Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akisalimiana na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe,Debnath Shaw
alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi Nchini,[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe,Debnath Shaw alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi Nchini, [Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe,Debnath Shaw baada ya mazungumzo yao leo, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi Nchini, [Picha na Ikulu.]
…………………………………………………..
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa hatua za India
za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali
ya maendeleo zinadhihirishwa uhusiano mwema na wa kihistoria uliopo
baina ya pande mbili hizo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo
wakati mazungumzo kati yake na Balozi wa India katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania anaemaliza muda wake wa kazi hapa nchini Mhe.
Debnath Shaw yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein
aliipongeza Serikali ya India kwa hatua yake ya kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za
maendeleo.
Dk.Shein alisema kuwa Tanzania
ikiwemo Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na India
ambao umeanzishwa na waasisi wa nchi hizo akiwemo marehemu Julius
Kambarage Nyerere na waasisi wa nchi hiyo akiwemo marehemu Indira
Gandhi.
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo
kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano kati yake na India
hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwepo ushirikiano katika
sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, biashara, viwanda na
nyenginezo.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi
kwa India kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta
zake za maendeleo ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wake katika
kuanzisha Chuo cha amali katika kijiji cha Kinyasini Mkoa wa Kaskazini
Unguja ambacho wakati wowote kitazinduliwa.
Utekelezaji wa mradi huo wa
ujenzi wa Chuo hicho ulidhihirishwa wakati wa ziara ya Dk. Shein nchini
India mnamo Febuari mwaka 2014 alipotembelea chuo cha ‘Barefoot”
kilichoko katika Jimbo la Jajasthan nchini India.
Katika mazungumzo na Balozi huyo,
Dk. Shein alieleza kuwa kukamilika kwa chuo hicho kutasaidia juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa mafunzo ya amali na ujasiriamali
sambamba na usambazaji wa umemejua na maeneo mengineyo ambapo mkazo
mkubwa ni kuwawezesha wanawake wa vijijini kujikwamua na umasikini.
Sambamba na hayo, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya India kwa nia yake ya
kuendelea kutoa ushirikiano wake na kuunga mkono miradi ya maji, elimu
na mengineyo huku akipongeza hatua zinazoendelea za kutekeleza
makubaliano yaliofika katika ziara yake nchini.
Nae Balozi wa India katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Debnath Shaw alipongeza uhusiano na
ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na kuadi
kuuendeleza kwa lengo la manufaa kwa pande mbili hizo.
Balozi Shaw alisema kuwa India
itahakikisha inakamilisha miradi yote ya maendeleo ilioanzishwa kwa
mashirikiano kati yake na Zanzibar kwa kutambua kuwa kukamilika kwa
miradi hiyo ndio chachu ya kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano
uliopo.
Aidha, Balozi Shaw alisema kuwa
ziara ya Dk. Shein nchini India imeweza kupata mafanikio makubwa na
kusisitiza imani yake kuwa makubaliano yote yaliofanyika baina ya India
na Zanzibar yatatekelezwa kwa lengo la mafanikio kwa pande zote mbili.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar