MAKAMBA AZIPIGA TAFU SHULE YA MSINGI KWEMBALAZI NA KWEULASI

September 11, 2013
Raisa  Said,BUMBULI.
Mbunge  wa  Jimbo  la  Bumbuli  January  Makamba  amekabidhi  msaada  wa  mabati  80 na fedha taslimu laki tano kwenye  shule  ya  msingi  Kwembalazi  na Kweulasi  kwa  ajili  ya  kusaidia  ujenzi  wa  madarasa  katika shule  hizo ambazo  ziko  pembezoni  mwa  jimbo  hilo .

Pia  Wajumbe   wa  Kamati   ya  maendeleo  ya  kata  ya  Milingano wameeleza kufurahishwa kwao na juhudi za Mbunge wa Jimbo hilo, January Makamba katika kuendeleza elimu,afya  na  kuleta maendeleo ya jumla ya jimbo hilo.

Akizungumza  kwa  niaba  ya  January  Diwani  wa  kata  ya  Milingano  Hoza Mandia  ambae pia  ni  Katibu  wa  mbunge huyo  alisema  lengo  la kutoa  msaada  huo  ni  kuunga  mkono  juhudi  mbalimbali  zinazofanywa  na  wananchi  hao.

Akieleza  furaha  hiyo  kwa  niaba  ya  wajumbe  hao  Mwenyekiti  wa  kijiji  hicho Amiri Kaniki alisema  juhudi hizo za Mbunge huyo zinatakiwa kuungwa mkono na wakazi wote wa jimbo hilo ili  kuweza  kuharakisha  maendeleo  ya  haraka  na  kukuza uchumi  wa  bumbuli.

Katika  kumuunga  mkono  Mbunge  huyo  ambaye  ni  Naibu  Waziri  Mawasiliano  Sayansi  na  Teknolojia January  Makamba , Calorine  Johnstone ambaye  asili yake  ni  wingereza  alichangia  katika  sekta  ya  afya  kwenye  vijiji  vya  milingano  na Yamba  pamoja  na kujenga  vyumba  2  vya  madarasa  shule  ya  msingi  kweulasi  vyenye  thaman  ya  shilingi  mil. 50.
 
Wakati  huo huo  wakazi  wa vijiji vya Kwempunda na Manga vilivyopo  pembezoni mwa jimbo la  bumbuli wamemuomba ,Mbunge wa jimbo hilo,Januari Makamba kuwajengea vituo vya afya katika vijiji hivyo ili kuondokana na vifo vinavyoepukika.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Mbunge huyo hivi karibuni wananchi hao walisema changamoto kubwa inayowakabili ni kukosekana kwa vituo vya afya katika vijiji vyao hali ambayo inawalazimu kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
 
Mwananchi wa kijiji cha Kwempunda Khamisi Shekigenda alisema wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya katika vijiji vya jirani swala ambalo wakati mwingine limekuwa likiwaathiri wakinamama wajawazito na watoto.
 
Mbunge wa jimbo hilo,Januari Makamba akijibu hoja za wananchi hao aliwaambia atashirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha wanaipata huduma hiyo na kuondokana na vifo ambavyo vinaweza kuepukika katika vijiji vyao.
 
Aliwaambia watenge maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo na kuonyesha mchango wao ili hatimaye waweze kuondokana na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa vituo hivyo.
 
"Ndugu zangu wananchi niko tayari kushirikiana nanyi, ninachowaomba kuanzia sasa muanze kutenga eneo ,mchimbe msingi pamoja na kusombelea mawe na mchanga,a hapo mtakapofikia mimi nitawasaidia,"alisema Makamba.
 

Rais Jakaya Kikwete ALIVYOZINDUA MRADI MAJI WA KIJIJI CHA KATUNGURU, WILAYANI SENGEREMA MWANZA JANA.

September 11, 2013

 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo ya utekelezaji wa mradi wa umeme wa MCC unaotekelezwa katika mikoa ya Mwanza na Geita wakati wa  hafla ya ufunguzi wa njia mpya za umeme kwenye mifumo ya kusambaza umeme mikoa ya Mwanza na Geita uliofanyika katika kijiji cha Bukokwa wilyani Sengerema,Mkoani Mwanza leo.Kulia ni Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.

 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Katika kijiji cha Katunguru/Nyamtelela wilayani Sengerema,Mkoani Mwanza leo.Kulia ni Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe.


