Makamu wa Rais Dkt Mohammed Gharib Bilal ateta na viongozi wa Selcom Wireless

November 05, 2013


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Selcom Wireless Tanzania, Meneja Miradi wa Selcom, Gallus Runyeta (katikati) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Selcom. (kushoto) ni Meneja Masoko na Muendesha Biashara, Juma Mgori. Picha na OMR
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Selcom Wireless Tanzania, Meneja Miradi wa Selcom, Gallus Runyeta (katikati) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Selcom. (wa pili kushoto) ni Meneja Masoko na Muendesha Biashara, Juma Mgori na Mhandisi wa Software, Godfrey Kiapinga.
 
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na Uongozi wa Kampuni ya Selcomwireless Tanzania na kufanya nao mazungumzo ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam Jumatatu Novemba 04, 2013. Uongozi wa Selcomwireless uliofika kukutana na Mheshimiwa Makamu ulikuwa pamoja na Meneja Miradi wa Selcom (Gallus Runyeta), Meneja Masoko na Muendesha Biashara (Juma Mgori) na Mhandisi wa Software (Godfrey Kapinga).

Wakiwa katika mazungumzo na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Meneja Miradi wa Selcomwireless Tanzania Gallus Runyetta alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, kampuni yao ambayo imejikita katika kutoa huduma za malipo ya Kielekroniki imekuwa ikifanya miradi mbalimbali ambayo imerahisisha malipo kwa wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja na malipo ya umeme wa Luku na sasa iko katika hatua za mwisho za kuzindua ushirikiano na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu uthaminishaji wa malipo ya magari hali ambayo itasaidia kupunguza usumbufu kwa wanaoagiza magari nje ya nchi.
Uongozi wa Selcomwireless pia ulimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Selcom inazidi kujitanua katika kutoa huduma za malipo sambamba na takwimu katika maeneo ya afya na mfano mzuri ni Zanzibar ambako huko Selcomwireless imeshiriki katika harakati za kutokomeza Malaria, harakati ambazo pia inashiriki kwa upande wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwataka Selcomwireless kuendelea kuisaidia nchi hasa katika suala zima la kukusanya mapato na akawataka kuhakikisha wanakutana na Uongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya ili kuwapa namna ya kusaidia wananchi hasa wa vijijini kulipia Bima zao kwa gharama wanazoweza kumudu.

“Mkiwasaidia watu wa Bima ya Afya na kuwafanya walipaji kuwa wanalipa kidogo kidogo kwa vipindi fulani inaweza kabisa kubadili hali ya huduma za afya hapa nchini,” alisema na kuongeza: “Tunakutegemeeni sana na jitahidini kutumia nafasi hizi ili kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanajitokeza kulipia Bima za afya kwa kuwarahisishia namna ya kupata huduma”.

Mheshimiwa Makamu wa Rais pia aliwataka Selcomwireless kutafuta namna ya kutatua changamoto ya ulipaji wa kodi za nyumba sambamba na kukutana na viongozi wa Wizara ya Ardhi, ili watu walio na Hati zao za viwanja na makazi waweze kulipa kodi zao kwa mtandao ili kurahisisha ukusanyaji na pia kutanua wigo wa mapato katika manispaa hapa nchini.

Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu, Dar es Salaam
Jumanne 05, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI

November 05, 2013
Release No. 190
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 5, 2013

ASHANTI UTD, SIMBA UWANJANI VPL
Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinaanza kesho (Novemba 6 mwaka huu) ambapo Ashanti United itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili chini ya mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ni sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Waamuzi wasaidizi ni Abdallah Mkomwa na Rashid Abdallah wote kutoka Pwani wakati mezani atakuwa Hamisi Chang’walu.

Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu Stars na Coastal Union (Uwanja wa Chamazi), Kagera Sugar na Mgambo Shooting (Uwanja wa Kaitaba, Bukoba) na Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Keshokutwa (Novemba 7 mwaka huu) raundi ya 13 kumaliza mzunguko wa kwanza itakamilika kwa mechi kati ya Yanga na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Azam itakuwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Rhino Rangers na Tanzania Prisons kutoka Mbeya.

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City, Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Rhino itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons.

TFF YATAKA ORODHA YA WALIOSAMEHEWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetuma waraka kwa vyama vya mpira wa miguu vya wilaya, mikoa na vyama shiriki kuvitaka kuwasilisha orodha ya wote waliofaidika na msamaha wa Oktoba 28 mwaka huu.

Oktoba 28 mwaka huu wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu baada ya uchaguzi, Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi alitoa msamaha kwa wote waliofungiwa kwa sababu mbalimbali.

Hata hivyo, msamaha huo hauwahusu waliofungiwa kutokana na makosa ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile haugusi adhabu zilizotolewa ndani ya klabu.

Vyama vya mikoa vinatakiwa kuhakikisha waraka huo unafika kwa wanachama wao (vyama vya mpira wa miguu vya wilaya). TFF inataka orodha ya wote waliofaidika na msamaha huo kwa ajili ya kumbukumbu zake (records).

