NA SELEMANI KIBUGO,MUHEZA.
MKUU wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu amepiga marufuku matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani humo kwa madai kuwa zinachangia matokeo mabaya ya mitihani
Wito huo umetolewa na mkuu huyo wa wilaya katika kikao cha wazazi wa wanafunzi hao kuwakumbusha juu ya ulipaji wa ada kwa wakati katika shule ya sekondari ya Mang’enya wilayani humo.
Amesema kuwa mwanafunzi yeyote akikutwa na simu walimu wazichukuwe wazipeleke ofisini kwake kwa ajili ya kuuzwa ili ichangie ujenzi wa maabara.
Mkuu huyo wa wilaya pia amewataka wazazi kulipa ada kwa wakati mpaka tarehe 30 mwezi huu wawe wazazi wamelipa ada zote wanazodaiwa.
Hata hivyo mkuu wa wilaya huyo amesema kuwa viboko virudishwe katika shule ya Mang’enya na mwanafunzi aadhibiwe kulingana na kosa lenyewe kama vile utoro,utovu wa nidhamu na kukutwa na simu.
Amesema atachangia katika shule huyo shilingi Laki tano kwa ajili ya ujenzi wa maabara huku akiwaomba wafadhili kujitokeza kuchangia ukarabati wa majengo utakoanza mwezi wa 9 mwaka huu.