KAMATI YA BUNGE YA ARDHI,MALIASILI NA MAZINGIRA YAVUTIWA NA UBUNIFU WA SHUGHULI ZA KITALII HIFADHI YA TAIFA YA ZIWA MANYARA.

January 24, 2018
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa),Allan Kijazi akizungumza kwenye kikao cha  wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Mazingira iliyofanya ziara ya kikazi kwenye Hifadhi ya Taifa  Ziwa Manyara mkoa wa Arusha,kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Japhet Hasunga.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Millanzi akizungumza kwenye kikao na kamati hiyo,kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Japhet Hasunga na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo,Kemilembe Lwota akifatilia kwa makini.

Mbunge wa jimbo la Sumve mkoa wa Mwanza,Richard Ndassa(kushoto),Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Japhet Hasunga(katikati) na Meneja Mawasiliano wa Tanapa,Pascal Shelutete wakiwa ndani ya Hifadhi hiyo.

Meneja Ujirani Mwema wa Tanapa,Hemed Mbugi akitembea juu ya daraja linalo ‘bembea’ ambalo ni moja kivutio kwa watalii wa nje na ndani.

Mbunge wa jimbo la Mtama mkoa wa Lindi  akifurahia  daraja linalo ‘bembea’ ambalo ni moja kivutio kwa watalii wa nje ya nchi na ndani.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Kemilembe Lwota  akitembea juu ya daraja hilo.

Meneja Mawasiliano wa  Tanapa,Pascal Shelutete naye hakua nyuma kutembea juu ya daraja hilo ambalo limeongeza shughuli za utalii kwenye hifadhi hiyo.

Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Mazingira wakiwa juu ya daraja maalumu lililojengwa kuwawezesha watalii kuwaona wanyama aina ya Viboko na aina mbalimbali za ndege.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Japhet Hasunga akifurahia mandhari ya daraja linalomwezesha mtalii kuona vizuri eneo la Ziwa Manyara.
Dk. Kigwangalla, hiyo wizara ina dhamana kubwa, usiichukulie poa!

Dk. Kigwangalla, hiyo wizara ina dhamana kubwa, usiichukulie poa!

