Waziri Mavunde apokea msaada wa kompyuta za Bayport

February 21, 2017
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mvunde (kulia) akipokea msaada wa Kompyuta Nne kwa Meneja Masoko na Mawasiliano wa Taasisi ya Kifedha Bayport Tanzania, Ngula Cheyo mjini Dodoma leo asubuhi. Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kati wa taasisi hiyo, Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kati wa taasisi hiyo, Christopher Kihwele.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services, jana imemkabidhi kompyuta nne Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira, Mheshimiwa Anthon Mavunde kwa ajili ya shule za Msingi za Majengo, Chigonge, Mahomanyika na Uhuru zilizopo mjini Dodoma.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Majengo, wakinyoosha mikono juu katika tukio la kukabidhiwa kompyuta nne za Bayport Financial Services, zikipokewa na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.

Makabidhiano hayo yalifanyika katika shule ya Msingi Majengo, ambapo kompyuta hizo zina lengo la kuongeza kiwango cha elimu mkoani Dodoma. Akizungumza leo mjini Dodoma, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba msaada huo wa kompyuta umetokana na dhamira yao ya kusaidia jamii kwenye sekta ya elimu kama njia ya kuikomboa jamii.

Alisema kwamba si mara ya kwanza kusaidia sekta ya elimu kutokana na kujitokeza mara kadhaa kujenga madarasa, kununua thamani za shule pamoja na kudhamini mikopo ya elimu ya juu na vitabu.
Baadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Majengo, wakisoma shairi mahususi kwa ajili ya Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana, Anthony Mavunde wakati anakabidhiwa kompyuta nne kutoka kwenye taasisi ya Bayport Financial Services.

“Bayport tuna lengo la kuikwamua jamii katika maendeleo kwa kuhakikisha kwamba tunakuza kiwango cha elimu, hivyo kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kuhamia Dodoma, tumeamua kutoa kompyuta nne kwa kuboresha miundo mbinu ya elimu ili nchi yetu isonge mbele.
Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo akizungumza jambo katika makabidhiano ya kompyuta nne kwa Naibu Waziri, wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mvunde (kulia) akizungumza kabla ya kukabidhiwa msaada wa kompyuta Nne kutoka Taasisi ya Kifedha ya Bayport Tanzania mjini Dodoma jana.

“Hatujaanza leo kusaidia jamii, ukizingatia kwamba kompyuta hizi nne zenye thamani ya Sh Milioni 10 kwa shule za msingi mjini Dodoma ni tofauti na zile 205 tunazotoa kwa serikali,” Alisema Cheyo.

Akipokea kompyuta hizo, Naibu Waziri aliwashukuru Bayport kwa msaada wao, akisema umekuja wakati muafaka na kuamini kuwa utasaidia kukuza kiwango cha elimu katika Mkoa wa Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya Tanzania.

“Tunawashukuru Bayport kwa msaada wenu, wananchi wa Dodoma tumeupokea kwa furaha kwa sababu unatufanya tupige hatua kubwa kukuza elimu, ukizingatia kuwa mipango yangu kama mbunge ni kusambaza kompyuta kwa kila shule ili wanafunzi wetu wafanye mitihani kila mwisho wa wiki kama sehemu yao ya kujiandaa na mitihani ya Taifa,” Alisema Mavunde.

Naye Afisa Elimu wa Manispaa ya Dodoma, Scolastica Kapinga, alisema juhudi zao za kukuza kiwango cha elimu utafanikiwa kwa kupokea kompyuta hizo zilizotolewa na Bayport kwa juhudi kubwa za mbunge wao.

Bayport ni taasisi inayotoa mikopo ya fedha na bidhaa, ikiwamo ardhi yenye hati, ambapo pia imekuwa ikijitokeza mara kadhaa kusaidia mambo ya kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali kama sehemu ya kurudisha faida kwa jamii.


UPIGAJI MARUFUKU MATUMIZI YA POMBE ZINAZOFUNGASHWA KATIKA VIFUNGASHIO VYA PLASTIKI (VIROBA)

February 21, 2017


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

UPIGAJI MARUFUKU MATUMIZI YA POMBE ZINAZOFUNGASHWA KATIKA
 VIFUNGASHIO VYA PLASTIKI (VIROBA)

Kufuatia kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyotoa tarehe 16/02/2017 huko Mererani, Mkoani  Manyara kuhusu kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi 2017; na kufuatia  Tamko la Serikali kuhusu dhamira hiyo lililotolewa Bungeni tarehe 2 Mei, 2016 na kwenye matangazo yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari tarehe 01 Desemba, 2016, Ofisi ya Makamu wa Rais  inachukua fursa hii kutangaza utaratibu wa utekelezaji wa maamuzi hayo ya Serikali.

(i)      Waziri mwenye dhamana ya Mazingira atatunga Kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio (viroba) vya pombe kali, kwa mujibu wa Kifungu 230 (2) (F) cha Sheria ya Mazingira ya  2004.  Kanuni hizi  zitaweka sharti la kutaka pombe kali inayozalishwa viwandani zifungashwe kwenye chupa zinazoweza kurejelezwa (recycled) na kwa ujazo usiopungua milligram 250.
                                                                                                  
Pia Kanuni hizo zitapiga marufuku uzalishaji, uuzaji, uingizaji nchini na matumizi  pombe  zilizofungwa kwenye viroba na mitambo ya malighafi ya vifungashio vya plastiki (viroba) vitakavyotumika kufungashia pombe kali.   Atakayebainika kukiuka masharti ya Kanuni hizi atawajibishwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja kama itakavyoainishwa kwenye Kanuni.

