Coastal Union kukipiga na Mwadui FC ya Shinyanga Alhamisi Mkwakwani”

December 16, 2014

MABINGWA wa soka Tanzania Bara mwaka 1988 Coastal Union “Wagosi wa Kaya”inatarajia kucheza mechi ya kirafiki na Mwadui ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa timu zote kujiandaa na michuano wanayokabiliana nayo.
 
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Alhamisi ya wiki hii kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani lengo likiwa ni kukipa makali kikosi cha Coastal Union kujiwida na mechi yao ya Ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Tanzania Prison itakayochezwa kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.


Akizungumza na Coastal Union Official Site,Katibu wa Coastal Union,Kassim El Siagi alisema kuwa mechi hiyo ni miongoni mwa michezo mbalimbali ya kirafiki wanayocheza ili kuweza kukiimarisha kikosi hicho ambacho msimu huu kimepania kufanya makubwa kwenye michuano ya Ligi kuu soka Tanzania.

El Siagi alisema kuwa timu ya Mwadau ya Shinyanga inatazamiwa kuwasili mkoani hapa Jumanne wiki hii tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa na upinzani mkali.
Hata hiyo aliwataka wadau wa soka mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo ikiwemo kuangalia wachezaji ambao wamesajiliwa msimu huu kwa ajili ya michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara.

   “Tunawajua Mwadui FC sio timu mbaya hivyo naamini kutakuwa na burudani ya kukata na shoka nawasihi wakazi wa mkoa wa Tanga wajitokeza kwa wingi ili kushuhudia mchezo huo “Alisema El Siagi.

Hata hivyo alisema kuwa baada ya kumalizika mechi hiyo wataangalia uwezekano wa kucheza mechi nyengine ya kirafiki kabla ya kutua jijini Mbeya ambapo watakwenda kucheza mechi yao ya Ligi kuu.

KOCHA WA KIUNGO MKENYA VICTOR WANYAMA ATUA COASTAL UNION,AHAIDI MAKUBWA

December 16, 2014

 Kocha Mkuu Coastal Union,James Nandwa kulia akilakiwa  na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Coastal Union,Dr.Ahmed Twaha mara baada ya kuwasilia mkoani Tanga jana.
HAPA NI KOCHA NANGWA WA KWANZA KULIA AKIELEKEZWA JAMBO NA MJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI COASTAL UNION,DR.AHMED TWAHA KUSHOTO NI KATIBU MKUU WA COASTAL UNION,KASSIM EL SIAGI

Kocha Mkuu Coastal Union,James Nandwa kulia akiwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Coastal Union,Dr.Ahmed Twaha mara baada ya kuwasilia mkoani Tanga jana.
NA MWANDISHI WETU,TANGA.
ALIYEWAHI kuwa Kocha wa Kiungo Mkenya, Victor Wanyama anayechezea soka lake kwenye klabu ya ,Southampton nchini Uingereza James Nandwa ameingia mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha timu ya Coastal Union ya Tanga.
Kocha huyo anachukua mikoba iliyoachwa na Kocha Yusuph Chippo aliyekwenda nchini kwao Kenya kutokana na matatizo ya kifamilia kuwa kwenye hali ambayo sio mzuri jambo ambalo lilipelekea kushindwa  kurejea nchini kwa ajili ya kuendelea kukinoa kikosi hicho.
Akizungumza mara baada ya kutua jijini Tanga leo ikiwemo kulakiwa na viongozi wa klabu hivyo wakiongozwa na Meneja wake ,Akida Machai wakiwemo Katibu Mkuu pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji,Kocha huyo alisema kuwa dhamira yake kubwa ni kuhakikisha anaipa mafanikio timu hiyo.
Akizungumza leo,Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga amesema kuwa ujio wa kocha huyo utawezesha timu hiyo kufikia malengo yao ambayo wamejiwekea ya kuhakikisha wanachukua ubingwa wa Ligi kuu Tanzania bara msimu huu.
Assenga amesema kuwa kutokana na uzoefu aliokuwa nao kocha huyo utawezesha kupelekea chachu kwa wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho kupambana wakiwa na lengo la kuipa mafanikio timu hiyo.
Kwa upande wake,Kocha  Nandwa amesema kuwa kitu cha kwanza ni kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo yake iliyojiwekea ya kuwa timu bora Tanzania ili iweze kupata nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya kombe la shirikisho.
   “Kwanza nashukuru kupata nafasi ya kuifundisha Coastal Union nitahakikisha nitaifikisha timu hii kwenye malengo waliojiwekea ya kuchukua ubingwa wa Ligi kuu soka Tanzania bara kutokana na uzoefu wangu niliokuwa nao “Amesema Nandwa.
Kocha Nandwa aliwahi kuzifundisha timu za soka za Harambee Stars,AFC Leopard ya Kenya pamoja na Utalii ya Kenya na kuipa mafanikio makubwa ikiwemo Ubingwa wa Ligi kuu nchini humo.