LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA NNE

September 17, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM. 
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya nne kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi saba katika viwanja saba tofauti.

Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonalewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya Ruvu Shooting ya Charles Boniface Mkwasa. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka inayochezwa na timu hizo.

Baada ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi iliyopita, Yanga inaendelea kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo itacheza na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mbelwa kutoka Pwani.

Nayo Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya Tanga katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi.

Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa ambayo wikiendi iliyopita ilicheza Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini Morogoro kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.

UWAKILISHI KWENYE MKUTANO MKUU TFF

September 17, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema uwakilishi wa ujumbe kwenye Mkutano Mkuu unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.

Mwongozo huo juu ya uwakilishi wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu umetolewa kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF kwa kamati hiyo iliyokutana jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini baadhi ya wajumbe wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.

Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba, kuna makundi ya aina tatu ya wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu.

Sekretarieti ya TFF imebaini kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa ambao pia ni viongozi wa vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, hivyo wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye Mkutano Mkuu.

Hivyo, kutokana na mwongozo huo ushiriki wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa TFF utaanzia chama cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu za Ligi Kuu.

Pia nafasi ambazo zinaweza kuwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu kama mhusika hayupo ni za Mwenyekiti atakayewakilishwa na Makamu Mwenyekiti, na Katibu atakayewakilishwa na Katibu Msaidizi.  Nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu hazina uwakilishi kama mhusika hayupo.

KAYUNI KUHUDHURIA KOZI YA WAKUFUNZI WA CAF

September 17, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni atashiriki warsha ya wakufunzi wa makocha wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika kuanzia Oktoba 22-24 mwaka huu.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya wakufunzi wake itafanyika nchini Cameroon. Wakufunzi 18 wa CAF kwa upande wa makocha watahudhuria warsha hiyo.

Madhumuni ya warsha hiyo ni kuainisha majukumu yao, kubadilishana uzoefu. Pia kuwapa methodolojia mpya ya ufundishaji na muongozo kuhusu mfumo wa leseni za makocha ambao watautumia katika nchi wanazotoka.

Mbali ya Kayuni Tanzania, wakufunzi wengine ni Ahmed Babiker (Sudan), Amadou Shaibu (Nigeria), Boy Bizzah Mkhonta (Swaziland), Duodu Fred Osam (Ghana), Edussei Anthony (Ghana), Fathi Nossir (Misri), Faouzy Altaisha (Sudan) na Fran Hilton Smith (Afrika Kusini).

Wengine ni Francis Oti-Akenteng (Ghana), Honour Janza (Zambia), Kasimawo Laloko (Nigeria), Mahmoud Saad (Misri), Paul Hamilton (Nigeria), Serame Letsoaka (Afrika Kusini), Shawky Abdel Shafy (Misri), Thondoo Govinder (Mauritius) na Ulric Mathiot (Seychelles),

JAJI MUJULIZI AELEZEA UMUHIMU WA TUME YA SHERIA NCHINI.

September 17, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
MWENYEKITI wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania,Jaji Aloysius Mujulizi amesema kuwa umuhimu wa tume ya sheria nchini ni mkubwa sana na tayari wameshaanza kujiandaa na upokeaji wa ongezeko la uhitaji la mapitio ya sheria mbalimbali hasa katika kipindi hiki taifa likiwa kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba mpya.

Alitoa rai hiyo leo wakati akifungua kikao cha tisa cha baraza la
wafanyakazi wa tume ya kurekebisha ya sheria kilichofanyika katika ukumbi wa hotel ya Tanga Beach Resort na kudhuhuriwa na wakuu wa idara,na vitengo mbalimbali vya tume hiyo.

Mujulizi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania alisema endapo katiba mpya itapitishwa ni wazi kutakuwa na hitaji la mabadiliko makubwa ya sheria na kueleza licha ya suala la katiba alifananua  kwa kusema lipo eneo linalokuwa muhimu kwa maendeleo ya Taifa ikiwemo rasilimali za gesi,mafuta ya asili.

Alisema tume hiyo inapaswa kujipangia mikakati  ya michango katika eneo husika ili kuwezesha uwepo wa mfumo mzuri wa sheria haki kwa kuzingatia mamlaka na uwezo tulionao pamoja na kuyaangalia kwa undani na upana wake kwenye kutekeleza majukumu yao.

Mwenyekiti huyo aliwataka kuchukua fursa hiyo kuwahimiza ikiwemo kutumia maadhimisho hayo ya miaka thelathini ya tume kama chachu ya kuwatangaza kwa kueleza umme kuhusu yale yaliyofanywa katika taifa letu na wananchi ili kuweza kuwa kitu kimoja.

Awali akizungumza,Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha
sheria,Winfrida Korosso alisema tume hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kukusanya mabadiliko yaliyofanywa kwenye sheria mbalimbali na kuzihuisha kuanzia mwaka 2002-2012 na kuziweka kwenye tovuti yao.

Korrosso alisema pia wameweza kufanya uchambuzi wa hukumu 200 za mahakama ya rufaa (extraction of legal principles) na kukabidhi kwa waziri wa katiba na sheria taarifa ya mapitio ya sheria za madai ikiwemo mila zinazofuata mkondo wa mama.

Aidha alisema tume hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo wanaendelea kuzifanyia kazi ili kuweza kuzipatia ufumbuzi na kukabili kazi mpya zinazokuja bila kuwa kwenye mipango akitolea mfano mchakato wa katiba .

JAJI MUJULIZI AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANGA.

September 17, 2013
KATIBU MTENDAJI WA TUME YA SHERIA ,WINFRIDA KOROSSO AKIZUNGUMZA WAKATI WA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA LEO KATIKA HOTEL YA TANGA BEACH RESORT

MWENYEKITI WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA,JAJI ALOYSIUS MUJULIZI AKITOA HOTUBA YAKE WAKATI AKIFUNGUA MKUTANO HUO.