Mchezo kati ya timu ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na Sixers ukiendelea
HABARI NA MATUKIO MBALIMBALI
Mchezo kati ya timu ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na Sixers ukiendelea
Na Mwandishi Wetu, TANGA
MBIO za ngalawa baharini, zikijumuisha timu 12, zimekuwa kivutio katika Maadhimisho ya 44 ya Siku ya Chakula Kimataifa, ambapo hapa nchini, yanafanyika mkoani Tanga.
Mashindano hayo yaliyoratibiwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na wadau wengine, yamefanyika jana kwenye ufukwe wa Deep Sea jijini Tanga.
Kwenye shindano hilo lililofanyika kwenye umbali wa jumla ya kilomita 12 majini, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na timu namba 010 iliyoongozwa na Idd Kileo na kusafiri kwa dakika 48:30.
Timu namba 012 iliyoongozwa na Amir Seleman ilichukua nafasi ya pili kwa kutumia dakika 48:49 wakati nafasi ya tatu ilichukuliwa na timu namba 009, ikiongozwa na Mahamud Rashid na ilitumia dakika 49:20.
Washindi hao watatunukiwa zawadi za ushindi kwenye kilele cha Siku ya Chakula Kimataifa Oktoba 16, 2025 na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa.
Timu nyingine zilizoshiriki na viongozi wake kwenye mabano ni namba 002 (Halfan Mnyeto), 007 (Mohamed Salim), 003 (Hamza Nguzo), 008 (Hussein Seif), 011 (Veso Kileo), 005 (Akida Koja), 001 (Kassim Abdi) na 006 (Jumaa Kibao).
Kaimu Mkurugenzi wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Nankondo Senzira, amesema mashindano hayo ni kilelezo cha ukweli kuwa uvuvi una mchango mkubwa katika ajira, lishe bora, kipato na fedha za kigeni.
Hivyo, amesema muhimu kuwepo ubunifu kama kufanyika kwa mashindano na kuwazawadia wavuvi ili kuonesha thamani na kuongeza tija katika shughuli zao.
Ametoa mfano kuwa mwaka 2024, uvuvi ulichangia asilimia 1.8 ya pato la taifa huku ikitoa ajira kwa Watanzania takribani milioni 6.
Mwakilishi Msaidizi wa FAO, Charles Tulahi, alisema mashindano hayo yanaendelea mpango wa kuzitafakari changamoto dhidi ya uzalishaji wa chakula ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, migogoro, gharama za maisha na kupungua kwa rasilimali kama ardhi, maji na bioanuai.
“Mashindano haya ya ngalawa siyo tu burudani, yana ujumbe kuhusu umuhimu wa Bahari na sekta ya uvuvi katika kuhakikisha usalama za chakula, lishe bora na ajira kwa jamii zetu,” alisema.
Alisema, yamefanyika kwenye Bahari ya Hindi iliyo hazina kubwa ya maliasili kwa samaki na viumbe wengine ambavyo ni chanzo cha protini, mafuta yenye afya na madini yanayosaidia ukuaji wa mwili na ubongo.
Risala ya washiriki wa shindano hilo ilieleza kuwa, wavuvi walitumia mwelekeo wa upepo, mawimbi na mbinu za jadi, na hivyo kuwawezesha kumaliza salama kwa kila mmoja wao.
Kwa mujibu wa risala hiyo, mashindano hayo yameonesha azma ya Serikali na wadau wake kuwatambua, kuwathamini na kuwashirikisha wavuvi wanaojinasibu kuwa mashujaa wa chakula na afya za watu nchini.
MWISHO
Dodoma
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma, Bw. Pendolake Elinisafi, ameongoza watumishi wa mamlaka hiyo kushiriki katika bonanza maalum la michezo lililolenga kujenga na kuimarisha afya pamoja na kuongeza mshikamano miongoni mwao.
Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya Kilimani Park jijini Dodoma, limehudhuriwa na watumishi kutoka vitengo mbalimbali vya TRA na lilipambwa na michezo ya kuvutia ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, mbio za magunia, kukimbiza kuku, kutembea na yai kwenye kijiko, na mpira wa pete.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo, Bw. Elinisafi alisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya bora na kuimarisha mahusiano kazini. “Michezo ni njia mojawapo ya kuimarisha afya ya mwili na akili, lakini pia huchangia katika kujenga mshikamano na ari ya kufanya kazi kwa pamoja kama timu,” alisema.
Watumishi walionekana kufurahia michezo hiyo ambayo iliibua ushindani wa kirafiki na kuongeza furaha, huku ikidhihirisha umuhimu wa matukio ya kijamii kazini. Washiriki walitunukiwa zawadi mbalimbali kama sehemu ya kutambua ushiriki wao na kuwahamasisha kuendelea na utamaduni wa kushiriki michezo kazini.
