KITU CHA AFYA PONGWE CHAKABILIWA NA CHANGAMOTO MBALIMBALI.

KITU CHA AFYA PONGWE CHAKABILIWA NA CHANGAMOTO MBALIMBALI.

October 08, 2013
NA OSCAR ASSENGA,PONGWE.   
KITUO cha Afya Kata ya Pongwe katika Halmashauri ya Jiji la Tanga kinakabiliwa na changamoto mbalimbali hali ambayo inapelekea kushindwa kufikia malengo yao waliojiwekea hasa katika utoaji huduma kwa wagonjwa wanaofika kituoni hapo.
Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho,Ally Bughe alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Tanga Raha ofisini  kwake na kueleza kuwa licha ya kuwepo hali hiyo lakini pia kituo hicho hakina uzio kitendo ambacho kinapelekea mifugo kuingia mpaka kituo wakati wa utoaji wa huduma.
Bughe alisema kituo hicho pia kinawakabili ni kukosekana kwa maabara ya kisasa kwa ajili ya kuchukulia vipimo vya wagonjwa licha ya kuwa na wataalamu wa kutosha.
Alisema licha ya kuwepo changamoto hizo wanatarajia kuanza kufanya upasuaji lakini hawana wodi maalumu ya kuwalaza wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji huo.
Aliongeza kwa kusema kuwa kituo hicho hakina gari maalumu la kubebea wagonjwa pindi wanapozidiwa na kuhitajika kupelekwa katika hospitali ya mkoa Bombo zaidi ya usafiri wa pick up ambayo sio salama kwao.
Aidha wanaiomba halmashauri ya Jiji la Tanga kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuweza kuzipatia ufumbuzi pamoja na kuhakikisha wanaondoa matatizo hayo.
Mwisho.

CUF MKINGA WAANZA MIKAKATI YA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015.

October 08, 2013
NA OSCAR ASSENGA,MKINGA.
CHAMA cha Wananchi CUF wilayani Mkinga kimeelezea mikakati yake ya kufanya mikutano ya hadhara katika kata zote zilizopo wilayani humo lengo likiwa kukiimarisha chama hicho pamoja na kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ili kuchukua kata zote.

Akizungumza hivi karibuni,Mwenyekiti wa Chama hicho,Mauya Kileo amesema anaamini lengo lao litafanikiwa kutokana na kukabalika vilivyo na wananchi maeneo mbalimbali wilayani humo kitendo ambacho kiliwawezesha chama hicho kupata kata saba kati ya 21 zilizopo.

Kileo amezitaja kata ambazo zimechukuliwa na chama hicho wilayani humo kuwa ni Mtimbwani, Kwale,Manza ,Boma,Doda,Moa na Duga Sigaya na kueleza mikakati yao ni kuongeza idadi ya kata kwenye uchaguzi huo mkuu kwani hilo linawezekana kutokana na mshikamano walionao.

Aidha aliwataka wanachama wa chama hicho kuendelea kuonyesha mshikamano ili kuweza kufanikisha malengo yao ya siku moja kuongoza halmashauri yaweze kufanikiwa.

KAMATI YA JAJI LUANDA KUSIKILIZA RUFANI ALHAMISI

October 08, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda itakutana keshokutwa (Oktoba 10 mwaka huu) kusikiliza rufani zilizowasilishwa mbele yake.

Waombaji uongozi watatu wamekata rufani katika Kamati ya Jaji Luanda wakipinga kutopitishwa kugombea katika uchaguzi wa TFF, uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ajili ya uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Warufani ni Samwel Nyalla aliyeondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda namba 2 ya mikoa ya Mara na Mwanza kwa kutojaza kikamilifu fomu namba 1 ya maombi ya kugombea uongozi TFF kwa kutoonesha malengo yake.

Ayoub Nyaulingo yeye anapinga kuondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda namba 6 (Katavi na Rukwa) kwa kutokuwa na uzoefu uliothibitika wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.

Naye Ayoub Nyenzi amekata rufani kupinga kuondolewa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha Kanda namba 7 (Iringa na Mbeya) kwa kushindwa kuthibitisha uraia wake.

UCHAGUZI BODI YA LIGI SASA OKTOBA 25

October 08, 2013
Uchaguzi wa viongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) sasa utafanyika Oktoba 25 mwaka huu badala ya Oktoba 18 mwaka huu.

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesogeza mbele uchaguzi huo kutokana na maombi ya Kamati ya Ligi kwa vile baadhi ya wajumbe wa Baraza la Bodi hiyo kuwa vilevile wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.

TFF itafanya Mkutano Mkuu wake Oktoba 26 mwaka huu ambao utakuwa na ajenda za kawaida kama zilivyoainishwa katika Katiba yake wakati ajenda ya uchaguzi itakuwa Oktoba 27 mwaka huu.

Wagombea uongozi TPL Board ni Hamad Yahya Juma anayewania nafasi ya Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti ni Said Muhammad Abeid. Wanaowania nafasi za ujumbe katika Kamati ya Uongozi ni Kazimoto Miraji Muzo na Omar Khatib Mwindadi.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu Mbwezeleni inatarajia wakati wowote kutangaza tarehe ya kuanza kampeni kwa wagombea katika uchaguzi huo. Baraza la Bodi linaundwa na wajumbe 38 ambao ni wenyeviti 14 wa klabu za Ligi Kuu na wenyeviti 24 wa klabu za Daraja la Kwanza.

MGAMBO SHOOTING MAJARIBUNI KWA AZAM VPL

October 08, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Baada ya kupoteza mechi mbili nyumbani, Mgambo Shooting iko ugenini kesho (Oktoba 9 mwaka huu) kuikabili Azam katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Mgambo Shooting yenye pointi tano, ikiwa nafasi ya pili kutoka mwisho imeshinda mechi moja tu dhidi ya Ashanti United huku ikipoteza mbili nyumbani dhidi ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Kocha Mohamed Kampira ana kibarua cha kuhakikisha anapata pointi mbele ya Azam.

Mechi nyingine za ligi hiyo ni Rhino Rangers itacheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati JKT Ruvu watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani Morogoro.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa shuhuda wa mechi kati ya wenyeji Oljoro JKT na Ruvu Shooting ya Pwani inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa.

NDANDA, WARRIORS ZASAKA UONGOZI FDL

October 08, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Green Warriors ya Dar es Salaam na Ndanda ya Mtwara zinaumana kesho (Oktoba 9 mwaka huu) katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo mshindi atakamata uongozi wa kundi A.

Mechi hiyo ya raundi ya tano itachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ambapo timu itakayoshinda itafikisha pointi kumi na kuipiku African Lyon inayoongoza sasa kundi hilo ikiwa na pointi tisa.

Kwa upande wa kundi B kutakuwa na mechi tatu ambapo Polisi Morogoro inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi tisa itakuwa ugenini dhidi ya Majimaji inayokamata mkia ikiwa na pointi moja. Mechi itachezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Kurugenzi itakuwa kwenye uwanja wake wa Wambi ulioko Mafinga mkoani Iringa kuikabili Burkina Faso ya Morogoro wakati Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi mkoani Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Kimondo na Mkamba Rangers.