USAJILI wa Tanzania hauna jipya"

July 14, 2013

Na Oscar Assenga,Tanga.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA)aliyejiuzulu,Mustapha Seleboss amesema usajili wa wachezaji wa vilabu vya hapa nchini hauna jipya kwa sababu wachezaji ni wale wale ambao wanasikika kutoka timu nyengine..

Akizungumza na blog hii mapema leo,Selleboss alisema hakuna wachezaji wapya walioibuliwa kwa sababu wale waliosajiliwa walishazoeleka kwa wadau wa soka hapa nchini huku wengine wakikosa mvuto kutokana na kuchokwa na vilabu vyao ambavyo waliwaacha.

Alisema walitegemea kuona toleo jipya la wachezaji lakini badala yake wachezaji waliowasajili ni waliokwisha kuzichezea vilabu mbalimbali hapa nchini na hivyo kutokuwa na muonekano mpya zaidi ya kubadilisha timu za kucheza.
 
"Kitendo cha vilabu kusajili wachezaji kutoka timu nyengine hapa nchini hakitaleta ushindani kwenye Ligi Kuu badala yake itapelekea kuleta hujuma kwa wachezaji hao hasa timu hizo zitakapokutana na timu zao walizotoka "Alisema Selle Boss

(Picha hiyo ni Salimu Bawaziri mwenye shuti nyeusi aliyekuwa akizungumza na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Tanga (TRFA)aliyejiuzulu,Mustapha Sellebosi jana)

Aliongeza kuwa ili kuwe na ushindani kwenye ligi kuu Tanzania lazima vikosi vya pili vya timu zinazoshiriki ligi kuwa na ligi yao ambayo itakuwa ikiandaliwa na shirikisho la soka hapa nchini TFF itakayoviwezesha vilabu hivyo kucheza pamoja na kupatikana bingwa wao.

Akizungumzia historia ya soka Tanzania alisema sio nzuri na ndio maana aliamua kukaa pembeni kwa kujiuzulu kutokana na matatizo makubwa yaliyopo kwenye vyama vya soka vya wilaya hapa nchini hali ambayo inaufanya mpira kukosa mafanikio.

Hata hivyo aliuzungumzia mfumo wa madaraja hapa nchini na kueleza mfumo huo unaua kiwango cha soka hapa nchini kutokana na wachezaji kushindwa kupata nafasi nyingi za kucheza mpira .

Akitolea mfano,mfumo wa ligi ya mabingwa wa mikoa ambapo alipendekeza kuwa ligi hiyo ingechezwa kwa mfumo wa vituo na sio mtoano kama ilivyokuwa hivi sasa hali ambayo inachangia kuua vipaji vya wachezaji wachanga.

Alisema kwenye mashindano hayo timu zingetakiwa kucheza kwenye vituo mbalimbali na timu zinazoshiriki ligi hiyo zisipangiwe kwenye vituo vyao vya nyumbani bali vitumie vyengine kama vyao vya kuchezea na timu mwenyeji zihame kutoka vituo vyao na kwenda vingine ili kukwepa ubabaishaji kwa mechi.

Aidha alilitaka shirikisho la soka hapa nchini likae mapema kuandaa ratiba ya ligi za wilaya,mikoa ,daraja la kwanza na ligi kuu ili kutoa nafasi za vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo kufanya maandalizi mapema na ratiba hizo zisiwe zinaingiliana na taratibu nyengine.

Mwisho.

MECHI YA STAND, KIMONDO NAYO KUPIGWA JUMAPILI

July 14, 2013

Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.

Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya inatarajiwa kuchezwa leo kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya.

Kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Kimondo ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwamuzi wa mechi hiyo ni Hans Mabena kutoka Tanga.