WAGANGA WAFAWIDHI NCHINI NA WATUMISHI NDANI YA SEKTA YA AFYA WATAKIWA KUTOKUWA KIKWAZO KWA WAWEKEZAJI

WAGANGA WAFAWIDHI NCHINI NA WATUMISHI NDANI YA SEKTA YA AFYA WATAKIWA KUTOKUWA KIKWAZO KWA WAWEKEZAJI

March 28, 2024




NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,akizungumza wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.



NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,akisisitiza jambo wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.


BAADHI ya Washiriki wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.


NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahela,akizungumza wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imewataka waganga wafawidhi nchini na Watumishi ndani ya Sekta ya Afya kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo ikiwemo uanzishaji wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika Jijini Dodoma kwa muda wa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki na kuchangia mada zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo.

“Sekta binafsi imesaidia kwa kiwango kikubwa kuipunguzia Serikali mzigo hasa upande wa ajira kwani vijana wengi wameajiriwa kupitia sekta binafsi, hali ambayo sio rahisi kuiachia mzigo serikali pekee.”amesema Dkt.Mollel

Aidha Dkt. Mollel amewaasa Wakurugenzi wa OR- TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia idadi ya Vijiji ambavyo havina Zahanati ili kuhakikisha vinapata vituo hivyo mapema iwezekanavyo.

“Tukijipanga kwa muda wa miaka miwili tukapunguza semina na makongamano na tukapunguza mambo mengine, tukapunguza kidogo kuboresha huku juu zaidi kwasababu huku tunaweza kwenda kwa pamoja, nawahakikishia kwa kipindi cha miaka miwili hakuna Kijiji kitakosa Zahanati”, amesema Mollel

“Tunataka tutakapokutana tena katika mkutano wa mwaka 2026 tutazungumza masula mengine kama kuajiri watumishi, kuweka vifaa na kuboresha huduma zingine zinazopaswa kuongezwa” amesisitiza Mollel.

Aidha amewaomba washiriki katika mkutano huo kuwasaidia wakurugenzi ambao bado wanaleta mgawanyiko katika kazi kuhakikisha suala hilo wanalimaliza na kuimarisha utendaji zaidi.

“Sekta ya Afya ni moja na kazi nyingi za afya zinaanzia katika ngazi ya msingi na dada yangu Dkt. Grace amesisitiza hapa hakuna huduma za afya bila msingi kwani huduma zote zinaanzia huko kwa wananchi walio wengi ndipo wanaanzia kabla ya kuja huku juu kupatiwa huduma,” amesema.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahela amesema kuwa kupitia mkutano huo mapendekezo mbalimbali yameweza kutolewa kupitia majadiliano yaliyofanyika ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa huduma za afya ya msingi.

“Mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza bajeti za afya za mifumo ya bima na jambo hili limesisitizwa kwa ukubwa na wakashauri vyanzo mbalimbali viweze kutumika ikiwemo kuwashirikisha wadau kama Wizara ya Fedha,”amesema.

Amesema pendekezo lingine lililotolewa ni kwa wadau pamoja na Serikali ni kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya ya msingi kwenye rasilimali watu na vifaa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora.

MISA TAN, TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA WASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO

March 28, 2024

 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bw. Patience Ntwina (kushoto) akibadilishana nyaraka na Mkurugenzi Mtendaji wa MISA TAN Bi. Elizabeth Riziki baada ya kutia saini mkataba wa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili.
Mwenyekiti wa bodi na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Amina Talib Ali akipongezana na Mkurugenzi Mtendaji wa MISA TAN Bi. Elizabeth Riziki (kulia) baada ya kutia saini mkataba wa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili.

****

Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-TAN) na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wamesaini mkataba wa miaka mitatu (2024- 2027) wa ushirikiano makubaliano ya kufanya kazi kwenye maeneo mbalimbali ya haki za binadamu na hasa haki za waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.


Hafla ya utiaji saini Mkataba huo imefanyika leo jijini Dodoma
na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa bodi na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Amina Talib Ali, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Mohamed Khamis Hamad, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bw. Patience Ntwina, Makamishina, wakurugenzi wa tume na kwa Upande wa MISA TAN, Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN Bw. James Marenga na Mkurugenzi Mtendaji wa MISA TAN bi. Elizabeth Riziki.

DKT. NCHEMBA AONGOZA MKUTANO WA WB KANDA YA AFRIKA

March 28, 2024

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiongoza mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati lililolenga kujadili namna mashirika ya fedha ya kimataifa yanavyoweza kuongeza fedha kuzisaidia nchi za kipato cha kati kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Mkutao huo umefanyika kwa njia ya Mtandao, kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akitoa wito kwa taasisi za fedha za kimataifa kuongeza fedha kwaajili ya kuzisaidia nchi za kipato cha kati wakati akifungua mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati lililolenga kujadili namna mashirika hayo ya fedha yanavyoweza kuongeza fedha kwa nchi hizo. Mkutano huo umefanyika kwa njia ya Mtandao kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwaka, akitoa mada wakati wa mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati, ambapo Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) aliongoza mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao, kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizaraya Fedha, Bi Amina Khamis Shaaban na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Fedha za Nje wa Wizara hiyo, Bw. John Kuchaka, wakifuatilia uwasilishwaji wa taarifa wakati wa mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati, ambapo Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao, kutokea Jengo la Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)


Na. Peter Haule, WF, Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameongoza mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati uliolenga kujadili namna mashirika ya fedha ya kimataifa yanavyoweza kuongeza fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za kipato cha kati ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi zao itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

Akifungua mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Dunia inakabiliwa na migogoro mingi na changamoto za maendeleo ya kiuchumi ambazo zinasababisha kutofikiwa kikamilifu kwa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Alisema kuwa kupungua kwa nafasi ya kifedha katika kushughulikia migogoro hiyo kunadhoofisha uwezo wa Serikali za nchi hizo kufadhili programu za kijamii, kuharakisha ufufuaji wa Uchumi na pia kuongeza madeni katika nchi hizo.

