SHIRIKA LA EMEDO LATOA MAFUNZO KWA WASANII WA MICHORO JIJINI MWANZA

October 24, 2023
Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) limetoa mafunzo kwa wasanii wa sanaa za uchoraji jijini Mwanza, ili kuwaongezea elimu na ujuzi zaidi wa kuelimisha jamii kupitia kazi zao za sanaa huku wakijipatia kipato.

Mafunzo hayo yalianza Oktoba 17, 2023 katika ofisi za shirika la EMEDO jijini Mwanza kwa kushirikiana na taasisi ya NAAM Festival ya nchini Kenya na Wasanii Visual Art Arts ya Dar es salaam kupitia mradi wa Sanaa Ziwani Nyanza unaofadhiliwa na balozi za Uswis na Noray nchini Tanzania.

Mkuu wa Idara ya Mazingira kutoka Shirika la EMEDO, Lawrence Kitogo amesema sanaa ina mahusiano makubwa na mazingira hivyo kupitia mafunzo hayo, washiriki watapata ujuzi zaidi wa kutoa elimu kwa jamii kupitia michoro yao.

"Wasanii wa sanaa za michoro wana mchango mkubwa wa kuelimisha jamii hivyo tunapaswa kuungana nao katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira hasa Ziwa Victoria kupitia kazi zao za michoro ambazo zinafikisha elimu kwa urahisi" amesema Kitogo na kuongeza;

"Sanaa ni mazingira, ndiyo maana msanii anachofikiria kuchora ndani yake ni mazingira hivyo baada ya mafunzo haya tunatarajia watatumia sanaa kuchora michoro inayotatua changamoto za jamii hasa utunzaji wa mazingira, Ziwa Victoria".

Naye Mkurugenzi wa taasisi ya NAAM Festival, Dave Ojay amewahimiza wasanii wa sanaa za michoro kufanya kazi kwa kuzingatia mahitaji ya jamii, kuchora michoro inayotoa majawabu ya changamoto za maisha na kufikisha ujumbe uliokusudiwa hatua itakayokuza soko la kazi zao ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wasanii wa sanaa za michoro kutoka kikundi cha Clour Mwanza, Edward Tibasima amesema sanaa ya michoro inafikisha ujumbe kwa urahisi na inadumu kwa muda mrefu hivyo ni vyema Serikali na wadau mbalimbali wakatambua hilo na kuwatumia kuelimisha jamii.

"Michoro yetu ni rahisi kufikisha ujumbe kwa watu wengi, pia inadumu kuliko jumbe zinazoonyeshwa kwenye luninga" amesema Tibasima akitolea mfano michoro inayoweza kuchora katika miamba na mawe makubwa jijini Mwanza kufikisha ujumbe kwa jamii.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Edwardina Njura amesema kupitia sanaa za michoro, uchongaji na ufinyanzi ni rahisi kuelimisha jamii, kuenzi utamaduni na kuhamasisha masuala mbalimbali ikiwemo utalii na utunzaji mazingira huku akiongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha zaidi kazi zao.

Mafunzo hayo yanatolewa kwa washiriki saba waliofudhu hatua ya mchujo kati ya wasanii 18 waliotuma maombi ambapo yamelengwa kuwaongezea ujuzi, kukuza vipaji vyao na kuwasaidia kujiongezea kipato kupitia kazi zao za sanaa.

Mafunzo yalianza Oktoba 17, 2023 yakitarajia kuhitimishwa Oktoba 28, 2023 kupitia maonesho ya kazi za sanaa yatakayofanyika katika ufukwe wa Kamanga jijini Mwanza.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Idara ya Mazingira kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Lawrence Kitogo akifungua mafunzo kwa wasanii wa sanaa za michoro jijini Mwanza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Editrudith Lukanga (hayuko pichani).
Mkurugenzi wa taasisi ya NAAM Festival ya nchini Kenya, Dave Ojay (kushoto) akizungumza wakati wa mafunzo kwa wasanii wa sanaa za michoro jijini Mwanza yenye lengo la kuwajengea uwezo kutumia sanaa kuelimisha jamii na kuleta suluhisho na changamoto mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira pamoja na Ziwa Victoria.
Wasanii wa sanaa wa michoro jijini Mwanza wakifuatilia mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali.
Mwenyekiti wa wasanii wa sanaa za michoro wanaounda kikundi cha Colour Mwanza, Edward Tibasima akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na shirika la EMEDO kwa kushirikiana na NAAM Festival kwa ufadhili wa ubalozi za Norway na Uswis nchini Tanzania.
Wasanii wa sanaa za michoro jijini Mwanza wakiwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kutumia sanaa zao kuchora michoro yenye kuelimisha jamii. 
Mshiriki wa mafunzo hayo, Edwardina Njura ambaye ni msanii wa sanaa za kiutamaduni akichangia mada kwenye mafunzo hayo.
Mwonekano wa Kituo cha Taarifa na Maarifa ya Mazingira kilichopo katika Ofisi za shirika la EMEDO jijini Mwanza ambapo mafunzo kwa wasanii wa sanaa yalianza Oktoba 17, 2023 hadi Oktoba 28, 2023 yatakapohitimishwa kupitia maonesho ya kazi za sanaa yatakayofanyika katika ufukwe wa Kamanga.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