January 24, 2018
Dk. Hamisi Kigwangalla, Mbunge wa Nzega Vijijini alipoteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii tarehe 7 Oktoba 2017 kutoka kuwa Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wachambuzi wengi wa mambo ya siasa na wa sekta ya maliasi waliona ametwikwa mzigo mzito katika kipindi muhimu ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imejizatiti kupambana na ufisadi na ubadhirifu. Sekta ya Maliasili ina mambo mengi na changamoto zake nyingi zinajulikana. Hakika Dk. Kigwangalla mwenyewe alionesha kutambua hilo alipowataka watanzania kuendelea kumuombea dua mara tu baada ya kupata taarifa za uteuzi wake kutekeleza majukumu yake mapya. Lakini katika utendaji wake miezi hii michache ya wadhifa wake huu mpya, wachambuzi hawana budi kujiuliza kama dua tu za watanzania zinatosha na kama kweli Dk. Kigwangalla ametambua nini kiini halisi cha changamoto za Sekta ya Maliasili hadi kuifanya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa kaa la moto hadi kufikia kufikia kuongozwa na mawaziri 13 ndani ya miaka 29. Labda anafahamu kuwa sekta hii ina mapato makubwa sana kutoka rasilimali za maliasili na utalii hivyo kuwa na maslahi kwa watu wengi hasa wafanyabiashara na wanasiasa na hivyo kusababisha tuhuma zisizoisha kuhusu rushwa na ufisadi. Kashfa za uuzwaji wa pori la Loliondo, kuuzwa kwa hoteli za serikali kwa bei ya kutupa, uuzwaji wa vitalu na biashara haramu ya pembe za ndovu ni baadhi tu kwenye orodha ndefu ya yanayozungumziwa vibaya juu ya sekta hii. Pia labda atakumbuka kashfa kubwa iliyotokana na Operesheni Uhai lililokuwa na lengo la kutukomeza vitendo vya ujangili na pia atakumbuka Anthony Diallo, aliyeshikilia wizara hiyo hapo awali aliwahi kusema kuwa hizara hiyo “imezungukwa na watu ambao wana mambo yao wanafanya” ikiwemo watendaji kumtengenezea majungu baada ya yeye kama waziri kuwabana kwenye biashara yao ya magogo. Pia hapo awali tembo wengi sana waliuawa na uwindaji haramu ulishamiri huku watendaji wakionekana kutofanya yanayohitajika ili kukabiliana na tatizo. Kwa maani hiyo, waziri yeyote aingiapo Wizara ya Maliasili na Utalii akithubutu kupambana na rushwa na ufisadi, basi ajue anatengeneza maadui wa ndani wakishirikiana na wenye maslahi binafsi huko nje ya wizara. Lakini kama kweli anayatambua haya na mengine mengi, mbona utendaji wake Dk. Kigwangalla unaonekana kama anataka kuingia kwenye mtego ambao waliomtangulia walifanya? Je, waziri huyu anategemea kupita njia ile ile waliyopita wenzake na kupata matokeo tofauti? Mara tu alipoanza majukumu yake mapya, alikutana na kazi ya wanamtandao wanaolinda maslahi ya wachache kwenye sekta ya maliasili iliyosambazwa mitandao ya kijamii: "BREAKING NEWS Mkakati mkali umeandaliwa na Waziri Kigwangalla, na timu yake ili kuzififisha taarifa zote za magazeti na televisheni juu ya kuwapo kwa makundi makubwa ya mifugo Loliondo. Taarifa za uhakika ni kuwa Waziri ameshauriwa afike Loliondo haraka iwezekanavyo ili apate picha za kuonyesha hakuna mifugo. Yote hii ni katika kusafisha hali ya hewa kutokana na agizo lake batili la kuruhusu mifugo kuivuruga Loliondo na pia Hifadhi ya Taifa Serengeti. Waziri atakuwapo huko kwa siri kubwa, akiwa na timu ya waandishi hasa wapigapicha wa televisheni. Ziara hii atatumia magari mawili hivi. Zitapigwa picha mahali kusikokuwa na mifugo na kuwaaminisha wananchi kuwa Loliondo na Serengeti hakuna mifugo. Atataka kuonyesha kuwa waandishi ni waongo! Usiku huu alitarajiwa kulala hoteli ya Acacia, Karatu, tayari kwa safari ya kesho Loliondo. Naambiwa tayari maandalizi yote yamekamilika hapo hotelini. Huu ndio ushauri aliopewa na washauri wake, Gambo, Nasha na wengine wa aina yao. Simameni imara kutetea uhifadhi. Usiku mwema.” Dk. Kigwangalla inambidi afikirie ‘nje ya boksi’ kama anataka kufanikiwa kuijenga Wizara hii kama dhamana aliyopewa na Mh. Rais. Alipopokea uteuzi huu alikuwa ana kati ya mawili: aidha ajiunge na mtandao wa ufisadi kwenye sekta ya maliasili au apambane na rushwa. Inavyoonekana, ameamua na kuchagua kupambana na vitendo viovu. Hivyo basi, hana budi kufanya tofauti na haya ni baadhi ya mikakati ambayo anaweza kuitumia: 1. La kwanza, afahamu fika hawa wanamtandao wabadhirifu katika sekta ya maliasili hawataacha kupambana naye eti kisa tu anakwenda na kasi ya mheshimiwa Rais ya kupambana na ufisadi na rushwa. Mtu akiwa anakula chake, ukitaka kumpokonya atapambana na yeye akishikilie kwa nguvu zote! Ndivyo wafanyavyo hawa ndugu zetu walio ndani ya wizara wakishirikiana na wafanyabiashara katika sekta hii. Hivyo basi, lazima awaoneshe hawa kuwa vita hii ni endelevu na amewatambua kuwa wao ni vikwazo. Morali yake ndiyo itashusha morali ya wasiotakia sekta hii mema maana wao watafahamu fika kuwa si tu Mheshimiwa Rais yuko nyuma yake, bali taifa nzima. 2. Kuna haja ya kuonge faragha na Mheshimiwa Rais juu ya vikwazo hivi apewe rungu zaidi kusafisha hii wizara. Malengo yake, ya wizara yanaendana na yake ya Rais na agenda ya serikali ya awamu ya tano. Sababu moja kwa nini kuna watendaji wenye viburi ni kwa sababu kama wengi wao husema “sisi siku zote tupo Mawaziri huja na hutuacha hapa!” Muda umefika kuonesha kuwa sasa upo uwezekano mkubwa waziri akabaki n awatendaji wakaondolewa kama si waaminifu! Mtandao wa kifisadi kamwe hauwezi kuvunjwa kwa kuwepo na uwoga kuwa watendaji hawawezi kubadilishwa. 3. Kama ‘mashine ya mawasiliano’ ndani ya Wizara nayo imetekwa na wanamtandao hawa na ndiyo wanashirikiana na waandishi wa habari wasio wazalendo kutendeneza mizengwe na kupika majungu ili waziri aondolewe? Basi hakuna budi waziri huyu kuhakikisha ana kuwa na mbinu mbadala za kufikisha taarifa muhimu kwa wananchi hadi pale watendaji wanaomuhujumu watakapobainika na kushughulikiwa. 4. Waziri akaribishe maoni kutoka kwa walio chini ya utawala wa juu wa wizara ya jinsi waonavyo kinatakiwa kifanyike kurudisha siyo tu heshima ya wizara bali pia kuiweka sekta nzima ya maliasili na utalii katika hali ya kuaminika na kuwa shirikishi kama vili ilivyolengwa kwenye dira na dhima ya wizara. Sambamba na haya, kuwe na mpango maalum wa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na watendaji wa serikali ambao ni wachapakazi na waadilifu. Muda umefika sasa kurudisha utamaduni wa wale wanaofanya mema kuthaminiwa na wabadhirifu kuaddibiwa. Kuna mengi zaidi Waziri anaweza kufanya ila kwa muda huu, haya ndiyo ya msingi. Akichelewa, yatamkuta ya mawaziri waliyopita.
Baadhi ya kurasa za mbele za magazeti zilizochapishwa juu ya Waziri Dk.Kigwangalla
-- Andrew Chale Blogger Personality | Journalist | Activist | Online Editor dewjiblog | Comedian |Volunteer Red Cross | Sauti za Busara & ZIFF Festivals 2007 to present. www.modewjiblog.com Email: andrewchale@gmail.com chalefamily@yahoo.com Phone: +255719076376 / +255767076376 / +255688076376 Telephone: +255222122830 Fax: +255222126833 Golden Jubilee Towers, Ohio Street,20th Floor Po Box 20660, Dar es Salaam,Tanzania
Helioum One yagundua heliamu ya futi za ujazo bilioni 98.9