“Mizozo inayoendelea nchini Urusi na Ukraine, Mashariki ya Kati na baadhi ya nchi nyingine za Afrika imechochea kupanda kwa bei ya vyakula na kuwasukuma mamilioni ya watu kwenye uhaba wa chakula”, alisema Dkt. Nchemba.

Aidha Dkt. Nchemba aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake wa kuzijengea uwezo taasisi katika kuyafikia maendeleo endelevu lakini pia kufufua uchumi kutokana na changamoto mbalimbali zinazotokea Duniani.

Vilevile alisema kuwa kukabiliana na changamoto zinazoikumba dunia sio kazi rahisi kwa nchi moja, hivyo ameomba kuwa na nguvu ya pamoja katika Kanda na Bara la Afrika katika kutafuta utatuzi wa changamoto hizo.

Dkt. Nchemba ameishukuru Benki ya Dunia kwa kummwamini kuongoza kikao hicho kikubwa lakini pia amewashukuru viongozi mbalimbali waliotoa mada ambazo zimewafunbua macho kwa kuona fursa zilizopo katika kukuza una kuwezesha biashara na pia kuwa na majadiliano mazuri wakati wa mikutano ijayo ya majira ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) itakayofanyika mwezi Aprili, 2024 jijini Washington D.C nchini Marekani.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwaka, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ilitoa misaada na mikopo nafuu yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni tatu kwa nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema kuwa mwaka wa fedha uliopita Benki ya Dunia kupitia Mfuko wa IDA ilitoa dola bilioni 2.4 na kwamba kiwango cha misaada na mikopo hiyo imeendelea kuongezeka na miongoni mwa nchi zilizonufaika na mpango huo ni Tanzania, Kenya na Eswatini.

Aidha, Bi. Kwakwa amevitaja vipaumbele vya Benki hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha nchi zitapata umeme wa uhakika, kuwa na maendeleo ya kidigitali, upatikanaji wa ajira, mapinduzi ya kiuchumi, kujenga uwezo kwa rasilimali watu na masuala ya elimu.

Baadhi ya Viongozi walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Kanda ya Afrika, Bw. Sergio Pimenta, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Bi. Anshula Kant, Mawaziri wa fedha na Mipango (Magavana) na wajumbe wengine.

PAC YAIPONGEZA WIZARA YA ARDHI UTEKELEZAJI MRADI

March 28, 2024

 


 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika halmashauri ya Mji wa Nzega mkoa wa Tabora.

 

Kauli hiyo imetolewa tarehe 27 Machi 2027 wilayani Nzega na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe, Japhet Hasunga wakati wa ziara ya Kamati yake kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji mradi wa LTIP kwenye halmashauri ya Mji wa Nzega mkoani Tabora.

 

Mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Mji wa Nzega umepewa lengo la kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 na kuongeza alama za msingi za upimaji 14.

 

"Niwapongeze kwa kazi hii mlioamua kuifanya tangu tupate uhuru tumekuwa na changamoto za ardhi kuanzia kutambua, kupima, kurasimisha na kadhalika, kumekuwa na shida" amesema Mhe, Hasunga.

 

Amesema, Mhe, Rais ameamua kutoa fedha nyingi za mradi wa LTIP na Bunge kuidhinisha ambapo kwa upande wa halmashauri ya Mji Nzega kiasi cha Shilingi Bilioni 1.4 kimeidhinishwa kwa ajili ya Kata tano hivyo wananchi watumie fursa ya kutambuliwa maeneo yao na hatimaye kupatiwa hati kupitia mradi huo.

 

Ameeleza kuwa, Kamati yake ya PAC itakwenda kupima thamani ya fedha zilizopitishwa na Bunge pale tu wananchi watakapokuwa na hati.

 

"Msipopata hati hii mingine yote ni michakato, sisi hatuhitaji michakato tunataka kuona watu wangapi wana hati" alisema Mhe, Hasunga.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amesema, wizara yake ina uhakika michakato yote itakapokamilika katika mji wa Nzega hati milki za ardhi zitaenda kutolewa kwa wananchi.

 

Kwa mujibu wa Mhe, Pinda utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaenda kutoa jumla ya hati milki za ardhi 1,500,000 kwa maeneo yote yanayopotiwa na mradi.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameweka wazi kuwa, kazi iliyofanyika kwa halmashauri ya Mji wa Nzega kwa sasa imefikia asilimia 55 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni asilimia 39.

 

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unatekelezwa kwa mkopo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milionin150 kutoka Benki ya Dunia kwa kupindi cha miaka 5 katika halmashauri 58 nchini. Mradi huo unalenga kuboresha utawala na usimamizi wa ardhi nchini pamoja na kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa wananchi.Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga akisalimiana na waratibu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) alipowasili na Kamati yake kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi huo  Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024.Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Waziri Mhe, Geophrey Pinda wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipokwenda kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024.Sehemu ya washiriki wa ziara Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipokwenda kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024.

Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipokwenda kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Katika Mji wa Nzega mkoa wa Tabora tarehe 27 Machi 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)