IMEWEKWA DESEMBA 18,2013 SAA 7:14 ASUBUHI.
|
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Mh. Amosi Makala (kushoto) akipongezwa na mmiliki wa Taasisi ya Right to Play,
Dr. Dennis Bright (kulia) baada yakufungua kongamano la wanawake wa Afrika
viongozi wa michezo linalofanyika nchini |
|
Nahodha wa timu ya Taifa ya wanawake, ‘Twiga stars’,
Sophia Mwasikili akiwatambulisha wachezaji wenzake (hawapo kwenye picha) kwenye
kongamano la wanawake wa Afrika viongozi wa michezo |
|
Mmiliki wa Anita Foundation, Dr. Anita White
akizungumza kwenye kongamano la wanawake wa Afrika viongozi wa michezo
lililofanyika nchini. Waliokaa wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Mh. Amosi Makala kushoto ni Kaimu katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Dkt Ole Gabriel na mmiliki wa Taasisi ya Right to Play, Dr. Dennis
Bright na mwisho ni Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo |
WASHIRIKI wa kongamano la wanawake viongozi wa Afrika
linalofanyika nchini leo watafanya bonanza la michezo yote katika Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo wa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ambaye ndiye mwandaaji wa
kongamano hilo Juliana Yasoda alisema
kuwa watafanya bonanza hilo ambalo litajumuisha michezo yote katika Uwanja wa
Taifa kuanzia saa 3:00 asubuhi.
“leo) tutafanya bonanza ambalo litahusisha michezo
yote kwani hapa kuna viongozi na wanamichezo wa michezo yote na baadae timu za
Taifa ya Twiga na ile U-20 watacheza mchezo wa kirafiki”, alisema Juliana.
Michezo ambayo itachezwa ni soka, riadha, kikapu, mikono,
wavu, magongo, kurusha tufe na kisahani pamoja na kuvuta kamba.
Pia alisema kongamano hilo limesaidia kutoa mwanga na dira
kwenye michezo miongoni mwa washiriki kutokana na kila mmoja kuelezea uzoefu
wake katika michezo ukilinganisha na sera za nchi anayotoka.
Awali juzi wakati akifungua kongamano hilo Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makala aliwataka washiriki hao
kupigania michezo katika nchi wanazotoka
kwani wanawake ni chachu ya mafanikio kwenye michezo mbalimbali hasa
wakipewa elimu ya maendeleo ya michezo.
Kongamano hilo lilikuwa la siku mbili na lilishirikisha
viongozi wanawake toka nchi za Msumbiji, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Zambia
na Ghana pamoja na wageni wengine toka Finland na
Marekani