingizwe kwenye mpango huu,” alisema. 

ZOEZI LA UPIGAJI CHAPA MIFUGO LAONGEZEWA MUDA WA MWEZI MMOJA

January 01, 2018
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina(wa pili kushoto) akipiga chapa ng’ombe katika hitimisho la zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa katika Kijiji cha Migato, Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.

Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina ameongeza muda wa mwezi mmoja kwa Halmashauri nchini kukamilisha zoezi la upigaji chapa mifugo na kuwataka watendaji wote wa Serikali wanaohusika kuhakikisha mifugo yote inapigwa chapa.

Waziri Mpina ameyasema hayo wakati wa kuhitimisha zoezi la upigaji chapa Kitaifa katika Kijiji cha Migato wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, zoezi ambalo lilianza rasmi Kitaifa mwezi Desemba, 2016 na kupangwa kukamilika Desemba 31, 2017.

“Kwa kuwa hadi sasa zoezi hili limetekelezwa kwa asilimia 38.5 kutokana na sababu mbalimbali, Mimi Luhaga Mpina Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa Mamlaka niliyopewa chini ya sheria ya Utambuzi, Usajili na ufuatiliaji wa mifugo ya mwaka 2010 na kanuni yake, ninaongeza muda wa kupiga chapa mifugo kutoka tarehe 01/01/ 2018 hadi 31/01/2018”alisititiza.

Mpina amesema miongoni mwa changamoto zilizopelekea Halmashauri nyingi kushindwa kutekeleza zoezi hilo kwa asilimia 100 ni baadhi ya halmashauri kutokutenga fedha kwa ajili ya zoezi hilo, kubaini mifugo kutoka nje ya nchi, baadhi ya wafugaji kushindwa kutaja idadi halisi ya mifugo yao na baadhi ya Halmashauri kuwatoza wafugaji zaidi ya shilingi 500 ambayo ndiyo bei elekezi, ambapo ameagiza wafugaji hao waliotozwa zaidi ya shilingi 500 warejeshewe fedha zao.

Ameongeza kuwa hadi kufikia Desemba 31, 2017 Halmashauri 30 hapa nchini hazijapiga kabisa chapa mifugo, halmashauri 23 zimeendesha zoezi hilo chini ya asilimia 10 na akaongeza kuwa orodha ya majina ya viongozi wa wilaya hizo walioshindwa kutekeleza agizo hilo la Serikali ameyawasilisha kwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa.

“Halmashauri 30 ambazo hazijapiga chapa kabisa hata ng’ombe mmoja na zile 23 ambazo zimepiga chini ya asilimia 10 majina ya viongozi wote na Halmashauri husika nimekabidhi orodha hiyo kwa Waziri Mkuu, hatuwezi kuendekeza ukaidi wa maagizo ya Viongozi Wakuu wa Nchi” alisema Mpina. Akiwasilisha taarifa ya zoezi la Upigaji Chapa katika Mkoa wa Simiyu, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa, Ndg.Elias Kasuka amesema zoezi hilo mkoani humo lilianza rasmi mwezi Aprili 2017 ambapo hadi sasa ng’ombe zaidi ya 764, 933 wameshapigwa chapa kati ya ng’ombe 1,500,000.

