DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA LAWAVUTA VIJANA WA MWANZA, SHINYANGA KUJIANDIKISHA

August 21, 2024
Wakazi wa Mkoa wa Mwanza wakiwa katika vituo vya Kuboreshea Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakijiandisha na kuboresha taariza zao leo ambapo uboreshaji huo umeanza kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Mikoa hiyo itafanya zoezi hilo kwa siku saba kuanzia leo Agosti 21 hadi 27, 2024.
Wakazi wa Mkoa wa Mwanza wakiwa katika vituo vya Kuboreshea Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakijiandisha na kuboresha taariza zao leo ambapo uboreshaji huo umeanza kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Mikoa hiyo itafanya zoezi hilo kwa siku saba kuanzia leo Agosti 21 hadi 27, 2024.
Vijana ni kundi kubwa la Wananchi ambao wameanza kujitokeza kwa wingi vituoni kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari (wapili kulia) akikagua zoezi la uboreshaji lililoanza leo Mkoani Mwanza ambapo alitembelea vituo mbalimbali katika majimbo ya Magu, Ilemela na Nyamagana mkoani humo.Kulia ni Afisa Mwandikishaji Msaidizi ngazi ya Kata kutoka Kata ya Buswelu Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Godson Egubo wakiwa katika kituo cha Shule ya Msingi Eden Valley.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari akikagua zoezi la uboreshaji lililoanza leo Mkoani Mwanza ambapo alitembelea vituo mbalimbali katika majimbo ya Magu, Ilemela na Nyamagana mkoani humo.
Afisa Mwandikishaji Msaidizi ngazi ya Kata ya Buswelu Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Godson Egubo (kushoto) akikagua mwenendo wa zoezi la Uboreshaji katika Kituo cha Shule ya Msingi Eden Valley kilichopo katika Kata yake.

Na Mwandishi wetu, Mwanza
Wakazi wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga wamejitokeza kwa wingi katika siku ya kwanza ya zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanza leo Agosti 21 na litaendelea hadi Agosti 27,2024.


Mwandishi wa habari hii, ameshuhudia uwepo wa wananchi wengi vituoni haswa vijana na wanawake waliojitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.


Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa tathmini ya mwenendo wa zoezi hilo kwa siku ya kwanza Mkoa wa Mwanza, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari amesema zoezi limeanza viziri na mwitikio wa wananchi ni mkubwa.


“Leo siku ya kwanza zoezi limeanza vizuri ambapo wananchi wamejitokeza, mawakala wapo vituoni na nimebahatika kuzungumza na mawakala, watendaji vituoni na wananchi. Kwa ujumla zoezi linakwenda vizuri,”amesema Jaji Asina.


Aidha, Jaji Asina amesema changamoto zilizojitokeza ni za kawaida na zinatatulika lakini changamoto kubwa ni wananchi wanaofika kuboresha taarifa zao kusahau majina waliyoyatumia awali kujiandikishia namna yanavyoandikwa kwa usahihi, hivyo inapelekea uchelewaji vituoni.


Amesema makundi mbalimbali ya wanawake wajawazito, wanaonyonyesha na kufika na watoto wao vituoni, Wazee, Wagonjwa na wenye ulemavu wameendelea kupewa kipaumbele kama Tume ilivyoelekeza.


Jaji Asina ambaye alifanikiwa kutembelea baadhi ya vituo katika Majimbo ya Magu, Nyamagana na Ilemela amewaasa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa siku sita zilizobaki na wasisubiri siku ya mwisho.


“Niwasihi wananchi wajitokeze katika vituo ili waweze kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ambapo katika vituo tumeona vijana wengi, hivyo watumie siku hizi zilizobaki kuboresha taarifa zao na kuajindikisha,amesema Jaji Asina.


Mjumbe wa Tume, Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri ambaye yupo Mkoani Shinyanga amesema mkoani humo zoezi hilo limeanza vizuri na wananchi wengi wamejitokeza kujiandikisha kwa wingi.


Mawakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Paul Msafiri na Wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Lydya Martin waliopo kituo cha Bulola Mlimani kilichopo eneo la Zahanati ya Nyerere katika Halmashauri ya Ilemela wamesema zoezi hilo linakwenda vizuri na hakuna changamoto iliyojitokeza.


Aidha, wakala Fatuma Athumani wa Chadema aliyopo kituo cha Miembeni A kilichopo eneo la wazi Nyakabungo A katika Halmashauri ya Jijini la Mwanza amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata haki yao ya kuwa na kadi ya Mpiga Kura.


Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga limeanza leo Agosti 21 hadi Agosti 27,2024 ambapo Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 400,082 kwenye mikoa hiyo.


Mkoani Mwanza wapiga kura wapya 190,131 wataandikishwa huku Shinyanga wapiga kura wapya wanaotarajiwa kuandikishwa ni 209,951.

HOME GUARD FC, SMALL PRISON ZAAGA MASHINDANO ULINZI CUP TANGA

August 21, 2024

Mratibu wa Mashindano ya Ulinzi Cup Sophia Wakati akisistiza jambo kwa wachezaji wa timu za Small Prison na Chote FC kabla ya kuanza mchezo wao wa Michuano hiyo

Na Oscar Assenga, TANGA.