Bonanza hilo limeonesha kuwa, mbali na majukumu ya kikazi, TRA inatambua umuhimu wa shughuli za kijamii na kiafya kwa ustawi wa watumishi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi, akiwasilisha hotuba yake wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR BONANZA 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo Jijini Mwanza akiwa ni Mgeni Rasmi wa Bonanza hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda wakimkabidhi Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mirongo vifaa mbalimbali vya msaada vilivyotolewa na OSHA kukiwezesha chuo hicho. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, makoti ya usalama na vifaa vya michezo.
Na Fredy Mgunda,Kwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mheshimiwa Amina Makilagi, amewataka waajiri na wafanyakazi kote nchini kuitekeleza kikamilifu Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ili kupunguza au kuondoa kabisa ajali na magonjwa yanayotokana na mazingira duni ya kazi.
Mheshimiwa Makilagi alitoa wito huo jana wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo, Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza. Bonanza hilo lilihusisha shughuli mbalimbali za kijamii na michezo kwa lengo la kuimarisha mshikamano kati ya OSHA na jamii inayohudumiwa, pamoja na kutoa msaada kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Mirongo, wakiwemo wenye ulemavu.
Katika tukio hilo, OSHA ilikabidhi vifaa mbalimbali kwa Chuo cha Ufundi Mirongo, vikiwemo kompyuta, vifaa kinga vya usalama kazini, pamoja na vifaa vya michezo kama mipira na jezi za michezo.
Akizungumza kama Mgeni Rasmi, Mheshimiwa Makilagi aliipongeza OSHA kwa juhudi zake za kuhakikisha mazingira salama na yenye afya sehemu za kazi na kuonesha moyo wa huruma kwa makundi maalum katika jamii.
“Nitoe rai kwa waajiri na wafanyakazi nchini kuisoma na kuitekeleza Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo, maeneo ya kazi yatakuwa salama, bila ajali wala magonjwa, hivyo kuongeza tija kazini,” alisema Mkuu wa Wilaya Makilagi.
Aidha, aliihakikishia OSHA ushirikiano wa Halmashauri na Ofisi yake katika kusimamia usajili na ukaguzi wa maeneo ya kazi, sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya maboresho ya mazingira ya kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, alisema Bonanza hilo ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo wa kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility) na kwamba msaada uliotolewa kwa Chuo cha Mirongo umetokana na tathmini iliyofanywa na wataalam wa OSHA baada ya kutembelea chuo hicho.
“Tunaamini kuwa kwa kusaidia vyuo vya ufundi kama Mirongo, tunachangia kwa kiasi kikubwa maandalizi ya wataalamu wa baadaye katika fani muhimu za kiufundi na kazi,” alisema Bi. Mwenda.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mirongo, Bi. Herieth Richard, pamoja na mwanafunzi wa fani ya ushonaji, Bi. Aneth Augustino, waliishukuru OSHA kwa msaada huo ambao wamesema umeongeza ari ya kujifunza na kushiriki katika shughuli za kijamii.
Bonanza hilo lilihusisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, na michezo ya jadi kama kukimbia kwenye magunia, kukimbia na ndimu kwenye kijiko, rede na kukamata kuku. Washiriki walitoka OSHA na vyuo vya Ufundi vya Mirongo, Nyakato na Kisesa.
Chuo cha Ufundi Mirongo kinamilikiwa na Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), na hutoa mafunzo ya umeme, useremala, ushonaji na uchomeleaji kwa vijana wakiwemo wenye mahitaji maalum.
📌 Tasnia ya Burudani na Michezo kwa mwaka 2024/2025 imekuwa kwa asilimia 18
📌 Watumishi 3,353 washiriki SHIMIWI mwaka 2025
📌 Awahimiza washiriki SHIMIWI kusikiliza kampeni za wagombea na kupiga kura Oktoba 29
📌 Serikali kujenga Kituo cha Kulea Vipaji Mwanza
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa rai kwa wanamichezo kufanya uchunguzi wa afya zao kwa kuhusisha vipimo vyote muhimu ikiwemo vya moyo, damu na viungo vyote vya mwili ili kuhakikisha usalama wa Afya zao.
Ameliomba Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kuendelea kushirikiana na Taasisi za Afya nchini na kuweka mfumo sahihi wa upimaji wa afya kwa wanamichezo.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Septemba 7, 2025 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati akifungua rasmi mashindano ya 39 ya SHIMIWI yaliyotanguliwa na maandamano ya watumishi wa umma.
Ametaja masuala mengine muhimu ya kuzingatiwa kwa wanamichezo “ Mazoezi ya awali na mbinu nyingine mbalimbali kwa kujenga uimara wa mwili kupitia mazoezi kama vile kukimbia, mazoezi ya nguvu na mazoezi mfano wa hayo. Pia, kuiandaa akili ili kuikabili michezo na mashindano kwa ujumla, wataalamu husema mafanikio huanza katika fikra,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kwa kusema Nimejulishwa kwamba, katika michezo ya mwaka wa jana mlisajili watumishi 2,995. Na mwaka huu 2025 mmesajili watumishi 3,353 kushiriki michezo hii ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 12 hongereni sana,”
Pia, ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na viongozi wa SHIMIWI kwa kazi kubwa ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza michezo nchini.