Akitoa maoni yake baada ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo, Paulo Mabula mfugaji kutoka Migato Itilima amesema wafugaji wamelipokea kwa furaha agizo la Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuongeza siku za kwa ajili ya kupiga chapa kwani litawasaidia wafugaji ambao bado hawajakamilisha ili kuondokana na changamoto ya wizi wa mifugo.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Itilima, Mhe.Mahamoud Mabula amemuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Luhaga Mpina kuwasaidia wafugaji wa Wilaya hiyo na maeneo mengine ya Mkoa huo kufanya vikao vya ujirani mwema na wale wa mikoa jirani ili kujadiliana namna ya kuondoa changamoto ya wizi wa mifugo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe.Benson Kilangi amesema viongozi na wataalam wa wilaya hiyo wamekuwa wakiwahamasisha wafugaji kupanga matumizi bora ya ardhi ili waweze kutenga maeneo kwa ajili ya malisho na kuyawekea miundombinu muhimu kwa ajili ya mifugo ikiwemo maji, majosho pamoja malisho.
Vijana wa Skauti wilaya ya Itilima wakimvisha skafu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina alipowasili wilayani humo kwa ajili ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo kitaifa, mkoani Simiyu.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akisalimiana na Afisa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Ally Mzee mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa, lililofanyika katika kijiji cha Migato wilayani Itilima.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi (wa tatu kushoto) akipiga chapa ng’ombe katika hitimisho la zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa katika Kijiji cha Migato, Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu ambalo limehitimishwa na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Daudi Nyalamu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Migato na vijiji jirani mara baada ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa lililofanyika kijijini hapo leo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Luhaga Mpina akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Migato na vijiji jirani mara baada ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa lililofanyika kijijini hapo.
Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe.Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Migato na vijiji jirani mara baada ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa lililofanyika kijijini hapo.
Ndg.Paulo Mabula akitoa mchango wake mara baada ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina kuhitimisha zoezi la upigaji chapa Kitaifa katika Kijiji cha Migato wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akisalimiana na Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Elias Kasuka mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ajili ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa, lililofanyika katika kijiji cha Migato wilayani Itilima.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akipokelewa na Viongozi wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa, lililofanyika katika kijiji cha Migato wilayani Itilima.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI LUHAGA MPINA ASHEREHEKEA SIKUKUU YA MWAKA MPYA KWA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI WA JIMBO LA KISESA KUHAMASISHA KILIMO BORA CHA ZAO LA PAMBA

January 01, 2018
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina akishirikiana na wakulima wa Kijiji cha Itinje Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu kupalilia shamba la pamba lililopandwa kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo wakati wa mapumziko yake ya sikukuu ya Mwaka Mpya jimboni kwake mapema leo.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akishirikiana baadhi ya wananchi wa jimbo la Kisesa Wilaya Meatu mkoani Simiyu kupalilia shamba la pamba ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji kilimo cha kuzingatia mbinu bora za kilimo ikiwemo kupanda kwa mistari pamoja na kutochanganya zao hilo na mazao mengine alipokuwa kwenye mapumziko ya sikukuu ya mwaka mpya jimboni kwake.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina akishirikiana mkulima wa Kijiji cha Itinje jimbo la Kisesa Wilaya Meatu mkoani Simiyu Mama Sagwa Njile kupalilia zao la pamba lililopandwa kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo wakati wa mapumziko ya sikukuu ya Mwaka Mpya jimboni kwake leo.
KONGAMANO LA VIJANA JIMBO LA MAGOMENI KUHUSU UDHALILISHAJI

KONGAMANO LA VIJANA JIMBO LA MAGOMENI KUHUSU UDHALILISHAJI

January 01, 2018

01
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar Nasima Haji Chum azungumza na Vijana wa Jimbo la Magomeni Zanzibar katika Kongamano la Wazi lilozungumzia udhalilishaji wa Kijinsia huko uwanja wa Magae ulioko katika Jimbo hilo.
 …………….
Na Maryam Kidiko /Mwashungi Tahir- Maelezo Zanzibar.        
MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar Nasima Haji Chum amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaumizwa sana na suala la udhalilishaji wa Kijinsia na inaendelea kupanga mipango madhubuti juu ya wanaofanya vitendo hivyo.
Hayo aliyasema katika Kongamano la Vijana wa Jimbo la Magomeni lililofanyika katika uwanja wa Magae mjini Unguja kuhusu suala la  udhalilishaji wa kijinsia unaoendelea kukithiri katika Jamii nini kifanyike ili suala hili liweze kupunguwa.
Alisema suala la udhalilishaji linaendelea kuzungumziwa kwa upana katika taasisi mbali mbali Unguja na Pemba hivyo  lengo na adhma   iliyokusudiwa na Serikali ya Zanzibar ni kulitokomeza suala hilo na kumalizika kabisa.
Nasima aliwataka wazazi kuwa karibu sana na vijana kuhusu kusimamia malezi ya watoto ili kujuwa tabia zao za kila siku katika maisha yao wanayoishi kwani kufanya hivyo kutapelekea kujuwa vikitokea kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa itajulikana kwa haraka.
“ili suala hili tuweze kulipatia taarifa za uhakika inatubidi sisi wazazi na walezi tuwe karibu sana na watoto wetu na wao watakuwa wawazi kusema suala hili la udhalilishaji litapowafikia”alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha alisema Wananchi wote washirikiane kwa pamoja na Wizara husika katika jambo hili kufanya hivyo kutapelekea kutokomeza kabisa suala la udhalilishaji katika Visiwa vyetu.
“Nawaomba Vijana muweze kuacha muhemko ambao unasababisha kuongeza suala hili la udhalilishaji “alitowa msisitizo Mkurugenzi huyo.
Nae Mwenyekiti wa Vijana Jimbo la Magomeni Ussi Jecha Haji alisema lengo la kongamano hilo ni kuisaidia Serikali ya Zanzibar kuweza kupambana na suala la udhalilishaji wa kijinsia kwa nguvu zote.
Mwenyekiti huyo aliwataka Vijana kutoka Majimbo mengine mbali mbali kuweza kuiga mfano wao ili kushirikiana pamoja na Serikali kupinga vitendo  vya udhalilishaji uliokithiri katika Jamii.