Mwakilishi wa Serikali ya watu wa Marekani Bwana Karl Fickenscher akitoa hati ya kukabidhi mradi wa MCC I kwa waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo wakati wa  hafla ya ufunguzi wa njia mpya za umeme kwenye mifumo ya kusambaza umeme mikoa ya Mwanza na Geita uliofanyika katika kijiji cha Bukokwa wilayani Sengerema,Mkoani Mwanza leo.Katikati akishuhudia ni Afisa mtendaji Mkuu wa Millenium Challenge Account-(MCC)Tanzania Bwana Bernard Mchomvu.

Habari kwa hisani ya Handenikwetu.blogspot.com.

MAJI MAREFU KUFUNGA MAZOEZI YA MCHEZO WA BAISKELI JUMAPILI.

September 11, 2013
Na Elizaberth Kilindi,Tanga.
MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Vijijini,Stephen Ngonyani "Maji Marefu" anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa mazoezi ya wachezaji wa timu ya mchezo wa Baiskeli mkoa wa Tanga ambao wanajiandaa na mashindano ya baiskeli Taifa yatakayofanyika Septemba 29 mwaka huu mkoani Dodoma.

Akizungumza na Blog hii ,Katibu wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Tanga(Chabata),David Manyilizu alisema wachezaji wa mchezo hu zaidi ya 10 mkoani hapa walianza mazoezi ya mchujo kwa ajili ya kujiaandaa na mashindano ya ngazi ya Taifa.

Manyilizu alisema mazoezi hayo yaliambatana na mchujo kwa wachezaji ambapo kati ya kumi waliojitokeza ni sita walifanikiwa kuchaguliwa kwa ajili ya kuuwakilisha mkoa kwenye mashindano hayo ambayo yanatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa.

Akifungua  mazoezi hayo,Manyilizu alisema mazoezi hayo yatasaidia kuwajenga vyema wachezaji hao ambao watachaguliwa kwenda kushiriki mashindano hayo na kuleta kombe mkoani hapa.

 "Mazoezi haya yatawajenga wachezaji wetu na tunatarajia watafanya vizuri huko tunapokwenda hivyo  ndio maana tunawaandaa mapema ili wafanye vizuri"Alisema Manyilizu.

Aidha aliwaasa wachezaji wa timu hiyo ya mkoa watakaochaguliwa kuhakikisha wanashiriki vema mashindano hayo ili waweze kupata nafasi katika mchujo wa wachezaji 10  wataunda timu ya Taifa ambayo itaenda kushiriki mashindano ya kimataifa Rwanda .

ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA KWA KUKUTWA NA NOTI BANDIA.

September 11, 2013
Na Hamisi Ramadhani,Korogwe.
Mfanyabiashara mmoja Water Mikiandua (44) mkazi wa Jijini Dar es Salaam anashikiliwa katika kituo cha Polisi wilayani Korogwe Mkoa Tanga kwa tuhuma za kupatikana na noti bandia zenye thamani ya Sh milioni 112.

Mfanyabiashara huyo alikamatwa juzi katika kizuizi cha polisi Wilayani hapa akiwa anasafiri baada ya polisi kulitilia mashaka gari alilokuwa amepanda aina ya Scania Basi Kampuni ya Sai baba, ambapo lilikuwa likitokea Arusha kwenda Dar es Salaam.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Juma Ndaki alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 6.30 mchana katika kizuizi cha polisi Wilayani hapa ambapo polisi walisimamisha na kuanza kulipekuwa wakazikuta pesa hizo zikiwa kwenye buti ambapo zilikuwa zimehifaziwa kwenye begi la nguo la Mfanyabiashara huyo.

Alisema pesa hizo zilikuwa za kitanzania Sh10,000 zikiwa 12300 zenye thamani ya Sh112 pia alikutwa na pesa za euro 60,000 zinazodhaniwa kuwa za bandia zenye thamani ya Sh11 milioni za kitanzania.

Hata hivyo alisema mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa Mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili mara baada ya Polisi kukamilisha taratibu za upelelezi.

Ndaki alitoa wito kwa wananchi wanaofanya biashara ya maduka na wengineo kuwa makini wanapopewa pesa wazikague kucheki saini na pia watoe ushirikiano kwa jeshi la polisi endapo watawabaini ili kuweza kukomesha wizi huo.