TANZANIA YAFANYA UFUNGUZI RASMI WA UBALOZI JIJINI ALGIERS, ALGERIA

August 03, 2023

 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wake jijini Algiers, Algeria tarehe 2 Agosti 2023.

Ufunguzi huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na kuhudhuriwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf,  Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania, Balozi Noureddine Djoudi na Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini Algeria.

Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nishati na Mambo ya Ndani ya Nchi.

Akihutubia kwenye ufunguzi wa Ubalozi huo Waziri Tax ameeleza kuwa Tanzania na Algeria zimejidhatiti kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa lengo la kukuza ushirikiano wenye maslahi kupitia sekta za kipaumbele.

‘’Ni imani yangu kuwa Ubalozi huu utaendelea kuwa kiunganishi kati ya serikali zetu kwa kutoa huduma za kidiplomasia, kuhudumia Watanzania” alisema Dkt. Tax

Naye Mhe. Attaf ameeleza kuwa ziara ya Waziri Tax imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kuzungumza masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji na sekta nyingine muhimu kwa maendeleo ya mataifa hayo mawili.

‘’Balozi zetu zitaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ili nia ya dhati ya kuimarisha na kukuza uhusiano iweze kuleta tija zaidi na kuziwezesha nchi zetu kunufaika kiuchumi,’’ alisema Mhe. Attaf.

Ufunguzi wa Ubalozi umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambao umemalizika kwa mafanikio na kuwezesha kusainiwa kwa hati 8 za makubaliano ya ushirikiano katika sekta za nishati, mafuta na gesi, elimu na teknolojia, mafunzo ya diplomasia, kumbukumbu na nyaraka, ulinzi na usalama, ushirikiano wa kidiplomasia, kilimo na afya. 

Uhusiano kati ya Algeria na Tanzania uliasisiwa mwaka 1963 mara baada ya uhuru wa Tanganyika. Tangu wakati huo nchi hizi zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa maslahi ya pande zote. Vilevile katika kuimarisha ushirikiano huo Tanzania imefanya ufunguzi wa Ubalozi wake nchini Algeria ambao ulianza kutekeleza majukumu yake tangu mwaka 2017.

=====================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikata utepe kuashiria ufunguzi wa ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023 jijini Algiers. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf na kulia ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mej. Jen. Jacob Kingu wakishuhudia ufunguzi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf wakikamilisha matukio ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipongezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf baada ya kukamilisha taratibu za ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.


Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (mwenye tai ya bluu) akifatilia hotuba zilizowasilishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Dkt. Tax na na Mhe. Attaf.



Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora ya Algeria, Balozi Selma Malika na Balozi Djoudi wakifatilia hafla ya ufunguzi huo.

Picha ya pamoja, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf.
Picha ya Pamoja, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf na Watumishi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria na ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimkabidhi zawadi Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania, Balozi Noureddine Djoudi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria.

TCAA YAHAMASISHA MATUMIZI YA DRONES

August 03, 2023

 *Kutumia katika umwagiliaji na unyunyuziaji dawa


Na Chalila Kibuda Michuzi TV

Mamlaka ya Anga Tanzania  (TCAA) imesema kuwa katika Maonesho ya Kilimo Nane Nane imejipanga kutoa elimu ya matumizi ya ndege isiyo na Rubani 'Drones' katika kutumia kwenye kilimo kwa matumizi ya umwagiliaji na unyunyuziaji wa dawa.

Hayo ameyasema Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano wa TCAA Yassaya Mwakifulefule kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nane Nane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale , jijini Mbeya.

Amesema kuwa ndege hiyo inaweza kutumika kumwagilia maji kwa kuanzia hekari 25 ambapo inamrahisishia mkulima kutumia muda mdogo kuliko kwa kutumaia mpira.
Amesema kuwa Teknolojia imerahisisha wakulima kuweza kutumia nguvu ndogo kuliko kutumia mbinu za kizamani.

Mwakifulefule amesema kuwa ni fursa kwa sekta ya kilimo kwa wakulima kuweza kutumia teknolojia hiyo kwa kununua na kujisajili pamoja na kupata mafunzo ya namna ya kutumia Drones.

Amesema kuwepo kwa mafunzo na kujisajili inatokana na kuweka usalama wa anga kwani ndege hiyo ikiruka kwenye anga ya ndege ya abiria madhara yake ni makubwa.

Aidha amesema kuwa mafunzo ya matumizi ya ndege hiyo ni wiki nne ambapo atatunukiwa cheti cha utambuzi wa kwenda kurusha ndege isiyo na rubani kwenye shughuli mbalimbali.

Amesema kuwa watu wanaomiliki Drones na kuzitumia bila kujisajili na bila mafunzo ni kosa la kisheria hivyo wanatakiwa kufuata sheria hiyo.

Mwakifulefule amesema kuwa katika kutoa huduma ya usafiri wa anga ni kutaka kuwa na usalama kwa ajili ya ndege zinazopita katika anga ya Tanzania.