(ii)    Dhamira ya Serikali sio kupiga marufuku vinywaji vya pombe kali bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi katika mazingira yaliyo safi, salama na yenye afya.  Haki hiyo pia imetiliwa mkazo katika sheria ya Mazingira ya 2004.  Hivyo, dhamira  ya Serikali ni kudhibiti upatikanaji kwa urahisi wa pombe kali kunakotokana na kufungwa katika plastiki na kwa ujazo mdogo, kunakopelekea kuongezeka kwa matumizi ya pombe kali hadi kwa watoto wadogo; kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kuzagaa kwa vifungashio hivyo; na kudhibiti ukwepaji mkubwa wa kodi kutokana na urahisi wa teknolojia na gharama za kutengeneza  pombe kali  inayofungashwa kwenye viroba. Inakadiriwa kwamba Serikali inapoteza shilingi bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ukwepaji kodi kwenye biashara ya pombe za viroba.

(iii)   Utekelezaji wa maamuzi haya ya Serikali unaanza mara moja.  Ingawa haitegemewi, lakini iwapo kuna Wazalishaji watakaohitaji muda wa ziada wa kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, wataomba kibali maalum cha muda mfupi ambacho hakitatolewa hadi muombaji awasilishe kabla ya tarehe 28/02/2017:- yafuatayo:-
i)        Ushahidi/Barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba amelipa kodi katika kipindi cha miaka  mitatu iliyopita.
ii)      Ushahidi/Barua/Cheti kutoka  Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwamba mzalishaji amekuwa na  kibali cha usalama wa kinywaji kwa miaka yote ambayo amekuwa anazalisha;
iii)    Cheti au Barua kutoka  Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwamba mzalishaji  anauza bidhaa inayokidhi viwango
iv)    Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) au Ukaguzi wa Mazingira (EA) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)/Ofisi ya Makamu wa Rais;
v)      Ushahidi kwamba katika kipindi cha mpito mzalishaji atatumia teknolojia ya kudhibiti utengenezaji wa vifungashio bandia (anti-counterfeit technology);
vi)    Uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuhusu usajili wa  kampuni na usajili wa chapa ya kinywaji (brand).

Zipo pombe za viroba zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi, hasa kwenye Mikoa na Miji ya mipakani.  Wakuu wa Wilaya , kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Kamati za Mazingira, wanaelekezwa kufanya operesheni ya kukamata na kuzuia viroba vinavyoingizwa nchini kinyume cha utaratibu. Operesheni hii pia inahusu udhibiti wa pombe haramu ya gongo.

Serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji na hatua hizi.  Kikosi hicho kinajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Fedha na Mipango,  Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi.  Doria za ukaguzi  wa utekelezaji wa hatua hizi zitaanza wakati wowote kuanzia sasa na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka.  Ofisi ya Makamu wa Rais itaratibu Kikosi hiki.

Kuhusu mifuko ya plastiki, Kanuni za Udhibiti zinaandaliwa na zuio litatangazwa wakati wowote.  Tunapenda kuwaasa wazalishaji, waagizaji na wauzaji  wa mifuko hiyo nao kujiandaa.

Hatua hizi za Serikali sio za ghafla au kushtukiza kwani taarifa ilitolewa Bungeni takribani mwaka mmoja sasa. Aidha Serikali ilitoa taarifa rasmi mwezi Agosti 2016 na Desemba 2016 kuhusu dhamira ya kuchukua hatua hizi.  Serikali ilitarajia kwamba wazalishaji wa pombe za viroba na mifuko ya plastiki watakuwa wamejiandaa kubadilisha teknolojia.
                                           
Ofisi ya Makamu wa Rais
20/02/2017

SBL yaanza kuuza bia Kenya

February 21, 2017

Dar es Salaam, Februari 20, 2017- Kwa mara ya kwanza, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imeanza kuuza nje ya nchi  bidhaa zake katika  soko la kikanda,  eneo la kwanza  likiwa ni nchi jirani ya Tanzania kwa upande wa Kaskazini, Kenya.
Shehena ya kwanza ya bia  inayofahamika kama Allsopps ilisafirishwa kwenda Kenya wiki iliyopita na hivyo kukiweka kiwanda cha SBL kuwa mmoja wachangiaji wakubwa katika soko la kanda.
 Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL, John Wanyancha alisema; “Hii ni hatua nyingine ya kufurahisha  katika kampuni yetu  na kimsingi kwa  bidhaa zetu. Ukweli unabakia kwamba kumudu  kupenyeza ndani ya soko la Kenya  kunaonesha kuwa  ubora wa bidhaa zetu  sio tu kwamba unakubalika  na wateja wetu wa ndani bali pia  zinakubalika katika soko  kubwa  la kikanda.”
Wanyancha alisema kuwa SBL inaangalia  uwezekano wa kupanua mauzo ya biashara katika masoko mengine ya kikanda, hatua ambayo iko  katika mkondo wa kuhamasisha  Jumuia ya Afrika Mashariki  na kada nyingine za kiuchumi  kuongeza biashara yake  ya kuvuka mpaka  ndani ya ukanda huo.
 SBL imekuwa inazalisha aina za bidhaa  zinazotambulika kimataifa  kama vile Pilsner Lager,Tusker Lager, TuskerLite, Kibo Gold, Guinness Stout, Uhuru, The Kick pamoja na bidhaa kuu ya Serengeti Premium Lager-ambayo peke yake  imeshajizolea medali  kumi zinazotambuliwa kimataifa.