VITA YA NAMBA YAANZA COASTAL UNION.

August 15, 2013
(Kocha Mkuu wa Coastal Union,Hemed Morroco juu kulia akizungumza na wachezaji wa timu hiyo jana mara baada ya kumalizika mazoezi yao ambayo yanaendelea uwanja wa Mkwakwani)

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
KIKOSI cha Coastal Union ya Tanga kimeonekana kuwa tishio sana baada ya kutokea vita ya wachezaji kugombea namba kutokana na kuwepo wachezaji wengi wenye uwezo na hivyo kupelekea ushindani kwenye kugombea nafasi za kucheza kwenye mechi.

Coastal Union ni miongoni mwa timu ambazo msimu huu zimefanya usajili wa kutisha na hivyo kuanza kuonekana makali yake kwenye mechi mbili za majaribio ambapo waliweza kuichapa Simba na URA ya Uganda na mwishoni mwa wiki kutoka suluhu pacha na 3 Pillars ya Nigeria. 


Kocha Mkuu wa timu hiyo,Hemed Morroco aliiambia Tanga Raha kuwa anafarijika na kitendo hicho ambacho msimu uliopita hakikuwepo na kueleza kutokana na hali hiyo anaimani watafanya mambo makubwa kwenye msimu mpya wa ligi kuu.

Morroco alisema ushindani unaonyeshwa kwenye mazoezi unampa faraja kutokana na wachezaji kujituma na kuwa na nidhamu ya hali ya juu na kueleza hali hiyo inampa jeuri ya kuchukua  pointi tatu muhimu kwenye mechi yao ya ufunguzi wa Ligi kuu Tanzania bara dhidi yao na JKT Oljoro itakayochezwa Agosti 24 katika uwanja wa Sheirh Amri Abeid mkoani Arusha.

Morroco alisema mechi za majaribio walizocheza zimempa mwanga mzuri wa kujua kikosi chake kinahitaji kitu gani kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu.

Alisema kutokana na usajili mzuri ambao ulifanywa na timu hiyo matumaini yake ni kuchukua ubingwa wa ligi hiyo ili kuweza kucheza kombe la shirikisho kwani hayo ni malengo yake ya kucheza kombe hilo siku zijazo.
   
Morroco alisema wanatarajia kuondoka mkoani hapa siku moja kabla ya mechi yao na Oljoro JKT na kueleza watakachokwenda kukifanya mkoani Arusha ni kufuata pointi tatu muhimu.

REDDS MISS ILALA KUONDOKA NA KITITA CHA SH,MILIONI 1.5

August 15, 2013
NA ASHA KIGUNDULA,DAR ES SALAAM.
MREMBO atakayetwaa taji la Redds Miss Ilala 2013, linalofanyika kesho Agosti  16, ataondoka na zawadi za jumla ya Sh. Milioni 1,500,000,huku mshindi wa pili atajipatia shilingi milioni moja na wa tatu shilingi laki saba.
 
Mbali na zawadi hiyo, washindi hao watatu watapata ofa ya ya miezi sita kutoka RIO gym & Spa, iliyopo Quality Center, kutumia vifaa vyote ndani ya gym hiyo ambayo gharama yake ni Milioni 900,000 kwa kila mtu.
 
Mratibu wa Shindano la Redds Miss Tanzania Kanda ya Ilala 2013, Juma Mabakila (katikati waliokaa), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akitangaza zawadi watakazopewa washindi wa shindano hilo litakalofanyika leo kwenye Ukumbi wa Golden Jubilee Dar es Salaam. Kutoka kushoto waliokaa ni Mkufunzi wa warembo hao Hafsa na William Malecela. Sh , 400,000 zitakwenda kwa mshindi wa nne na atakayeshika nafasi ya tano yeye ataibuka na Sh 300,000. Washiriki wengine ambao hawatabahatika kuingia katika nafasi ya tano bora, wote watapewa Sh,200,000 kwa maana ya kifuta jasho.
 
Tumelenga zawadi za fedha zaidi, hii ni kutokana na ugumu wa maandalizi kwa warembo ambao hugharamika zaidi, kiasi nasi kuona kuna kila namna ya kuwapunguzia maamivu hayo.
 
Shindano hilo, linatarajiwa kuwa na burudani ya kipekee kutoka kundi zima la Tanzania House of Talent (THT) wakiongozwa na mwanadada mwenye sauti ya chiriku, Lina na Barnaba.
Kundi la Wanne Star nalo litajumuika katika kuufanya usiku wa kesho kuwa wa burudani tosha kutokana na kuja kivingine kabisa katika nyimbo za asili za Afrika.
 