WAZIRI MKUU ATEMBELEA MAONESHO YA NANENANE UWANJA WA JOHN MWAKANGALE MBEYA

August 03, 2023

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama zabibu zilizokaushwa bila kupoteza virutubisho wakati alipotembelea banda la wilaya ya Chunya katika Maonesho ya Wakulima ya Kimataifa Nanenane kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya, Agosti 3, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mafuta ya kula yaliyotokana na alizeti wakati alipotembelea banda la wilaya ya Chunya katika maonesho ya Wakulima ya Kimataifa  Nanenane kwenye uwanja  wa John Mwakangale jijiii Mbeya, Agosti 3, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama fuvu la tembo wakati alipotembelea banda la maonesho la Wilaya ya Chunya katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Agosti 3, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ufugaji wa kisasa wa samaki aina ya Sato wakati alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika maonesho ya wakulima  ya kimataifa Nanenae kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya, Agosti 3, 2023. Kushoto kwake ni Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson. (Picha na Ofisi a Waziri Mkuu)
 

PSSSF: WAKULIMA NA WAFUGAJI NI WADAU WAKUBWA WA MFUKO KWENYE UWEKEZAJI WETU KATIKA VIWANDA

August 03, 2023


 NA MWADISHI WETU, MBEYA

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema Maonesho ya mwaka huu ya Nanenane yana maslahi mapana kwa Mfuko huo kutokana na uwekezaji ambao umefanya kwenye maeneo ya kilimo na mifugo, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe amesema.

Bwana Mlowe amebainisha hayo leo Agosti 3, 2023 kwenye Banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane 2023 yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Alisema Mfuko unayo majukumu manne ambayo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kisha kulipa mafao.

“Katika eneo hili la Uwekezaji, Mfuko umewekeza kwenye maeneo mbalimbali mojawapo ni eneo la viwanda, eneo hili tumewekeza kwenye kiwanda cha Kuchakata Tangawizi, Mamba Miamba kilichoko Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro na Kiwanda cha Chai Mponde, kilichoko Wilayani Lushoto Mkoani Tanga.”Alisema na kuongeza  kuwa PSSSF imewekeza kwenye Machinjio ya Kisasa Nguru Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (KLIC), na hii ni fursa kwa wafugaji.” Alifafanua Bw. Mlowe.

Alisema kwa sababu hiyo Wakulima na Wafugaji ni wadau muhimu wa Mfuko na kuwataka watembelee kwenye banda la PSSSF ili kujua fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Mfuko katika maeneo hayo ya uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo.

Akizungumzia kuhusu majukumu mengine ya msingi ya Mfuko, Bw. Mlowe alisema PSSSF inatoa huduma kwa Watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa zaidi ya asilimia 30%

“Hata kaulimbiu ya mwaka huu ya ‘Vijana na Wanawake ni Msingi imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula’ inatuunganisha,  tunapokuwa na chakula cha kutosha tunajenga nguvu kazi imara ambayo ni vijana na hawa wanapoajiriwa Serikalini wanakuja kuwa wanachama wetu.” Alifafanua Bw. Mlowe.

Akieleza zaidi ushiriki wa Mfuko katika Maonesho hayo alisema “Hapa bandani ni ofisi kamili, tunawahudumia wanachama wetu kama ambavyo wanavyohudumiwa kwenye ofisi zetu zilizoeneo nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar.” Alifafanua.

Alisema wanachama wakiwemo wastaafu wakitembelea kwenye banda hilo watakutana na watumishi wanaojali mteja, waaminifu na wenye weledi na utayari wa kuwahudumia na wataweza kupata Taarifa kuhusu Michango, Taarifa za Mafao yatolewayo na Mfuko, Taarifa za Uwekezaji lakini pia wastaafu wataweza kujihakiki kwa njia ya alama za vidole (Biometric).

Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Bi. Grace Kabyemela, amewahakikishia Wanachama wakiwemo Wastaafu kuwa Mfuko uko katika hali nzuri ya kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati kwa mujibu wa Sheria.

“Sheria inatutaka kuwa mwanachama anayestaafu anapowasilisha nyaraka zilizokamilika anapaswa awe amelipwa mafao yake ya mkupuo ndani ya siku 60, lakini sisi PSSSF tumejiwekea malengo ndani ya siku 30 tunafanya malipo.” Alidokeza Bi.Kabyemela.

Aidha kuhusu malipo ya pensheni ya kila mwezi, Bi. Kabyemela alisema Mfuko unahakikisha ikifika tarehe 25 ya kila mwezi wastaafu wanakuwa wamelipwa pensheni zao mwezi.

Habiba Khalid Mhina yeye ni Mwanachama wa PSSSF ambaye alitembelea banda la PSSSF ili kupata taarifa za michango yake na baada ya kuhudumiwa aliipongeza PSSSF kwa kumpatia taarifa zake kwa haraka

“Mimi ni Mfanyakazi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dodoma, nimefika banda la PSSSF kupata taarifa za michango na kwakweli chini ya dakika 5 nimepata huduma na kukabidhiwa taarifa ya michango yangu.” Alisema.