NUNDU awapa muda wa miezi mitatu wananchi.

NUNDU awapa muda wa miezi mitatu wananchi.

March 30, 2013

Na Oscar Assenga, Tanga.
MBUNGE wa Jimbo la Tanga,Omari Nundu amewapa muda wa miezi mitatu wananchi waliochukua fedha katika mfuko wa  Zindaba Fund wawe wamekwisha kuzirejesha la sivyo watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wake na wananchi wa kata za Marungu,Kirare,Tongoni na Tangasisi ziliyopo jijini Tanga alisema wananchi hao wamechukua fedha hizo na kushindwa kuzirejesha licha ya kuandikiwa barua za mara kwa mara kufanya hivyo bila kuwepo kwa mafanikio yoyote yale.

Hatua ya mbunge huyo ameichukua kutokana na wananchi hao mbalimbali jijini Tanga kuchukua fedha katika mfuko huo kiasi cha sh.milioni 78 huku baadhi yao wakirudisha nusu nusu na wengine wapatao 33 wakishindwa kuzirudisha fedha hizo ili ziweze kuwasaidia na wananchi wengine shughuli zao mbalimbali.

Alisema hata akichukiwa na mtu yoyote hatajali badala yake ataendelea kufanya kazi ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia kwa wakati pamoja na kufanyia kazi changamoto zinazowakabili.

Akizungumzia tatizo la usalama nchini,Nundu alisema haiwezekani makanisa yakachomwa moto na serikali kuendelea kuyafumbia macho na kuitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuywazibiti wahalifu wa aina hiyo ili kudumisha hali ya usalama na amani hapa nchini.

Aidha pia alitumia fuksa aliyoipata kuwaasa viongozi wa vyama vya upinzani wanapokuwa kwenye mikutano yao waongelee sera na sio mambo mengine yasiyo na tija kwa wananchi wao.

    “Tunapotaka kuwaletea maendeleo wananchi wetu tusiangalie itikadi za vyama vyetu bali tuangalie namna ya kufanya ili wananchi tunaowaongoza waweze kupata unafuua wa maisha kwa  kuangalia jinsi gani tunaweza kutatua kero zao zinazowakabili “alisema Nundu.

Katika mkutano huo,mwananchi wa kata hiyo,Abdallah Mnyamisi alimueleza mbunge huyo kuwa wanamatatizo kwenye ofisi yake hakuna watendaji wazuri na kumuomba mbunge huyo kuwa fedha zake za mfuko wa jimbo azipeleke katika kutatua kero mbalimbali za wananchi vijijini.

Akijibu swali hilo,Nundu alihaidi kuzifanyia kazi changamoto zote zinazowakabili wananchi katika maeneo yao kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi ya vijiji na kata ili kuweza kuyapatia ufumbuzi kwa haraka iwezekanavyo.

Awali akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga,Kassimu Mbuguni alisema pamoja na mbunge huyo kufanya mkutano huo lakini pia walienda kusikiliza ilani ya chama hicho na kuhaidi kuyafanyia kazi maneno yaliozungumzwa na wananchi katika mkutano huyo ili yaweza kufikia malengo yao.

Mwisho
CHABATA yaanza mikakati ya kuandaa timu ya Mkoa

CHABATA yaanza mikakati ya kuandaa timu ya Mkoa

March 30, 2013
Na Mwandishi Wetu, Tanga.

CHAMA cha mchezo wa Baiskeli Mkoa wa Tanga (Chabata) kimeanza mikakati ya kuandaa timu ya mkoa kwa ajili ya kushiriki mashindano ya mchezo huo taifa ambayo mwaka huu yatafanyika mwezi wa saba mkoani Dodoma.

Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Tanga, Dege Masoli aliliambia gazeti hili kuwa timu ya mkoa itachaguliwa kutokana na mashindano ya mchezo huo ngazi ya mkoa ambayo yataanza mwezi mei ambapo pia katika watayatumia kwa ajili ya kuwachuja wachezaji ambao wataunda timu ya mkoa.

Masoli alisema licha ya kuwa na mikakati hiyo lakini pia chama chao kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa fedha hali ambayo inapelekea timu ya mchezo huo kushindwa kuanza maandalizi mapema.

