WATAKIWA KUZIDISHA JUHUDI KUPUNGUZA UKATILI

December 12, 2023

 Na. Jeshi la Polisi Dodoma


Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu CP Suzan Kaganda amewataka Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kote nchini kuzidisha juhudi katika kutoa elimu ili kupunguza vitendo vya ukatili katika Jamii.

Kamishna Kaganda ameyasema hayo leo Disemba 12, 2023 wakati akizungumza na Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar wakati wa Kikao cha Watendaji hao kinachoendelea Jijini Dodoma

Alisema kazi inayofanyika ni kubwa ingawa bado kuna vitendo vya ukatili hivyo Watendaji hao wazidishe kutoa elimu pamoja na kubaini na kuzuia vitendo hivyo.

Aidha, aliwataka Watendaji hao kuendelea kushirikiana na wadau mambo mbalimbali ikiwemo kutoa elimu na kazi zingine ambazo zinahitaji raslimali fedha na vifaa ili kazi za Dawati ziweze kuendelea kwa kasi.

Vilevile aliwataka wote waliohudhuria kikao hicho kilichoambatana na mafunzo kuhakikisha kuwa wanakwenda kuwafundisha Watendaji na Askari ambao hawakupata fursa ya kufika Jijini Dodoma kwa ajili ya Kikao na Mafunzo hayo.

Kwa Upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Maria Nzuki alisema kutokana na kazi nzuri ya kutoa elimu kwenye nyumba za ibada iliyofanyika siku ya Jumapili katika makanisa mbakimbali Jijini Dodoma tayari Makanisa zaidi ya 20 yameomba Watendaji hao kwenda kutoa elimu Jumamosi na Jumapili ijayo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Kimataifa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Renata Mzinga alisema watendaji hao wamejitokeza kwa wingi kuhudhuria Kikao hicho na kila Mkoa umeleta Wawakilishi.


NDEJEMBI AMBANA MKURUGENZI WA PANGANI KWA KUSHINDWA KUSIMAMIA MIRADI

NDEJEMBI AMBANA MKURUGENZI WA PANGANI KWA KUSHINDWA KUSIMAMIA MIRADI

December 12, 2023




OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Isaya Mbenje na watendaji walio chini yake kujitafakari juu ya mwenendo wa utendaji kazi wao kutokana na kushindwa kusimamia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo.

Mhe Ndejembi ametoa kauli hiyo leo alipotembelea miradi ya elimu ya msingi na sekondari inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa mwaka mpya wa masomo 2024.

Katika ziara yake, Mhe Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Pangani Halisi iliyogharimu kiasi cha Sh. Bilioni Moja, Shule ya Sekondari Masiaka inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP inayogharimu Sh. Milioni 585 na Shule ya Msingi Bushiri iliyogharimu Sh. Milioni 440 ikijengwa kupitia mradi wa BOOST.
- Advertisement -


Amesema Shule ya Pangani Halisi ilipaswa iwe imeshakamilika lakini mpaka sasa ujenzi huo haujakamilika huku halmashauri ikiwa imeishiwa fedha ikilinganishwa Shule ya Masiaka ambayo imepata sh. Milioni 580 majengo yake yapo kwenye hatua kubwa na inaendelea na ujenzi.

“Ofisi ya Rais-TAMISEMI chini ya Waziri Mhe Omary Mchengerwa hatutomchekea yeyote anayechezea fedha za umma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na wasaidizi wako mjitafakari kwa sababu hawamsaidii kazi Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika ngazi ya huku chini kuna tatizo la usimamizi wa miradi na kutojali fedha zinazoletwa kutekeleza miradi hii. Sasa kwa TAMISEMI hii hatuwezi kuja tukakuta usimamizi mbovu wa miradi tukashindwa kuchukua hatua,”amesema.