Serikali yaipongeza CRDB Bank Foundation kuwawezesha kiuchumi vijana na wanawake wajasiriamali nchini

June 03, 2024

 

Mkurugenzi wa Jinsia wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Badru Abdunuru aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 150 Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Data Sustainable Development Organization, Sihaba Madenge ambazo ni mtaji wezeshi kwa baadhi ya wanachama wa asasi hiyo waliokidhi vigezo vya Programu ya Imbeju inayotekelezwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa BUTA Vicoba, Semeni Gama (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa (wa pili kushoto, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Benki ya CRDB, Badru Iddi (wa nne kulia), Mkuu wa Kitengo cha Kuendeleza Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Fadhil Bushagama (wa kwanza kulia) pamoja na wanachama wa Asasi ya Data Sustainable Development Organization.

========     =========      ==========

Dar es Salaam: Serikali imeipongeza Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kutoa mafunzo ya ujasiariamali na elimu ya fedha pamoja na mitaji wezeshi zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa vijana na wanawake wajasiriamali nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Jinsia wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Badru Abdunuru wakati wa hafla ya mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha pamoja na kukabidhi mitaji wezeshi ya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 150 kwa wanachama wa Asasi ya Data Sustainable Development ya Dar es Salaam. Katika mafunzo hayo, ilibainishwa kuwa kati ya shilingi bilioni 10 za mtaji wezeshi zilizotolewa mpaka sasa, wakazi wa Dar es Salaam wamepokea zaidi ya shilingi bilioni 3.6.
Abdunuru amesema ni ukweli wa dhahiri kuwa wanawake na vijana ndio injini ya uchumi kwani wana uwezo mkubwa wa kuliinua taifa kiuchumi. Kwa kuzingatia Ripoti ya Sensa na Makazi ya mwaka 2022, amesema asilimia 51 ya watu wote nchini ni wanawake na asilimia 75 ni vijana hali inayodhihirisha umuhimu wa kundi hili kwa nguvukazi ya taifa.

“Hata hivyo, wanawake na vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo mila na desturi kandamizi, elimu duni, ukosefu wa mitaji na stadi za ujasiriamali. Tukizitambua changamoto hizi, serikali imechukua hatua mbalimbali zinazolenga kujenga uchumi jumuishi na shirikishi ili kuwakomboa kiuchumi,” amesema Abdunuru.

Aliongezea kuwa, “Tunaendelea kufanya kazi kwa bidii kufikia malengo ya Jukwaa la Kimataifa ya Kukuza usawa wa Kijinsia hususan katika haki na usawa wa kiuchumi. Nawapongeza Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kuja na ubunifu huu unaounga mkono jitihada za serikali kuwakomboa kiuchumi vijana na wanawake.”
Ili kuwawezesha zaidi wajasiriamali wanawake na vijana, Mkurugenzi huyo amesema ni muhimu kwa wadau wote wa maendeleo wakashiriki mkakati huu kwani serikali pekee haitoweza kutatua changamoto zote zilizopo. 

“Niipongeze CRDB Bank Foundation kwa kuja na programu hii ambayo inalenga kuboresha maisha na kuimarisha biashara za vijana na wanawake kwa kuwapa mafunzo na ushauri wa namna bora ya kusimamia na kuendesha biashara zao, pamoja na kuwapa mitaji wezeshi. Naamini mmefungua milango kwa taasisi nyingine kubuni namna zinavyoweza kuyashirikisha makundi haya katika mipango yao,” amesema Abdunuru.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa  amesema mpaka mwishoni mwa Mei wameshatoa mafunzo kwa zaidi ya wanawake na vijana 400,000 ambao baadhi yao wamenufaika na mitaji wezeshi yenye thamani ya shilingi bilioni 10.

“Uwezeshaji huu umefanyika kupitia madirisha mbalimbali yaliyo chini ya programu yetu ya Imbeju ikiwamo Imbeju Ng’ara ambalo limejielekeza kuwawezesha wanawake, Imbeju Buni kwa ajili ya vijana wenye biashara changa, na Imbeju Kilimo linalowasaidia wakulima wadogo pembejeo na zana za kilimo pamoja na kuwalinda kupitia bima ya maisha na mazao. Vilevile, tuna Imbeju Nishati Safi, dirisha linalotoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa mama lishe,” amesema Tully. 

Mafanikio hayo, Tully amesema yasingeweza kufikiwa bila kuwashirikisha  wabia wao wa kimkakati kama ilivyo Asasi ya Data Sustainable Development yenye zaidi ya wanachama 1,800 na wengine wengi kuanzia mashirika ya kimataifa, taasisi za serikali na vikundi vya wanawake wajasiriamali.
“Katika zaidi ya shilingi bilioni 10 tulizozitoa nchini kote kama mtaji wezeshi kwa wajasiriamali, shilingi bilioni 3.6 tumezitoa kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na leo tunajivunia kutanua wigo wa wanufaika kwa kutoa mitaji wezeshi kwa wanachama wa Asasi ya Data Sustainable Development ambao tumeingia nao mkataba wa ushirikiano hivi karibuni,” amesema Tully wakati wa kuakikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 150 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa asasi hiyo, Sihaba Madenge.

Akipokea mfano wa hundi hiyo kwa ajili ya wanachama wake, Sihaba amesema ubunifu wa CRDB Bank Foundation ni wa kipekee kwani umeliona kundi kubwa ambalo ni muhimu ila lenye vikwazo vingi kupata huduma za fedha hasa mikopo ya kukuza biashara zao.

“Wanawake wengi wanapambana na maisha kuhakikisha wanazihudumia familia zao kwa kufanya biashara ndogondogo. Kikwazo kikubwa kwao ni mtaji kwani wengi hawana dhamana zinazohitajika katika benki nyingi hivyo kujikuta wakikwama kwa muda mrefu. Fursa hizi za kupata mtaji wezeshi kupitia Programu ya Imbeju bila masharti yoyote hakika ni ukombozi wa kiuchumi kwa wanawake wengi tunaipongeza na kuishukuru sana Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa ubunifu huu,” amesema Sihaba.
 
Mkurugenzi huyo pia ameiomba CRDB Bank Foundation kupeleka fursa za Programu ya Imbeju mpaka vijijini waliko wanawake wengi kwani kuna mwamko mkubwa wa wanawake kujishughulisha kiuchumi japo suala la upatikanaji wa mitaji linawakwamisha wengi. 





RAIS SAMIA ATANGAZA NIA YA KUJENGA CHUO CHA MASUALA YA ANGA

June 03, 2024

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema ana nia ya kujenga chuo cha masuala ya anga nchini Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea.

Rais Samia ameyasema hayo wakati wa shughuli ya Kutunukiwa Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Honoris Causa) katika sekta ya anga na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korea Aerospace University).

Amesema sekta ya anga ya Tanzania baina ya mwaka 2021 - 2023 imekua, kwani abiria wameongezeka kila mwaka kwa takriban asilimia 28 na pia idadi ya ndege zinazofanya safari za kimataifa zimeongezeka kutoka 26 hadi 33.

Idadi ya wasafiri wa ndani imeongezeka kwa asilimia 26.5 baada ya Covid-19 kutoka abiria milioni 3 hadi kufikia milioni 3.8 kwa mwaka wa 2023.

Rais Samia amesema nia ilikuwa kuwekeza kimkakati na hasa katika kufufua kampuni ya Air Tanzania Limited (ATCL) na kuendeleza miundombinu, ikiwemo mfumo wa kujenga rada na pia kukarabati na kupanua viwanja vya ndege kote nchini.

Kabla mwaka 2016, ATCL ilikuwa na ndege moja inayofanya kazi ambapo hadi kufikia Machi 2024 zimeongezeka ndege 14 za abiria na moja ya mizigo. Ndege 6 kati ya hizo zimenunuliwa katika kipindi cha miaka mitatu ikiwemo ndege ya mizigo.

Vile vile mtandao wake umepanuliwa kutoka maeneo 4 tu nchini hadi 24, ikiwemo safari katika miji minane barani Afrika na mitatu ya kimataifa (Guangzhou, Dubai na Mumbai).

Rais Samia amesema kufufua shirika hilo kumesaidia kuongeza mapato kutoka Shilingi za Kitanzania Bilioni 23 mwaka 2016/17 hadi 380.4 Bilioni mwaka 2022/23.