  “Tatizo la uhaba wa fedha katika chama chetu limekuwa suala kubwa sana hivyo tunawaamba wadau mbalimbali kuweza kujitokeza kwa ajili ya kutusapoti ili tuweze kushiriki vema mashindano ngazi ya Taifa “Alisema Masoli.

Aliongeza kuwa wanawaomba wadau kutoka maeneo mbalimbali,wakiwemo viongozi wa serikali,makampuni, na taasisi binafsi kuangalia namna gani wanaweza kuisaidia timu hiyo iweza kufikia malengo yake.

Mwenyekiti huyo alisema wachezaji 5 ndio ambao watachaguliwa ili kwenda kuuwakilisha mkoa katika mashindano ya Taifa ambapo kwa sasa timu ya mkoa wa Tanga ilianza mazoezi .

Mwisho.
WANANCHI wamkaanga diwani mbele ya DC

WANANCHI wamkaanga diwani mbele ya DC

March 30, 2013

Na Oscar Assenga, Lushoto.

WANANCHI wa Kijiji cha Ungo Kata ya Mlola wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamelazimika kumueleza Mkuu wa wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga kuwa diwani wa Kata hiyo, Shekallage Rashid amekuwa akishindwa kusimamia miradi ya maendeleo na hivyo kumuomba kumuajibisha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi iliopo kwenye kijiji hicho ikiwa ni ziara yake ya siku nne ya mkuu huyo wa wilaya ya kukagua miradi ya maendelo na kusikiliza kero za wananchi zinazowakabili.
Wananchi hao walisema kuwa waliazimia kujenga zahanati na waliamua kupanga kuwa wananchi wanaoishi katika kijiji hicho wawajibike katika kutengeneza matofauti ambayo yatajengea zahanati hiyo.

Akizungumza mmoja wa wananchi wa kijiji hicho,Rashid Mtangi alimueleza mkuu huyo wa wilaya kuwa baada ya kukubaliana hivyo walianza kazi hiyo mara moja na kufanikiwa kufetua matofali na kuyaweka karibu na eneo la shule kwa ajili ya ujenzi huo na kuchukua muda wa kipindi cha miaka miwili lakini ukashindwa kufanyika na matofauti hayo kuharibika.

Mtangi alisema kutokana na kitendo hicho wananchi wa eneo hilo huenda wakashindwa kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao kutokana na viongozi wazembe ambao wanashindwa kusimamia majukumu yao na kusababisha nguvu za wananchi kupotea.
  “Diwani wetu haitishi hata mikutano ya wananchi kitendo ambacho kinawafanya wananchi kushindwa kuona umuhimu wao katika nafasi wanazoziongoza kwani hawaelewi anafanya kazi gani kwao“Alisema Mtangi.

Aidha aliongeza kuwa kijiji hicho kimekuwa hakina mtendaji kwa muda mrefu hali ambayo inapelekea wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kushindwa kuelezwa mapato na matumizi yao kwa muda mrefu na hivyo kuchangia kurudisha nyuma kasi ya maendeleo.

Akijibu tuhumu hizo,Diwani Rashid alimueleza Mkuu wa wilaya kuwa  hakuna mahali popote alipokwamisha ujenzi za zahanati hiyo bali aliambiwa na mbunge wa jimbo hilo,Henry Shekifu na mganga mkuu wa wilaya hiyo aliyehamia kilombero mkoani Morogoro kuwa kuwa umbali wa kituo cha Afya cha Mlola na eneo ambalo kulitakwa kujengwa zahanati hiyo ni karibu.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga alisema hatamuangalia tu kwa cheo chake wala thamani aliyonayo katika jamii kutokana na kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi atahakikisha wachukulia hatua zinazostahili.

    “Watu wanataka serikali ichukiwe kuwa haikufanya kitu kutokana na watendaji wazembe hatutokubali hali hii iendelee lazima wale wote ambao wanakwamisha miradi ya maendeleo ya wananchi wachukuliwe hatua stahiki “Alisema DC Mwanga.

Mwanga aliwaomba wananchi wampe muda aende akaangalie kuwa mradi huo wa zahanati hiyo na kuwataka viongozi mbalimbali katika kata hiyo kuheshimu maamuzi ya serikali hasa za vijiji.