Helioum One yagundua heliamu ya futi za ujazo bilioni 98.9

January 24, 2018
Kampuni ya uchunguzi na utafiti wa madini, Helium One, ambayo kwa sasa inafanya utafiti wa gesi ya heliamu mkoa wa Rukwa imegundua kuwapo kwa futi za ujazo bilioni 98.9 za gesi hiyo katika maeneo iliyokwishafanyia uchunguzi.
Hayo yalielezwa katika warsha ya siku moja iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na kuratibiwa na Idara ya Jiolojia ya chuo hicho, Helium One na Chuo Kikuu cha Oxford.
Akizungumza katika warsha hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Helium One, Thomas Abraham-James, alisema kwamba kampuni yao imetafuta leseni 23 za uchunguzi na kwamba nyingine tatu zimeombwa.
Alisema kwamba leseni hizo zote zinamilikiwa na kampuni hiyo kwa asilimia 100 na kwamba ina haki za kipekee za gesi hiyo ya heliamu .
Pamoja na kutoa taarifa hiyo,alisema lengo la kuwa na warsha ni kuwaita wataalamu na wadau mbalimbali wa hapa nchini na kimataifa kubadilishana uzoefu na taarifa zilizopo kuhusu gesi hiyo na kuangalia fursa zinazoambatana na uwapo wa gesi hiyo katika harakati za kitaifa za kuwa na taifa la viwanda.
“Helium One inaamini kwamba kuna fursa kupitia utafiti huu kuweza kutengeneza utaalamu wa kiwango cha juu na utaalamu wa hapa nchini juu ya uendelezaji wa gesi hiyo. Tutaendelea kujenga uhusiano na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuweza kubadilishana elimu, kutoa mafunzo kwa wanafunzi na maofisa wizara ya madini na kutengeneza mpango wa ufadhili wa masomo,” alisema.
Kwa mujibu wa Abraham-James, warsha hiyo ilihudhuriwa na wanasayansi waandamizi wa gesi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza na Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam,UDSM, watu wenye mamlaka na maamuzi, wadau wa maendeleo, watengeneza sera kutoka serikalini, watafiti na sekta binafsi.
Aidha kampuni hiyo imetoa ufadhili wa masomo ngazi ya shahada ya uzamili kwa wanafunzi wawili wa UDSM kusoma katika Chuo Kikuu cha Oxford , ikiwa ni sehemu ya kuingiza utaalamu wa hali ya juu wa kisayansi kwa watanzania na pia kuendeleza uhusiano mzuri kati ya Helium One na UDSM.
Wakati wa warsha hiyo, Profesa John Machiwa, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, Prof Cuthbert Kimambo, alisema kwamba jukwaa hilo ni jema kwa wanafunzi, wakufunzi na Chuo kizima kutafuta njia ya kuona namna ya kushirikiana na Helium One.
“Tunaweza kufanyakazi pamoja na kunoa taaluma na pia kupata utaalamu katika utafiti wa heliamu uzalishaji na usafirishaji wake,” alisema.