TIMU za soka Small Prison na Home Guard zimeaga Mashindano ya Ulinzi Cup baada ya kila mmoja kufungwa katika mchezo wa hatua ya mtoano inayoendelea kwenye viwanja vya Ziwani Pongwe Jijini Tanga.

Mashindano hayo yanaratibiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga yakiwa na lengo la kutoa elimu kwa vijana kujiepusha na vitendo vya uhalifu katika jamii wanazoishi ikiwemo kuwa mabalozi wa amani kwenye maeneo yao

Katika mchezo wa awali wa ufunguzi wa mashindano hayo timu ya soka TFC waliigaragaza Home Guard bao 1-0 bao ambalo lilifungwa na Mohamed Saidi dakika ya 5 hya mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani.


Huku mchezo wa pili uliochezwa Agosti 21 mwaka huu timu ya Chote FC waliweza kuwapigisha kwata maafande wa Jeshi la Magereza Small Prison bao 1-0 ambalo lilifungwa na Boniface Majere dakika ya 47.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mashindano hayo,Diwani wa Kata ya Pongwe (CCM) Mbaraka Sadi alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuhakikisha Jeshi la Polisi linakuwa karibu na Jamii jambo ambalo ni muhimu katika kuhakikisha kuimarisha ulinzi.

Mbaraka alisema kwamba kufanyika kwa mashindano hayo katika maeneo mbalimbali yanasaidia na kuwawezesha vijana kuweza kuyatumia kama njia muhimu ya ajira,kujenga afya pamoja na kusaidia kuwaondoa vijana kwenye masuala ya uhalifu na dawa za kulevya na wanaamini mashindan hayo yatakuwa chachu kubwa ya kuinua vipaji vya wachezaji.

Naye kwa upande wake Mratibu wa Mashindano hayo Sophia Wakati alivitaka vilabu vinavyoshiriki kwenye mashindano hayo kuhakikisha wanazingatia sheria 17 za mpira wa miguuu zilizowekwa ikiwemo kuacha kuwachukia waamuzi.

“Lengo la Mashindano hayo ni kujenga undugu baina ya Jeshi la Polisi na Jamii lengo kujenga urafiki msijengeane chuki hakikisheni mnacheza kwa kuzingatia nidhamu ambayo itakuwa chachu ya mafanikio kwenye jambo lolote lile lakini msiwachukie waamuzi kutokana na kwamba wakati mwengine kunakuwa na makosa ya kibinadamu”Alisema

Naibu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii avutiwa na Kamati ya Ulinzi wa Mtoto Stendi ya Nyegezi, Mwanza

August 21, 2024
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu amekagua shughuli za kamati ya ulinzi wa watoto wanaoishi mazingira magumu/ mitaani iliyopo stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi jijini Mwanza.

Mdemu amekagua shughuli za kamati hiyo Jumanne Agosti 20,2024 akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii mkoani Mwanza.

"Nimevutiwa sana na kamati hii, sote tukiungana na kuwajibika pamoja, tutafanikiwa kuwalinda watoto na vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini pia kuwaondoa katika maeneo ya stendi" amesema Mdemu huku akipongeza wazo la uanzishaji wa kamati hiyo akisema linaweza kusaidia kuwa na kamati za aina hiyo katika stendi mbalimbali nchini.

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Kamati hiyo, Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Ngegezi, Edith Ngowi amesema tangu mwaka 2021 kamati hiyo imewaokoa watoto 297 katika stendi ya mabasi Nyegezi.

"Kwa kushirikiana na shirika la Railway children Africa na Jeshi la Uhamiaji, watoto 230 wameunganishwa na familia zao ingawa tumepata changamoto ya watoto 30 ambao wamerejea tena mitaani baada ya kuumganishwa na familia zao huku wengine wakitoa taarifa ambazo si sahihi na hivyo kushindwa kuwapata ndugu zao" amesema Ngowi.

Aidha Ngowi amebainisha kuwa watoto hao wamekuwa wakifika stendi kwa njia mbalimbali ikiwemo kudandia malori na mabasi kutoka mikoani huku wengine wakitumikishwa kazi za usafi wa kuosha magari hayo kwa ujira mdogo wa hadi shilingi 500.

"Hali hiyo inawashawishi kuvutiwa kubakia stendi hivyo tunaendelea kutoa elimu kwa makondakta kuacha kuwatumia watoto hasa wa kiume kwenye kazi za kuosha magari" amesema Ngowi akibainisha kuwa wengi wana umri kati ya miaka saba hadi 14.

