KAILIMA AMPONGEZA WAZIRI MHAGAMA KWA BAJETI KUPITA BUNGENI

April 13, 2023

 

Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa akiwa Bungeni pamoja nae ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (wapili kushoto),  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (wapili kulia) na Naibu Waziri ,Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Paschal Katambi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista J. Mhagama akichangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2023/24 Bungeni Jijini Dodoma leo Aprili 13,2023. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima akimpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista J. Mhagama pamoja na viongozi wengine wa Wizara baada ya kuhitimishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2023/24 Bungeni Jijini Dodoma leo Aprili 13,2023.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako pamoja na manaibu Waziri na Makatibu wakuu wa Wizara zao wakiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kuhitimishwa kwa bajeji ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 Bungeni jijini Dodoma Aprili 13,2023. 
***************

Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista  Mhagama amesema Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu imezingatia vipaumbele muhimu katika maeneo yote yanayoratibiwa na Ofisi hiyo ili kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija kwa Taifa.

Ametoa kauli hiyo mapema leo wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Mwaka wa fedha  2023/24 wakati wa Kikao cha Bunge la 12 Mkutano wa 11 Kikao cha sita Mjini Dodoma.

Waziri Mhagama amesema pamoja na mambo mengine, Bajeti ya Mwaka huu ya Ofisi ya Waziri Mkuu imezingatia masuala muhimu ikiwemo la Uratibu wa shughuli za Serikali kwa kueleza tayari ofisi hiyo umeunda  Idara ya ufuatiliaji na Tathimini ya utendaji wa serikaliambapo itawezesha kuwa na taarifa sahihi za utekelezaji wa Shughuki za Serikali.

Akizungumzia kuhusu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Waziri Mhagama amesema, Mamlaka imefanya   kazi ya kutosha katika maeneo yote manne ya kimkakati ya kupambana na dawa za kulevya, kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya, kufanya ukaguzi katika maeneo yanayofanya biashara ya kemikali bashirifu na kufanya maboresho ya sheria na kuteketeza mashamba mengi ya bangi nchini.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Mamlaka imefanya vizuri katika kutoa elimu ya uelewa kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya.

“Tumefanya vizuri katika kupunguza athari za madhara ya dawa za kulevya kwa waathirika, na huduma ya za kutibu urahibu wa dawa za kulevya na bado tunaendelea kufanya mashirikiano ya nchi, kikanda na kimataifa ili kukabiliana na jambo hili mtambuka.”Alisisitiza  

Kwa Upande wa suala la  Sera ya lishe, Waziri amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, itakuja na Mkakati wa kuwa na Sera ya lishe, UKIMWI na Janga la matumizi ya Dawa za kulevya.

Pamoja na hilo, Waziri alieleza kuwa ofisi yake inasimamia Dawati la Afya Moja linaloshughulikia uratibu wa magonjwa ya mlipuko yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, ili kuweza kukabiliana nayo na kuangalia usalama wa wananchi.

Aidha alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kwa falsafa yake ya kuliwezesha Taifa kuwa na ustahimilivu na kuleta mabadiliko makubwa ya kiuongozi, kidemokrasia, kiuchumi na mahusiano ya kimataifa na kuwataka  wabunge kuunga  mkono falsafa hiyo.

.

SERIKALI HAIJASHINDWA KULIPA MIKOPO

April 13, 2023


Na Farida Ramadhani WFM -Dodoma.

Serikali imeeleza kuwa hakuna mikopo ambayo imeshindwa kulipa katika kipindi cha Awamu zote sita za uongozi.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bunda, Mhe. Boniphace Mwita Getere aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kupata mkopo wa fedha nyingi wa muda mrefu kwa masharti nafuu ili kulipia madeni sumbufu katika Awamu zote sita (6).

Mhe. Chande alisema katika kipindi cha Awamu zote sita (6) Serikali imeendelea kukopa na kulipa mikopo kulingana na mtiririko wa malipo kwa kila mkopo na hakuna mikopo ambayo Serikali imeshindwa kulipa.

“Malipo ya madeni yote ikiwemo madeni sumbufu yanaendelea kulipwa kupitia mpango na bajeti za Serikali za kila mwaka”, alifafanua Mhe. Chande.

Alisema Serikali inaendelea kusimamia deni la Serikali kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134 inayobainisha vigezo vya kuzingatia wakati wa kutafuta fedha za mikopo kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli za Serikali, hususani miradi ya maendeleo.

Alibainisha kuwa Sheria hiyo pia inatumika kama nyenzo ya kudhibiti ongezeko la deni la Serikali kwa kulipa mikopo iliyoiva na kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu.

Mwisho.


DKT. NCHEMBA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA RAIS WA BENKI YA DUNIA JIJINI WASHINGTON

April 13, 2023


Na Benny Mwaipaja, Washington D.C


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Dunia, Bw. David Malpass, na kujadiliana masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo, yatakayoiwezesha nchi kupiga hatua zaidi kimaendeleo.


Katika majadiliano hayo, Bw. Malpass, alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuvutia ushiriki wa Sekta Binafsi na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na katika kukuza uchumi wa nchi na maisha ya watanzania Tanzania.


Aidha, Bw. Malpass alihamasisha juhudi zaidi katika kulinda uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuwa ni nguzo katika kukuza uchumi na kushauri Sekta binafsi kupewa kipaumbele katika kusukuma ajenda ya maendeleo jambo ambalo litachochea uzalishaji, kuongeza ajira pamoja na kuboresha Maisha ya watu.


Vilevile, Rais Malpass ameishukuru Tanzania kwa kuridhia kuwa wenyeji wa mikutano miwili mikubwa ya kimataifa ambayo ni Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uendelezaji wa Rasilimali Watu (Africa Human Capital Summit) utakaofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Julai mwaka huu, na Mkutano wa Mapitio ya Utekelezaji wa Nusu Muhula wa Mgao wa Fedha katika Mzunguko wa 20 wa IDA (IDA 20 Mid-Term Review) mahususi kwa ajili ya utoaji mikopo na misaada kwa nchi wanachama wa Benki ya Dunia, utakaofanyika mwezi Desemba 2023 visiwani Zanzibar.


Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Rais Malpass, kwa kuisaidia Tanzania kutimiza agenja zake mbalimbali za Maendeleo katika kipindi chake cha uongozi kama Rais wa Benki ya Dunia.


Alisema katika kipindi chake cha uongozi, Bw. Malpass ameimarisha ushirikiano wa Benki ya Dunia na Tanzania na kumfahamisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki ya Dunia, Tanzania imepata fedha za mkopo nafuu na misaada mbalimbali iliyosaidia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya kimkakati.


Aidha, amerejea shukrani zake kwa Benki ya Dunia kwa kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi 29 ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati ambayo imefikia gharama ya zaidi ya shilingi trilioni 16.7, ambapo miradi 24 ni ya kitaifa na mingine 5 ni ya kikanda.