MWANDISHI WA HABARI APIGWA RISASI

October 13, 2013
Mwandishi wa Habari na mtangazaji wa ITV, Ufoo Saro
MWANDISHI wa Habari ambaye pia ni Mtangazaji wa ITV, Ufoo Saro, amepigwa risasi na mchumba wake aitwaye Antel Mushi. Baada ya kufanya unyama huo, Mushi ambaye alikuwa Mfanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa nchini Sudan, alimuua kwa risasi mama yake Ufoo, Anastazia Saro (58) kisha naye akajiua.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea jana alfajiri, eneo la Kibamba, Dar es Salaam. “Tukio hilo limetokea leo (jana), asubuhi saa 12 alfajiri eneo la Kibamba CCM, baada ya Mushi ambaye ni mzazi mwenzake na Ufoo, kurejea nchini juzi akitokea Sudan na kufikia nyumbani kwa Ufoo.

“Kabla ya tukio, inaonekana kulikuwa na mazungumzo kati ya wawili hao na mama yake Ufoo, ambapo walishindwa kuelewana na Mushi akampiga risasi kifuani mama yake Ufoo na kumuua kisha akampiga Ufoo tumboni na mguuni na yeye akajiua,” alisema Kamanda Kova.

Alisema kwamba, Ufoo baada ya kujeruhiwa, alikimbizwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha na baadaye akahamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alifanyiwa upasuaji katika maeneo aliyojeruhiwa.

Hata hivyo, Kamanda Kova alisema jitihada za kupata maelezo ya Ufoo zilishindikana baada ya kuwaambia polisi kwamba atazungumza baada ya kupona.

Ufoo ana mtoto mmoja aitwaye Alven Mushi mwenye umri wa miaka 10 ambaye alimzaa na marehemu Mushi.


Source:Rai Jumatatu

MBEYA CITY YAIPA MKONGOTO MGAMBO SHOOTING.

October 13, 2013

NA OSCAR ASSENGA,TANGA
TIMU ya Mbeya City ya Mbeya leo imefanikiwa kuifunga Mgambo Shooting ya Tanga bao 1-0 ikiwa ni mechi ya Ligi kuu Tanzania bara uliopigwa kwenye dimba la soka Mkwakwani.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wenye upinzani mkali ambapo Mbeya City waliandika bao lao la kwanza katika dakika ya 20 kupitia Jeremia John baada ya kumalizia kazi nzuri iliyokuwa imefanywa na Alex Seth.

Bao hilo lilidumu mpaka timu zote zinakwenda mapumziko ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya mashambulizi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu baada kufanya mabadiliko kwenye baadhi ya wachezaji wao.

Mabadiliko kwa upande wa Mbeya City waliwatoa Alex Seth,Jeremia John na Deus Kaseke ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hamad Kibopile,Fransis Casto na Peter Mapunda.

Kwa upande wa Mgambo Shooting wao waliwatoa Mohamed Samata na kuingia Twaha Mihinga kutokana na mabadiliko hayo mgambo waliweza kufanikiwa kucheza kwa vema huku walilishambulia lango la wapinzani wao bila mafanikio yoyote.

Katika dakika ya 72 mgambo shooting walipata pigo baada ya mchezaji wao Salum Mlima kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo,Oden Mbaga kutoka DSM kwa kumchezea rafu mchezaji wa Mbeya City Yusuph Wilson.

Kikosi cha Mbeya City leo ni Gk,David Burhan,John Kabanda,Hassan Mwasapili,Yusuph Abdallah,Deogratius Julius,Anthony Matogolo,Alex Seth,Steven Mazanda,Paul Nonga,Jeremia John na Deus Kaseke.

Mgambo Shooting waliwakilishwa na Gk JohnKavishe,Salum Mlima,Ramadhan Kambwili,Salum Kipanga,Bakari Mtama,Novart Lufunga,Nassoro Gumbo,Mohamed Samata,Mohamed Netto,Malimi Busungu na Peter Mwalyanzi.

MECHI YA SIMBA, PRISONS YAINGIZA MIL 60/-

October 13, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 13, 2013

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Simba na Tanzania Prisons kutoka Mbeya iliyochezwa jana (Oktoba 12 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 60,521,000.

Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi hiyo namba 55 na kushuhudiwa na watazamaji 10,494 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Kila klabu ilipata mgawo wa sh. 14,191,002.55 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,232,016.95.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,215,763.96, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,329,458.37, Kamati ya Ligi sh. 4,329,458.37, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,164,729.19 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,683,678.26.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

PICHA ZA MATUKIO UZINDUZI WA MRADI WA KUWAJENGEA UWEZO WASICHANA MKOA WA TANGA.

