BRIGEDIA JENERALI MABENA AWEKA JIWE LA MSINGI MAHANGA YA VIJANA KIKOSI CHA 824 KJ KANEMBWA

BRIGEDIA JENERALI MABENA AWEKA JIWE LA MSINGI MAHANGA YA VIJANA KIKOSI CHA 824 KJ KANEMBWA

May 08, 2024

 

Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.


Na.Alex Sonna-KAKONKO

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limeishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na majengo ili kuchukua vijana wengi wanaohudhuria mafunzo ya lazima kwa mujibu wa sheria pamoja na kundi la kujitolea

JKT ilikuwa na uwezo wa kuchukua vijana 5000 lakini kwa sasa inaweza kuchukua vijana 50,000 katika kundi hilo kwa wakati mmoja kutokana na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kutoa fedha.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, wakati akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.

Brigedia Jenerali Mabena amesema Serikali imekuwa ikiendelea kufanya hivyo toka kurejeshwa kwa mafunzo ya kundi la kujitolea.

"Ikumbukwe wakati mafunzo yale ya lazima yanarejeshwa JKT ilikuwa na uwezo wa kuchukua vijana 5000 tu lakini kwa sasa inaweza kuchukua vijana 50,000 katika kundi hilo kwa wakati mmoja,"amesema Brigedia Jenerali Mabena.

Amesema yote hayo yanatokana na JKT kuendelea kupewa fedha za maendeleo na Serikali.

Kuhusu kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Brigedia Jenerali Mabena,amesema wakati kikosi kinaanza kilikuwa hakina uwezo wa kuchukua vijana 1000 lakini kwa sasa kina chukua 4000 mpaka 5000.

"Na mimi niseme tu katika kikosi hichi tulichopo cha 824 Kanembwa Kakonko Mkoa wa Kigoma.Kikosi hichi tulikabidhiwa kutoka katika Kambi ya wakimbizi waliokuwa wanakaa hapa ilianza kuwa kiteule na baadae ikapewa hadhi ya kuwa kikosi,"amesema Brigedia Jenerali Mabena.

Amesema kikosi hicho wameendelea kukiongezea uwezo kwa kuweka mahanga ya kulala vijana pamoja na bwalo na miundombinu mingine ambayo itatumika katika kulea vijana.

Brigedia Jenerali Mabena amesema katika mwaka wa fedha ambao utaishia Juni 30,2024 kikosi hicho kimepewa Sh bilioni 1.47 ambapo fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kuhakikisha majengo yanakuwa sawa sawa.

Amesema katika fedha hizo kikosi kinaenda kutengeneza mahanga saba yenye uwezo wa kuchukua vijana 100 kila hanga moja.

"Kwa hiyo unaona tayari kutakuwa na ongezeko la vijana 700 katika ile idadi ya 4000 mpaka 5000,"amesema Brigedia Jenerali Mabena.

Amesema kuna kituo cha Kiteule ambacho kipo Misenyi Mkoani Kagera kwa ajili ya shughuli za ufugaji

Amesema kule wana Kilimo,ufungaji pamoja na Uvuvi ambapo kitatumika kama sehemu ya kufugia na vijana watakitumia kupata mafunzo.

"Unaona kwa jinsi ambavyo Serikali imeendelea kutoa fedha na miundombinu inaendelea kukaa sawa na kuchukua vijana wote kwa wakati mmoja,"amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi wa fedha JKT,Luteni Kanali Eveline Kibisa amesema kama Mjumbe wa kamati ya fedha za maendeleo wanawapongeza wakuu wa vikosi sehemu zote walizopita kwani majengo yamejengwa vizuri na yanathamani.

Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa namna ambayo imewezesha kwani wameweza kuwapatia fedha za kutosha ambapo katika kila kikosi wameweza kuongeza idadi ya vijana.

"Nitoe rai kwa wakuu wa vikosi kuendelea kuzisimamia vizuri fedha hizo ili angalau Serikali ikiona kuna matumizi mazuri ipate moyo wa kuendelea kusapoti."amesema Luteni Kanali Kibisa

Nay,Kamanda wa Kikosi cha 824 KJ, Luteni Kanali Mantage Nkombe,amesema katika kikosi hicho wamepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mahanga saba.

"Tumeona ni mafanikio kwa sababu tunaenda kuongeza wigo na namba ya Vijana kujiunga JKT Kanembwa inaenda kuongezeka zaidi ya awali,"amesema Luteni Kanali Nkombe

Amesema kupitia fedha za maendeleo wanaenda kutekeleza miradi hiyo kwa kutekeleza maagizo kutoka Makao Makuu

"Kwa kuhakikisha majengo yanakamilika kwa wakati kulingana na fedha iliyotumwa na kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa na majengo yanajengwa katika ubora na kwa muda sahihi,"amesema

Amesema wanataraji ifikapo 30 June 2024 majengo yatakuwa yamekamilika kwa ajili ya vijana wapya ambao watakuja kujiunga na JKT katika kikosi hicho.

Kuhusu faida watakayopata katika miradi hiyo,amesema:"Kimsingi ni faida na kijana anapata ujuzi na ujuzi hauzeeki na ni manufaa kwake na atatumia kujiongezea kipato".

Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akipokea taarifa ya ujenzi kabla ya kuweka wakati akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.
  
Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.



Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena,(kulia) akipiga makofi mara baada ya kuweka jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.Kushoto ni Kamanda wa Kikosi cha 824 KJ, Luteni Kanali Mantage Nkombe.

 

Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akikagua maendeleo ya ujenzi mara baada ya kuweka jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.



Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuweka jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.


Mkurugenzi wa fedha JKT,Luteni Kanali Eveline Kibisa,akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.




,akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la Msingi ujenzi wa Mahanga ya Vijana katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa,Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.

SERIKALI KUJENGA KITUO CHA KUPOZA UMEME NA SWITCHING STATION SONGWE- MHE. KAPINGA

May 08, 2024

 -- Lengo ni kuimarisha upatikanaji umeme mkoani Songwe

--- Uboreshaji wa miundombinu ya umeme unaendelea

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme itakayoboresha upatikanaji umeme mkoani Songwe ikiwemo ujenzi wa kituo cha umeme na switching station .

Naibu Waziri Kapinga amesema hayo tarehe 8 Mei, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Mbozi, Mhe. George Mwenisongole aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa Kituo cha upoza Umeme Kakozi, Tunduma utaanza.

Akijibu swali hilo Mhe. Kapinga alisema "Serikali kupitia mradi wa TAZA unaotekelezwa na TANESCO ipo katika hatua za awali za ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nkangamo (Tunduma) kilichopo takribani kilomita 28 kutoka Kijiji cha Kakozi, Mbozi. Ujenzi wa kituo hiki unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo kwa sasa mkataba kati ya TANESCO na mkandarasi atakayejenga kituo hiki tayari umeshasainiwa."

Ameongeza kuwa, kukamilika kwa kituo hicho cha Nkangamo (Tunduma) kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Kijiji cha Kakozi na maeneo mengine ya Jimbo la Mbozi.

Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme kwa ujumla mkoani Songwe, Kapinga amesema kuwa mkoa huo unapata umeme kutoka kituo cha Mwakibete kilichopo mkoani Mbeya ambapo laini hiyo ya umeme ni ndefu sana na kupelekea kutokea kwa changamoto za upatikanaji umeme mkoani Songwe.

Kutokana na hilo amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kujengwa switching station mkoani Songwe pamoja na kituo cha umeme kitakachojengwa kupitia mradi wa TAZA huku uboreshaji wa miundombinu ya umeme ukiendelea.

Akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Mhe. Margaret Sitta aliyetaka kufahamu ni lini kituo cha umeme cha Uhuru kitakamilika, Mhe. Kapinga amesema kituo kipo ukingoni kukamilika na hivyo kuboresha hali ya umeme wilayani Urambo.

MALIPO YA WATOA HUDUMA HUZINGATIA MIKATABA YA ZABUNI

May 08, 2024


 Na. Peter Haule, WF, Dodoma

Serikali imesema kuwa ulipaji wa madai yanayotokana na kupokelewa kwa bidhaa au huduma huzingatia masharti ya mikataba ya zabuni au kandarasi iliyoingiwa kati ya Serikali na mtoa huduma.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba(Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Temeke Mhe. Dorothy George Kilave, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwasaidia wafanyabiashara kulipwa madai na riba wanapo cheleweshewa malipo.

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali hulipa au hulipwa riba iwapo masharti ya mikataba ya zabuni au kandarasi imekiukwa.

 

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo la kuitaka Serikali kutoa maelekezo ili wazabuni walipwe madai yao pamoja na riba wakicheleweshewa fedha baada ya kuingia mikataba, Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inaangalia namna ya kuliweka jambo hilo kwenye kanuni za ununuzi ili kuwalinda wazabuni wa ndani ambao si tu kwamba wanacheleweshewa malipo yao, bali pia Wakandarasi kutoka nje wanaoingia nao mikataba ya kazi huwalipa kwa shilingi ya Tanzania wakati wao wanalipwa kwa dola za Marekani.

 

Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inakamilisha kanunui za ununuzi baada ya Bunge kurekebisha Sheria ya ununuzi wa umma, lengo ni kuhakikisha wakandarasi wa ndani wananufaika na kazi wanazozifanya.

 

Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Cosato David Chumi, kuhusu muda ambao Serikali itaanza kurejesha asilimia 20 (Retention) ya Kodi ya Ardhi kwenye Halmashauri kama ilivyopitishwa katika Sheria ya Fedha 2023/2024, Dkt. Nchemba alisema kuwa urejeshwaji wa kodi hiyo utaanza baada ya zoezi la kukusanya kodi ya ardhi litakapoanza kutekelezwa rasmi na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

 

“Utaratibu wa kurejesha asilimia 20 ya kodi ya ardhi kwenye Halmashauri unatarajiwa kuanza kabla au ifikapo Juni 30, 2024”, alisema Dkt. Nchemba.

 

Alisema kuwa hadi Aprili 2024, taratibu za kuwezesha halmashauri kuanza kukusanya kodi ya ardhi hazikukamilika hususan kufungamanisha mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na mfumo wa kukusanya mapato ya halmashauri – TAUSI.

 

Alisema mwaka 2023/24, Serikali ilifanya maboresho ya ukusanyaji wa kodi ya ardhi ambapo halmashauri kupitia Ofisi ya Rais -TAMISEMI zinatakiwa kukusanya kodi ya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.