TETE FOUNDATION YAADHIMISHA SIKU YA HEDHI DUNIANI KATIKA KITUO NA SHULE YA AMANI, MVOMERO MOROGORO

May 29, 2023







Tarehe 28/5/2023 TETE FOUNDATION  imeungana na jamii kuadhimisha Siku ya Hedhi Duniani, ambapo Taasisi hiyo imefanya maadhimisho hayo katika kituo na shule Amani iliyopo Mvomero - Mkoa wa Morogoro 

Shule/ kituo cha Amani, ni kituo kinachojumuisha malezi ya kitaalam na kijamii Kwa Watoto Wanaoishi kwenye mazingira magumu, Uhitaji na wenye Ulemavu.

Ndani ya kituo hicho kuna Shule ya Msingi kuanzia darasa la awali Hadi darasa la saba na Shule ya Sekondari kuanzia kidato Cha kwanza hadi Cha Pili

Takwimu zinaonyesha kwamba mtoto wa kike anaeishi kwenye mazingira magumu, uhitaji na wenye ulemavu hukosa darasani siku 5 - 7 darasani kwa kukosa taulo za kike. 

Katika maadhimisho hayo Mkurungezi wa TETE FOUNDATION, Bi. Suzana Senso amesema kutokana na takwimu hiyo, mwaka huu tumekuja  na dhima "Sitakosa Shule Campaign" ambapo mwaka huu tumegawa taulo za kike za kutumia kwa muda wa miezi 6  kwa kila binti zaidi ya 50 waliopo kwenye  shule ya Amani 

Shukurani za kipekee kwa wadau walioshirikiana na TETE FOUNDATION kufanikisha hili zoezi ikiwemo UAP INSURANCE TANZANIA kwa kuwa sehemu ya kufanikisha zoezi hili bila kusahau wazalishaji wa taulo za kike za HQ PAD na Ministry ya “love of Christ Ministry” kwa kuwa sehemu ya kuhakikisha kila mtoto wa kike wa Shule ya Amani hakosi darasani kwa muda wa miezi 6 kutokana na kuwa kwenye hedhi

Asante kwa kuwa sehemu ya kurudisha tabasamu kwa mtoto wa kike 🙏🏾🙏🏾🙏🏾

@tete_foundation

TASAC YATOA ELIMU YA USALAMA, ULINZI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA MKOANI PWANI, KIBITI

May 29, 2023

 



Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa elimu ya Usafiri Salama Majini kwa wadau mbalimbali wa Wilaya ya Kibiti katika mialo ya Nyamisati Mkoani Pwani tarehe 25 Mei, 2023.


Elimu hiyo iliyotolewa katika mialo iliyozunguka Nyamasati iliwajumuisha wavuvi, manahodha wa vyombo, wamiliki wa vyombo, wafanyabiashara na watumiaji wa vyombo vidogo vya usafiri majini.


Watoa mada mbalimbali kutoka TASAC, TPA na BMU walitoa elimu ya jinsi ya kutumia vifaa vya uokoaji pindi inapotokea dharura au ajali majini;  utumiaji vifaa vya uokoaji pamoja na matumizi ya kizimia moto (fire extinguisher) na umuhimu wa kuwa na kifaa hicho kwenye vyombo vidogo vya majini.


TASAC imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri majini kutoa elimu katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwahamasisha wamiliki wa vyombo kuweka vifaa vya kujiokolea lakini pia manahodha na wavuvi kuvaa jaketi okozi wakati wote wawapo safarini au kuendesha shughuli za uvuvi.

MCHENGERWA, WANANCHI WA VIJIJI VYENYE MIGOGORO YA MIPAKA HIFADHI YA SERENGETI WAYAJENGA, WAIPONGEZA SERIKALI, WATAKA USHIRIKISHWAJI.

May 29, 2023

 



Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amekutana na kufanya vikao na wananchi wa vijiji vyenye migogoro ya mipaka na Hifadhi ya Serengeti na kuutaka uongozi wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA) kuimarisha program za ujirani mwema na kuwashirikisha wananchi wanaozunguka hifadhi wakati wa kupanga mipango yao ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu kwenye uhifadhi wa raslimali hizo na kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Mei 28, 2023 wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tarime na kufanya mikutano kwenye vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi ya Serengeti vilivyokuwa na migogoro na mipaka katika zoezi la uwekaji wa vigingi vya mipaka ambapo wananchi wa maeneo hao wamepongeza kwa hatua hiyo ya Serikali ya kuja na kuwasikiliza na kuahidi kushirikiana na Serikali kwenye uhifadhi.

Mhe. Mchengerwa aliambatana Naibu Katibu Mkuu wa Wizara yake Anderson Mutatembwa na Kamishna wa TANAPA, Afande William Mwakilema na kupokewa na uongozi wa Mkoa wa Mara, uongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime na Mbunge wa Tarime vijijini Mhe. Mwita Waitara ambapo katika mikutano hiyo yote Mhe. Mchengerwa aliongoza vikao hivyo kwa kuwapa wasaa wa wananchi kutoa maoni na mawazo yao na mwisho alitolea ufafanuzi wa hoja hizo na nyingine kuzichukua kwa hatua zaidi.

