JERRY MURO APIGWA FAINI MILIONI 5

May 08, 2015

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF iliyoketi jumanne tarehe 5 Mei, 2015 imempiga faini ya sh. 5,000,00 (milioni tano), Afisa Habari wa klabu ya Yanga SC Jerry Muro kwa kutoa kauli za chuki, kisirani na uchochezi dhidi ya uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) nchini na TFF.

Akitoa utetezi wake mbele ya Kamati ya Nidhamu, Jerry Muro alikiri na kujutia kufanya kosa hilo na kudai ilitokana na ugeni wake katika uongozi wa michezo, kwa kuzingatia hilo kamati ilimuepusha na adhabu ya kufungiwa..

Kwa mujibu wa Ibara ya 53 (2)ya Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012, kwa kuidhalilisha TFF na Bodi yake ya Ligi mbele ya umma, kamati imemtoza faini ya sh. 5,000,000 (millioni tano), Jerry Muro na kuwaonya viongozi wengine wa familia ya mpira wa miguu kutojihusisha na vitendo vya matamshi ya aina hiyo.

Shitaka linalomhusisha mchezaji wa Yanga, Amissi Tambwe kumshika kwa kumdhalilisha mchezaji wa Simba SC Juuko Mursheed, na kiongozi wa Friend Rangers Hery Chibakasa wa Friends Rangers kuhamasisha vurugu katika mchezo wa timu yake na dhidi ya Majimaji ya Songea Januari 29, 2015, kamati imeahirisha mashitaka hayo mpaka tarehe nyingine itakapopangwa.

Kamati iliahirisha malalamiko dhidi ya Mohamed Hussein, Muhibu Kanu, Manfred Luambano, Venance Joseph, Mussa Senyange, Saleh Ali, Shafii Maganga na Ismail Salim baada ya kupokea taarifa za udhuru zilizosbabishwa na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria ya mikoani.

RAIS TFF AAGIZA USIMAMIZI MECHI ZA MWISHO VPL

May 08, 2015

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewaagiza wasimamizi wa vituo vya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuhakikisha sheria na taratibu zote za mechi zinafuatwa.

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu huu 2014/2015 inafikia tamati kesho (Mei 9, 2015) ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani katika mechi ambazo ndizo zitakazotoa hatma ya timu zinazoshuka daraja.

Mechi hizo zitakuwa kati ya Ndanda na Yanga (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara), JKT Ruvu na Simba (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Azam na Mgambo Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Stand United na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), Kagera Sugar na Tanzania Prisons (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mbeya City na Polisi Morogoro (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

KUMRADHI WANAHABARI
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Mwesigwa Selestine ameomba radhi kwa vyombo kufuatia madai ya waandishi wa habari kupata usumbufu wakati wa utoaji wa Zawadi kwa Mabingwa na washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Mwesigwa alisema kwa niaba ya TFF anaomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata waandishi na wadau wote walioshindwa kushuhudia vema tukio hilo.

“TFF na FIFA vinatambua umuhimu na nafasi ya wanahabri na vyombo vya habari si tu katika kuutangaza mchezo, bali pia katika kutia chachu maendeleo ya mchezo wenyewe “ alisema Mwesigwa.

Hali mbaya ya hewa ilivuruga utaratibu uliokuwa umepangwa awali kuanzia itifaki ya shughuli za kabla na wakati wa mchezo na zile za utoaji tuzo.

Aidha Mwesigwa alisema TFF itaendelea kushirikiana vema na jumuiya ya wanahabari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wana mazingira mazuri wanapofanya kazi kwenye matukio ya mpira wa miguu.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
UNESCO, SERIKALI WATIA SAINI MRADI WA MAFUNZO YA TEHAMA KWA WALIMU

UNESCO, SERIKALI WATIA SAINI MRADI WA MAFUNZO YA TEHAMA KWA WALIMU

May 08, 2015
DSC_0023
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues (wa pili kulia), Balozi wa China nchini, Mh. LU Youqing (kushoto), Afisa utawala na fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha (kulia), Ofisa anayeshughulikia masuala ya Elimu Kitaifa wa UNESCO, Tumsifu Mmar pamoja na mkalimani wa Balozi wa China wakifurahi jambo wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome (hayupo pichani) akiwasili kwenye chumba cha mikutano Wizara ya Elimu kwa ajili ya hafla fupi ya kutiliana saini mkataba utakaowezesha kutekelezwa kwa mradi wa kuwezesha walimu wa Tehama vyuoni nchini. (Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na Modewji blog team
SERIKALI na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jana wametiliana saini mkataba utakaowezesha kutekelezwa kwa mradi wa kuwezesha walimu wa Tehama vyuoni nchini.
Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema mradi huo ni mkombozi mkubwa katika maandalizi ya kufundisha kwa kutumia Tehama nchini.
Alisema mpango huo wenye kuwezesha walimu kujifunza Tehama unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ambao ndio wamepitisha fedha zao UNESCO.
Katika utiaji saini huo ambapo Balozi wa China nchini Dk. Lu Youqing alikuwepo, katika jumla ya uhai wa mradi ambao ni miaka miwili , miundombinu ya ufundishaji masomo ya sayansi na hesabu katika vyuo vya walimu vya Monduli na Tabora itaboreshwa.
Katika mradi huo walimu watafundishwa elimu ya Tehama, namna ya kufundisha na kujifunza.
Katibu mkuu Mchome alisema kwamba vyuo hivyo viwili vitawezeshwa kuwa na mtandao ambao utaunganishwa na vyuo vingine vinane vya masomo ya sayansi na hesabu kwa ajili ya kubadilishana taaluma.
Pia vyuo hivyo vitawezeshwa kuandaa programu zenye kuelezea mfumo wa utoaji huduma za Tehama kwa ajili ya walimu wa masomo ya sayansi na hesabu.
DSC_0037
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues (katikati) akisalimina kwa furaha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome (kulia) na kushoto ni Balozi wa China nchini, Mh. LU Youqing (aliyeipa mgongo kamera).
Profesa Mchome alisema ili taifa liweze kusonga mbele katika mpango wake wa kufundisha kwa kutumia Tehama ni vyema kuandaa walimu na fedha za China kupitia Unesco zitasaidia maandalizi hayo.
“Tunaamini tukiwekeza katika vifaa vya kupromoti Tehama, walimu wakifundishwa na kuandaliwa vyema, wataenda kusaidia kufundisha na kuwezesha matumizi ya Tehama katika shule zao.” Alisema Profesa Mchome.
Alisema japo zipo program ndogo nyingine , program waliyotia saini jana ilikuwa kubwa na yenye tija itakayoimarisha ubora wa elimu kwa kuwapa wanafunzi elimu ya kujitegemea, elimu yenye kuwakwamua kiujuzi na kuutumia ujuzi huo kwa maendeleo yao na taifa.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa barani Afrika ambayo mapema wametambua thamani ya kufundisha kwa njia ya Tehama ili kuboresha elimu na mfumo wa elimu.
Taasisi zitakazohusika na mradi huo ni pamoja na Chuo Kikuu Huria (OUT) na Taasisi ya Elimu nchini(TIE) kwa kuratibiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
DSC_0074
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues (katikati) pamoja na Balozi wa China nchini, Mh. LU Youqing (kushoto) kabla ya kutiliana saini mkataba huo.
DSC_0080
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues akizungumza jambo kabla ya kusaini mkataba huo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome na Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO, Dr. Moshi Kimizi. Waliosimama wakishuhudia tukio hilo kutoka kushoto ni Joel Nanauka wa UNESCO, Afisa tawala msaidizi wa UNESCO, Rahma Islem, Afisa mipango wa utamaduni wa UNESCO, Rehema Sudi, Balozi wa China nchini, Mh. LU Youqing, Ofisa anayeshughulikia masuala ya Elimu Kitaifa wa UNESCO, Tumsifu Mmar pamoja na Afisa utawala na fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha.
DSC_0084
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome wakitiliana saini mkataba utakaowezesha kutekelezwa kwa mradi wa kuwezesha walimu wa Tehama vyuoni nchini unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China. Wanaoshuhudia tukio hilo waliosimama ni Balozi wa China nchini Tanzania, Mh. LU Youqing (wa pili kushoto), Ofisa anayeshughulikia masuala ya elimu kitaifa wa UNESCO, Tumsifu Mmar (wa pili kulia), Afisa mipango wa utamaduni wa UNESCO, Rehema Sudi (kushoto), Afisa utawala na fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha na Kulia aliyeketi ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO, Dr. Moshi Kimizi.
DSC_0086
Zoezi la kusaini mkataba likiendelea.
DSC_0089
Wakifurahi kwa pamoja mara baada ya zoezi la kutia saini kukamilika.
DSC_0090
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome wakibadilishana hati za mkataba utakaowezesha kutekelezwa kwa mradi wa kuwezesha walimu wa Tehama vyuoni nchini unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Balozi wa China nchini Tanzania, Mh. LU Youqing(wa pili kushoto) pamoja na Afisa utawala na fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha (kulia).
DSC_0091
DSC_0103
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues akizungumza jambo baada ya kutiliana saini mkataba huo.
DSC_0068
Afisa utawala na fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha (kulia) akizungumza jambo na Afisa wa ubalozi wa China (katikati) na Kushoto ni Afisa Utawala msaidizi wa UNESCO, Rahma Islem.