Kwa upande wa risala ya Vijana Jimbo la Magomeni walieleza kuwa Jamii yetu katika Nchi imekubwa na janga kubwa la ukatili wa udhalilishaji wa kijinsia kwa kukithiri vitendo vya udhalilishaji na ulawiti kwa watoto wadogo wa kike na wa kiume ambavyo vinafaywa na watu wasio na hofu.
Hivyo Jumuiya ya Vijana (UVCCM) jimbo la Magomeni inaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi kutunga Sheria mpya itakayozuwia uingizaji wa picha za ngono, Dawa za kuongeza nguvu za kiume imeonekanwa ndio sababu kubwa ya kuongezeka vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika jamii.
Wakati huo huo Muwasilishaji wa Zafela huduma na sheria Siti Abasi Ali aliweza kutowa mada ya masuala ya udhalilishaji alisema suala la simu kwa Vijana linapelekea kuongezeka kwa masuala ya udhalilishaji kwa kuangalia mambo yanayochochea vitendo hivyo.
Vile vile alisema kuwa wazazi wawe makini sana na watoto wao wakati wa kuwafanyia usafi wa mwili na wa nguo zao ili wakifanyiwa udhalilishaji waweze kujuwa haraka.
“Nawaomba Wazazi na Walezi wa watoto wetu tuwache tabia ya kuwabebesha kila kitu wadada wa kazi kwa kuwafanyia kila kitu watoto bila sisi kuwashuhulikia hivyo tujenge tabia ya kuwashuhulikia watoto wetu sisi wenyewe “alisema Mwanasheria wa Zafela.
Kauli mbiu ya kongamano hilo ilibeba ujumbe muhimu unaosema (USIKUBALI, ZUNGUMZA, TOA TAARIFA) kwa pamoja tushirikiane kuzuwia aina zote za udhalilishaji.
Kongamano hilo la wazi limeandaliwa na Vijana wa Jimbo la Magomeni lililozungumzia mada za udhalilishaji ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra ya kuazimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
     
             IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

NAIBU WAZIRI ULEGA AAGIZA WATENDAJI WA VIJIJI NA WENYEVITI KUWASOMEA MAPATO NA MATUMIZI WANANCHI

January 01, 2018
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akizingumza na wananchi wa kijiji cha Kiziko alipofanya ziara katika jimbo la Mkuranga.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mkuranga, Juma Abeid akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiziko juu ya mikakati ya Halmashauri katika uboreshaji wa sekta mbalimbali.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiwasili katika kijiji cha cha Kitonga katika ziara ya vijiji jimbo la Mkuranga. 


Na Chalila Kibuda,Globu ya jamii.

NAIBU waziri wa Mifugo na Uvuvi (Mbunge) wa Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani Abdalla Ulega ametoa agizo kwa Watendaji wa vijiji na Wenyeviti kuwasomea mapato na matumizi wananchi wao ili kuepuka kurudisha nyumba uchangiaji wa shughili za maendeleo.