Kamati hiyo inaundwa na viongozi mbalimbali wakiwemo maafisa maendeleo ya jamii, wenyeviti wa Serikali za mitaa, polisi, uongozi wa stendi ya Nyegezi, wafanyakazi kwenye mabasi na shirika la kutetea haki za watoto wanaoishi mazingira magumu la Railway Children Africa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa afua za Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu akizungumza na kamati ya ulinzi wa mtoto stendi ya Nyegezi jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu akizungumza na kamati ya ulinzi wa mtoto stendi ya Nyegezi jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu akizungumza na kamati ya ulinzi wa mtoto stendi ya Nyegezi jijini Mwanza.
Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Ngegezi, Edith Ngowi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kamati ya ulinzi wa mtoto Stendi ya mabasi Nyegezi jijini Mwanza.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mtoto Stendi ya mabasi Nyegezi jijini Mwanza.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mtoto Stendi ya mabasi Nyegezi jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu (katikati) akiwasili Ngudu wilayani Kwimba kuendelea na ziara ya kukagua afya mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara hiyo.

MAJALIWA: TAASISI ZA SERIKALI ZINAZODAIWA NA TEMESA KUKIONA

August 21, 2024

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala, kuwasilisha Ofisini kwake orodha ya Taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na Wakala huo ili aweze kuwaandikia baraua ya kusisitiza kulipa madeni yao.


Agizo hilo amelitoa leo, Agosti 20, 2024 jijini Arusha wakati akifungua kongamano la Tatu la madereva wa Serikali ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza Wakuu wa Taasisi kuhakikisha wanalipa madeni hayo mara moja ili TEMESA iweze kuhakikisha wajibu wa vyombo vya usafiri vinakuwa salama na vinatengenezwa kwa wakati.

“Wakuu wa Taasisi, popote mlipo mnanisikia, kama mpo hapa ndani au kupitia vyombo vya habari, hakikisheni mnalipa madeni yenu TEMESA, mkiwalipa hawa matengenezo ya magari yenu yatafanyika kwa muda sahihi” amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ameipongeza TEMESA kwa kuwa na mitambo ya kisasa ya kutengeneza magari na kuwataka kuongeza ubunifu na uadilifu ili kuleta tija katika utengenezaji wa magari ya Serikali.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka viongozi kuthamini kada ya madereva kwa kuwapa mahitaji yao ili wafanye kazi kwa ufanisi na hivyo kulinda usalama wa viongozi, wananchi na magari wanayoyaendesha.

Ameongeza kuwa Serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini mchango wa madereva nchini na itaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto za madereva ili kuikuza kada hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Naye Naibu waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kukilea chama cha madereva ili kikue na kufanya kazi kwa weledi.

"Wizara itahakikisha madereva wanapata elimu stahiki ya magari wanayoyaendesha ili kuendelea na ukuaji wa teknolojia na kuwawezesha kushiriki vikao vyao ili kukuza weledi.

Zaidi ya madereva 1200 kutoka Tanzania bara na Zanzibar wanashiriki kongamano hilo linaloongozwa na kauli mbiu isemayo " Dereva wa Serikali jitambue, timiza wajibu wako, usalama barabarani unaanza na wewe kazi iendelee".

TOENI ELIMU ZAIDI KWA WANANCHI JUU YA UGONJWA WA MPOX;WAZIRI MHAGAMA

TOENI ELIMU ZAIDI KWA WANANCHI JUU YA UGONJWA WA MPOX;WAZIRI MHAGAMA

August 21, 2024

 Na WAF, Namanga- Arusha

Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama amewataka wataalamu wa Afya nchini kuongeza kasi ya kutoa elimu ya ugonjwa wa Mpox ili wananchi wawe na uelewa mpana dhidi ya ugonjwa huo.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo leo Agosti 21, 2024 wakati wa ziara kwenye Kituo cha Forodha cha Mpaka wa Namanga Halmashauri ya Wilaya ya Longido mkoani Arusha alipofika kuona utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Mpox.

“ Nimezungumza na mmoja wa wasafiri lakini hajui dalili za za ugonjwa wa Mpox hivyo ipo haja ya kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi ili kuwa na uelewa juu ya ugonjwa huo”, ameeleza Mhe. Mhagama na kuongeza

“Kuwe na mabango na vipeperushi vinavyotoa elimu juu ya ugonjwa kuelezea Dalili, unaambukizwaje na namna ya kujikinga ili kila msafiri anayeingia na kutoka nchini awe na uelewa mpana” amesisitiza Waziri Mhagama.

Mhe. Mhagama amesema kwa sasa mpaka Tanzania ni Salama na hakuna mgonjwa yeyote aliyebainika kuwa na ugonjwa huo hivyo wananchi waendelee kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Mpox .

“ Natoa wito kwa wananchi kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake pale atakapo ona dalili za ugonjwa huo kwa mtu basi atoe taarfa kwa wataalamu wa afya, Kituo cha kutolea huduma za afya kilichopo karibu yake au kuwasiliana na Wizara ya Afya kwa Namba ya 199 ili kuhakikisha nchi inakuwa salama”, ametoa wito.

Akihitisha ziara yake Waziri Mhagama amewahakikishia watanzania kuwa Wizara yake imejipanga kikamilifu kwa kuimarisha Huduma za uchunguzi na maabara maeneop ya mipakani ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini