POLISI TANGA YAWATAHADHARISHA WANANCHI KUELEKEA SIKUKUU

December 21, 2017
Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga,Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Edward Bukombe akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matukio yaliyotokea kwa kipindi cha mwaka mzima ambapo alisema Jumla ya Silaha 14 za moto zilikamatwa  kulia ni RCO wa mkoa wa Tanga,Justine Masejo
JESHI la polisi mkoani Tanga, limewahadharisha wananchi kuelekea katika msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kama ulipuaji baruti na fataki ikiwemo kuchoma moto matairi barabarani, kwa yeyote atakayefanya hivyo atachukulia hatua za kisheri.
Kamanda mpya wa mkoa huo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Edward Bukombe, alisema kwamba jeshi hilo linapiga marufuku kwa mtu yeyote kulipua au kusababisha milipuko ikiwemo baruti, fataki na Eksozi za magari, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria namba 13 ya sheria ya milipuko.

“Hivyo wakazi wa mkoa wa Tanga, ni marufuku kuchoma matairi hovyo na kulipua baruti bila kibali, kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakae kiuka agizo hili,” alisema RPC Bukombe.

Alisema uzoefu unaonesha kuwa siku za sikukuu watu wengi hujisahau kujiwekea ulinzi ikiwemo kuwaangalia watoto hivyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi kuhakikisha wanachukua hatua za kuwalinda watoto pamoja na nyumba zao ili wahalifu wasitumie mwanya huyo kufanya uhalifu wa kuvunja au watoto kupotea mitaani.

Kamanda Bukombe alisema kwamba jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu bali aliwakumbusha kuzingatia taratibu za kumbi za burudani kufungwa nyakati za saa 6:00 usiku na hata ibada za mkesha wa Krismasi na Mwaka mpya zimalizike muda huo.

Katika hatua nyingine Kamanda huyo wa polisi alisema mwenendo wa uhalifu mkoani humo, katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka 2017, umeendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu ma hakuna matukio yanayotishia usalama kwa wananchi baada ya kuyadhibiti kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola.

Hata hivyo, alisema kwamba katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu, katika misako waliyoiendesha na operesheni mbalimbali waliweza kukamata wahalifu waliofanya matukio mbalimbali ambapo kesi za bangi zilikuwa 237 kwa bangi yenye uzito wa kilogramu 76.1 na mirungi kesi zilikuwa 37 na uzito wa mirungi ilikuwa kilogramu 5,396.740.

Kwa upande wa wahamiaji haramu jeshi hilo walikamata wahamiaji haramu wapatao 224 kati ya hao Wasomali walikuwa 55 na Waethiopia walikuwa 149 na Wakenya walikuwa 20 ambao wote walifikishwa katika vyombo vya sheria.

Kamanda huyo pia alisema kuwa katika kudhibiti ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha, jeshi hilo katika kipindi hicho lilifanikiwa kukamata jumla ya silaha 14 za moto ambapo bastola zilikuwa 2, shortgun 3 na magobore yaliyotengenezwa kienyeji yalikuwa 9.
 Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga,Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Edward Bukombe akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matukio yaliyotokea kwa kipindi cha mwaka mzima ambapo alisema Jumla ya Silaha 14 za moto zilikamatwa, kushoto ni Afisa Mnadhimu wa Jeshi hilo Mkoani Tanga,Leonce  na kulia ni RCO wa mkoa wa Tanga,Justine Masejo
 Sehemu ya waandishi wa habari wakichukua taarifa

WATU WANAOISHI NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI MKOANI TANGA WATAKIWA KUACHA KWENDA KWA WAGANGA WA KIENYEJI

