BALOZI IDDI ATEMBELEA KUJIONEA NYUMBA YA SALIM AHMED SALIM ILIYOBOMOKA MJINI ZANZIBAR, AKUTANA NA WAWEKEZAJI WA INDIA

May 12, 2014

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijumuika pamoja na baadhi ya wananchi kuangalia athari iliyotokea na  nyumba ya Bwana Salim Ahmed Salim baada ya ukuta na dari yake kuanguka  saa sita usiku juzi mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
 Sehemu ya mbele ya Nyumba ya Bwana Salim Ahmed Salim iliyoporomoka  Mtaa wa Vuga mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja.
Hata hivyo hakuna mtu aliyejeruhiwa kutokana na athari hiyo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akizungumza na Meneja wa Kampuni ya Kimataifa ya uwekezaji vitega uchumi  wa Kampuni ya Lucky Exports kutoka Nchini India Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Balozi Seif akisalimiana na Menaja wa Kampuni ya Lucky Exports ya India inayotaka kuwekeza katika sekta za Afya na Viwanda vidogo vidogo vya mazao ya Baharini.
Balozi Seif akisalimiana na Mwakilishi wa Kampuni ya Lucky Exports Tawi la Tanzania Bwana Kim Mghaya. Kati kati yao ni Meneja wa Kampuni hiyo yenye makao makuu yake Nchini India Bwana Ravi  Rai.
*********************************
Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Usafiri zimekumbushwa kuendelea kuzuia uingiaji wa  gari kubwa zenye uzito wa zaidi ya Tani Mbili katika eneo la Mji Mkongwe ili kunusuru majengo yaliyono ndani ya mamlaka hiyo.
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi  kukagua athari ya nyumba  iliyoporomoka ukuta na Dari yake juzi usiku iliyopo Mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja  Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema ukaidi wa baadhi ya madereva  wa gari kubwa kupitisha Gari gari zao katika eneo hilo umesababisha uchafuzi wa mandhari na haiba ya Mji mkongwe wa Zanzibar ambao hivi  sasa uko katika urithi wa Kimataifa.
“ Jeshi la Polisi wakati huu litahitajika kuwa na kazi ya ziada katika kuhakikisha agizo lililotolewa na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar  linatekelezwa ipasavyo “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimpa pole Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana  Salim Ahmed Salim  kwa hasara  aliyoipata alimtaka kuwasiliana na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar  katika juhudi zaujenzi wa nyumba hiyo utakaozingatia  mpango  halisi wa uhifadhi wa Mji huo.
Akitoa ufafanuzi wa athari nyingi zilizojitokeza ndani ya nyumba za Mji Mkongwe, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano na Utafiti cha Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Bibi Madina Haji Khamis alisema ujenzi usiozingatia utaalamu wa Mamlaka  husika pamoja na upitishwaji wa gari kubwa ndio sababu kubwa za msingi za athari hizo.
Bibi Madina alifahamisha kwamba baadhi ya  wamiliki wa nyumba hizo walikuwa wakipandishia kuta  wakati wa ujenzi au matengenezo zaidi ya uwezo wa msingi wa nyumba hizo hali  inayoleta athari ya mipasuko ya nyumba hizo sambamba na mitetemeko ya gari kubwa zinazopitishwa pembezoni mwa nyumba hizo.                           
Mapema Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Salim Ahmed Salim alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif kwamba dalili za kuanguka kwa jengo hilo zilijionyesha mapema kutokana na kuvimba na baadaye kupasukwa kwa eneo la mbele la ukuta wa nyumba hiyo.
Bwana Salim alifahamisha kwamba kutokana na hali hiyo alilazimika kuuarifu Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliolazimia baadaye kwa kushirikiana na jeshi la Polisi kuchukuwa hatua za kuifunga bara bara hiyo.
“ Nilijaribu kuufuata Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe uniruhusu kuifanyia matengenezo makubwa nyumba yangu  ili baadaye niitumie kwa makazi na familia nyangu lakini bado sijapata jibu na huku inaporomoka “. Alieleza Bwana Salim Ahmed Salim.
 Nyumba hiyo ya ghorofa moja mpaka inaporomoka ukuta na dari yake majira ya saa sita juzi usiku lakini hamna watu waliokuwa wakiishi ndani yake.

Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi nyengine zimelazimika  kuzuia  Gari zote zinazotumia  Bara bara hiyo kutoka Vuga kuingia Shangani au kupitia Serena  ili kujaribu kuepuka hatari katika kipindi hichi cha Mvua za Masika.
 Kwa mujibu wa hali halisi ilivyo hivi sasa gari zote zinazokusudia kuingia ndani ya eneo la Mamlaka ya Mji Mkongwe zinalazimika kutumia Bara bara itokayo Malindi na zisizidi uzito wa zaidi ya Tani mbili.
Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa miaka kadhaa sasa imo ndani ya Ramani ya Dunia ya urithi wa hifadhi ya Kimataifa chini ya usimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni  { UNESCO }.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na ujumbe wa Kampuni ya uwekezaji vitega uchumi vya sekta za Afya, Kilimo, Umeme, viwanda vidogo vya mazao ya Baharini ya Lucky Exports kutoka Nchini India.
Kampuni hiyo ambayo imefungua Matawi yake katika mataifa mbali mbali Barani Afrika tayari imeshapata usajili wa kufungua Tawi lake Nchini Tanzania.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar  Meneja wa Kampuni hiyo Bwana Ravi Rai  alisema Taasisi yake imelenga kutoa huduma za afya pamoja na viwanda vidogo vidogo vya mazao ya Baharini.
Bwana Ravi Rai alisema wakati Uongozi wa Taasisi yake ukisubiri kuanza na hatimae kukamilisha taratibu zote za uwekezaji uwekaji wa miradi hiyo umekusudia kusaidia kutoa ajira kubwa kwa wazalendo pamoja na kuongeza mapato ya Taifa.
Alifahamisha kwamba utafiti  wa wataalamu wa Taasisi hiyo utafanywa ili kuangalia miradi ambayo kampuni hiyo inaweza kuiwekeza hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“ Tunafarajika kuona kwamba miradi yoyote tutakayoamuwa kuitekeleza  kwenye uwekezaji wa mataifa mbali mbali duniani na hasa tukilenga zaidi Bara la Afrika inafadhiliwa na Serikali ya India “. Alisema Meneja huyo wa Lucky Exports.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema miradi iliyofikiriwa kuanzishwa na Uongozi wa Kampuni hiyo hapa Zanzibar  ya Sekta ya Afya na Viwanda Vidogo vidogo vya mazao ya Baharini  itasaidia kustawisha maisha naustawi wa Jamii Nchini.
Balozi Seif aliuagiza  Uongozi wa Kampuni hiyo ya Lucky Exports kutoka Nchini India kurahisisha maombi yao ya uwekezaji ili taasisi zinazohusika na uwekezaji ziweze kuyapitia na kutoa maamuzi yanayostahiki kwa wakati muwafaka.
Kampuni ya Uwekezaji ya Lucky Exports ya Nchini India ambayo tayari imeshafungua matawi yake katika Mataifa ya Ethiopia, Guinea Bisau,  Malawi na Tanzania inajihusisha zaidi na uwekezaji wa miradi ya Afya, Kilimo, Viwanda vya mazao ya Baharini, Umeme pamoja na huduma za Reli.
Rais Kikwete aongoza Sherehe Siku ya Wauguzi Duniani mjini Arusha

Rais Kikwete aongoza Sherehe Siku ya Wauguzi Duniani mjini Arusha

May 12, 2014


3 (6)  
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisikiliza kwa makini jinsi wauguzi  wanavyotoa huduma ya afya kwa wagonjwa wakati alipotembelea mojawapo ya mabanda ya maonyesho ya Wauguzi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid mjini Arusha leo.1 (6) 4 (3)  
Wauguzi wakiandamana wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani wakiwa na mabango mbalimbali katika uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha leo(picha na Freddy Maro) 2 (6)
RUCO MABINGWA WA POOL VYUO VIKUU WAPONGEZWA

RUCO MABINGWA WA POOL VYUO VIKUU WAPONGEZWA

May 12, 2014


SAM_4505 
 Nahodha wa timu ya Pool ya chuo kikuu cha Ruco , Said Mohamed akimkabidhi mgeni rasmi kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Ramadhani Mungi kikombe cha ubingwa wa mchezo huo baada kuandaliwa hafla ya kuwakaribisha iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hill  juzi kushoto ni meneja mauzo wa tbl mikoa ya Iringa,Njombe na Ruvuma Raymond Degera.
SAM_4480 
Kikosi cha timu ya Ruco kikiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili mkoani Iringa
Na Denis Mlowe,iringa
 
WANAFUNZI wa chuo kikuu cha Ruaha (RUCO) cha mkoani Iringa nchini wameshauriwa kuundeleza mchezo wa Pool sambamba na kufanya vema katika masomo yao na kuwapongeza kwa kuuletea sifa mkoa wa Iringa katika mchezo huo kwa vyuo vikuu.
 
Wito huo umetolewa na mgeni rasmi, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa, ACP Ramadhani Mungi katika hafla ya kuwapongeza  mabingwa wa mchezo huo kitaifa katika ngazi ya vyuo vikuu uliondaliwa na kampuni ya TBL kupitia kinywaji chake cha safari Lager na chuo cha RUCO kuchukua ubingwa kwa mara ya kwanza iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Gentle Hill.
 
Mungi alisema wanafunzi wengi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kubanwa na mambo ya burudani na michezo na kuwapongeza vijana hao kuwa na ratiba nzuri ya masomo na michezo hadi kufanikiwa kuchukua ubingwa wa vyuo vikuu kitaifa.
 