October 13, 2013
Add captionNaibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na
Watoto,Ummy Mwalimu  akiongoza maandamano ya wanawake walipokuwa
wakiingia uwanja wa Mkwakwani kusherehekea maadhimisho ya siku ya
msichana Duniani mbayo yalikwenda sambamba na uzinduzi wa mradi wa
kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga unaoendeshwa na shirika la
Tawode chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Denmark kupitia (DANIDA)

 Wanawake kutoka Wilaya za mkoa wa Tanga
wakishiriki maandamano ya kuadhimisha siku ya msichana Duniani
yaliyoandaliwa Jijini Tanga na Shirika la Tawode chini ya ufadhili wa
Ubalozi wa Denmark kupitia (DANIDA)

wanafunzi wa shule ya msingi Msambweni Jijini
Tanga wakishiriki maandamano ya kuadhimisha siku ya msichana Duniani
yaliyoandaliwa Jijini Tanga na Shirika la Tawode chini ya ufadhili wa
Ubalozi wa Denmark kupitia (DANIDA)

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na
watoto Ummy Mwalimu akitoa maelezo ya mradi wa kuwajengea uwezo
wasichana wa mkoa wa Tanga unaoendeshwa na shirika analoliongoza la
Tawode ,mradi huo unafanyika chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Denmark
kupitia (DANIDA)

Mwakilishi wa Balozi wa Denmark nchini Ester
Msuya akitoa salamu za Balozi wakati wa uzinduzi wa mradi wa
kuwajengea uwezo wasichana wa Mkoa wa Tanga utakaofanyika katika
Wilaya mbalimbali mkoani hapo,mradi huo umefadhiliwa na ubalozi huo
kupitia DANIDA na unaendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Tanga
Woman Development Initiative (Tawode).

Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa
akizungumza wakati wa kuzindua mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa
Mkoa wa Tanga utakaofanyika katika Wilaya mbalimbali mkoani hapo,mradi
huo umefadhiliwa na ubalozi Denmark Nchini  kupitia DANIDA na
unaendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Tanga Woman Development
Initiative (Tawode).

Picha zote na Burhani Yakub
UBALOZI WA DENMARK UMEHAIDI KUENDELEA KUTOA MISAADA YA ELIMU KWA WATOTO WA KIKE NCHINI

UBALOZI WA DENMARK UMEHAIDI KUENDELEA KUTOA MISAADA YA ELIMU KWA WATOTO WA KIKE NCHINI

October 13, 2013
Burhani Yakub,

Tanga.Serikali ya Denmark imeahidi kuendelea kutoa msaada kwa maeneo mbalimbali nchini yatakayojikita  katika  kutoa kipaumbele cha elimu kwa watoto wa kike ili kuwawezesha kuinua hali zao za maisha kiuchumi na kiafya.

Ahadi hiyo ilitolewa na Mwakilishi wa balozi wa Denmark nchini,Ester Msuya wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa Mkoa wa Tanga unaoendeshwa na shirika la Tanga Woman Development Initiative (Tawode)na kufadhiliwa na ubalozi huo kupitia DANIDA).

“Mkakati wa sasa wa Serikali ya Denmark kuhusu ushirikiano wa maendeleo ya kimataifa unaitwa “Haki ya maisha bora”tunajua kwamba uwekezaji ulio bora ambao Serikali yoyote inawaza kufanya ni ku-elimisha watoto wa kike”alisema Msuya.

Mwakilishi huyo wa balozi alisema Serikali ya Denmark inaamini katika haki za mtoto wa kike na mwanamke kupata elimu au angalau fursa ya kupewa stadi za maisha ili kuishi maisha bora na kuchangia katika maendeleo ya jamii kwa ujumla

Alilipongeza shirika la Tawode kwa kufanikisha mchakato wa kuanza kwa mradi huo wa kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga na akaahidi kuwa ubalozi utatoa ushirikiano wa hali na mali ili kufanikisha mradi huo.

Akitoa melezo kabla ya kuzinduliwa mradi huo,Mwenyekiti wa Tawode ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto,Ummy Mwalimu alisema  lengo la kuendesha mradi huu ni kutokana na ukweli kwamba mtoto wa akike anabiliwa na changamoto nyingi kuliko wa kiume likiwamo suala la kutojitambua .