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI ZA WILAYA MKOA WA MARA WAIMWAGIA SIFA AGPAHI

January 24, 2018
Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoa wa Mara wamelipongeza Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa kutekeleza kikamilifu mradi wa “Boresha” unaotoa huduma za kinga, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi mkoani humo.
Pongezi hizo zimetolewa Januari 23,2018 na Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoa wa Mara, Charles Kitamuru Chacha ambaye ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Rorya wakati akifunga mafunzo kuhusu taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili ‘Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC)’.
Mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili yaliyoanza Januari 22,2018 hadi Januari 23,2018 yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mwembeni na kuhudhuriwa na wakurugenzi na viongozi wa timu za afya za mikoa na wilaya.
Mwenyekiti huyo wa wakurugenzi alisema shirika la AGPAHI limekuwa msaada mkubwa katika sekta ya afya kwenye halmashauri za wilaya mkoani humo hususani katika miradi yake ya Ukimwi na kusisitiza kuwa halmashauri zote zitaendelea kuunga mkono shughuli zinazofanywa na AGPAHI.
“Kwa niaba ya wakurugenzi wenzangu nikiwa kama mwenyekiti wa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani hapa, natoa shukrani za pekee kwa wadau wetu AGPAHI na Watu wa Marekani kupitia CDC kwa shughuli mnazofanya kufanikisha huduma za kinga, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi”, alieleza Chacha.
“Shirika hili limekuwa la mfano katika masuala ya Ukimwi na kila mtu mkoani hapa amekuwa na mtazamo chanya na AGPAHI, ndiyo maana tumekuwa tukiwashirikisha hata kwenye vikao vyetu vya mkoa ikiwemo Baraza la Ushauri la mkoa (RCC) na kuwapa nafasi ya kueleza mambo wanayofanya”,aliongeza Chacha.
Aidha alitumia fursa hiyo kuziomba halmashauri za wilaya kutumia vizuri fedha za wafadhili shilingi bilioni 7.2 zilizotolewa na AGPAHI mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Boresha mkoani Mara huku akisisitiza uwasilishwaji wa taarifa za mradi kwa wakati.
Naye Meneja wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele alizishukuru halmashauri za wilaya na serikali ya mkoa wa Mara kwa ushirikiano wanaotoa katika kuhakikisha kuwa malengo ya shirika hilo kutekeleza miradi ya Ukimwi yanafanikiwa.
Kwa upande wake, Afisa Ruzuku Mwandamizi wa shirika la AGPAHI, Leticia Gilba alisema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wakurugenzi wa halmashauri na timu za afya za mkoa na wilaya kuhusu namna ya kutumia fedha za mfadhili sawa sawa na matakwa na makubaliano kati ya AGPAHI na serikali ya Marekani.
Alisema miongoni mwa mada zilizotolewa wakati wa mafunzo hayo kuwa ni vigezo na masharti ya mkataba wa utekelezaji wa mradi wa Boresha, taratibu za matumizi ya fedha za wafadhili, uandaaji wa ripoti na viambatanisho sahihi vya malipo pamoja na utunzaji wa rasilimali. 
Washiriki wa mafunzo hayo walikuwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya Mji wa Bunda na Tarime Mji, Manispaa ya Musoma, Bunda Vijijini, Butiama, Musoma Vijijini, Rorya,Tarime Vijijini na Serengeti na timu za afya za mkoa na wilaya.
ANGALIA PICHA WAKATI WA KUFUNGA MAFUNZO 
Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya 9 za mkoa wa Mara, Charles Kitamuru Chacha akizungumza wakati wa kufunga mafunzo kuhusu taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili "Watu wa Marekani kupitia CDC" katika ukumbi wa Mwembeni uliopo katika manispaa ya Musoma.
Chacha akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia mambo waliyojifunza ili kuboresha utendaji kazi kwenye maeneo yao.
Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Mara, Dk. Oning'o Felix akilishukuru shirika la AGPAHI kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kuboresha huduma katika vituo vya afya.
Meneja wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele akizishukuru halmashauri za wilaya na uongozi wa mkoa wa Mara kwa kuendelea kushirikiana na AGPAHI kutekeleza miradi ya Ukimwi mkoani humo.
Afisa Ruzuku Mwandamizi wa shirika la AGPAHI, Leticia Gilba akiwapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuwa wasikivu katika mada zote zilizotolewa kwa muda wa siku mbili.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Mratibu wa AGPAHI mkoa wa Mara, Alio Hussein akitoa neno la shukrani wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
TRA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA KODI KWA WADAU MBALIMBALI

TRA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA KODI KWA WADAU MBALIMBALI