Naibu waziri huyo ametoa agizo hilo wilayani humo akiwa katika mwendelezo wa ziara za vijijini ambapo akiwa katika kijiji cha Kiziko, kilichopo Kata ya Mwarusembe baada ya kupokea malalamiko ya wananchi juu ya viongozi wao ngazi ya kijiji kushindwa kusoma taarifa ya mapato na matumizi.

Alisema kushindwa kusoma taarifa za mapato na matumizi kunachangia kwa asilimia kubwa wananchi kushindwa kuchangia maendeleo katika maeneo hayo hivyo lazima wananchi wajulishe kinachoingia na kinavyotumika.

"Natoa agizo hili kwa watendaji na wenyeviti kusoma mapato na mapato na matumizi na hapa naagizi mtendaji wa Kata ya Mwarusembe kuhakikisha hadi kufika Januari 2 ,2018 niwe nimepata taarifa za kushindwa kusoma mapato na matumizi katika kijiji hiki cha kiziko. "alisema Ulega

Alisema wananchi wanatamani kujitolea kwa lengo la kuchangia maendeleo lakni wanavunjwa moyo viongozi hao huku akisisitiza kupewa ifika January 2 awe amepata taarifa nakuhaidi kulifuatilia jambo hilo kwa ukaribu zaidi.

Pia akiwa katika kijiji hicho cha alitoa mifuko 50 ya saruji pamoja na shilingi laki tano kwa ajili kuchangia ujenzi ya serikali ya kijiji hicho ikiwa pamoja na matundu ya vyoo katika shule ya msingi kiziko huku akitoa ahadi ya shilingi tisa. Kwa ajili ya kuchangia vikundi tisa vya Vikoba.

Awali wakitoa kero zao kwa Mbunge huyo walisama wamakerwa sana na kukithiri kwa mifugo aina ya ng'ombe hali inayosababisha umasikini na njaa kwa wananchi hao kutokana na mazao yao.Pia walilalamikia kukosekana kwa barabara, inayounganisha kijiji hicho cha kiziko na vijiji vingine pamoja na Daraja linalounganisha vitongoji vya Gwanzo, Chakande vyenye wakazi wengi zaidi.

"kwakweli tuna kero nyingi mno hapa kijijini kwetu kwani mbali na barabara na Daraja lakini pia tunakero ya kukosa Daktari kwenye Zahanati hii yetu hali inayosababisha wananchi kukosa kupatiwa huduma stahiki. "alisisitiza Mojamed Ally mjumbe wa serikali ya kijiji.

Naye Ofisa Kilimo wa Kijiji hicho... Alisema wananchi hao ambao waliowengi ni wakulima lakini wanakosa dhana za kisasa za kilimo pamoja na ukosefu wa gereta ili kusikuma maji kwenye kisima cha maji kilichopo shule ya msingi kiziko ili wanafunzi na raia wengine wapate maji.

Mbali na kijiji hicho pia Naibu waziri Ulega aliendelea na ziara katika kijiji cha Kitonga kata hiyo ya Mwarusembe ambapo pia alipokea kero ya kuvamiwa na ng'ombe kwenye mashamba ya wananchi huku wakimtaka kumaliza kero hiyo.

Wakati huohuo wananchi hao walilalamika kwa Kiongozi wao huyo juu ya kutoridhishwa na huduma zinazotolewa katika Hospitali ya wilaya hiyo nakudai kwamba wakinana mama wanapohitaji kujifungua kuambiwa wabebe vifaa vya uzazi mbali Serikali kusema huduma hiyo bure.

"Naibu waziri kwakweli wananchi wako sisi tunaumia. Pale Hospitali ya Wilaya ya mkuranga ni tatizo bado panafigisu na kona kona nyingi tunaomba tusaidie. "alisema mmoja wa wananchi katika mkutano huo.

SALAMU ZA MWAKA MPYA KUTOKA KWA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA Dkt. Faustine Ndugulile

January 01, 2018

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuungana nanyi nyote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha salama siku hii ya leo tunapoanza mwaka mpya 2018. Hii ni neema pekee ambayo Mwenyezi Mungu  ametujaalia  kwani kuna wengi walitamani kuifikia siku hii lakini hawakubahatika. Hivyo, nawatakieni nyote kheri na fanaka katika mwaka huu mpya.
Napenda kutumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Wanataaluma na Watoa huduma za afya wote kwa kuendelea kutoa huduma kwa ari, juhudi, uaminifu na uadilifu licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila siku.  Nami nawatia shime na hamasa ili muendelee na moyo huo wa kuwahudumia na kuwatumikia Wananchi.
Natambua kuwa  Sera yetu ya Afya inataka tuijenge jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi pamoja na yale ya Taifa.  Aidha, Sera na Sheria zetu mbali mbali zinatambua umuhimu na nafasi ya Mabaraza ya kitaaluma katika kuboresha na kusimamia viwango vya maadili ya wanataaluma walio chini ya Wizara yangu. Jambo hili ni muhimu sana hususan tukizingatia ongezeko la minong’ono, manung’uniko na hata malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya baadhi ya  watoa huduma ambao wanakiuka taratibu au miiko ya kazi zao na hivyo kuathiri ubora wa utoaji huduma.
Nimeona kama sehemu ya salamu zangu za mwaka mpya wa 2018, nitoe maelekezo yatakayoweza kutusaidia kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya kupitia Watoa Huduma za Afya na Mabaraza ya Kitaaluma na pia kuwakumbusha wananchi juu ya haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za afya na wajibu wao wa kuhakikisha hilo linatokea.
  • Wanataaluma wa Afya:
Nawakumbusha Wanataaluma wote katika Sekta ya afya, yaani Madaktari, Wauguzi, Wakunga, Wafamasia, Wataalam wa Maabara, Madaktari na Wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno, Wataalam wa Mionzi, Wataalam wa viungo bandia na Wafiziotherapia,  kwamba taaluma hizi ni za Kuheshimika sana (Noble), na hivyo kazi na majukumu mnayoyatekeleza yamejengwa  katika  misingi ya kuaminiwa (Trust) na Jamii, na kwamba  kuaminiwa  huko ndio kiini cha heshima ya taaluma hizi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwanataaluma kutekeleza majukumu yake akiongozwa na msingi huu mkuu, pamoja na misingi mingine ya kimaadili ambayo ni: HURUMA, UKWELI, FARAGHA, USIRI, UAMINIFU, USAWA, HAKI, UTU na MAHUSIANO MEMA.
Aidha, naendelea kuwakumbusha kuwa, utekelezaji wa majukumu yenu siku zote ni lazima uzingatie matakwa ya Katiba ya Nchi ambayo ndiyo Sheria Mama. Mkumbuke kuwa Dira Kuu katika  utekelezaji wa wajibu wenu kama wanataaluma ni uzingatiaji wa haki, heshima, usawa na utu kwa wote wanaokuja mbele yenu kupata huduma za kitaaluma. Vile vile mkumbuke kuwa siku zote mnao wajibu wa kutekeleza majukumu yenu ya kitaaluma kwa kuzingatia Sheria nyingine za nchi,  Kanuni, Sera, pamoja na  Miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi, pamoja na Miongozo na Matamko  ya Kimataifa ambayo tumeridhia kuyatekeleza na kuyazingatia.
Aidha, nawakumbusha Wanataaluma wote Waandamizi na Viongozi katika Sekta ya Afya kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa Wanataaluma na watoa huduma wote walio chini yao wanazingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Weledi (Professionalism) pamoja na Maadili (Ethics) ya taaluma au kazi zao na kuchukua hatua stahiki za nidhamu, kwa mujibu wa Sheria, kunapotokea ukiukwaji. Pia kila Mwanataaluma ana wajibu wa kuhakikisha kuwa Wanataaluma wanaomzunguka wanatekeleza majukumu yao kwa misingi hii iliyotajwa na ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi panapotokea ukiukwaji au kuonekana viashiria vyake. Jambo hili ni muhimu sana ili kama Wanataaluma msikubali kazi nzuri inayofanywa na wengi iharibiwe na wakorofi wachache miongoni mwenu.