“Naupongeza sana uongozi wa chuo cha ruco kwa kuweka ratiba nzuri ya vipindi na michezo, utaratibu wa kujua ni wakati gani wa kusoma, wakati gani wa kufanya mazoezi hivyo bila uongozi wa chuo hicho msingefikia hapo na ndio chanzo hadi nyie kuchukua ubingwa huu na kuuletea sifa mkoa wa Iringa nawapongeza uongozi wa chuo cha ruco na vijana wangu” alisema Mungi
 
Alisema kuwa mchezo wa pool unazidi kukua kwa kasi kubwa nchini na lakini viongozi wake wanatakiwa kuwa makini na vijana wanaoweza kuharibu sifa ya mchezo huo hasa kwa vijana wanaofanya pool kama kijiwe cha kuvutia bangi.
 
Aliongeza asilimia kubwa ya vijana wanajiajiri kwa kuppitia michezo hivyo juhudi kubwa inatakiwa kuwekwa kuweza kuwawezesha vijana kuingia katika sekta ya michezo kwa kuwa ni ajira tosha katika maisha ya sasa.
 
Mungi alisema kupitia michezo hata uhalifu huwa unapungua kwa kuwa wengi wamekuwa wakijishughulisha hasa katika tasnia ya burudani kwa kuwa  hata wao wanapenda kujishughulisha katika michezo.
 
“Katika burudani uhalifu huo unapungua kwani wahalifu nao wanapenda kuburudika kwa hiyo tujitahidi sana kushughulikia michezo na burudani kuweza kupunguza uhalifu, mfano mmoja ni kuwa kuna tamasha kubwa liliwahi kufanyika hapa mkoani iringa katika kuripoti matukio siku ya pili kwa kweli polisi kulikuwa hakuna tukio lolote la uhalifu siku hiyo kwa kuwa wahalifu hao walikwenda nao kuburudika siku hiyo” alisema na kuwafanya wageni waalikwa kucheka .
 
Aliitaka serikali kuwa jirani na sekta ya michezo yote na kuiboresha kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana ambao asilimia kubwa hawana ajira na kuongeza kuwa michezo uleta afya ya akili na afya ya mwili hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kufanya mazoezi.
 
Mungi alivitaka vijiwe vyote vya mchezo wa pool kujiepusha na kuuza na kununua madawa ya kulevya na kuahidi kufanya msako mkali kwa kila kijiwe cha mchezo huo wanaojihusisha na biashara hiyo kwa kuwa vinajulikana na jeshi la polisi.
 
Alivitaja vijiwe vinavyojihusisaha na biashara hiyo kwa kigezo cha mchezo wa pool kuwa ni Mashine tatu, Ipogoro, Kihesa na Mlandege ndio vinaongoza kwa biashara hiyo inayoharibu sifa ya mchezo wa Pool.
 
Kwa upande wake nahodha wa timu ya mchezo wa Pool kutoka Ruco, Said Mohamed aliutaka uongozi wa chuo hicho kuwapa ushirikiano katika kuundeleza mchezo huo kwa kuwaandalia ratibu nzuri ya mazoezi na muda wa masomo.
 
Alisema kupitia mchezo huo wamefanikiwa kukitangaza chuo kitaifa na kimataifa hivyo ni jukumu la chuo sasa kuweka kipaumbele katika michezo mingine kuweza kukiletea sifa chuo na mkoa kwa ujumla.
 
Aliupongeza uongozi wa Tbl kuptia kinywaji cha Safari Lager kwa kudhamini mchezo huo na kuongeza soko la ajira kupitia michezo na kuutaka kuendelea  kudhamini mchezo huo.
 
Naye meneja mauzo mikoa ya Iringa,Njombe na Ruvuma Raymonda Degera aliwapongeza mabingwa hao na aliwataka kuongeza juhudi na maarifa ilikuweza kuuchukua tena mwakani katika mashindano mengine ya vyuo vikuu nchini wa mchezo wa pool

STARS, ZIMBABWE KUUMANA DAR JUMAPILI

May 12, 2014
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors) itafanyika Jumapili (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Awali mechi hiyo tulipanga ichezwe Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kwa nia ya kuhakikisha mikoa yote ya Tanzania inapata fursa ya kuwa mwenyeji wa mechi za kimataifa.

Ili Uwanja wa Sokoine uweze kuchezwa mechi za kimataifa za mashindano, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilituma Mkaguzi (inspector) wake kwenye uwanja huo Jumamosi (Mei 10 mwaka huu) ambapo imeamua kuwa marekebisho yanayofanyika hayatamalizika katika muda stahili, hivyo mchezo huo kutochezwa Sokoine.

Tunatoa mwito kwa wamiliki wote wa viwanja kuwasiliana na TFF ili Idara ya Ufundi iwaelekeze maboresho ya kufanya ili viwanja vingi iwezekanavyo viweze kukidhi viwango vinavyotakiwa na CAF na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini mkoani Mbeya itarejea Dar es Salaam keshokutwa (Mei 14 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)