January 24, 2018
1
Afisa Muelimishaji Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rose Mahendeka akiwaelimisha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi na Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2017/18 katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018.
2
Msaidizi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Chama Siriwa akiwasilisha mada mbele ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi ya Majengo, katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018.
3
Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Valentine Baltazar akiwasilisha mada mbele ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Taratibu za Kiforodha, katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari, 2018.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-TRA
…………….
Na: Veronica Kazimoto
Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepongezwa kwa kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa ofisi za Serikali na Asasi za Kiraia kwa ajili ya kuongeza ufahamu na kuwa mabalozi wa masuala yanayohusu kodi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya elimu ya kodi kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) yaliyofanyika leo ofisini hapo,  Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Bw. Edwin Rutageruka amesema TRA inastahili kupongezwa kwa kazi inayoifanya ambayo imepelekea kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.
“Ni dhahiri kwamba, sasa hivi  TRA inafanya kazi kubwa ya ukusanyaji wa mapato na kutoa elimu ya kodi kwa vikundi na taasisi mbalimbali, hivyo, fursa hii tuliyoipata tuitumie vizuri ili kuongeza uelewa wa kutosha kuhusu kodi ili tuwe  mabalozi wazuri kwa wengine”, amesema Rutageruka.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania  Bi. Rose Mahendeka, akiwasilisha mada ya Kodi na Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 amesema,  kila mwananchi anajukumu la kudai risiti kila anaponunua bidhaa na kila mfanyabiashara anatakiwa kutoa risti kila anapofanya mauzo.
“Suala la kulipa kodi lipo kwa mujibu wa sheria hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kudai risiti wakati wote anaponunua bidhaa na vivyo hivyo kwa upande wa wafanyabiashara wanapaswa kutoa risiti kila wanapofanya mauzo”, amesisitiza Mahendeka.
Muelimishaji mwingine kutoka TRA aliyewasilisha mada kuhusu Kodi ya Majengo Bw. Chama Siriwa amewahimiza wafanyakazi hao wa TANTRADE kuwahi kulipa kodi ya majengo ya mwaka huu wa fedha 2017/18 ili kuepuka usumbufu usio wa lazima na msongamano wa watu ambao mara nyingi hujitokeza kulipa mwishoni.
“Watu wengi wana tabia ya kusubiri tarehe za mwisho kulipia kodi ya majengo suala ambalo linasababisha msongamano usio wa lazima na hivyo kuchelewa kupata huduma kwa wakati”, amefafanua Bw. Siriwa.
Siriwa ameongeza kuwa, Kodi ya Majengo hulipwa kuanzia mwezi Julai Mosi ya mwaka wa fedha husika hadi Juni 30 ya mwaka unaofuatia na kusisitiza kuwa muda huu ni muafaka kabisa wa wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo mpaka ifikapo tarehe 30 Juni, 2018.
Mamlaka ya Mapato Tanzania, katika kipindi cha miezi 6 iliyopita imefanya jumla ya semina 137 kwa wafanyakazi wa Serikali, Asasi za Kiraia, wafanyabiashara na vikundi mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu na kuongeza uhiari katika ulipaji wa kodi.
JAFO AKERWA NA UTENDAJI MBOVU ROMBO

JAFO AKERWA NA UTENDAJI MBOVU ROMBO

January 24, 2018
JAFO ROMBO (1)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa watendaji wa Halmashauri ya Rombo
JAFO ROMBO (2)
Ujenzi wa jengo la upasuaji linaloendelea katika Kituo cha Afya Karume wilayani Rombo
JAFO ROMBO (3)
Nyumba ya daktari inayojengwa katika Kituo cha Afya Karume wilayani Rombo
JAFO ROMBO (4)
Jengo la wodi ya wazazi inayojengwa  katika kituo cha Afya Karume.
…………………………………………………………………………………………….
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ameonyesha kukerwa na kutoridhishwa na kasi ya utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo na watendaji wake wa chini kwa kushindwa kwenda sambamba na kasi anayoitaka katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Hali hiyo ilijitokeza leo wakati Jafo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Amesema Halmashauri ya wilaya ya Rombo ni miongoni mwa Halmashauri zilizopokea fedha za awamu ya kwanza ya uboreshaji vituo vya afya lakini licha ya kupokea fedha hizo tokea mwezi Agosti mwaka 2017 bado wapo nyuma ukilinganisha na halmashauri zingine zilizopata fedha kwa wakati mmoja.
Akikagua kituo cha afya Karume , Waziri Jafo amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  kufanya kazi kwa weledi na kuwapa ushirikiano  wa kutosha watendaji walio chini yake ili waweze kumaliza kazi hiyo kabla Februari 25, mwaka huu.
Kadhalika, Jafo amewapongeza Mkuu wa wilaya ya Rombo Agness Hokololo na Katibu Tawala wake wa wilaya Asenga kwa kazi kubwa wanayofanya ya kusimamia maendeleo ya wilaya hiyo.

MRADI WA MAJI NA JENGO LA UZAZI ZAHANATI YA YOMBO/BAGAMOYO YAKWAMA

January 24, 2018
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo.

Wakazi wa kijiji cha Yombo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamelalamikia mradi wa maji uliofadhiliwa na Bank ya Dunia na kugharimu milioni 297, ambao haufanyikazi huku wakiwa hawanufaiki nao tangu ukamilike.

Aidha wamelalamikia kukwama kwa mradi wa jengo la uzazi, katika zahanati ya Yombo,ambalo limetumia kiasi cha sh.mil.55 na kuwekwa jiwe la  msingi na katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa,Abdulrahman Kinana tangu mwaka 2014.

Kilio hicho kimetolewa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ,wakati wa mkutano wa wananchi uliomwita diwani wa kata ya Yombo ,Mohammed Usinga kwenda kuwaeleza hatua zinazochukuliwa ili kukamilisha miradi hiyo .

Mkazi wa Yombo,Jabir Omary ,alisema inasikitisha kuona serikali na wafadhili wanatumia mamilioni ya fedha kwenye miradi ya maendeleo lakini haiendelezwi na haifanyikazi.

Alieleza mradi huo wa maji umetumia fedha nyingi ,hivyo ni jukumu la serikali kuisimamia ili ilete tija ndani ya jamii.Mkazi mwingine ,Abubakar Harubu alimtaka diwani wa kata hiyo pamoja na bodi ya maji ya kata kufuatilia na kusimamia kero hizo kwa maslahi ya wakazi hao.