  • Mabaraza ya Taaluma
Natumia fursa hii pia kuyakumbusha Mabaraza yote ya Kitaaluma yaliyo chini ya Wizara yangu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu Sheria zinazosimamia Wanataaluma wao. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa  mtu yeyoye anayetaka kutoa huduma za kitaaluma ni lazima awe na elimu na ujuzi  unaokubalika, na atambulike kwa kupewa usajili na leseni ya kufanya kazi za kitaaluma. Dhima ya Wizara ni kuona kuwa jamii inapata huduma zilizo sahihi, salama na zenye ubora unaokubalika. Hivyo, Mabaraza yana wajibu wa kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kukiuka Sheria na taratibu zilizowekwa.
  • Wanajamii
Napenda kuwajulisha wanajamii wote kuwa mnayo haki ya kupata huduma za afya zilizo salama, bora na ambazo zinazingatia misingi ya usawa, haki na zinazozingatia heshima na utu wa binadamu.  Pia, mnayo haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya afya au ugonjwa, na kupata ushauri au tiba kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika. Hivyo, wanajamii mnao wajibu wa kutoa taarifa wakati wowote mnapobaini kuwepo kwa viashiria au vitendo vya ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu zilizowekwa kwa misingi ya Sheria za Nchi.  Kati ya vitendo visivyo kubalika ni pamoja na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, wizi, lugha chafu, matusi, dharau, mavazi yasiyo na heshima, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, uropokaji wa siri za wagonjwa, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya simu za mkononi na tabia nyingine zote zinazofanana na hizi.
Hitimisho na Maagizo,
Nahitimisha salamu zangu kwa kutoa maagizo yafuatayo:
  • Wanataaluma na Watoa Huduma,
  1. Kila Mwanataaluma na mtoa huduma anapaswa kuvaa kitambulisho chenye jina lake kamili  wakati wote awapo eneo la kazi. Hii ni pamoja na uvaaji wa sare nadhifu za kazi.
  2. Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Masanduku ya kutolea maoni yanayoonekana kwa uwazi na urahisi, na kwamba maoni yanayotolewa yanafanyiwa kazi ipasavyo.
  3. Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Ofisi za kuwasilisha malalamiko zilizo karibu ili kufikiwa na wateja wote wenye uhitaji.
  1. Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya wanapaswa kuweka wazi namba zao rasmi za simu kwenye mbao za matangazo ambazo mwananchi atazitumia kutoa taarifa au kuwasilisha maoni au malalamiko.
  2. Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa au Kiongozi mwenye mamlaka katika utoaji wa huduma za afya ana wajibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwanataaluma anayetuhumiwa katika Baraza la Taaluma husika pindi panapotokea vitendo vya ukiukwaji wa weledi (Professionalism) na maadili (Ethics).
  • Mabaraza ya Taaluma
Kila Baraza la taaluma pamoja na Wawakilishi wao waliopo katika Wilaya, Mikoa na ngazi ya Taifa waweke wazi utaratibu wa kisheria wa uwasilishwaji wa malalamiko na taratibu za Uchunguzi wa vitendo viovu dhidi ya wanataaluma. Hii ni pamoja na kuweka wazi namba za simu na anuani za barua pepe (e-mails).
  • Wanajamii kwa ujumla:
    1. Nawasihi Wanajamii kuwaheshimu na kuwathamini Watoa huduma za Afya nchini
  • Nawasihi wanajamii wote kutoa taarifa, maoni au malalamiko dhidi ya wanataaluma au watoa huduma wanaokiuka misingi ya Taaluma zao, au wanaotoa huduma kinyume na Taratibu zilizopo kwa:
  • Uongozi wa kituo husika,
  • Mganga Mkuu wa Wilaya,
  • Mganga Mkuu wa Mkoa,
  • Ofisa wa TAKUKURU,
  • Baraza la Taaluma Husika,
  • Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, au
  • Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, au kwa
  • Kiongozi yeyote wa Serikali, ili awasilishe taarifa hizo kunakostahili.
Aidha ni vema taarifa itolewe kwa kumtaja mhusika ili kurahishisha ufuatiliaji.
Nawatakieni nyote Kheri na Afya Njema kwa mwaka mpya wa 2018.
Ahsanteni sana.
Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO.
31/12/2017.