MATUKIO YA UZINDUZI WA UHAMASISHAJI WANANCHI KUJIUNGA MFUKO WA AFYA YA JAMII(CHF)WILAYANI KILINDI

November 19, 2014
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya Mkoa wa
Tanga(NHIF)Ally Mwakababu kulia akimuelezea mikakati ya mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Mkuu wa wilaya ya Kilindi,Suleimani Liwowa kulia kwake kabla ya kufanya uzinduzi wa Uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii wilayani humo (CHF) zoezi ambalo linaendeshwa
na Meneja huyo na maafisa kutokana makao makuu na mkoani Tanga kwa muda wa siku kumi.

Mkuu wa wilaya ya Kilindi,Suleimani Liwowa akizungumza na viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Tanga(NHIF) na watumishi wa Halmashauri hiyo Idara ya Afya ofisini kwake kabla ya kuanza uzinduzi wa uhamasishaji wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii(CHF).




Afisa Uanachama wa Mfuko wa Bima ya Taifa Mkoa wa Tanga (NHIF) Miraji Swalehe akiwaelimisha waendesha pikipiki kwenye kijiji cha Muheza Kata ya Masagalu wilayani Kilindi juu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuweza kupata matibabu muda wote.

Katikati ni Mwanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF) tokea ulipoanzishwa wilayani humo akimuonyesha kadi zake Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Tanga(NHIF) Ally Mwakababu.


AFRICAN SPORTS YAVUTWA SHATI NA FRIENDS RANGERS WALAZIMISHWA SARE YA KUFUNGANA BAO 1-1,MKWAKWANI LEO

November 19, 2014
KIKOSI CHA FRIENDS RANGERS LEO.
NA MWANDISHI WETU, TANGA
TIMU za Soka Friends Rangers ya Dar es Salaam na African Sports “wanakimanumanu” leo zimeshindwa kutambiana baada ya kulazimishana sare ya kufungana bao 1-1,ikiwa ni muendelezo wa Michuano ya Ligi daraja la Kwanza inayoendelea kutimua vumbi kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mechi hiyo ilichezwa leo kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani na kushuhudiwa na wadau wa soka mkoani hapa kutoka maeneo mbalimbali.

 Katika mchezo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani huku timu zote zikionekana kushambuliana kwa zamu ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko Friends Rangers walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Iddi Ismaili baada ya kupokea krosi iliyopigwa na Credo Dancan upande wa magharibi.

Bao hilo liliweza kudumu mpaka timu zote zinakwenda mapumziko ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi kutokana na timu kufanya mabadiliko kwa baadhi wa wachezaji wake hali ambayo ilipelekea kucheza kwa kujiamini na kucheza kwa umakini ikiwemo mashambulizi ya hapa na pale.



 Wakionekana kujipanga vizuri,Friends Rangers waliweza kutulia na kuanza kufanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa African Sports kwa dakika kadhaa lakini bahati haikuweza kuwa yao baada ya wachezaji wake kupiga mashuti makali yaliyokuwa yakipaa juu ya lango la wapinzani wao hao.

Hata hiyo timu hiyo iliweza kuendeleza wimbi la mashambulizi langoni mwa African Sports mithili ya mbogo aliyejeruhiwa na hatimaye kuweza kupata bao la kusawadhisha katika dakika ya 84 kupitia Maulid Abasi ambaye alitumia uzembe wa mabeki wa wapinzani wao kupachika wavuni bao hilo.

Akzungumza mara baada ya kumalizika,Kocha wa Friends Rangers,Ally Yusuph Tigana alisema kuwa wanamshukuru mungu kwa kuweza kupata pointi moja wakiwa ugenini ambayo itawasogeza kwenye nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

     “Tunamshukuru mungu kuweza kupata pointi moja ugenini hii ni muhimu sana kwetu tutakwenda kujipanga ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri mechi yetu inayofuata “Alisema Tigana.

WATU 13 WATIWA MBARONI KWA MADAI YA KUHUSIKA NA MAUAJI YA KITETO

November 19, 2014


Polisi mkoani Manyara wanawashikilia zaidi ya watu 13 wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya wakulima na wafugaji yaliyotokea wiki iliyopita katika Kata za Matui na Kiperesa wilayani hapa.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki amesema bado wanaendelea na uchunguzi kabla ya kuchukua hatua ya kuwafikisha mahakamani watu hao.

 
“Hatuwezi kutaja idadi kamili wala majina yao ila ni zaidi ya watu 13 tunawashikilia, wanadaiwa kuhusika na tukio hilo la mauaji na baada ya uchunguzi wetu wahusika tutakaowabaini tutawafikisha mahakamani,” alisema.

 
Hata hivyo, jana na juzi hali ilikuwa shwari katika eneo hilo huku wakazi wilayani humo wakishuhudia helikopta ya polisi ikiwa na makamishna kutoka Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam ikizunguka angani kuendelea na ulinzi.

 
Naye, Mkuu wa Mkoa huo, Eraston Mbwilo akizungumza kwenye kikao cha ushauri cha mkoa, alisema chanzo cha mgogoro wa ardhi na mauaji hayo ya Kiteto yanasababishwa na baadhi ya watu kuhodhi ekari za ardhi bila ya kuwa na vibali.

 
“Hili suala la baadhi ya watu kudai kuwa Kiteto imegeuka kuwa Somalia siyo kweli, mgogoro wa Emboley Murtangos unasababishwa na baadhi ya watu kujimilikisha ekari nyingi za ardhi kiholela,” alisema Mbwilo na kuongeza:

 
“Unamkuta mtu anamiliki ekari zaidi ya 500 kiholela, huu ni ukiukwaji wa sheria, vijiji vina utaratibu wa kugawa maeneo, kwa nini wasiufuate?” alihoji.

 
Alisema kwa sasa hali ni shwari katika eneo hilo na wanaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa jamii ya wakulima na wafugaji ili kuhakikisha kuwa mauaji na vurugu hizo havitokei tena.