KAMATI YA USALAMA BARABARANI YAKABIDHI MAGARI NA PIKIPIKI KWA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA

March 04, 2024

 



KAMATI ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya imekabidhi magari mawili na pikipiki mbili kwa Jeshi la Polisi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu hasa doria za barabara kuu, utoaji wa elimu na kudhibiti ukiukwaji wa sheria za usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari Machi 04, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga katika hafla fupi ya mapokezi ya magari na Pikipiki ameishukuru Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya kwa msaada wa magari na Pikipiki hizo kwani zitasaidia sana katika kufanikisha kutekeleza majukumu kwa ufanisi na haraka.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mhandisi Rajabu Ghuliku ameeleza kuwa "Kamati imeona vema kutoa msaada wa pikipiki na magari kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu katika Kikosi cha Usalama barabarani Mkoani Mbeya"

Aidha, Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu wa Polisi Hussein Gawile amesema kuwa, vitendea kazi hivyo vinakwenda kuongeza ufanisi na nguvu katika kuzuia na kudhibiti ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Jumla ya magari mawili na pikipiki mbili yenye thamani zaidi shilingi Milioni 31 yamekabidhiwa katika hafla hiyo.

Benki Ya CRDB Kanda Ya Ziwa Yazindua Kampeni Ya 'SimBanking Transact By Finger'

March 04, 2024

 

Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa imezindua kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger' inayolenga kuhamasisha wafanyakazi wa benki hiyo kuwaunganisha wateja na kuwaelimisha ili kutumia huduma ya SimBanking.

Uzinduzi huo umefanyika Jumatatu Machi 04, 2024 katika tawi la CRDB Nyanza jijini Mwanza ambapo katika kampeni hiyo, wafanyakazi watakaowaunganisha wateja wengi zaidi na huduma ya SimBanking watajishindia zawadi mbalimbali.

"Kupitia SimBanking, mteja anaweza kufanya mihamala hadi millioni 20 kwa siku, tukiwaelekeza namna ya kutumia huduma hiyo, tutapunguza msongamano kwenye matawi yetu" amesema Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta.

Naye Kiongozi wa kampeni hiyo, May Mosi Ndunguru amewahamasisha wafanyakazi wa benki ya CRDB kuhamasisha wateja wengi kutumia SimBanking kwani inarahisisha upatikanaji wa huduma huku wote, wateja na wafanyakazi wakijishindia zawadi kutoka CRDB.
Kampeni hiyo itadumu kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Machi 04, 2024.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger' inayolenga kuhamasisha wafanyakazi wa benki hiyo kuwaunganisha na kuwaelimisha wateja kutumia huduma ya SimBaking huku wakijishindia zawadi mbalimbali.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger'.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger'.
Kiongozi wa kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger' kutoka benki ya CRDB, May Mosi Ndunguru akihamasisha wafanyakazi wa benki hiyo kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma ya SimBanking ili kujishindia zawadi.
Keki kwa ajili ya uzinduzi wa huduma ya 'SimBanking Transact By Finger' jijini Mwanza.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta akikata keki kwenye uzinduzi wa kampeni ya 'SimBanking Transact by Finger' Kanda ya Ziwa.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta akiwalisha keki wafanyakazi wa benki hiyo.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta akiwalisha keki wafanyakazi wa benki hiyo.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta akiwalisha keki wafanyakazi wa benki hiyo.
Meneja wa CRDB Tawi la Nyanza, Eugenius Mashishanga (kulia) akimlisha keki Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta (kushoto).
Meneja wa CRDB Tawi la Nyanza, Eugenius Mashishanga (kulia) akimlisha keki Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta (kushoto).
Meneja wa CRDB Tawi la Nyanza, Eugenius Mashishanga (kulia) na Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta (kushoto) wakifurahia baada ya uzinduzi wa kampeni ya SimBanking Transact By Finger jijini Mwanza.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta na wafanyakazi wa benki hiyo wakigonga 'cheers' wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
Wafanyakazi wa CRDB wakifuatilia uzinduzi wa kampeni ya SimBanking Transact By Finger inayolenga kuhamasisha wafanyakazi kuwaunganisha wateja na huduma ya SimBanking.
Zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa wafanyakazi wa CRDB watakaowaunganisha wateja wengi na huduma ya CRDB.
Kiongozi wa kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger' kutoka benki ya CRDB, May Mosi Ndunguru akionyesha zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa wafanyakazi.
Kiongozi wa kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger' kutoka benki ya CRDB, May Mosi Ndunguru akionyesha zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa wafanyakazi.
Kampeni ya 'SimBanking Transact By Finger' itadumu kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Machi 04, 2024.

NMB Yaunga Benki Nyingine 17 Kwenye Mtandao Wake Wa ATM

March 04, 2024


Ushirikiano wa Benki ya NMB na UBX inayounganisha Benki 17 kwenye mtandao wake wa Umoja Switch umeiwezesha Benki ya NMB kuunganisha benki hizo 17 kwenye mtandao wake wa mashine za kutolea fedha (yaani ATM interoperability).

Ushirikiano huu unalenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa mashine za ATMs na kupunguza gharama za miamala ya ATM kwa wateja wa Benki hizi, na Watanzania kwa ujumla.

Kupitia ushirikiano huu wa Benki ya NMB na UBX, Watanzania watanufaika na mambo yafuatayo:


--Upatikanaji wa Huduma za ATM - Wateja wa Benki zote 17 za Umoja Switch na wateja wa Benki ya NMB watakuwa na uwezo wa kufanya miamala na kupata huduma za kibenki wakati wowote kupitia mtandao wa ATMs zaidi ya 700 za NMB zinazopatikana nchi nzima na ATMs za Umoja Switch (zaidi ya 280) na hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma.

--Unafuu wa Gharama kwa Wateja - Ushirikiano huu unaongeza ufanisi na kuleta unafuu mkubwa wa gharama za miamala ya ATM. Gharama za miamala ya ATM kwa wateja wa Benki hizi 17 waliokuwa wanatumia ATM za NMB na wateja wa NMB waliokuwa wanatumia ATM za benki hizi zinaenda kupungua kwa zaidi ya asilimia 70%.

--Ujumuishwaji wa Kifedha – Ushirikiano huu utaongeza matumizi ya kadi kwenye ATM nchini na kupunguza foleni matawini – hii ni njia mbadala ya kuongeza ujumuishaji rasmi wa kifedha nchini.

--Ufanisi wa Mabenki - Benki shiriki zitaweza kufikia maeneo yaliyo mbali na ambayo hapo awali ilikuwa vigumu kwa taasisi moja kuyafikia kwa kuweka ATM.

--Unafuu wa Gharama kwa Mabenki - Ushirikiano huu pia, unakwenda kupunguza gharama za uendeshaji kwa benki shiriki. Miamala yote inayofanyika nchini haitakuwa na ulazima tena wa kupitia nje ya nchi, miamala hii itakamilishwa ndani ya mtandao wa NMB na UBX na hivyo kupunguza gharama kubwa za uendeshaji tulizokuwa tukilipa awali, hasa gharama za fedha za kigeni kwa ajili ya kuweka dhamana kwenye taasisi za nje zilizokuwa zinatoa huduma za mtandao kwa ajili ya kukamilisha miamala hii.

Hii ni mara ya kwanza kwa makubaliano ya namna hii kufanyika na hivyo makubaliano haya yanaandika historia mpya katika sekta ya kifedha nchini Tanzania

Akiongea kwenye hafla hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB - Bi. Ruth Zaipuna alisema: “Nina Imani ya kuwa ushirikiano huu utakuwa mwanzo na chachu ya mashirikiano mengine mengi na ya kimkakati katika sekta yetu ya kibenki nchini Tanzania kwa manufaa ya wateja wetu na Watanzania kwa ujumla. Kupitia mashirikiano ya kimkakati kama haya tutaweza kupiga hatua zaidi katika utoaji wa huduma nafuu, rahisi na salama za kibenki kwa watanzania wote, na hivyo kuchochea ukuaji wa kiuchumi wa mtanzania mmoja mmoja na taifa letu kwa ujumla.”

Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi huu alikuwa Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) Naibu Waziri wa Fedha ambaye aliipongeza Benki ya NMB na UBX na kushauri mashirikiano kama haya yaendelee kwa manufaa ya nchi yetu.

Hafla hii ilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UBX, ndugu SabaSaba Moshingi na viongozi kutoka mabenki mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na viongozi wa Benki 17 zilizo chini ya Umoja Switch.

Benki zilizo chini ya Umoja Switch ni pamoja na Access Microfinance Bank, Akiba Commercial Bank, Azania Bank, Bank of Africa, DCB Commercial Bank, Letshego Bank, Maendeleo Bank na Mkombozi Commercial Bank. Zingine ni MUCOBA Bank, Mwalimu Commercial Bank, MwangaHakika Bank, Peoples’ Bank of Zanzibar, TCB Bank, Uchumi Commercial Bank, International Commercial Bank na United Bank for Africa.