"TUTUNZE MAZINGIRA ILI TUPAMBANE NA MABADILIKO YA TABIA NCHI," MHE. DKT CHRISTOPHER TIMBUKA

October 24, 2023

 

Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Dkt Christopher Timbuka akipanda mti wakati akizindua kampeni ya utunzaji mazingira iliyopewa jina (Go green, save nature) iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita iliendana na kongamano la siku mbili lililowajumuisha wadau mbali mbali wa misitu.
Mhifadhi Mkuu (TFS) West Kilimanjaro PCO Robert Faida akipanda mti wakati akizindua kampeni ya utunzaji mazingira iliyopewa jina (Go green, save nature) iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita iliendana na kongamano la siku mbili lililowajumuisha wadau mbali mbali wa misitu.
Mratibu wa kampeni hiyo, Mensieut Elly akipanda mti wakati akizindua kampeni ya utunzaji mazingira iliyopewa jina (Go green, save nature) iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita iliendana na kongamano la siku mbili lililowajumuisha wadau mbali mbali wa misitu.
Mmoja ya wadau wa Mazingira toka nchini Kenya, Jesca nae alipata wasaa wa kupanda mti na kushuhudiwa na viongozi.
Kongamano kwa njia ya mtandao likiendelea.
Mhifadhi Mkuu (TFS) West Kilimanjaro PCO Robert Faida akifafanua jambo mbele ya wanahabari.
Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Dkt Christopher Timbuka (kushoto) akijadiliana jambo na Mhifadhi Mkuu (TFS) West Kilimanjaro PCO Robert Faida mara baada ya kumaliza zoezi la upandaji miti katika kampeni ya "Go green, save nature".
Na Cathbert Kajuna - MMG/Kajunason, West Kilimanjaro.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia hifadhi ya Misitu ya West Kilimanjaro wakishiriana na Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wameanzisha kampeni ya Upandaji wa Miti ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi.

Kampeni hiyo inajumuisha kutoa elimu kwa Jamii, upandaji wa miti hasa pembezoni mwa milima Kilimanjaro ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo ya utunzaji mazingira iliyopewa jina (Go green, save nature) iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita iliendana na kongamano la siku mbili lililowajumuisha wadau mbali mbali wa misitu na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Dkt Christopher Timbuka.

Mhe. Dkt Timbuka alisema kuwa ni vyema jamii ikajiongeza katika utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ili kusaidia upatikanaji wa mvua kwa wakati.

"Eneo la Siha lilikuwa kijani ila shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata miti na uchomaji holela wa maeneo imepelekea kuwa jangwa na kufanya wananchi wapolomoke kiuchuni, wananchi wanategemea mvua sasa ikikosekana hali inakuwa ngumu," alisema Dkt Timbuka.

Aliwaomba wana Siha wote kujitokeza kupata elimu ya utunzaji wa mazingira pamoja na kupanda miti ili kusaidia upatikanaji wa mvua na kurejesha uoto wa asili.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu (TFS) West Kilimanjaro PCO Robert Faida alisema ili kuhuhisha uharibifu ilikuokoa adhari za mabadiliko ya tabia nchi ni vyema jamii ikaacha tabia ya kuchoma moto pindi wanapoandaa mashamba jambo ambalo husababisha athari za kuunguza misitu na kusababisha hasara.

Aliongeza kuwa TFS West Kilimanjaro kwa sasa wameshaanza kutoa elimu kwa jamii inayoizunguka na kuwapa miti wapande ili kufanya Siha inakuwa ya Kijani.

Alisema endapo Jamii itafuata yale yote ambao wakuwa wakifundishwa kayika utunzaji wa mazingira basi tunaweza kukabiliana moja kwa moja na mabadiliko ya tabia nchi pia aliishukuru TFS na Serikali ya Wilaya ya Siha pamoja na wadau wa maendeleo kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakifanya pamoja katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.