"Mradi huu ni donda ,hauna manufaa ,;"Sisi hatutaki kusikia sijui mradi umerithishwa kutoka kwa diwani aliyepita ,tunachotaka kuona ni muendelezo wa miradi iliyoanzishwa kipindi cha nyuma iendelezwe na sio vinginevyo"

"Mradi huu umetumia mamilioni ya fedha ,jamani hata hamsikii uchungu wa fedha hizi ,yaani tanki la maji hadi linaweka uchafu ndani kutokana na kukosa maji,tunaomba viongozi wetu kutatua kero hizi za maji na afya" alisema Harubu.Kuhusu kukwama kwa jengo la uzazi kwenye zahanati ya Yombo,Jabir alisema akinamama wanadhalilika na kukosa huduma hiyo muhimu .

Alielezea kuwa ,zahanati hiyo pia ilikuwa kwenye mpango wa kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya lakini wanashangaa ujenzi hauendelezwi na kuelezwa kuna muongozo uliotolewa kuwa kunatakiwa hekari sita ndipo kujengwe kituo hicho.

Nae afisa tatibu wa zahanati ya Yombo,Donald Malamsha ,alisema makisio ya ujenzi ya jengo la uzazi ilikuwa ni sh.milioni 87 na hadi kufikia ujenzi ulipokomea imeshatumika milioni 55.

Malamsha alielezea fedha iliyokwisha tumika ni nyingi hivyo halmashauri na serikali iangalie changamoto zinazokwamisha mradi na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.Akielezea juu ya kero hizo,diwani wa kata ya Yombo,Usinga aliitaka bodi ya maji kusimama kidete ili watu wapate huduma ya maji.

Alisema atasimamia tatizo la transformer liweze kufanya kazi na kuagiza vituo vichache vyenye tija vifunguliwe na visivyofaa viache kwa sasa.Usinga ,aliwaasa wananchi kuacha kuhujumu mradi huo kwa kukata mabomba ,kuiba baadhi ya vifaa na kuharibu miundombinu na badala yake walinde miundombinu ya mradi ili udumu kwa muda mrefu.

Akizungumzia kuhusu jengo la uzazi ,Usinga alisema halmashauri imeshatenga sh.milioni 20 ili kukamilisha ujenzi huo wakati ikisubiri kupatikane eneo lenye hekari 4-6 la kujengwa kituo cha afya cha Yombo kwani eneo la sasa halikidhi mahitaji.

Mwenyekiti wa bodi ya maji ,Yombo ,Yahaya Omary alisema mradi huo umetekelezwa kwa fedha kutoka bank ya dunia ,ulianza ujenzi July 2013 na kukamilishwa Octoba 2015 lakini haufanyi kazi iliyotarajiwa .

Alikiri mradi huo kukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo transformer kutokuwa imara,pump kuwa na shoti za mara kwa mara ,mabomba kupasuka na kuibwa kwa baadhi ya vifaa.Yahaya aliongeza, bomba zilizotumika ni ndogo kulingana na mradi wenyewe na endapo mradi huo ungekamilika ungeweza kulisha watu zaidi ya 2,000.

Alifafanua kuwa ,mradi wa maji bado haujakabidhiwa rasmi kwa wananchi ila ulikabidhiwa kwa majaribio kwa miezi sita ambayo imepita huku kukiwa na changamoto lukuki ambazo zinapaswa kutatuliwa kabla ya kukabidhi .

Mwandishi wa habari hii,alimtafuta kwa mara kadhaa kwa njia ya simu mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu,kutolea ufafanuzi zaidi juu ya miradi hiyo ,hakupokea wala kujibu sms.

Mkutano huo uliazimia kuunda timu ya watu kumi ,ambayo itakwenda kufuatilia suala hilo katika ngazi na idara husika ili kupata ufumbuzi.
 Diwani wa kata ya Yombo wilayani Bagamoyo, Mohammed Usinga akizungumza na wakazi wa kijiji cha Yombo kuhusiana na baadhi ya miradi ya maendeleo isiyofanyakazi na mengine kushindwa kuendelezwa.(picha na Mwamvua Mwinyi)
 Jengo la wodi ya uzazi katika zahanati ya Yombo, Bagamoyo likiwa limekwama kwenye ujenzi na kuwekwa jiwe la msingi na katibu mkuu wa CCM Taifa ,Abdurahman Kinana mwaka 2014 .

Mradi wa maji uliofadhiliwa na bank ya dunia na kugharimu mamilioni ya fedha huko kata ya Yombo Bagamoyo, ambao haufanyi kazi iliyotarajiwa na wananchi hawanufaiki nao tangu ukamilike 2015.

MCHEZO WA MWADUI VS NJOMBE MJI WASOGEZWA

January 24, 2018
AZAM, YANGA KUPIGWA SAA 10 CHAMAZI 

Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018 kati ya Azam FC na Young Africans utachezwa saa 10 jioni Azam Complex Chamazi. 