UFUNGUZI WA MKUTANO WA MAWAZIRI WA SHERIA WA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA MADOLA

March 04, 2024

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 04 Machi, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 04 Machi, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Viongozi  na wageni waalikwa wakiwa wamesimama wakati wa wimbo wa Taifa kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 04 Machi, 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Viongozi wengine wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 04 Machi, 2024.

Baadhi ya wageni waalikwa kutoka nchi wanachama za Jumuiya ya Madola wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 04 Machi, 2024.

14 WATEULIWA KUWANIA UDIWANI KATA YA KIMBIJI KIGAMBONI

March 04, 2024

Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kimbiji, Bw. Ricky Pascal na Bi. Twidike Ntwima wakibandika fomu za utezi wa wagombea wa udiwani Kata ya Kimbiji leo baada ya muda wa uteuzi kumalika Saa 10:00 jioni ya Machi 4,2025. Wagombea 14 waliochukua fomu wameteuliwa kuwania nafasi hiyo. 
Wagombea wa Udiwani Kata ya Kimbiji wakitazama fomu za uteuzi zilizobandikwa katika ubao wa Matangazo katika Ofisi za Kata ya Kimbiji. Wagombea 14 waliochukua fomu wameteuliwa kuwania nafasi hiyo. 
Wagombea wa Udiwani Kata ya Kimbiji wakitazama fomu za uteuzi zilizobandikwa katika ubao wa Matangazo katika Ofisi za Kata ya Kimbiji. 
Wagombea 14 waliochukua fomu wameteuliwa kuwania nafasi hiyo. 

Wagombea wakikabidhiwa fomu zao za uteuzi baada ya Tume kuwateua kuwa wagombea udiwani Kata ya Kimbiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dares Salaam wamerejesha fomu na kuteuliwa kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi Mfogo wa udiwani uyakaofanyika Machi 20,2024.

ELIMU YA HUDUMA YA KWANZA YAWAKOSHA MADEREVA BODABODA JIJINI TANGA, AMEND WATOA NENO

March 04, 2024



Na Mwandishi Wetu,Tanga

UBALOZI wa Uswisi kupitia ufadhili walioufanya kwa taasisi isiyo ya kierikali ya AMEND kwa ajili ya kutoa elimu ya usalama barabarani ikiwemo elimu ya huduma ya kwanza kwa madereva bodaboda, umewasaidia madereva hao kuwa na uwezo wa kutoa msaada pindi ajali zinapotokea.

Wakizungumza na wandishi wa habari Jijini Tanga baada ya kupewa elimu ya usalama barabarani na taasisi ya AMEND madereva wa kituo cha Mikanjuni hospitali Ally Zuberi na Faky Hamis wamesema ukosefu wa elimu umekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani kwa madereva wengi wa bodaboda.

Hivyo wameeleza kwamba elimu waliyoipata kuhusu usalama barabarani itawasaidia kuendesha kwa tahadhari pindi wanapokuwa barabarani na hivyo kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikisababisha video na ulemavu wa kudumu.

Akieleza zaidi Mwenyekiti wa Bodaboda Kituo cha Mikanjuni Hospitali Mwin'dadi amesema kutozitambua sheria na alama za barabarani imekua ndio sababu ya ajali ya nyingi kutokea huku akibainisha elimu waliyoipata itawasaidia kujiepusha dhidi ya ajali.

Wakizungumzia kuhusu elimu ya huduma kwanza madereva hao wamesema watakuwa mstari wa mbele kutoa msaada pale ajali itakapotokea ambapo wameendelea kusema kuwa elimu hiyo watawashirikisha na madereva wenzao ili kushiriki katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Benilda Mtumbuka ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii kata ya Magaoni ametoa shukrani kwa Ubalozi wa Uswisi na taasisi ya AMEND kutokana na elimu ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda.

Ametoa mwito kwa bodaboda waliopata elimu kuitumia vyema jambo litakalosaidia kupunguza ajali huku akiwata AMEND kuendelea kutoa elimu hiyo kwa madereva wengine.

Wakati huo huo Ofisa Miradi wa AMEND Ramadhani Nyanza amesema elimu ya huduma ya kwanza waliyoitoa kwa madereva bodaboda imeleta mwanga kwa madereva hao kwa kujua namna bora ya kutoa msaada pale kunapotokea ajali.