December 21, 2017
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt Asha Mahita
akizungumza wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo WAVIU washauri   ili waweze kuwaunganisha wateja kutoka kwenye Jamii kwenda kwenye vituo vya Afya iliyoratibuwa na Shirika la  Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Care Initiative (AGPAHI) mkoani Tanga juzi kushoto ni Kaimu Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Tanga,Anita Temu na kulia ni Afisa
Mradi wa Huduma Unganishi wa Shirika hilo,Madina Paulo
Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani Tanga wametakiwa kuachana na kasumba za kukimbia kwa waganga wa kienyeji na  kuendelea na utaratibu walipangiwa na wahudumu wa afya wa kutumia dawa  kwani hali hiyo inaweza kuwasababishia matatizo makubwa.
Hayo yalisemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt Asha Mahita wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo Waviu washauri ili waweze kuunganisha jamii kwenda katika vituo vya afya. Warsha hiyo inaratibiwa na Shirika la AGPAHI mkoani hapa.
Alisema vitendo vya wagonjwa kuacha dawa vinaweza kuwaweka kwenye wakati mgumu ikiwemo kupata usugu ambao unaweza kupelekea kupoteza maisha kutokana na kushindwa kufuata utaratibu uliowekwa na kuwataka kuondokana na tabia za namna hiyo.
“Kuna tabia ambayo imejengeka baadhi ya wagonjwa kuacha kutumia dawa na kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kwani wanapoacha kutumia dozi na kutumia dawa nyingine.. virusi vinakuwa na usugu hali inayowasababishia hali mbaya zaidi na hata uwezekano wa kupoteza maisha “Alisema.
“Mpaka watu watambue kuwa hakuna dawa iliyothibitishwa kutibu VVU hivyo waendelea kuzitumia dawa za kupunguza makali ya VUU (ARV) ikiwemo kuacha kwenda kwa waganga wa kinyeji kwani wanaweza kukumbana na matatizo makubwa sana “Alisema.
Aidha alisema pia katika mpango wa mkoa wa Tanga wataendelea kuhamasisha wananchi kwenda kwenye vituo vya afya ili waweze kujua afya zao ikiwemo kuweza kuchukua hatua iwapo watabainika wameathirika.
“Lakini pia kwa watoto maana upimaji wao upo chini ikiwemo kuhakikisha watoto wanaopata maambuzi wanaanzishiwa dawa mapema kwani zitawasaidia kuongeza maisha yao na kuishi na afya njema”Alisema. 
Awali akizungumza katika semina hiyo,Afisa Mradi Huduma Unganishi wa Jamii wa Shirika la AGPAHI mkoani Geita Richard Kambarangwe alisema warsha hiyo ni kuwapa elimu zaidi Waviu washauri wanaosaidia kutoa huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC) kwa watu wanaoishi na VVU.
Alisema pia kuweza kuwasaidia kupata ujuzi zaidi ili kujifunza mbinu za kuwatafuta na kuwaunganisha wateja wa CTC na vituo kwa jamii kuweza kupunguza idadi ya kupotea kwa wateja.
“Lakini pia takwimu za Tanzania na mkoa inaonyesha watu wengi wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU wanaweza kupotea kwenye huduma hivyo shirika la AGPAHI mara kwa mara linazingatia kutoa elimu  itakayowasaidia watu kupata uelewa wa lishe na matumizi sahihi ya dawa “Alisema.
Kaimu Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Tanga,Anita Temu akizungumza wakati wa semina hiyo kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt Asha Mahita na kulia ni  Afisa Mradi wa Huduma Unganishi wa shirika la AGPAHI,Madina Paulo

Mganga M kuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt Asha Mahita katika akiteta jambo na Mratibu wa Ukimwi wa Jiji la Tanga,Moses Kisibo mara baada ya kufungua semina hiyo
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt Asha Mahita akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa semina hiyo mara baada ya kuifungua