Mchezo huo namba 115 utachezwa Jumamosi Januari 27, 2018.

Viingilio kwenye mchezo huo ni shilingi elfu kumi(10,000) kwa Jukwaa Kuu na shilingi elfu saba (7,000) kwa majukwaa ya kawaida. 

Waamuzi wa mchezo huo wote ni kutoka Dar es Salaam ambapo muamuzi wa kati ni Israel Nkongo akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Josephat Bulali na mwamuzi msaidizi namba mbili Soud Lila, mwamuzi wa akiba Elly Sasii wakati Kamishna wa mchezo huo ni Omar Abdulkadir. 

MCHEZO WA MWADUI VS NJOMBE MJI WASOGEZWA 

Mchezo namba 114 kati ya Mwadui FC ya Shinyanga na Njombe Mji ya Njombe uliokuwa ufanyike Ijumaa Januari 26, 2018 imesogezwa kwa siku moja kupisha mazishi ya aliyekuwa kocha msaidizi wa Mwadui Jumanne Ntambi. 

Mchezo huo sasa utachezwa Jumamosi, Januari 27, 2018.

Kocha huyo msaidizi wa Mwadui alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu kabla ya kufikwa na mauti.

CAF YATAJA WAAMUZI WATAKAOCHEZESHA MECHI YA YANGA NA SAINT LOUIS FC LIGI YA MABINGWA
Shirikisho la Mpira wa miguu Barani Africa CAF limetaja waamuzi watakaochezesha mchezo wa kwanza na mchezo wa pili wa Ligi ya mabingwa Africa kati ya Yanga ya Tanzania dhidi ya Saint Louis FC ya Seychelles.
Mchezo wa kwanza utachezwa Februari 10, 2018 uwanja wa Taifa na utachezeshwa na waamuzi kutoka Ethiopia na Kamishna wa mchezo akitokea nchini Namibia.
Mwamuzi wa kati atakuwa Belay Tadesse Asserese akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Tigle Gizaw Belachew na mwamuzi msaidizi namba mbili Kinfe Yilma Kinfe wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Amanuel Heleselass Worku na Kamishna Frans Vatileni Mbidi.
Mechi ya pili itakayochezwa Seychelles kati ya Februari 20 na 21,2018 itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar na kamishna atatoka Mauritius.
Mwamuzi wa kati atakuwa Andofetra Avombitana Rakotojaona akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina na mwamuzi msaidizi namba mbili Pierre Jean Eric Andrivoavonjy na mwamuzi wa akiba Hamada el Moussa Nampiandraza,kamishna wa mchezo huo Ahmad Nazeer Hossen Bowud.

WAAMUZI WA SUDAN KUSINI KUCHEZESHA SIMBA VS GENDARMERIE TNALE KOMBE LA SHIRIKISHO AFRICA
Waamuzi kutoka Sudan Kusini wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF kuchezesha mchezo wa kombe la Shirikisho kati ya Simba ya Tanzania na Gendarmerie Tnale ya Djobouti itakayochezwa Februari 21,2018 Uwanja wa Taifa.
Mwamuzi wa kati atakuwa Alier Michael James akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Abdallah Suleiman Gassim ,mwamuzi msaidizi namba mbili Gasim Madir Dehiya wakati mwamuzi wa akiba akiwa ni Kalisto Gumesi Simon Samson na Kamishna wa mchezo huo kutoka Botswana ni Mmonwagotlhe Edwin Senai.
Mchezo wa marudiano utakaochezwa Djibouti kati ya Februari 20 na 21,2018 wenyewe utachezeshwa na waamuzi kutoka Burundi na Kamishna wa mchezo atatokea nchini Rwanda.
Mwamuzi wa kati ni Eric Manirakiza akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Pascal Ndimunzigo,mwamuzi msaidizi namba mbili Willy Habimana,mwamuzi wa akiba Pacifique Ndabihawenimana na kamishna Gaspard Kayijuka.