Warembo watakaopanda jukwaani Julai 5 ni kutoka Kigamboni, Kurasini na Chang'ombe ambao wanawania taji linaloshikiliwa na Miss Tanzania namba tatu, Edda Sylvester walikuwa chini ya wakufunzi Suzy Mwenda na Shadya Mohamed wakati kwenye kucheza nako walikuwa na walimu wawili Super Bokilo na Charles.
 
Warembo wataoapanda jukwaani hityo kesho ni 14 Diana Kato, Martha Gewe, Alice Issac, Irine Mwelelo, Clara Bayo, Natasha
Mohamed, Doris Molel, Upendo Lema, Kabula Kibogoti, Shamim Mohamed, Kazunde Kitereja, Rehema Mpanda, Johanither Kabunga,Anna Johnson.
 
Shindano hilo limedhaminiwa na kinywaji cha Redd's, Dodoma Wine, Gazeti la Jambo Leo, Cloud’s Media, Blogu ya Wananchi (Le Mutuz), Fredito Entertainment, CXC Africa tours & Safaris, RIO Gym& Spa, Smile Internet, Delina Interprises na Kitwe General Traders.
 
Ilala Interteinment  ndiyo inayoandaa mashindano haya, inatanguliza shukrani zake wadhamini wetu kwa miaka hiyo, sanjari na vyombo vyote vya habari kwa ujumla wake, kwani ndio waliofanikisha kufanikisha shughuli yetu ya kesho

YANGA, AZAM KUVAANA NGAO YA JAMII J’MOSI

August 15, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga na makamu bingwa Azam wanavaana Jumamosi kwenye mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa 2013/2014.

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa kivutio kwa wapenzi wa mpira wa miguu nchini itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni ambapo mshindi atakabidhiwa ngao.


Iwapo dakika 90 za mechi hiyo hazitatoa mshindi, timu hizo zitatenganishwa kwa mikwaju ya penalti huku asilimia 10 ya mapato ya mechi hiyo yakienda kwa kituo cha kulelea watoto cha SOS.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000.

LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA SEPT 14

August 15, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoshirikisha timu 24 zilizogawanywa katika makundi matatu msimu huu (2013/2014) itaanza kutimua vumbi Septemba 14 mwaka huu.

Kila timu itakayoongoza kundi lake katika ligi itakayochezwa kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini) ndiyo itakayopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2014/2015.

Mechi za ufunguzi kwa kundi A zitakuwa kati ya Tessema vs Green Warriors (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam) wakati Septemba 15 mwaka huu ni Transit Camp vs Polisi Dar (Uwanja wa Mabatini, Pwani), Ndanda vs Friends Rangers (Uwanja wa Nangwanda, Mtwara) wakati Villa Squad vs African Lyon itachezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Kundi B ni Burkina Faso vs Polisi Moro (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Mkamba Rangers vs Lipuli (Uwanja wa CCM Mkamba, Morogoro), Majimaji vs Mlale JKT (Uwanja wa Majimaji, Songea) wakati Septemba 15 mwaka huu Kimondo SC vs Kurugenzi (Uwanja wa Sokoine, Mbeya).

Mechi za ufunguzi kundi C ni Polisi Mara vs Polisi Dodoma (Uwanja wa Karume, Musoma), Kanembwa JKT vs Polisi Tabora (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Stand United vs Mwadui (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), na Pamba vs Toto Africans (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza).

Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Oktoba 26 mwaka huu wakati wa pili utamalizika Machi 22 mwakani. 

MKURUGENZI WA VIJANA TAIFA ATOA SEMINA KWA VIJANA MKOA WA TANGA.

August 15, 2013

Mgeni rasmi Bw. Ramadhani  Kaswa, Mkuu wa kitengo cha Mipango  katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa akifungua semina hiyo. Bw. Kaswa amemwakilisha Katibu Tawala Mkoa.


Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Tanga Bi Digna Tesha akiteta jambo wakati wa semina


Profesa Elisante Ole Gabriel akitoa neno katika semina hiyo.



Profesa Elisante Ole Gabriel,kushoto,kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Taifa akiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ajili ya semina ya vijana.


Baadhi ya vijana waliohudhuria semina.  Ni Maafisa vijana na vijana wa wenye umri wa miaka 15 hadi 35 kutoka Halmashauri zote mkoani Tanga.


Baadhi ya vijana waliohudhuria semina.  Ni Maafisa vijana na vijana wa wenye umri wa miaka 15 hadi 35 kutoka Halmashauri zote mkoani Tanga.


Baadhi ya vijana waliohudhuria semina.  Ni Maafisa vijana na vijana wa wenye umri wa miaka 15 hadi 35 kutoka Halmashauri zote mkoani Tanga.


Baadhi ya vijana waliohudhuria semina.  Ni Maafisa vijana na vijana wa wenye umri wa miaka 15 hadi 35 kutoka Halmashauri zote mkoani Tanga.
Habari na picha kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa “www.mkoatanga.blogspot.com”