KANISA LA UKOMBOZI LATEMBELEA AMANI, LAKUMBUSHA KUJALI WATOTO

December 21, 2017
WATANZANIA wamekumbushwa kuwajali na kuwangaalia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwatimizia mahitaji yao ya kimwili na kiroho.
Aidha, wamepaswa kutambua kwamba wana wajibu wa kusaidia watoto hao kwa kuwa wanawekeza kwa manufaa ya taifa na wao wenyewe.
Kauli hiyo imetolewa na Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam, akizungumza baada ya kukabidhi vifaa, bidhaa na mahitaji mbalimbali ya watoto yatima wa kituo cha Amani, kilichopo Bagamoyo, kiasi cha kilomita 65 kutoka Dar es salaam.
na Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (mwenye gauni la bluu) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akizungumza jambo mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani, Margareth Mwegalawa (katikati) kukabidhi vitu mbalimbali kituoni hapo akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa kanisa, waumini na wamama.
Akitoa maneno yanayogusa nyoyo huku akikariri maandiko Mchungaji Faith alisema:“Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu baba ni hii, kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa”
Alifafanua kwamba Kanisa lisiloangalia yatima na wajane si Kanisa, alisema na kuongeza kuwa waumini wanastahili kuwajibika kwa hilo.
Aidha, alisema kama Kanisa wanajali watoto na ndio maana wamefunga safari kwenda kuwaona na wamefurahi kuwaona na kushiriki nao tafrija fupi baada ya kuwakabidhi zawadi mbalimbali.
na Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (wa kwanza kulia) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam na baadhi ya viongozi, wakinamama na waumini wakifungua tafrija hiyo fupi kwa maombi kabla ya kukabidhi mahitaji mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo kijiji cha Zinga, Bagamoyo.
Waumini wa kanisa hilo walikabidhi mahitaji ya shule ya watoto, mavazi na chakula.
Aliwataka watanzania kuwa na tabia ya kujali watoto hao kwa kuhakikisha wanapata mahitaji yao kila siku na sio siku ya sikukuu tu.
Alisema watoaji wanapaswa kutoa kwa hali na mali kwa ajili ya kuondoa dhiki za watoto hao, ikiwa ni sehemu ya Baraka kamili kwa Mungu na pia kwa taifa.
Alisema watoto hao hawajulikani kesho watakuwa watu gani na kama watalelewa vyema watakuwa ni sehemu ya taifa lenye uadilifu na woga kwa Mungu.
Baadhi ya wakinamama wa kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam wakishiriki maombi baada ya kuwasili kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani kilichopo katika kijiji cha Zinga, mjini Bagamoyo.
Alisema kwa kuwezesha utulivu wa watoto hao, watoto watamjua Mungu na hivyo kujenga taifa lenye maisha yenye utukufu wa Mungu.
Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Esther Pilila alisema kwamba kama wanawake katika Kanisa lao wamesukumwa na haja ya kuwaangalia watoto hao kama wajibu wao.
Akizungumza kushukuru Mkurugenzi wa kituo hicho Margareth Mwegalawa aliomba watanzania kuwakumbuka watoto hao na kuitafadhalisha serikali kuwapitia kila mara kwa kuwa wao ndio walezi wa watoto.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akisaini daftari la wageni alipowasili katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani kilichopo katika kijiji cha Zinga, Bagamoyo.
Alisema pamoja na chakula walichopewa wanatamani watu mbalimbali kuendelea kuwajali watoto kwa kuhakikisha wanakuwa salama.
Alisema wadau mbalimbali wasiangalie tu vituo vya mashirika ya dini bali vituo vyote ambavyo vinabeba mzigo wa malezi kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Alisema kituo cha Amani chenye watoto 40 kinahitaji kupata uzio ili kuhakikisha watoto wapo salama.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akiwa amempakata mtoto Nicolaus (1.5) wakati wakitazama burudani kutoka kwa watoto wa kituo cha kulelea yatima cha Amani kilichopo katika kijiji cha Zinga, Bagamoyo.
Naye mtoto Salama Ismail (12) alishukuru kwa misaada hiyo ya mavazi na chakula, mafuta ya kupakaa, miswaki na madaftari na kutaka wananchi wamjue Mungu kwa kuwajali.