WATANZANIA TISA KUCHEZESHA NA KUSIMAMIA LIGI YAMABINGWA NA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRICA
 Waamuzi nane kutoka Tanzania wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF kuchezesha mechi za Ligi ya Mabingwa Africa na Kombe la Shirikisho.
Waamuzi wanne wameteuliwa kuchezesha mchezo wa Ligi ya mabingwa kati ya Lydia Ludic Burundi Academic ya Burundi na Rayon Sports ya Rwanda.
Mwamuzi Mfaume Ali Nassoro atakuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Frank John Komba wakati mwamuzi msaidizi namba mbili atakuwa Soud Idd Lila na mwamuzi wa akiba Israel Omusingi Njunwa Mujuni huku kamishna wa mechi hiyo akitokea nchini Zimbabwe Gladmore Muzambi.
Mchezo huo utachezwa kati ya Februari 20 na 21, 2018 nchini Burundi.
Waamuzi wengine wanne wa Tanzania watachezesha mchezo wa Kombe la Shirikisho kati ya Masters Security Services FC ya Malawi dhidi ya Atletico Petroleos de Luanda ya Angola nutakaochezwa kati ya Febriari 20 na 21,2018 nchini Malawi.
Elly Ally Sasii atakuwa mwamuzi wa katikati kwenye mchezo huo akisaidiwa na Mwamuzi msaidizi namba moja Salim Mkono Mohamed na mwamuzi msaidizi namba mbili Ferdinand Chacha na mwamuzi wa akiba Alphonce Mwandembwa Emmanuel wakati kamishna wa mchezo huo atatokea Ethiopia Luleseged Gegashaw Asfaw.
Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF limemteua Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Ndugu Michael Richard Wambura kuwa Kamishna wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Africa kati ya Bidvest Wits ya Africa Kusini na Pamplemousses SC ya Mauritius utakaochezwa Februari 10, 2018 kwenye uwanja wa Johannesburg-Bidvest.
Wambura atasimamia mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutokea Seychelles.
Mwamuzi wa kati Nelson Emile Fred akisaidiwa na Hensley Danny Petrousse na James Fedrick Emile wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Allister Barra
Huu unakuwa ni muendelezo kwa CAF kuteua viongozi mbalimbali wa Tanzania kuwa makamishna wa mechi zinazoandaliwa na Shirikisho hilo.
Tayari Rais wa TFF Ndugu Wallace Karia licha ya kuteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya fainali za Africa kwa wachezaji wanaocheza ndani CHAN pia ameteuliwa mara mbili kuwa Kamishna wa mechi ya ufunguzi ya CHAN wenyeji Morocco walipocheza dhidi ya Mauritania Februari 13, 2018 na mchezo mwingine uliowakutanisha Namibia na Zambia uliochezwa Februari 22, 2018
Aidha mjumbe mwingine wa kamati ya utendaji Ahmed Iddi Mgoyi naye ameteuliwa na CAF kuwa kamishna wa mchezo wa Kombe la Shirikisho kati ya AFC Leopards ya Kenya dhidi ya Fosa Juniors ya Madagascar mchezo utakaochezwa kati ya Februari 9,10 na 11,2018 nchini Kenya.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF

WAZIRI WA NISHATI ARIDHISHWA NA KAZI YA UJENZI WA NJIA YA UMEME KUELEKEA STIEGLERS GORGE

January 24, 2018
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha Umeme wa msongo wa kV 33 inayojengwa kuelekea eneo litakalotumika kuzalisha Umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

Dkt. Kalemani aliyasema hayo mkoani Morogoro wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa kazi ya maandalizi ya ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2100 pamoja na kuzungumza na wananchi katika vijiji vinavyopitiwa na miundombinu hiyo ya kusafirisha Umeme.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Umeme wa Stiegler’s yanajumuisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya Barabara na usafirishaji Umeme kuelekea eneo la Mradi ili mradi huo mkubwa utekelezwe kwa ufanisi. 

Alieleza kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo ya usafirishaji umeme unatekelezwa na kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO na kwamba miundombinu hiyo inajengwa kutoka katika kituo cha kituo cha kupoza umeme cha Msavu hadi Mto Rufiji ambapo ni takriban kilometa 170.

“Kwa Vijiji ambavyo vinapitiwa na mradi huu wa njia ya kusafirisha umeme, wananchi watafungiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kama ilivyo katika vijiji vingine vinavyopitiwa na miradi ya usambazaji umeme vijijini na hakuna fidia kwa wananchi watakaopisha miundombinu hii,” alisema Dkt Kalemani.

Alisema kuwa, mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Februari mwaka huu mara baada ya Mkandarasi kupatikana na kwamba ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea eneo hilo la mradi umetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 80 na utakamilika mwezi Aprili mwaka huu.

Meneja Mradi wa Stiegler’s Gorge kutoka TANESCO, Florence Gwang’ombe, alisema kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme utaboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo hayakuwa na Umeme ikiwemo baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Morogoro, vijiji vya Matombo, Dakawa, Kisaki pamoja na kambi ya Maafisa wa Wanyamapori ya Matambwe.

Alisema kuwa, mradi unatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 6.1 hadi kukamilika kwake na kwamba nguzo zinazotumika katika mradi huo ni za miti na zege na katika sehemu nyingine umeme utasafirishwa kwa kutumia nyaya zitakazopitishwa ardhini.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alimpongeza Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya uamuzi wa kuanza kutekeleza mradi huo wa Stieglers Gorge ambao alisema kuwa utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini, utainua uchumi wa nchi kutokana na kuchochea uanzishwaji wa viwanda pamoja na maendeleo ya mtu mmoja mmoja kupitia shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( wa Nne kushoto) akikagua maeneo ambayo miundombinu ya usafirishaji umeme inajengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo na wengine ni watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO wakati alipokuwa katika kijiji cha Dakawa mkoani Morogoro kukagua miundombinu ya usafirishaji umeme inayojengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100.

Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100 ikiendelea. Kazi hiyo inatekelezwa na  kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.