COASTAL UNION WAANZA KAZI RASMI,WAICHAPA OLJORO JKT KAMA IMESIMAMA.

August 24, 2013


NA HAFIDHI KIDOH,ARUSHA.
TIMU ya Coastal Union "Wagosi wa Kaya"leo wameanza vema Ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kuibamiza JKT Oljoro mabao 2-0,katika mchezo uliochezwa uwanja wa sheirh Amri Abeid Mkoani Arusha.

Katika mchezo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani mkuwa ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko Coastal Union walikuwa wakiongoza kwa bao ambalo lilifungwa na Abdi Banda kwenye dakika ya 11.

Baada ya bao hilo,Coastal Union waliweza kuongeza nguvu ya mashambulizi langoni mwa JKT Oljoro na kufanikiwa kuandika bao lao la pili katika dakika ya 36 bao ambalo lilifungwa na mchezaji hatari na mahiri wa kikosi hicho Crispian Odulla.

Licha ya JKT Oljoro kutaka kufurukuta langoni mwa Coastal Union walishindwa kubadilisha matokeo mpaka dakika 90 na kusomeka Coastal Union 2 na JKT Oljoro 0.
 

MGAMBO SHOOTING YASHINDWA KUUTUMIA VEMA UWANJA WA NYUMBANI ,YACHAPWA VIWILI NA JKT RUVU.

August 24, 2013
NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
MABAO mawili ya dakika ya 80 na 83 yaliyofungwa na Bakari Kondo wa JKT Ruvu yalitosha kuwahakikishia ushindi kwenye mechi yao na Mgambo JKT iliyochezwa leo kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Uzembe wa Mabeki wa Mgambo Jkt ndio kitu pekee ambacho kiliwapelekea kupoteza mchezo wa leo wa ligi kuu soka Tanzania bara licha ya wachezaji wake kucheza kwa kujituma na kuonyesha kandanda nzuri na la kusisimua.

Dakika ya 5 ya mchezo huo,JKT ruvu watajilaumu wenyewe kwa kukosa bao la wazi baada ya kupata penati iliyotokana na mchezaji wa Mgambo Shooting Salum Kipanga kuunawa mpira eneo la hatari na mwamuzi wa mchezo huo Dominick Nyamisana kutoka Dodoma kuamuru ipigwe penati.

Penati hiyo ilipigwa na Stanley Nkomola ambaye alishindwa kuitendea haki baada ya kupiga mpira huo nje ya lango la Mgambo shooting.

Mchezo huo uliokuwa mkali na wenye upinzani mkubwa ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzie ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi.

Ambapo katika kipindi hicho Mgambo shooting waliweza kufanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake kwa kuwatoa Mohamed Samatta na kuingia Fully Maganga aliyeongeza nguvu ya mashambulizi langoni mwa JKT ruvu bila mafanikio yoyote yale.

Wakionekana kujipanga na kucheza kwa umakini JKT ruvu waliweza kuutawala mchezo huo kwa kiwango cha hali ya juu kwa wachezaji wake kucheza pasi fupi fupi na ndefu ambapo walifanikiwa kuandika mabao yao mfululizo ambapo la kwanza lilifungwa dakika ya 80 na lengine likifungwa dakika 83.
 

KUWENI MAKINI KATIKA KUTOA MAONI KWENYE RASIMU MPYA WA KATIBA

August 24, 2013
 Ofisa Mtendaji kata ya Kwediboma,Issaya Joshua Magembe wakati akifungua mkutano wa kudusuru rasimu ya katiba mpya ambao ulishirikisha asasi mbalimbali za kirai zilizopo wilayani hapa ulioratibiwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Tanga(Tasco)

MAJINA YA WAOMBAJI UONGOZI TFF, TPL BOARD YAWEKWA WAZI

August 24, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
 Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imebandika rasmi kwenye ubao wa matangazo majina ya waombaji uongozi kwenye uchaguzi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) ili kutoa fursa kwa pingamizi.

Kipindi cha pingamizi kinaanza leo agosti 24 hadi sas 10 kamili jioni ya Agosti 26 mwaka huu ambapo waweka pingamizi wanaruhusiwa kupitia taarifa za wale wanaokusudia kuwawekea pingamizi kabla ya kuwasilisha pingamizi husika.

Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi, Agosti 27 hadi 29 mwaka huu ni wawekaji pingamizi na wawekewa pingamizi kufika mbele ya Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kusikiliza pingamizi.

Waombaji kuwania uongozi katika TFF ambao majina yao yamebandikwa ni Athuman Jumanne Nyamlani, Jamal Emil Malinzi, Omari Mussa Nkwarulo na Richard J. Rukambura (urais). Nafasi ya Makamu wa Rais ni Imani Omari Madega, Ramadhan Omari Nassib na Walace John Karia.

Walioomba nafasi za ujumbe kuwakilisha kanda ni Kanda Namba Moja (Kagera na Geita) ni Abdallah Hussein Mussa na Kaliro Samson. Kanda Namba Mbili (Mara na Mwanza) ni Jumbe Odessa Magati, Mugisha Mujwahuzi Galibona, Samwel Nyalla na Vedastus Kalwizira Lufano.

Kanda Namba Tatu (Shinyanga na Simiyu) ni Epaphra Amana Swai, Mbasha Matutu Mong’ateko na Stanslaus Haroon Nyongo. Kanda Namba Nne (Arusha na Manyara) ni Ally Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omari Walii Ali.

Kanda Namba Tano (Kigoma na Tabora) ni Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamisi Kitumbo. Kanda Namba Sita (Katavi na Rukwa) ni Ayoub Nyaulingo, Blassy Mghube Kiondo, Nazarius A.M. Kilungeja. Kanda Namba Saba (Iringa na Mbeya) ni Ayoub Shaibu Nyenzi, Cyprian Charles Kuyava, David Samson Lugenge, Elias Lusekelo Mwanjala, Eliud Peter Mvella na John Mwachendang’ombe Kiteve.

Waombaji wa Kanda Namba Nane (Njombe na Ruvuma) ni James Patrick Mhagama, Kamwanga Rajabu Tambwe na Stanley William Lugenge. Kanda Namba Tisa (Lindi na Mtwara) ni Athuman Kingome Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder.

Kanda Namba Kumi (Dodoma na Singida) ni Charles Komba, Hussein Zuberi Mwamba na Stewart Ernest Masima. Kanda Namba 11 (Morogoro na Pwani) ni Farid Salum Mbarak, Geoffrey Irick Nyange, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala na Twahil Twaha Njoki.

Wanaowania kuteuliwa kugombea kupitia Kanda Namba 12 (Kilimanjaro na Tanga) ni Davis Elisa Mosha na Khalid Abdallah Mohamed wakati Kanda Namba 13 (Dar es Salaam) ni Alex Chrispine Kamuzelya, Muhsin Balhabou, Omar Isack Abdulkadir, Shaffih Dauda Kajuna na Wilfred Mzigama Kidao.

Kwa upande wa TPL Board waliotangazwa kuomba kuwania uongozi wa juu ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti) na Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti).

Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Kazimoto Miraji Muzo, Michael Njunwensi Kaijage, Omari Khatibu Mwindadi, Salum Seif Rupia na Silas Masui Magunguma.