Benki ya CRDB yazindua SimBanking App mpya inayotumia teknolojia ya kisasa kutambua mahitaji ya wateja na kurahisisha miamala

July 19, 2023
 
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa SimBanking App inayotumia teknolojia ya kisasa zaidi inayowezesha kutambua mahitaji ya wateja na kurahisiha hudumana miamala yenye muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence), iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam leo tarehe 19 Julai 2023.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, akiwa mbele ya kifaa kinachotumia teknolojia ya kisasa zaidi inayowezesha kutambua mahitaji ya wateja na kurahisiha huduma na miamala yenye muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence) ambayo inatumika katika SimBanking App mpya iliyozinduliwa leo katika hafla , iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam leo tarehe 19 Julai 2023.
 
===========   =========   ========== 
 
Wakati dunia ikishuhudia mabadiliko makubwa ya teknolojia yanayochagiza maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha, leo Benki ya CRDB inayoongoza kwa ubunifu nchini imezindua SimBanking App inayotumia teknolojia ya kisasa zaidi kutambua mahitaji ya wateja.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema SimBanking App hii mpya imetengenezwa kwa muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili bandia (Artificial intelligence).
“Teknolojia iliyotumika katika SimBanking App hii inampa uwezo mteja kuchagua mpangilio wa huduma kwa namna ambavyo yeye mwenyewe angependelea, teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kutambua ni huduma gani mteja anapendelea zaidi na kumrahisishia namna ya kuipata,” alisema.
 
Nshekanabo alibainisha kuwa teknolojia hiyo mpya ni ya kimapinduzi katika kufikisha huduma za fedha kwa wateja kwani itaongeza wigo wa huduma zinazoweza kutolewa kidijiti huku kasi ya miamala ya wateja ikirahishwa kwa kiasi kikubwa.
 
“Eneo jingine ambalo tumelipa uzito mkubwa katika SimBanking App hii mpya ni ulinzi na usalama wa taarifa na miamala ya wateja. Tunatumia teknolojia ya biometriki kuhakikisha usalama kwa wateja. Hii inatufanya kuwa Benki pekee nchini na kati ya chache barani Afrika inayotumia teknolojia hii,” aliongezea Nshekanabo.
Akizungumzia huduma mpya ambazo zimeongezwa, Meneja Mwandamizi wa Huduma za Kidijiti na Ubunifu wa Benki ya CRDB, Jacklina Jackson amesema SimBanking App inatoa fursa za uwekezaji kwa wateja kwa kuwawezesha kuwekeza kupitia akaunti za uwekezaji (Fixed Deposit) kidijiti.
 
“Wateja pia sasa hivi wanaweza kupanga uhamisho wa fedha na malipo yanayojiruida au ya mara kwa mara kwa urahisi. Uhamisho unaweza kupangwa kila siku, kila wiki au kila mwezi. Tumeboresha upande wa kumbukumbu za taarifa ya miamala ambapo wateja wanaweza kupata risiti ya miamala yote wakati wowote kwa urahisi,” alisema Jacklina.
 
Katika upande wa malipo, alisema SimBanking App imeboresha malipo kupitia watoa huduma za kidijiti kwa kuwezesha ukusanyaji wa malipo kupitia programu hiyo ambapo mteja ana uwezo wa kutoa ruhusa ya malipo kwa kutumia mfumo wa namba ya siri ya mara moja (one time passcode). 
“Vilevile tumefanya maboresho katika huduma za bima kwa kuongeza kasi na muda wa upatikanaji wa huduma,” aliongezea Jacklina kuhusu huduma hiyo ya bima za vyombo vya moto ambayo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza kupitia SimBanking App mwaka 2020 benki ilipofanya maboresho.
 
Aidha, SimBanking App mpya inakuja na programu ya uaminifu (loyalty program) inayowawezesha wateja kupata kupata alama wanapotumia application na kisha kujishindia zawadi. Wateja pia aplikesheni hii mpya pia inatoa fursa kwa wateja kutoa maoni yao kila wakati wanapokamilisha miamala mfumo unaohusisha uwasilishaji wa maandishi na matumizi ya emoji kuonyesha hisia juu ya huduma.
 