Naye Haji Joseph (11) aliomba viongozi wa serikali kuwatembelea kwani wao ndio wazazi wao na kuwasaidia kuimarisha upatinakaji wa nishati katika kituo chao hasa umeme wa REA.
“Tunaomba viongozi wa serikali watutembelee tuwajue na hasa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa” alisema mtoto huyo.
Watoto wa kituo cha kulelea yatima cha Amani kilichopo Zinga, Bagamoyo wakitoa burudani sambamba na Mkurugenzi wa kituo hicho Margareth Mwegalawa walipotembelewa na waumini wa kanisa la Ukombozi wakiongozwa na Mchungaji Faith Tetemeko (hawapo pichani) wakati wa tafrija fupi ya kukabidhiwa mahitaji mbalimbali ya kujikumu kituoni hapo.
Pichani juu na chini ni baadhi ya wakinamama wa kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam walioshiriki tafrija hiyo.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (mwenye gauni la bluu) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akicheza sambamba na mtoto Haji Joseph (11) katika tafrija fupi ambapo Kanisa la Ukombozi lilikabidhi vitu mbalimbali zikiwemo sare za shule, vyakula, madaftari, nguo na mahitaji mengine ya kujikimu.
Pichani juu na chini ni wakinamama wa kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam wakiwa wamebeba vitu mbalimbali vilivyotolewa kwenye kituo cha watoto yatima cha Amani kilichopo Zinga, Bagamoyo.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko (katikati) wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akikabidhi vifaa, bidhaa na mahitaji mbalimbali ya watoto wa kituo cha Amani cha watoto yatima, kilichopo Bagamoyo kwa Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Margareth Mwegalawa (kulia) katika hafla fupi iliyofanyika kituoni hapo Bagamoyo. Kushoto ni , Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Kanisa la Ukombozi tawil la Dar es Salaam, Esther Pilila.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo, watoto pamoja na walezi wa kituo hicho.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam katika picha ya pamoja na wakinamama wa kanisa hilo na walezi wa kituo hicho mara baada ya kukabidhi msaada huo.
Mwalimu Heavenlight (kushoto) na Mwanaukombozi Favour wakipozi na mtoto Nicolaus (1.5) kuonyesha upendo kwa mtoto huyo.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akigawa chakula kwa watoto yatima wa kituo cha Amani kilichopo Bagamoyo mara baada ya kukabidhi vitu mbalimbali kituo hapo.
Watoto yatima wa kituo cha Amani kilichopo Bagamoyo wakifurahia chakula cha pamoja kilichoandaliwa na wakinamama wa kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akishiriki chakula cha pamoja na watoto yatima wa kituo cha Amani kilichopo Bagamoyo.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akimlisha chakula mmoja wa watoto yatima wa kituo cha Amani kilichopo Bagamoyo mara baada zoezi la kukabidhi misaada mbalimbali kituoni hapo.
Pichani juu na chini ni Wakinamama wa kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam wakicheza michezo mbalimbali na watoto yatima wa kituo cha Amani ukiwemo 'Tulinge Baiyoyo' mchezo ambao katika makuzi kila mtu aliupitia.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam, Esther Pilila akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa kituo hicho mara baada ya kuhitimisha zoezi la kukabidhi msaada huo.
Mwana wa Nabii BG Malisa Mchungaji, Faith Tetemeko wa Kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam akizungumza na kituo cha televisheni cha Channel Ten mara baada ya kukabidhi misaada hiyo kituoni hapo.
Mtoto Haji Joseph (11) wa kituo cha watoto yatima Amani akitoa neno la shukrani kwa kanisa la Ukombozi kwa kupokea misaada hiyo katika tafrija fupi iliyofanyika kituoni hapo.
Mtoto Salama Ismail (12) wa kituo cha watoto yatima cha Amani akitoa shukrani kwa misaada hiyo ya mavazi na chakula, mafuta ya kupakaa, miswaki na madaftari iliyotolewa na wakinamama wa kanisa la Ukombozi tawi la Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kituo cha watoto yatima cha Amani kilichopo Bagamoyo, Bi. Margareth Mwegalawa akisisitiza jambo wakati wa mahojiano na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kupokea msaada huo.