TANZANITE KWENDA MAPUTO KESHO
Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) kinaagwa kesho (Novemba 6 mwaka huu) saa chache kabla ya kuanza safari ya kwenda Maputo, Msumbiji.

Hafla fupi ya kuikabidhi bendera Tanzanite itafanyika kesho saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF wakati kikosi hicho kinatarajiwa kupaa saa 11 jioni kwa ndege ya LAM na kuwasili Maputo saa 3.45 usiku.

Msafara wa Tanzanite ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 10-0 karibu wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Kidao Wilfred.

Mechi hiyo ya marudiano itachezwa Novemba 9 mwaka huu Uwanja wa Taifa wa Zimpeto, na timu itarejea nyumbani Novemba 10 mwaka huu saa 8.30 mchana kwa ndege ya LAM.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

YANGA, MBEYA CITY, AZAM FC PATACHIMBIKA KESHO.

November 05, 2013


MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajia kumalizika kwa michezo ya kesho Novemba 6 na keshokutwa Novemba 7 huku kukiwa na sintofahamu nani atamaliza akiwa kileleni.

Imekuwa na mazoea kuwa katika ligi hiyo timu zinazokuwa kileleni ni Yanga, Azam na Simba SC lakini msimu huu ni tofauti kutokana na ushindani ulioibuka kutoka kwa timu kama Mbeya City.

Mbeya City, timu ambayo ni mpya katika ligi hiyo imeongeza ushindani mkubwa na kuna uwezekano ikamaliza mzunguko wa kwanza ikiwa katika kileleni mwa msimamo. 

Timu hiyo inayonolewa na Juma Mwambusi ipo katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 26 sawa na vinara Azam FC na timu hizo zitamaliza mzunguko huo kwa kuvaana mechi ambayo itatoa maamuzi nani atakuwa kinara.

Michezo ya mwisho itakuwa kama ifuatavyo, Novemba 6 ni JKT Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Chamazi, Ashanti United na Simba Uwanja wa Taifa, Kagera Sugar na Mgambo Shooting Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na Ruvu Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini.

Novemba 7 kutakuwa na mechi kati ya Azam FC na Mbeya City Chamazi, Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, wakati Rhino itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora.

Mechi ambazo zinatarajiwa kuteka hisia za mashabiki wa soka nchini ni zitakazochezwa Novemba 7 kati ya Yanga na Oljoro, lakini kwa maana ya mechi ya kufungia msimu, basi itakuwa Chamazi Azam na Mbeya City.

Mshindi wa mechi hiyo moja kwa moja atamaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu akiwa kileleni, na atakayefungwa anaweza kuporomoka hadi nafasi ya tatu, iwapo Yanga SC itashinda mechi yake na Ojoro. 

Wakitoka sare, Azam itabaki juu ya Mbeya City na Yanga inaweza kupanda kileleni ikishinda. 

Mbeya City na Azam ndizo timu pekee ambazo hadi sasa msimu huu hazijapoteza mechi, wakati mabingwa watetezi, Yanga waliopoteza mechi moja tu mbele ya Azam, wanakaa nafasi ya tatu kwa pointi zao 25.

HANDENI WATAKIWA KULITUMIA VEMA TAMASHA LA HANDENI KWA KUTAFUTA FURSA.

November 05, 2013
Na  Mwandishi Wetu, Handeni
MKUU wa wilaya Handeni, DC Muhingo Rweyemamu, amewataka wananchi wa Handeni, mkoani Tanga kulitumia Tamasha la Handeni kwa ajili ya kutafuta fursa za kimaendeleo.

Akizungumza jana mjini Handeni, Muhingo alisema kutokana na tamasha hilo kufanyika mwisho wa mwaka, Desemba 14, itakuwa chachu ya kuwaunganisha watu wote, sanjari na kujadili changamoto zinazoikabiri Handeni na Tanzania kwa ujumla.

Muhingo alisema kuwa tamasha hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na kuandaliwa maalum kwa ajili ya Watanzania kwa ajili ya kuangalia ngoma na matukio mbalimbali ya kijamii.

“Wakati napongeza kwa dhati kuandaliwa kwa tamasha hili wilayani hapa, pia nawaomba watu waje kwa wingi kushuhudia namna gani Handeni imepiga hatua kimaendeleo na kuangalia namna gani wanaweza kusonga mbele.

“Naamini tutafikia hatua nzuri kwa kushirikiana na wadau wote, hivyo wale wanaoishi mbali na Handeni pia ni wakati wao kurudi nyumbani mwishoni mwa mwaka kujifunza mambo ya utamaduni wao, sanjari na kufanya juhudi za kupiga hatua kimaendeleo,” alisema.

Tamasha hilo linaloandaliwa na Mratibu wake Kambi Mbwana, hadi sasa limedhamiwa na Phed Trans, Clouds Media Group, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group.

Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu.com, huku likipangwa kuanza saa 2 za asubuhi hadi saa 12 za jioni.