Pia soko la shirika la ATCL la safari za ndani limefika asilimia 53 asilimia kutoka asilimia 2.4 tu mwaka 2022/23, huku idadi ya abiria imeongezeka kwa asilimia 42 kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 6.8 mwaka 2024.

Mbali na hapo, idadi ya marubani waliosajiliwa na wahandisi wa ndege imeongezeka kufikia 604 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 na wahandisi kufikia 76 ambalo ni ongezeko la asilimia 181 mpaka mwisho wa mwaka 2023.

Rais Samia amesema kuwa mchango katika sekta ya anga kwenye Pato la Taifa la Tanzania umeongezeka kutoka asilimia 0.9 mwaka 2018 hadi asilimia 2.5 mwaka 2023.

Rais Samia anatarajia kesho kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

BRELA YAWATAKA WAFANYABIASHARA KUJISAJILI ILI KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOTANGAZWA NA SERIKALI

June 03, 2024
 Afisa Sheria za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (Brela) Lupakisyo Mwambiga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya 11 ya Biashara na Utalii yanayofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Usagara Jijini Tanga.



Na Oscar Assenga,TANGA

 

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) umewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya kujisajili na wakala huo kutokana na kwamba kama haujasajiliwa hauwezi kuomba tenda rasmi ambazo zinatangazwa na Taasisi mbalimbali za Serikali na Idara zake.

 

Hayo yalisemwa leo na Afisa Sheria za Wakala huo Lupakisyo Mwambiga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya 11 ya Biashara na Utalii yanayofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Usagara Jijini Tanga.

 

Lupakisyo alisema kwamba ni vema wafanyabiashara na wajasiriamali kuona umuhimu wa kurasimisha biashara zao  kwa kusajili brela na kupata leseni inayostahili ili waweze kutekeleza majukumu yao.

 

“Wengi wanachanganya leseni kati ya daraja A na B ambazo zinatolewa na halmashauri na Manipsaa kuna biashara zenye sura ya kitaifa na kimataifa unatakiwa kupata leseni kutoka brela hivyo nawahimiza wafanyabishara waje kupata elimu kwa kueleza biashara wanazofanya “Alisema

 

“Kwa lengo la kushauriwa ni leseni gani anapaswa kuomba kutoka brela na wale wafanyabiashara wenye viwanda vidogo vidogo tunatoa leseni za viwanda watu wengi hawajua unapoanzisha viwanda lazima uwe na leseni kutoka Brela”Alisema

 

Alisema kwamba kuna leseni ya uanzishwaji wa kiwanda na leseni  biashara kwa wajasirimali wenye viwanda vidogo na wafanyabiashara wenye viwanda vikubwa huku akiwataka kutembelea banda lao ili waone ni vitu gani wanaweza kufanya kupata leseni.

 

Hata hivyo alisema kwamba wapo kushiriki kwenye maonyesho ya biashara na utalii kutokana na kwamba ni moja ya taasisi za kusimamia usajili wa biashara pamoja na leseni na wamekuja kutoa elimu na huduma za papo kwa papo ikiwemo usajili wa kampuni ,majina ya biashara.

 

Alisema pia wanatumia maonyesho hayo kutoa  leseni kundi A na utoaji wa leseni za viwanda na usajili wa alama za biashara kwa wateja wao huku akiwataka  wananchi wa mkoa wa Tanga kuendelea kujitokeza kufika kwenye banda lao ili wawez kupata ushauri jinsi gani wanaweza kusajili kampuni ,jina la biashara au alama ya bisharaa na waliokuwa tayari wanasajiliwa kupitia mtandao kwa kuwasaidia kwa sababu wapo kwenye maonyesho na wamekuwa wakitoa elimu kwa wafanyabiashara umuhimu wa kusajili au kurasimisha biashara maana wengi mpaka wakipata changamoto Fulani ndio wanakilimbia brela.

 

“Wengi mpaka wanapopata changamoto ndio wanakimbili brela labda amepata tenda unatakiwa kupeleka cheti kutoka brela ndio wanahangaika kusajili au benki wakitaka taarifa kuhusu brela ndio wanakwenda kusajili”Alisema