MIKOA YA KUSINI KUPATA UMEME WA UHAKIKA

December 21, 2017
 Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Dkt. Alexender Kyaruzi (katikati) na wajjumbe wa bodi ya Shirika hilo, wakipatiwa maelezo walipotembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mahumbika mkoani Lindi
Na Yasini Silayo
Shirika la Umeme Tanzania  TANESCO limewahakikishia Umeme wa uhakika wakazi wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kutokana na uboreshwaji mkubwa wa huduma za Uzalishaji, Usafirishaji na Usambazaji Umeme zinazoendelea katika Mikoa hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi alipofanya Ziara ya kikazi katika mikoa ya Lindi na Mtwara akiambatana na wajumbe wengine wa bodi pamoja na viongozi waandamizi wa TANESCO Makao Makuu na Kanda ya Kusini.
Akiongea na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali Mkoani Lindi, Dkt. Kyaruzi amesema kuwa tayari TANESCO imefanya matengenezo makubwa katika mitambo ya kuzalisha umeme wa Gesi wa Megawati 18. Mtambo huo unahudumia Mikoa ya Mtwara pamoja na Baadhi ya maeneo ya Lindi kupitia laini mpya ya 132kV Mtwara-Mahumbika iliyokamilika tangu mwezi Julai mwaka huu ikijengwa na mafundi wazawa kutoka ndani ya TANESCO kupitia kampuni Tanzu yake iitwayo ETDCO.
"Mbali na hali ya umeme kuimarika hivi sasa kutokana na matengenezo ya mitambo ya Mtwara, Shirika hivi sasa linaendelea na maandalizi ya ujenzi wa miradi miwili mikubwa ya Uzalishaji Umeme wa jumla ya megawati 540 Katika Mikoa hii pamoja na kuunga mikoa ya Kusini katika Umeme wa Grid ya Taifa kwa Laini kubwa ya Msongo wa Kilovolt 400. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Mradii huu itakuwa kutoka Kinyerezi DSM mpaka somangafungu Lindi ambapo patajengwa mtambo wa kuzalisha umeme wa Megawati 240, mradi tayari umekwishaanza kwa kulipa fidia wananchi walioko eneo la mradi ili wapishe kupitisha laini hiyo. Awamu nyingine itaunga Somanga mpaka Mtwara ambapo kutajengwa pia mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Megawat 300. Songea tayari inaunganishwa na gridi kupitia makambako na mradi unaelekea kukamilika kwa asilimia kubwa" alisema Dkt. Kyaruzi
Aliongeza kuwa kutokana na mikakati ya muda mfupi, ya kati na muda mrefu iliyowekwa na TANESCO na Serikali ya awamu ya tano kwa ujumla, matatizo ya umeme katika mikoa hiyo yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi wa kudumu na hivyo kuchochea hamasa ya maendeo ya kiuchumi na Kijamii katika ukanda huo.
Aliongeza kuwa TANESCO inatarajia kupanua mifumo yake ya kusambaza umeme na kuiunga na mifumo ya pamoja ya nchi za Kusini mwa bara la Africa, Southern African Power pool (SAAP) kupitia Zambia pamoja na ile ya Africa Mashariki Kupitia Nchi ya Kenya. Baada ya kuunganisha mifumo
hiyo Nchi itaweza kununua na hasa kuuza ziada ya umeme kwa Nchi hizo pale itakapohitajika.
Aidha naye Mjumbe wa Bodi hyo Dkt. Lugano Wilson alisisitiza wakandarasi wa miradi ya umeme katika mkoa huo na mikoa mingine kwa ujumla kuhakikisha wanazingatia Viwango na Ubora wa kazi ili miradi hii iweze kutimiza lengo kusudiwa la kuwahudumia wananchi kwa umeme wa uhakika na kuchochea maendeo ya kiuchumi na kijamii.
"Mnapotekeleza miradi hii kwa ubora na viwango vinavyotakiwa, wananchi watapata umeme wa uhakika na kwa Upande wa TANESCO mtatupunguzia gharama za matengenezo ya mara kwa mara yatokanayo na ujenzi wa laini yenye kiwango duni" alisema Dkt. Lugano
Kwa upande wa wananchi wa maeneo hayo walionesha kufarijika na kupata shauku kubwa ya kuunganishwa na kuboreshewa huduma za umeme ambapo mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Shabani alisema kuwa "Licha ya changamoto za Umeme tulizokuwa nazo kipindi cha nyuma lakini kwa kweli tumeshuhudia juhudi kubwa za viongozi wa Serikali, Wizara na TANESCO wanaotutembelea na kutufariji kuwa hali itakuwa shwari, na kweli sasa mambo yameanza kuwa mazuri umeme haukatiki tena mara kwa mara" alisema Mwananchi huyo

Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Dkt. Alexender Kyaruzi akiongea na wananchi wa Mtama Mkoani Lindi wakati wa ziara ya Bodi ya wakurugenzi wa TANESCO Katika mikoa ya Lindi na Mtwara
-- Khalfan Said Photojournalist K-VIS MEDIA P.o.box 77807 Dar es Salaam, Tanzania Mobile: +255-784-646-453/+255-653-813-033 Blog: khalfansaid.blogspot.com

DK. KIGWANGALLA ATEUA WAJUMBE WENGINE WA KAMATI YA KUANDAA MWEZI WA URITHI WA TANZANIA

December 21, 2017

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAZINDUA VYOMBO VYA KUSIMAMIA BIASHARA YA UTALII NCHINI

December 21, 2017

  1. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na Wajumbe na Wenyeviti  kwenye hafla ya uzinduzi wa vyombo vya kusimamia Biashara ya Utalii nchini (TTLB) vikijumuisha  Bodi ya Leseni ya Biashara ya Utalii, Kamati ya ushauri ya Utalii na Mamlaka ya Rufaa ya Utalii zilizonduliwa leo jijini Dar es Salaam. ( Picha na Lusungu Helela- MNRT)
  1. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( wa kwanza kulia) akizungumza na  Mwenyekiti wa Bodi ya Leseni za Biashara za Utalii  Saleh Pamba ( wa pili kushoto)   katika hafla ya uzinduzi wa  vyombo vya kusimamia Biashara ya Utalii (TTLB) nchini iliyofanyika  leo jijini Dar es Salaam. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Alovce Nzuki,     ( wa tatu kushoto) Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Deograsias Mdamu, ( wa pili kulia)  Mjumbe wa Bodi ya TTLB, Michael Kamba  (wa  kwanza kushoto) ( Picha na Lusungu Helela- MNRT)
  1. Mwenyekiti wa Bodi ya Leseni za Biashara za Utalii  Saleh Pamba ( wa pili kushoto) pm akizungumza na  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( wa kwanza kulia)   katika hafla ya uzinduzi wa  vyombo vya kusimamia Biashara ya Utalii (TTLB) nchini iliyofanyika  leo jijini Dar es Salaam. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Alovce Nzuki, ( wa tatu kushoto) Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Deograsias Mdamu, ( wa pili kulia)  Mjumbe wa Bodi ya TTLB, Michael Kamba  (wa  kwanza kushoto) ( Picha na Lusungu Helela- MNRT)
  1. Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufaa ya Utalii, Balozi Mwanaidi Maajar akizungumza na Wajumbe na Wenyeviti  kwenye hafla ya uzinduzi wa vyombo vya kusimamia Biashara ya Utalii nchini (TTLB)  vikijumuisha  Bodi ya Leseni ya Biashara ya Utalii, Kamati ya ushauri ya Utalii na Mamlaka ya Rufaa ya Utalii zilizonduliwa leo jijini Dar es Salaam. ( Picha na Lusungu Helela- MNRT)
Mwenyekiti wa Kamati ya  Ushauri ya Utalii, Prof Wineaster Anderson akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekeiti kwenye kamati hiyo kwenye hafla ya uzinduzi wa vyombo vya kusimamia Biashara ya Utalii nchini (TTLB) vikijumuisha  Bodi ya Leseni ya Biashara ya Utalii, Kamati ya ushauri ya Utalii na Mamlaka ya Rufaa ya Utalii zilizonduliwa leo jijini Dar es Salaam. ( Picha na Lusungu Helela- MNRT