Dkt. Biteko pia amewataka waajiri kutekeleza maagizo ya Rais Samia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi wanaoshiriki SHIMIWI huku akiwaeleza watumishi kuwa Rais Samia anawatakia kila la heri katika michezo yao na kuwa yuko tayari kuendelea kushirikiana nao ili kupata mahitaji yao.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa, Tasnia ya Burudani Tanzania ambayo michezo ipo ndani yake imeendelea kukua kwa kasi na kuchangia sehemu muhimu katika Pato la Taifa na kuongeza ajira nchini.
Ametolea mfano kwa mwaka 2022/2023 sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 na mwaka 2023/24 kwa asilimia 18. Aidha, uwepo wa watumishi wanaoshiriki SHIMIWU zaidi ya 3,000 Jijini Mwanza umesaidia kutengeneza ajira na kuchangia mzunguko wa fedha.
“Nawaomba viongozi muweke mikakati ya kuhakikisha manufaa haya yanawagusa Watanzania wa maeneo yote nchini kwa maslahi mapana ya Taifa kwa ujumla,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Halikadhalika amewaasa wachezaji wote kujenga fikra ya kupendana na si kuchukiana baina yao pamoja na kufuata na kuzingatia taratibu zote za michezo.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewasihi wanamichezo hao kuhimizana kushiriki kwa amani katika zoezi la kusikiliza kampeni za wagombe na kukumbushana umuhimu wa kupiga kura.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza katika michezo ambapo inajenga Kituo cha Kulea Vipaji katika Chuo cha Michezo Malya.
Pia, amesema shughuli za kampeni mkoani humo zinaendelea vizuri na Oktoba 29, 2025 wananchi watajitokeza kwa wingi kupiga kura.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuruhusu kufanyika kwa mashindano ya SHIMIWI kwa watumishi wa umma kwa miaka mitano mfululizo kwa kuwa yameendelea kuwa na faida kubwa.
“ Wizara yetu itaendelea kuhakikisha michezo hii inafanyika kwa haki, sisi kama Wizara tunamshukuru Mhe. Rais kwa maelekezo yake na kutoa raslimali fedha ili kukuza sekta ya michezo nchini,” amesema Msigwa.
Ametaja jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya michezo ni pamoja na kukamilisha viwanja na shule za michezo katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika michezo kimataifa katika ngazi mbalimbali.
Katika salamu zake za utangulizi, Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa imefanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuleta matokeo chanya.
Awali, Dkt. Biteko ametembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambapo ameelezwa majukumu na huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Mashindano ya Michezo ya 39 ya SHIMIWI kwa mwaka 2025 yanayoongozwa na kaulimbiu “ Michezo kwa Watumishi Huongeza Tija Kazini, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 29 Oktoba 2025 kwa Amani na Utulivu Kazi Iendelee.”yatafikia tamati Septemba 16, 2025.
Mwisho
📌 *Yawa kinara katika kundi C*
Wakati mashindano yaliyoandaliwa na Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yakishika kasi jijini Mwanza kwa hatua za awali, Wizara ya Nishati imetinga katika hatua ya 16 bora katika mchezo wa Netiboli kwa kuwa na jumla ya alama tisa (9).
Wizara ya Nishati ipo katika kundi C ambapo kundi hilo linaundwa na Timu ya RAS Singida, RAS Shinyanga, Wizara ya Kilimo, pamoja na Hazina.
Awali, Wizara ya Nishati ilitupa karata yake ya kwanza dhidi ya RAS Singida na kuibuka na ushindi wa magoli 40 kwa 0 (sifuri), Mchezo wa Pili Nishati ilicheza na Wizara ya Kilimo na kushinda kwa magoli 34 kwa 22, mchezo wa tatu Nishati ilipoteza dhidi ya timu ya Hazina kwa magoli 36 kwa 21, huku katika mchezo wa nne Nishati ikicheza na Timu ya RAS Shinyanga na kuibuka na ushindi wa magoli 27 kwa 19 na hivyo kuwa kinara katika kundi C ikiwa na jumla ya magoli 122.
Aidha, Timu ya Wizara kwa sasa inasubiri taratibu za upangaji wa makundi ambayo yanatarajiwa kupangwa mwisho wa juma hili ambayo ni tarehe 6-7 Septemba, 2025.
![]() |
Michezo ya SHIMIWI ilianza Septemba Mosi 2025 ambapo ufunguzi utafanyika Septemba 07, 2025 na mashindano yatamalizika Septemba 16, 2025.
Katika michezo hiyo, Wizara ya Nishati imepeleka timu mbalimbali ikiwemo timu ya mpira wa miguu,riadha,karata,draft,mchezo wa Vishale, mchezo wa bao na baiskeli.
Mashindano ya SHIMIWI yamebeba na kauli mbiu isemayo "Michezo kwa Watumishi Huongeza Tija Kazini, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025,kwa Amani na Utulivu".