Wananchi wamepongeza hatua hiyo ya Waziri Mchengerwa kwenda na kuwasikiliza huku wakieleza kuwa kumekuwa na ushirikishwaji mdogo na kuiomba Serikali kupanga kwa pamoja ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.

Diwani wa kata ya Nyanungu Tiboche Richard amesema kuwa wananchi wa Kata yake wapo tayari kushirikiana na Serikali kwenye kila jambo endapo watashirikishwa na hifadhi.

“Mhe. Waziri napenda kukuhakikishia kuwa leo unatufanya tulale usingizi maana umetumwa na Mhe. Rais wetu kuja kutujengea mahusiano mazuri, na sisi hiki ndicho tulichokuwa tunakikosa.” Amesisitiza diwani Richard

Akiwa kwenye mkutano katika Kijiji cha Karakatonga wilayani Tarime, Mhe. Mchengerwa ameutaka uongozi wa TANAPA kushuka chini kwa wananchi na kwenda kuzungumza nao kwa kuwa hifadhi hizo ni za wananchi na wananchi ndiyo wahifadhi namba moja.
Aidha, amesema wazo la uhifadhi wa raslimali katika taifa la Tanzania limeasisiwa miaka mingi ambapo uongozi katika awamu zote toka enzi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hadi Rais Samia Suluhu Hassan limezingatiwa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Akiwa kwenye Kijiji cha Kegonga, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi hao kushirikiana na uongozi wa Serikali wakati wote na kuacha tabia za kugomea kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanachochea migogoro.
“Kwa hiyo wanapokuja viongozi wa Serikali kuja kujadili mpango wa matumizi bora ya ardhi wasikilizeni msikatae kusikiliza, shaurini tufanye nini.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Amewataka kutambua kuwa wahifadhi ni sehemu ya jamii yao kwa kuwa baadhi ya watumishi hao ni sehemu ya familia zao na watoto wao.

ALIYOYASEMA DC JOKATE BAADA YA KUFANYIKA MAMATHON KOROGWE

May 29, 2023

 


Na Mwandishi Wetu Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo amesema kuwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu za huduma mbalimbali ya afya lengo lake ni kumsogea huduma karibu na mwananchi.

Jokate ametoa kauli hiyo baada ya kufanyika kwa mbio ambazo zilikuwa zimeaandaliwa kwa wanawake wajawazito wilayani humo na kupewa jina la Mamathon ambapo zaidi ya wajawazito 2000 wameshiriki sambamba na kupatiwa vifaa kwa ajili ya kujifungulia.

"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaguswa na changamoto mbalimbali husani huduma za akina mama na watoto na wao, hivyo kupitia Mamathon tunaenzi yale mema na mazuri ambayo Rais wetu amekuwa akiyafanya kupitia Serikali yake ya Awamu ya sita kwa watanzania na zaidi kwenye kundi la akina mama na watoto."

"Sisi akina mama ndio walezi wa jamii zetu, ndio wajenzi wa Taifa kwa maana ukizungumzia watoto wanatoka tumboni mwetu ndio kwa namna moja ama nyingine na wanaume wao wamekuwa wakitusaidia katika malezi lakini kubwa zaidi , akina mama ndio wanatunza hawa watoto."

Jokate amesema Korogwe waliandaa Mamathon ni mahususi kwa ajili ya kumsemea Rais Dk.Samia Suluhu Hassan Samia ambaye ameweika mbele ajenda za mwana mama na mtoto"Kwa hiyo hili tukio sio tukio tu la kutembea lakini kubwa kwenda kuwa mabalozi wa Rais wetu kwani mwendo ameuaza vizuri ,mwendo atauendeleza na sisi wote tunatakiwa kuungana naye."

Aidha amewaeleza akina mama wajawazito kuwa Serikali ya Awamu ya Sita lengo lake nikupeleka huduma za afya kwenye maeneo yao na kwa Wilaya ya Korogwe hakuna kata ambayo haina huduma ya afya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah na Meya wa Temeke mkoani Dar es Salaam Abdallah Mtimika wametumia nafasi hiyo kumpongeza Jokate kwa kufanya tukio la kuleta hamasa kwa wamama wajawazito kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah amesema jambo ambalo amelifanya Mkuu ws Wilaya Jokate ni kubwa na ni jambo la mama."Nimekuja hapa kwa niaba ya wakuu wa Wilaya wote Mkoa wa Tanga, tunampongeza kwani anaupiga mwingitangu ameingia wilayani Korogwe."

Amesema wananchi wa Wilaya ya Korogwe wamelamba dume na kama ni madini basi ya Tanzanite ambayo yanazalishwa Tanzania peke yake.

Amefafanua Jokate ameupiga mwingi akiwa katika Wilaya ya Kisarawe,Temeke na Meya wa Temeke ametoa ushuhuda lakini kubwa zaidi amewaeleza wananchi wa Korogwe kwamba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewapendelea kwani amewapelekea jembe na sasa wanashuhudia Mamathon.

Amesema kupitia Mamathon , Jokate amefanya jambo kubwa kubwa linalowagusa maisha ya wanawake.