1.0. MAISHA YAKE
Ndugu
John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1959 katika
kijiji cha Chato, Wilayani Biharamulo katika Mkoa wa Kagera. Hivi sasa
Chato ni Wilaya katika Mkoa wa Geita. Ndugu Magufuli ni Daktari wa
Falsafa (PhD) ya Kemia. Ana mke na watoto saba. Alichaguliwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba, 2015 kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (C.C.M). Aliapishwa na kuanza rasmi majukumu yake ya
kuiongoza Tanzania tarehe 5 Novemba, 2015.
Tangu
ameingia madarakani, Rais Dkt. Magufuli, ameonesha kuwa ana sifa zote
muhimu za uongozi. Ana dira, maono na malengo kuhusu anakotaka Taifa
liende. Ana mikakati ya kutekeleza dira na maono yake. Haogopi kufanya
maamuzi makini. Ana kiu ya kuona Taifa linapata maendeleo. Amejipambanua
kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge na dhamira yake kubwa ni kuona
wananchi wanapata huduma bora za jamii na kero zao zinaondoka.
2.0. ELIMU NA MAFUNZO
Rais
Dkt. Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya msingi Chato
mwaka 1967 na kumaliza mwaka 1974. Mwaka 1975 alianza masomo ya
sekondari katika Shule ya Seminari ya Katoke Mkoani Kagera. Mwaka 1977
alihamia shule ya sekondari ya Lake iliyopo Mkoani Mwanza na kuhitimu
kidato cha Nne mwaka 1978. Kuanzia mwaka 1979 hadi 1981 alifanya masomo
ya kidato cha Tano na Sita katika shule ya Sekondari ya Mkwawa Mkoa wa
Iringa .
Mwaka
1981 hadi 1982 alisoma Chuo cha Ualimu Mkwawa na kuhitimu Stashahada ya
Ualimu ya Masomo ya Kemia na Hisabati. Mwezi Julai hadi Disemba mwaka
1983, Dkt. Magufuli alipata mafunzo ya kijeshi katika Jeshi la kujenga
Taifa kikosi cha Makutupora mkoa wa Dodoma. Mwezi Januari hadi Machi
1984 alihamishiwa kikosi cha mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa Makuyuni,
Arusha. Mwezi huo wa Machi alihamia kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa
Mpwapwa Dodoma na kumaliza mafunzo mwezi Juni 1984.
Mwaka
1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusoma Shahada ya kwanza
ya Sayansi na Ualimu akijikita katika masomo ya Kemia na Hisabati.
Alitunukiwa Shahada hiyo mwaka 1988. Mwaka 1991 hadi 1994 alisoma na
kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani ya Kemia iliyotolewa na Chuo
Kikuu cha Dar es salaam na Chuo Kikuu cha Salford cha Uingereza. Mwaka
2006 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya Shahada ya
Uzamivu katika Fani ya Kemia na kufanikiwa kuhitimu mwaka 2009.
3.0. UZOEFU WA NDANI YA SERIKALI
Baada
ya kuhitimu masomo yake ya Stashahada ya Ualimu, mwaka 1982 hadi 1983
Dkt. Magufuli alikuwa Mwalimu katika shule ya Sekondari ya Sengerema
iliyopo Mkoani Mwanza akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati. Mwaka
1989 alijiunga na Chama Cha Ushirika cha Nyanza Mkoani Mwanza, ambapo
alifanya kazi kama Mkemia Mkuu hadi mwaka 1995.
Mwaka
1995 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki Mkoa wa
Kagera. Baada ya Uchaguzi, Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin
William Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi nafasi
ambayo aliitumikia hadi mwaka 2000. Mwaka 2000 alichaguliwa kwa mara
ya pili kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki lakini mara hii
akipita bila kupingwa. Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Waziri kamili wa
Wizara ya Ujenzi hadi mwaka 2005.
Mwaka
2005 Rais Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya tatu kuwa mbunge wa
jimbo la Biharamulo Mashariki, kwa mara nyingine akipita bila kupingwa.
Baada ya uchaguzi, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 ambapo alihamishiwa Wizara ya
Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi hadi hadi mwaka 2010.
Mwaka
2010 Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya nne kuwa Mbunge lakini,
kufuatia mgawanyo wa majimbo uliofanyika, mara hii katika Jimbo jipya la
Chato. Baada ya uchaguzi, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia
mwaka 2010 hadi mwaka 2015.
Wakati
akiwa Mbunge na Waziri, Dkt. Magufuli amefanya shughuli na kushika
nyadhifa kadhaa ndani na nje ya nchi. Mwaka 2014, Dkt. Magufuli
alishiriki katika Bunge Maalum la Kutunga Katiba Mpya akiwa ni Mjumbe
wa Bunge hilo. Aidha, wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi aliweza kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza (Co-Chair) wa
Mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi
(UN-Habitat).
Tarehe
25 Oktoba, 2015 Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alichaguliwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tarehe 5 Novemba, 2015 aliapishwa
kushika rasmi wadhifa huo.
4.0. UZOEFU WA UONGOZI NDANI YA CHAMA
Rais
Dkt. Magufuli alijiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977.
Amekuwa Mwanachama mwaminifu na ameshika nafasi mbalimbali za uongozi
ndani ya Chama. Nafasi alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Mjumbe wa
Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya,
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa,
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Sambamba
na kushika nafasi mbalimbali za uongozi, Dkt. Magufuli mara zote
alijitoa kukitetea Chama na kuhakikisha kinapata ushindi. Alishiriki
kikamilifu kuwafanyia kampeni wagombea wa CCM katika Chaguzi Ndogo
zilizofayika katika majimbo ya Busanda, Biharamulo Magharibi na Igunga
na kupata ushindi. Katika Mkutano Mkuu wa CCM wa tarehe 11 – 12 Novemba
mwaka 2012, Dkt. Magufuli alikuwa miongoni mwa Mawaziri wachache
waliopata fursa ya kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya Chama ya Mwaka 2010 – 2015. Alielezea mafanikio ya
utekelezaji wa Ilani, hususan katika sekta ya miundombinu.
Tarehe
11 mwezi Julai, 2015 Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ulimchagua na kumteua
Dkt. Magufuli kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliinadi vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM (2015) na kukiwezesha Chama
kupata ushindi mkubwa. Tarehe 25 Oktoba, 2015 alichaguliwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nafasi hiyo imemwezesha kuwa Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa.