Malaika wamwagia sifa Mashauzi, Dully Sykes na Cassim Mganga

November 10, 2013


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
 
UONGOZI wa bendi ya Malaika, umejigamba kwa uwezo wa kundi la taarabu la Mashauzi Classic, sambamba na Cassim Mganga na Dully Sykes, wataosindikiza uzinduzi wao Novemba 15 katika Ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Michael Rocky, alisema tayari wamekubaliana nao juu ya kushiriki katika uzinduzi wa bendi yao.



"Tuliwaomba kama wasanii wenzetu, walikubali na kutuahidi kutoa burudani nzuri katika onesho hilo maalumu la kuzaliwa kwa bendi mpya," alisema.


“Tuna nyimbo sita zilizofaniwa mazoezi, mbili zimerekodiwa, nne bado hazijarekodiwa, zote zitasikika siku ya uzinduzi wa bendi yetu," alisema Mkurugenzi huyo.


Bendi hiyo ya Malaika inaongozwa na Mfalme Christian Bella, Katibu Mkuu ni Andrew Sekedia akisaidiwa na Emmanuel Karonji 'Totoo Zebingwa’.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

November 10, 2013

DIRISHA DOGO KUFUNGULIWA NOVEMBA 15
Usajili wa wachezaji kwa dirisha dogo kwa msimu wa 2013/2014 Tanzania Bara unafunguliwa Novemba 15 mwaka huu na utafungwa rasmi Desemba 15 mwaka huu.

Kwa mujibu wa kanuni, klabu zenye fursa ya kusajili wachezaji katika dirisha dogo ni zile ambazo hazijatumia nafasi zote 30 za wachezaji.

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zimemaliza duru la kwanza msimu huu. Duru za pili litaanza kutimua vumbi Januari mwakani.

Kwa mujibu wa Kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) matukio ya Novemba na Desemba ni dirisha dogo la usajili na mechi za kirafiki za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date.

Matukio mengine ni michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za VPL na michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika Nairobi, Kenya.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)