KITANDULA ATAKA WALIMU KUONGEZA BIDII DARASANI

May 08, 2015


NA SALUM MOHAMED,MKINGA.
 
MBUNGE wa jimbo la Mkinga, Dustun Kitandula, amewataka walimu shule za msingi na sekondari Wilayani hapa kuzidisha bidii ya ufundishaji darasani lengo likiwa ni kufuta alama ziro.

Akizungumza katika wiki ya Elimu iliyoadhimishwa Kiwilaya Wilayani humo jana, Kitandula alisema jitihada zaidi za walimu zinahitajika ili kuziwezesha shule zao kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa.

Alisema kipindi cha miaka ya nyuma shule za Mkinga zilikuwa zikishika nafasi za mwisho kimkoa na kitaifa na hivyo sasa walimu  kuonyesha bidii zao darasani ikiwa na panmoja na kuwa na mahusiano mazuri za wazazi wa wanafunzi.

“Tunatambua kuwa walimu wako na changamoto nyingi shuleni na nje ya shule----changamoto hii iwe chachu ya kufaulisha wanafunzi  na kufuta alama  ziro” Alisema Kitandula

Alisema Wilaya ya Mkinga mbali ya kuwa changa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu lakini inaweza kupiga hatua mbele katika maendeleo kwa kuwandaa vijana katika elimu ili kuweza kuinua maendeleo ya Mkinga baadae.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Afisa elimu Sekondari Wilaya ya Mkinga, Omary Kombo, aliwataka wazazi na walimu kuhakikisha ujenzi wa maabara unakamilka kama ulivyopangwa.

Alisema kuwepo kwa maabara kila shule kutasaidia wanafunzi kusoma kwa vitendo pamoja na kufanya vizuri katika masomo yao ya sayansi na kuondosha uhaba wa walimu wa somo hilo.

Alisema Wilaya ya Mkinga iko na uhaba wa walimu wa somo la sayansi jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kufanya vibaya katika mitihani yao ya Taifa.

“Wilaya ya Mkinga iko na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi----nawaomba wanafunzi muliopo hapa jikiteni katika somo hili ili kuja kuwasaidieni ndugu zenu hapo baadae” alisema Kombo na kuongeza

“ Nanyi wazazi tushikamane kuwabidiisha vijana wetu kukosa masomo shuelni kwani huko nje kuna vishawishi vingi kama uvuaji wa samaki katika bahari yetu tunayopakana nayo” alisema

Aliwataka walimu kuwa na ushirikiano na wazazi pamoja na kamati zao ili kuweza kuleta maendeleo ya wanafunzi pamoja na mazingira ya shule na kumaliza majengo ya maabara.

                             


Mwanafunzi wa shule ya Sekondari  ya Gombero Wilayani Mkinga MkoanI Tanga, Mwabai Heri, akionyesha utaalamu wa kuchanganya kemikali za maabara wakati wa sherehe za  wiki ya Elimu Wilayani Mkinga leo asubuhi.


Mwanafunzi wa shule ya Sekindari ya Mapatano Wilayani Mkinga Mkoani Tanga, Haruni Justics, akionyesha utaalamu wa kuchanganya kemikali za maabara wakati wa sherehe za wiki ya Elimu Wilayani Mkinga juzi asubuhi.



Wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari Wilayani Mkinga Mkoani Tanga, wakisherehekea wiki ya elimu iliyofanyika kiwilaya Wilayani humo leo asubuhi.