WAZIRI SULUHU KATIBA MPYA INALENGA KUIJENGA TANZANIA YA SASA NA IJAYO

September 23, 2013

NA SUSSAN UHINGA,TANGA.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya  Makamu wa Rais Muungano,Samia Suluhu amesema uandikaji wa katiba mpya unalenga kuijenga Tanzania ya sasa na siku zijazo hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa makini katika kila hatua ili kuweza kufanikisha mchakato huo.

Suluhu alitoa kauli hiyo  wakati akifungua Kongamano la Wazanzibar waishio bara katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa na kusema kwenye mchakato huo,tume ya mabadiliko imefanya kazi nzuri ya kusikiliza maoni ya wananchi kwenye maeneo na makundi mbalimbali.

Alisema ofisi yake imeona umuhimu wa kufanya tathimini ya miaka hamsini ya utekelezaji kwenye masuala ya muungano na kuweka mwelekeo mzuri wa kushughulikia masuala hayo ikiwemo maoni yaliyokusanywa na tume ya mabadiliko ya katiba.
   
“Kuna haja ya kupata maoni ya makundi haya kwa umahususi wao,katiba ni mali ya Taifa na dira yetu sote pamoja na mwongozo muhimu kwa taifa ili kuhakikisha linasonga mbele “Alisema Waziri Suluhu.

Aidha alisema kwa kuzingatia misingi hiyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kubaini kuwa hakuna aliye na haki zaidi ya mwengine katika mchakato huo na kueleza katiba bora ni ile inayotokana na watu pia inayoakisi matakwa ya watu kwa kulenga kujenga na kustawisha maisha ya wana chi husika.

Aliongeza kuwa wakati huu mchakato wa katiba mpya unaendelea ni vema kila mmoja wetu atambue kuwa nchi yetu ina bahati kubwa sana kwa mwenyezi mungu kuijalia mchakato huo kuwa  katika mazingira mazuri ya amani na utulivu kwani ni nchi chache sana duniani zilizojaliwa kuandika katiba zao katika mazingira hayo.

Alieleza kuwa nchi nyingi sana zinapofikia uamuzi wa kuwa na katiba mpya baada ya machafuko, vita, mifarakano na hata mapinduzi yanayosababisha umwagaji wa damu lakini watanzania wameamua kufanya jambo hilo kwa dhamira njema   na katiba inayokidhi mazingira ya sasa na kuharakisha maendeleo kwa wananchi wake.

    “Rai yangu kwa mkusanyiko huu na watanzania wote kwa ujumla ni kwamba tuzidi kuvumiliana  na kuwa watulivu katika mchakato huu na kila mmoja wetu aweke mbele maslahi ya taifa  na katiba tunayoiandaa sasa iwe msingi mkuu wa kudumisha amani,mshikamano na umoja wa taifa letu kwa kizazi cha sasa na kijacho “Alisema Suluhu.
Mwisho.

PAMBANO LA AZAM, YANGA LAINGIZA MIL 138/-

September 23, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Azam na Yanga lililochezwa jana (Septemba 22 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 138,188,000.

 Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 33 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 walikuwa 24,020.

 Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 33,065,409.1 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 21,079,525.42.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 16,812,919.89, tiketi sh. 5,022,342, gharama za mechi sh. 10,087,751.93, Kamati ya Ligi sh. 10,087,751.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,043,875.97 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,923,014.64.

Mechi iliyopita ya VPL kwenye uwanja huo kati ya Simba na Mbeya City iliingiza sh. 123,971,000
.

MECHI YA TOTO, POLISI DOM KUPIGWA J2

September 23, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Mechi namba 12 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Toto Africans na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza imesogezwa mbele kwa siku moja.

Timu hizo za kundi C sasa zitapambana Jumapili (Septemba 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo ili kupisha mechi namba 10 kati ya Pamba na Stand United FC ya Shinyanga itakayochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu).

Mechi nyingine za kundi hilo zitakazochezwa Jumamosi ni Mwadui na Polisi Tabora (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) wakati Kanembwa JKT na Polisi Mara zitacheza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.