Hii ni mara ya pili kwa Benki ya CRDB kufanya maboresho makubwa katika huduma ya SimBanking baada ya maboresho yaliyofanyika mwaka 2020. Tarifa ya Benki hiyo inaonyesha sasa hivi asilimia 96 ya miamala yote inafanyika kidijitali huku SimBanking ikichangia sehemu kubwa.
 
Huduma ya SimBanking ambayo ilianzishwa mwaka 2022 imekuwa ikitajwa kuwa moja ya huduma bora zaidi za kidijitali ambazo zinatoa mchango mkubwa katika ujumuishi wa kifedha nchini na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi. 
 
SimBanking imepata tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo tuzo za Consumer Choice Awards, tuzo za za Global Finance zinazotolewa nchini Marekani, na hivi karibuni imepata tuzo ya huduma bora ya kidijitali katika tuzo za Tanzania Digital Awards.




TUME YA MADINI YATOA SIKU SABA KWA WAMILIKI WA LESENI KUTEKELEZA MASHARTI

July 19, 2023

 










 Dodoma Julai 19, 2023 

Tume ya Madini imetoa siku saba kwa wamiliki wote wa leseni za madini zikiwemo leseni za utafutaji wa madini, leseni za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa wa madini, leseni za uchenjuaji wa madini, leseni za uyeyushaji wa madini na leseni za usafishaji wa madini kuhakikisha wanatekeleza masharti  ya leseni zao kwa mujibu wa Sheria.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula leo jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa ya Sekta ya Madini.

Amesema kuwa, zipo kampuni za  madini ambazo zimeaminiwa na Serikali kwa kupewa leseni za madini lakini wamekuwa wakikiuka masharti ikiwa ni pamoja na kutoendeleza maeneo ya uchimbaji wa madini hivyo kukosesha fursa kwa waombaji wengine wenye nia ya kuchimba madini na Serikali kupata mapato yake.

“ Tumetoa muda wa siku saba ( kuanzia tarehe 19 hadi 25 Julai, 2023 kwa wamiliki wote kutekeleza masharti ikiwa ni pamoja na wamiliki wote wa leseni za madini ambao leseni zao zimetoka lakini hawajazichukua kuhakikisha wamezichukua, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka kuhakikisha wamelipia na leseni ambazo hazijaendelezwa kuhakikisha zinaendelezwa ndani ya muda ulioainishwa sambamba na kuwasilisha taarifa ya kuanza kazi na taarifa za kila robo mwaka kuwasilishwa,” amesema Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amewataka waombaji wote wa leseni za madini wenye mapungufu kurekebisha mapungufu hayo ndani ya siku saba ikiwa ni pamoja na maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi, maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi  na ada ya pango kwa mwaka.

Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa wamiliki au waombaji wa leseni watakaoshindwa kurekebisha mapungufu ndani ya muda wa siku saba, Profesa Kikula amefafanua hatua hizo kuwa kwa leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka, leseni ambazo haziendelezwi na leseni ambazo  zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria na kwa maombi yote ya leseni ambayo hayakidhi vigezo, yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.

Aidha, Profesa Kikula amesisitiza kuwa dhumuni la Serikali ni kuweka mazingira rahisi na wezeshi kwa wawekezaji wote nchini na kuongeza kuwa Serikali haitamfumbia macho mwekezaji wa ndani au kutoka nje ya nchi ambaye ameshikilia maeneo bila ya kuyaendeleza au kuyatumia maeneo hayo kujipatia fedha kisha kuwekeza nje ya nchi.

Pia, Profesa Kikula ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika madini ya kimkakati yanayohusika katika utengenezaji wa vifaa vya kisasa na kieletroniki ikiwemo magari yanayotumia umeme ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Wakati huohuo, Profesa Kikula ameongeza kuwa Serikali imekamilisha kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii za mwaka 2023 ambazo zitasaidia wamiliki wa leseni kuwa na mwongozo wa namna bora ya kutoa huduma kwa jamii zinazozunguka migodi yao.