Nyanza amesema mpaka sasa madereva bodaboda takribani 126 katika Jiji la Tanga wamefikiwa kwa kupatiwa elimu ambapo amebainisha malengo ni kuwafikia madereva 500 kwa mkoa Tanga.

JKCI YAOMBWA KUTOA ELIMU YA LISHE KWA WANANCHI.

March 04, 2024
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Mlagwa Yango akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group Laetitia Kokutangaza akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Mfamasia kutoka kampuni ya Microlabs Laborex Zawadi Mbasa akimpatia dawa mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Picha 4: Daktari wa Hospitali ya JKCI Dar Group Masanja James akipa maelekezo mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Watafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Saadi Kamtoi na Loveness Mfanga wakiwafanyia utafiti wananchi waliofika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Picha na: Khamis Mussa

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam wameiomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kutoa elimu ya lishe bora ambayo itawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanywa na wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo walisema licha ya kupata huduma za matibabu pia wamefurahia kupata elimu ya lishe ambayo imewasaidia kufahamu namna bora ya kuchagua makundi ya vyakula.

Mzee Abdalah Yasini mkazi wa Temeke alisema inawezekana kupatwa kwake kwa tatizo la mishipa ya damu kuziba kulisababishwa na kutokupata elimu ya lishe bora kwani angejua toka zamani namna ya kula chakula chenye mchanganyiko wa makundi yote ya vyakula kwa kiasi angeweza kuepuka tatizo la mishipa yake ya damu kuziba.

“Ninawaomba wataalamu wa lishe watafute namna ya kufikisha elimu ya lishe bora kwa jamii hata ikiwezekana katika vyombo vya habari kuwe na kipindi cha lishe kitatusaidia sana”, alisema Mzee Abdalah

Mzee Abdalah alisema kama jamii itazingatia lishe bora kwa kutumia makundi yote ya vyakula kwa kiasi kutasaidia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuwa na jamii yenye afya bora.

Mama Yusta Joseph mkazi wa Kimbiji Dar es Salaam alisema elimu ya lishe aliyoipata inaenda kumbadilisha kwa kiasi kikubwa kwani kuna vitu amekuwa akivifanya ili kupunguza uzito kumbe alikuwa akifanya kimakosa.

“Elimu niliyoipata leo itaenda kunisaidia kwani nilikuwa najitahidi kupambana kupunguza uzito kwa kutumia njia ambayo si sahihi, nilikuwa sili milo ya asubuhi na mchana nakula usiku tu lakini nilivyofika hapa mtaalamu amenipa maelekezo kuwa ninapokula jioni na kwenda kulala sehemu kubwa ya chakula hutunzwa kama mafuta”, alisema Yusta

Yusta alisema mtaalamu wa lishe amemshauri kupunguza mlo wa jioni na namna ya kupata chakula bora kuanzi mlo wa asubuhi hadi jioni huku akimpa mbinu za kupunguza uzito wake bila ya kuleta athari nyingine za kiafya.

“Kwakweli elimu niliyoipata leo haitakuwa ya msaada kwangu tu bali ninaenda kuisaidia familia yangu kwasababu mimi ndio mama yao na mimi ndio mpishi hivyo ninaenda kuwasaidi pia katika kuboresha afya zao”, alisema Yusta

Mkuu wa Kitengo cha Lishe Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Maria Samlongo alisema wamekuwa wakitoa elimu ya lishe bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo pamoja na wananchi wanaohudumiwa katika kambi ambazo wamekuwa wakizifanya.

Maria alisema wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu ya lishe bora inawafikia wananchi wengi zaidi.

“Bado elimu ya lishe haijaweza kuwafikia watu wote kutokana na uchache wa wataalamu wa lishe, kama JKCI tumetengeneza vipeperushi mbalimbali vinavyotoa elimu ya umuhimu wa lishe bora katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Maria

Katika kambi hiyo jumla ya watu 364 walipatiwa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo ambapo kati yao watoto walikuwa 41 na watu wazima 323.

Watoto 11 walikutwa na matundu kwenye moyo, shida za valvu na mishipa ya damu huku watu wazima 161 sawa na asilimia 50 walikutwa na matatizo ya shinikizo la damu pamoja na magonjwa mengine ya moyo ikiwemo mishipa ya damu na matatizo ya valvu za moyo.