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na  Wajumbe na Wenyeviti  kwenye hafla ya uzinduzi wa vyombo vya kusimamia Biashara ya Utalii nchini (TTLB) vikijumuisha   Bodi ya Leseni ya
  1. Biashara ya Utalii, Kamati ya ushauri ya Utalii na Mamlaka ya Rufaa ya Utalii zilizonduliwa leo jijini Dar es Salaam. ( Picha na Lusungu Helela- MNRT)



Wizara ya Maliasili na Utalii  imefanya uzinduzi wa vyombo vya kusimamia biashara ya utalii nchini katika Chuo cha Taifa cha  Utalii kilichopo jijini Dar es salaam, ambapo vyombo hivyo vimejumuisha kamati ya ushauri,Mamlaka ya rufaa pamoja na Bodi ya mamlaka ya leseni.


Akiongea leo katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japheth Hasunga amewapongeza wanakamati wote waliochaguliwa na kusema kuwa anaamini kuwa watafanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inapiga hatua kusonga mbele.


Pia, Naibu  Waziri Hasunga amesisitiza kuwa vyombo hivyo vya kusimamia biashara ni vyombo muhimu sana katika kuendeleza sekta ya utalii na wajumbe wa vyombo hivyo ni muhimu kwa kusimamia sekta ya utalii nchini.


"Ni vyombo muhimu sana katika kuendeleza sekta ya utalii na wajumbe wa vyombo hivi ni muhimu sana kwa kusimamia sekta ya utalii hapa nchini" amesema Hasunga.


Aidha, Hasunga ameiomba Bodi ya Leseni ya Utalii iliyochaguliwa kufanya kazi katika misingi mikuu mitatu ya utawala bora ambayo ni Uhuru, uwazi, usawa na uzalendo ili kuepukana na migongano na kutokuelewana nyakati za kazi.


"Nawaomba mfanye kazi katika misingi ya utawala bora Uhuru, usawa, Haki na uzalendo"amesema Hasunga.


Katika hatua nyingiune, Naibu Waziri Hasunga amesema  kuwa sekta ya utalii ni sekta  inayochangia  kiasi kikubwa pato la Taifa  pia inasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa urahisi, hivyo amewaomba watanzania kuwa wazalendo kwa kuhamasisha uhifadhi wa mazingira pamoja na utamaduni wa mtanzania ili vivutio vizidi kuwepo kwani wasipotunza mazingira utalii hautaendelea kuwepo.


Pia amesema kuwa japo Tanzania ina vivutio vingi vya utalii bado mapato ni madogo ukilinganisha na vivutio vilivyopo hivyo ameeleza mikakati ya serikali kuwa imepanga kufikia watalii milioni mbili mpaka ifikapo mwaka 2020 ambapo jukumu hilo ni la kila Mtanzania.

"Mapato ni madogo ukilinganisha na vivutio vilivyopo na serikali tumepanga kufikia watalii milioni mbili ifikapo mwaka 2020 ni jukumu letu sote kuhakikisha tunafikia idadi hiyo. amesema Hasunga.


Pia ameisistiza Bodi ya leseni ya utalii kuhakikisha leseni za biashara zinatolewa kwa wakati na kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizopo.


"Mhakikishe leseni zinatolewa kwa wakati sahihi bila kucheleweshwa kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria kama inavyosema"amesema Hasunga.