Sports yaishukuru Yanga,Yasema undugu wao ni wa kweli

Sports yaishukuru Yanga,Yasema undugu wao ni wa kweli

May 31, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
UONGOZI wa Klabu ya African Sports "Wanakimanumanu"umeishukuru uongozi wa Dar es Salaam Young  African kwa kuwapokea vema
walipokuwa jijini Dar es Salaam pamoja na kuwaandalia malazi mazuri ambayo yaliifanya timu hiyo kujisikia kama wapo nyumbani wakati timu hiyo ilipokwenda kucheza na Friends Rangers ya Kinondoni kwenye uwanja wa Chamazi.
 
Shukrani hiyo zilitolewa jana na Katibu wa Klabu hiyo,Khatib Enzi ambapo alisema mapokezi waliyoyapata wakati wakiwa jijini humo yalikuwa ya aina yake na hivyo kuamini hali ambayo inaonyesha mapenzi walionayo baina ya timu hizo mbili.
 
  'Hawa ndio ndugu zetu ukarimu wao na ushirikiano wao wakati tukiwa jijini Dar es Salaam ulidhihirisha kuwa mapenzi yao kwetu ni makubwa zaidi hivyo tunahaidi kuendelea kuudumisha undugu huo "Alisema Enzi.
 
Mchezo huo ulimalizika kwa African Sports kukubali kichapo cha mabao 2-1 na hivyo watalazimika kushinda bao 2-0 kwenye mechi yao ya marudinao itakayochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini hapa Jumapili wiki hii ili timu hiyo iweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo.
 
Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo,Enzi alisema wachezaji wao wanaendelea vizuri na mazoezi yao kila siku katika uwanja wa shule ya sekondari Usagara chini ya kocha wao Edmund Nyoni ambaye kazi yake ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika michezo yao mbalimbali kwenye mashindano hayo.
 
Alisema licha ya mandalizi hayo kuendelea vizuri lakini wana mchezaji mmoja majeruhi,Rashid Mbu ambaye huenda akaikosa mechi hiyo ambayo ni muhimu kwao kushinda ili kuweza kusonga mbele kwenye mechi zao zijazo na kuweza kutimiza azma yao ya kushiriki ligi daraja la kwanza msimu ujao.
 
Aidha waliomba wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo imedhamiri kurudi ilipotokea na hivyo kuleta hamasa na ushindani kwenye soka mkoani hapa na Tanzania kwa ujumla.
 
Mwisho.