Alitolea mfano wa tafiti zilizopo za viashiria vya ukimwi na malaria nchini zilizofanyika mwaka 2011 na 2012 zinaonyesha kiwango cha maambukizi kwa wasichana ni cha juu kuliko wavulana hususani walio katika umri wa miaka 23 na 24.

Alisema maambukizi kwa wasichana walio katika umri kwa kati ya miaka 23 na 24 ni asilimia 6.6 wkati kwa wavulana wa umri kama huo ni asilimia 2.8 pekee.

Mradi huo ulizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye alipokea maandamano ya wanawake na wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali mkoani hapa na pia alikagua mabanda ya maonyesho ya kazi za mikono zinazofanywa na wanawake.

                                        MWISHO

RC GALLAWA -UPO UMUHIMU WA KUWASAIDIA WASICHANA.

October 13, 2013

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
MKUU wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa amesema kuwa upo umuhimu wa wasichana kusaidiwa,kutiwa moyo na kuhamasishwa kupenda kupata maendeleo yao pamoja  na kuwalinda watoto hao na vitendo vyote vya ukatili likiwemo la kuwaozesha mapema.

Gallawa ametoa kauli hiyo wakati akitoa hotuba yake katika uzinduzi wa mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga iliyoratibiwa na Tasasi ya Tawode na kufadhiliwa na Denmark kupitia shirika lake Maendeleo la DANIDA.

Amesema jukumu la kuwalinda watoto wa kike ni la kitu mtu na kuitaka jamii itambue kuwa hakuna mtu mmoja au taasisi yenye ujuzi,maarifa na rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji yote ya kuwalinda watoto hao.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wadau wote wa maendeleo ya mtoto wa mkoa wa Tanga kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa na taasisi hiyo katika kuwawezesha watoto hao kujitambua ikiwemo kujithamini.

Aidha ameitaka jamii kutambua umuhimu wa kuzingatia haki za watoto wa kike na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Ameongeza kuwa serikali ya mkoa wa Tanga itatoa ushirikiano wa kutosha wakati wa utekelezaji wa mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa matokeo yake yatawezesha kukuza uchumi na kuondoa umaskini katika mkoa.

Gallawa ameipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa mpango maalumu wa kufadhili wasichana wanafunzi waishio katika mazingira magumu, wasichana wazazi wadogo na wanawake wenye uhitaji zaidi wapatao 1000 ili kujiunga na mfuko wa bima ya Afya (NHIF) kuanzia mwaka 2014.
Mwisho.

WASANII NGULI WA FILAMU NCHINI WAASWA

October 13, 2013

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
WASANII Nguli wa Filamu hapa nchini wametakiwa kuacha kuwabagua wasanii wachanga badala yake washirikiane nao ili kufanya nao kazi kwa pamoja lengo likiwa ni kusukuma gurudumu la maendeleo yao.
 
Ushauri huo ulitolewa leo na Msanii kipukizi wa Filamu mkoani Tanga,Mohamed Kilua “Action Made”ambaye hivi sasa anatamba katika tasnia hiyo hapa nchini.

Kilua ambaye anatamba katika filamu za Kata K aliyocheza na Mzee King Majuto,Gentlemen aliyoshirikiana na Richie Mtambalike na Impossible aliyecheza na marehemu Sharomilionea pamoja na kitale.

Alisema katika filamu hiyo ya kata K alicheza yeye kama ndio muongozaji wakati nyengine alishiriki kwenye upande tofauti tofauti .

Kilua alisema changamoto kubwa inayowakabili wasanii wachanga ni ulipwaji umekuwa sio mzuri kutokana na kulipwa malipo kidogo ambayo hayalingani na kazi wanayoifanya.

Aidha alilishauri Baraza la Sanaa Tanzania(Basata)kuwaangalia wasanii wachanga ambao wanachipukia ili waweze kuona umuhimu wa fani hiyo kwa kupewa nafasi.

LIGI KUU KUINGIA RAUNDI YA TISA LEO.

October 13, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
LIGI KUU Tanzania bara inaingia raundi ya tisa leo kwa michezo mbalimbali ambayo itapigwa kwenye viwanja vya Mabatini, Mkwakwani,Azam Complex na Manungu Turian mkoani Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari,Ofisa Habari wa Shirikisho la soka hapa nchini TFF,Boniface Wambura amesema kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini, Mlandizi), Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu, Turiani).

Alizitaja mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia TBC1 wikiendi hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.