Aidha alisema suala la wananchi wao kutokuwa na mtendaji kwa muda mrefu alihaidi kulishughulikia na kubwa baraza la madiwani walikumbushie ili liweze upata ufumbuzi haraka iwezekanayo.

Akizungumzia suala la wanafunzi ambao hawajaripoti mashuleni tokea shule hizo zilipofunguliwa aliwaagiza watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yote wilayani humo kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti haraka iwezekanavyo na wampelekee taarifa zao ofisini wake.

Mwisho.
Tawi la Chama cha Mapinduzi Chuo kikuu Eckenforde kufunguliwa hivi karibuni

Tawi la Chama cha Mapinduzi Chuo kikuu Eckenforde kufunguliwa hivi karibuni

March 30, 2013

 


 


Na Oscar Assenga, Tanga
CHUO Kikuu cha Eckenforde-Tanga kinatarajia kufungua tawi la Chama cha Mapinduzi (CCM)  chuoni hapo katika kuitikia  azimio la Mkutano Mkuu wa CCM  wa kuanzishwa matawi  ya Chama kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu hapa nchini.
Akithibitisha habari hiyo, Katibu wa muda wa Jumuiya hiyo chuoni hapo, Rehema Maclean alisema Jumuia ya wananfunzi katika Chuo hicho wanatarajia kufungua tawi hilo baada ya kukidhi kigezo cha kufikia wanachama wanaozidi 50.
Maclean aliliambia blog hii jana kwamba sherehe za ufunguzi wa tawi hilo zinatarajiwa kufanyika mwezi Januari 5, mwaka huu lakini zimesongezwa mbele kutokana na sababu mbalimbali.
Akifafanua zaidi, Katibu huyo alisema kufunguliwa kwa tawi hilo Chuoni hapo kutaongeza idadi ya matawi kuwa mawili, ambayo ni pamoja na Chuo Kikuu cha SEKOMU kilichoko wilayani Lushoto.
Aidha, alisema kufunguliwa kwa tawi hilo ni kutekeleza azma ya kuunda mkoa wa Vyuo Vya Elimu  ya Juu kama ilivyoridhiwa na Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma mwaka huu.
 Hivi karibuni, akihutubia mkutano wa Jumuiya hiyo jijini hapa, Katibu wa Mkoa wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Christopher Ngu Ngubiagai alisema kufunguliwa kwa matawi ya Chama cha Mapinduzi katika Vyuo vya Elimu ya Juu ni hatua iliyochukuliwa kwa maksudi kwa lengo la kukisogeza Chama kuwa karibu zaidi na watu.
Alisema kuwa Chama kimedhamiria kuleta mageuzi makubwa yatakayoendana na dhamira ya kuwaingiza vijana katika safu ya uongozi wa nchi pamoja na mashirika na taasisi za umma.
Akasema vijana wana wajibu wa kulelewa kulingana na maadili ya Kitanzania na kuongeza kuwa uzalendo hauteremshwi kutoka mbinguni, bali hujengwa na moyo unaokataa rushwa.
 "Vijana wakijengewa uwezo wanaweza  kuongoza kwani wengi wao ni wazalendo wanaoipenda nchi yao kwa dhati”,alibainisha.  
Kwa kutambua hilo, alisema, tayari Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, J.K. Kikwete  ameanza kuwaingiza vijana katika nafasii mbalimbali za uongozi wakiwemo Wakuu wa Wilaya ambao wanaongoza kwa wingi katika safu hiyo.
Katibu huyo wa Mkoa wa Vyuo Vya Elimu ya Juu alifafanua kuwa CCM mlango wa kujenga mahusiano ya karibu baina ya wanafunzi hao wa Vyuo Vya Elimu ya Juu na CCM.
Alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa Mkoa wa Vyuo vya Elimu ya Juu ni kueneza itikadi ya CCM pamoja na kujenga uzalendo na maadili ya kitaifa.
Hata hivyo Ngubiagai alitahadharisha kwamba shughuli zote za kisiasa zitafanyika nje na maeneo ya Vyuo na kwamba wanachama ni vanavyuo tu.
Katibu wa Muda wa Tawi hilo,Rehema Maclean alisema wanachama hao tayari wamejiandaa kikamilifu tayari kwa ufunguzi wa tawi lao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
 (Mwisho).