TAASISI ZOTE ZINAZOTOA HUDUMA ZA KIJAMII KUUNGANISHWA UMEME - MHE. KAPINGA

July 23, 2024

 -REA yapongezwa kufikisha umeme katika shule vijijini

-Vijiji vyote Wilaya ya Nyasa vyafikiwa na umeme

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa Taasisi zote zinazotoa huduma za kijamii kama shule na vituo vya afya pamoja na nyumba za ibada zitafikishiwa umeme.

Naibu Waziri Kapinga ameyasema hayo leo Julai 22 wakati akiwasha umeme katika Shule ya Sekondari Nyasa iliyoko katika Kijiji cha Chimate wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.

“Sisi kama Wizara ya Nishati ni kuhakikisha tunaongeza tija katika taasisi hizi zinazotoa huduma kwa kufikisha umeme. Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anahangaika usiku na mchana kutafuta fedha za kuboresha maisha ya Watanzania kila siku na kazi yetu kubwa ni kuhakikisha taasisi na maeneo yote yenye umuhumi yanafikiwa na umeme.

Tayari TANESCO na REA wamejidhatiti maeneo ambayo kuna taasisi za kijamii kama shule, vituo vya afya, makanisa, misikiti vyote vinafikiwa na umeme ili kuboresha huduma za kijamii katika Taifa letu,” amesema Naibu Waziri Kapinga.

Amesema kuwa uwepo wa umeme shuleni umesaidia hata kuongeza ufaulu kwa kuwa wanafunzi wamekuwa wakipata muda wa kujisomea hata usiku tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya miradi ya kusambaza umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) haijaanza.

Awali akitoa taarifa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Eng. Robert Dulle amesema kuwa gharama za kufikisha umeme katika kijiji hicho ni shilingi Milioni 286.

Eng. Dulle ameongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma unajumla ya Vijiji 554 na mpaka kufikia Julai 2024, vijiji 542 sawa na asilimia 97.8 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi inayotekelezwa na REA na kwa Wilaya ya Nyasa kuna jumla ya vijiji 84 ambapo vyote vimepata umeme.

Eng. Dulle pia amewahamasisha wananchi kuchangamkia fursa za uwepo wa umeme vijijini kufanya shughuli za kiuchumi zitakazoboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyasa, Mwalimu John Ndelwa ameipongeza REA kwa kuwafikishia umeme shuleni kwao na kuahidi kuwa watatumia fursa ya kuwepo umeme kuwafundisha wanafunzi masomo ya jioni na hivyo kuongeza ufaulu.

Ameongeza kuwa uwepo wa umeme utawawezesha kuwa na mitihani mingi ya majaribio kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kuchapa mitihani wenyewe shuleni tofauti na awali ambapo walikuwa wanalazimika kutumia gharama kubwa kwenda kuchapisha katika steshenari.







LIPENI KODI KUIWEZESHA TBA KUJENGA NYUMBA NYINGI ZAIDI - WAZIRI BASHUNGWA

July 23, 2024

 * TBA yapongezwa kwa ubunifu katika upangaji miji na teknolojia


Na Leandra Oltmanns, Dar es Salaam

WAZIRI Wa Ujenzi Innocent Bashungwa amewataka wapangaji wanaoishi katika nyumba za makazi zinazosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) kulipa kodi kwa wakati na kuiagiza Wakala hiyo kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu wote kwa mujibu wa sheria za mikataba ili fedha hizo zitumike katika ujenzi wa majengo mawili kwa ajili ya watumishi wa Umma (Block C na D,) Magomeni Kota awamu ya pili ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 15.

Akizungumza leo Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam katika hafla ya ufunguzi wa jengo moja la ghorofa saba linalobeba Kaya 16 lililogharimu shilingi Bilioni 5.6 Bashungwa amesema; Serikali imeendelea na jitihada za kujenga makazi bora kwa watumishi ili kupunguza changamoto za makazi na kuwataka watumishi waliopata fursa ya kuishi katika nyumba hizo kutimiza wajibu kwa kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha TBA kujenga nyumba nyingi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuwa uhitaji wa nyumba bora umefikia zaidi ya nyumba milioni tatu kwa ongezeko la nyumba laki tatu na tisini elfu kila mwaka.

Ameelekeza Wakala hiyo kuendelea kufanya kazi kiwango bora na ubunifu zaidi kwa wakati huu ambao Serikali imerekebisha sheria ya Wakala kwa kutoa fursa kwa TBA kushirikiana na sekta binafsi pamoja na Taasisi za fedha katika uendelezaji milki, kujenga nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma pamoja na watanzania kwa ujumla.

Aidha ameipongeza Wakala hiyo kwa kuwa wabunifu katika ardhi na mipango ya majengo ya kisasa katika miradi wanayoisimamia, ambapo katika eneo la Magomeni lenye hekari 32 awali lilikuwa na wakazi 645 na baada ya TBA kusimamia ujenzi na ukadiriaji majengo ekari 9 zimejengwa nyumba za makazi zilizotosheleza wakazi 645.

"TBA inakwenda katika mwelekeo sahihi katika ubora wa majengo pamoja na teknolojia ikiwemo hii ya kitasa janja itakayosaidia kuwadhibiti wanaokwepa kulipa kodi.....TBA chukueni hatua kwa wadaiwa sugu bila kuangalia wadhifa." Ameongeza Bashungwa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro amesema mradi huo umegharamiwa na Serikali kwa fedha za ruzuku zipatazo shilingi Bilioni 5.687 na utekelezaji wake ulianza Novemba 2022.

Amesema jengo hilo ni la pili kati ya majengo 5 yanayojengwa katika eneo hilo kwa ajili ya makazi ya watumishi wa Umma ambapo jengo moja tayari limekamilika na limepangishwa na hadi kukamilika kwa majengo yote matano jumla ya kaya 80 zitakuwa zikiishi hapo, Na ujenzi wake umezingatia kanuni na misingi ya ujenzi wa majengo ya Serikali.

"Jengo A limekamilika na tayari limepangishwa, jengo B ni hili ulilolizindua leo na majengo mawili C na D ujenzi wake umefikia asilimia 15 na ukamilishaji wa majengo hayo yaliyosalia kadiri ya mpango kabambe uliopo utategemea upatinaji wa fedha." Amesema.

Kuhusiana na ubunifu unaofanywa na Wakala hiyo Kondoro amesema; ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM,) ya 2020/2025 ibara ya 55 (h) inayoelekeza maeneo yaliyorejeshwa Serikali Kuu chini ya Wakala hiyo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelezwa kwa kujenga nyumba zinazoweza kubeba familia nyingi (apartments.) bora na za kisasa.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema, uzinduzi huo ni matokeo mazuri ya utendaji kazi TBA chini ya Wizara ya Ujenzi ambao wamekuwa wakitekeleza miradi kwa teknolojia ya ubora na upangaji wa miji.

"Nyumba hizi msiwape wahuni, wanaofanya kazi ya udalali na baadaye kuleta taharuki za madai ya kodi kubwa na gharama nyingine na kuharibu taswira ya eneo hili, nyumba hizi zinapangishwa kwa gharama ndogo ikilinganishwa na kodi ya soko." Amesema.

Aidha amemuomba Waziri wa Ujenzi kuweka mkakati wa pamoja wa kuipanga Dar es Salaam kwa kushirikiana Sekta binafsi akitolea mfano wa maeneo yaliyopo pembezoni mwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ili kuliweka jiji hilo kuwa moja ya Miji mikubwa Afrika ifikapo 2030.

"Tutumie ubunifu katika kukusanya mapato ili kuendeleza Jiji hili...Tunaweza kuinusuru Dar es Salaam na mafuriko ambayo hadi sasa inahitajika takribani Bilioni 600 kwa TARURA Pekee ili kurudisha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko; kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tunaweza kujenga nyumba za gharama nafuu na watu wakaishi katika miji iliyojengeka vizuri...Serikali ibaki kufanya marekebisho huku mifuko ya watu binafsi ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya makazi."

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge amesema, wameridhika na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TBA katika Manispaa hiyo kwa kuwa imeboreshwa kwa kuzingatia mipango miji na mradi huo wa nyumba za watumishi wa Umma umezidi kupendezesha Manispaa ya Kinondoni pamoja na kupunguza changamoto ya makazi.


Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa (kulia,)akisogeza kitambaa kuashiria ufunguzi rasmi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma awamu ya pili zilizojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA.) Katika eneo la Magomeni Kota, kushoto ni Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro. Leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi Magomeni Kota awamu ya pili 'B' zilizojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) na kuiagiza TBA kukusanya kodi kutoka kwa wadaiwa sugu kwa mujibu wa sheria ili fedha hizo zitumike katika ujenzi na nyumba nyingine zaidi. Leo jijini Dar es Salaam.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa Wakala hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi ili kupunguza changamoto iliyopo. Leo jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi Magomeni Kota awamu ya pili 'B' zilizojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) na kueleza kuwa mradi huo ni matokeo chanya ya utendaji kazi wa TBA chini ya Wizara ya Ujenzi. Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.




TPA YATEKELEZA MAAGIZO YA BODI YA TASAC BANDARAI YA NYAMISATI

July 23, 2024

 *Mkurugenzi Mkuu TASAC asema zaidi ya Bilioni Mbili kununua boti za Uokozi


Na Chalila Kibuda ,Rufiji
Bodi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imesema maagizo walioyatoa kwa Mamlaka ya Bandari (TPA)katika Bandari ya Nyamisati yametekelezwa kwa asilimia 95.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya ziara ya Bodi hiyo katika Bandari ya Nyamisati iliyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani Mwenyekiti wa Bodi Nah.Mussa Mandia amesema kuwa TPA wametekeleza kwa asilimia 95 huku wakibakiza baadhi ya maeneo machache.

Mandia amesema kuwa katika ziara walioifanya katika Bandari ya Nyamisati 2020 ilikuwa ni kutaka maboresho ya Bandari ili iweze kujiendesha kibiashara kama moja ya Bandari ya mkakati.

"Tumeridhishwa na utekelezaji wa TPA kutekeleza ni kuona Bandari ya Nyamisati inafanya kazi kutokana na kuwa wateja katika mizigo na abiria"amesema Nahodha Mandia.

Mandia amesema kuwa katika mahitaji ya Bandari hiyo inahudumia visiwa 15 ambapo idadi abiria katika ya 500 hadi 1000 kwa siku huku mizigo ikiwa mingi.

Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed Salum amesema katika mkakati wa mwaka huu ni ununuzi wa boti za Uokoaji Sita zenye thamani ya zaidi ya Bilioni Mbili ambazo zitasambazwa katika vituo vya bandari.

Amesema Vyombo vilivyopo katika Bandari ya Nyamisati vimesajiliwa na vifaa vya uokozi hivyo kadri ya kila siku na mikakati iliyopo itafanya kuwa bora katika utoaji wa huduma.

Amesema mahitaji ya msingi ni mashine ya kupakia na kunyanyua mizigo 'Forklift' na miundombinu ya eneo Bandari kusakafiwa Kitaalam kwa abiria na mizigo.

Meneja wa Bandari ya Nyamisati Issa Unemba amesema kuwa Bandari ya Nyamisati itakwenda kuipita Bandari ya Bagamoyo kutokana na wahitaji wa mizigo kwenda katika nchi za Comoro na Madagascar.

Amesema kuwa utekelezaji kwa mizigo ya nje ya nchi kunatakiwa kuwepo kwa Afisa forodha kwani sehemu za maghala zipo za kutosha kwa vyakula na bidhaa zisizo za Chakula.
Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC Nahodha Mussa Mandia akizungumza na Waandishi wa Habari wakati Bodi hiyo ilipofanya ziara katika Bandari ya Nyamisati wilayani Rufiji Mkoani Pwani kuangalia uendelezaji wa Bandari hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed Salum akieleza kuhusiana na mipango ya mkakati katika Bandari ya Nyamisati katika kutoa huduma za Usafiri kwa Vyombo Vidogo vya Majini.
Meneja wa Bandari ya Nyamisati Issa Unemba akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na utendaji wa Bandari hiyo pamoja na maboresho yaliyofanyika wakati Bodi ya TASAC ilipotembelea Bandari ya Nyamisati wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed Salum akiangalia chombo kidogo chenye vifaa vya uokozi (hakipo pichani) katika Bandari ya Nyamisati.
Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC Nahodha Mussa Mandia akizungumza katika Bandari ya Nyamisati wakati Bodi hiyo ilipofanya ziara Bandari hapo.