OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANONA MAZINGIRA YAWAJENGEA UELEWA WAHARIRI KUHUSU BIASHARA YA KABONI (HEWA UKAA)

June 19, 2023

 

NA K-VIS BLOG, UDSM

BIASHARA ya Kaboni (Hewa Ukaa-Co2) ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema.

Bw. Mitawi ameyasema hayo katika warsha ya kuwajengea uelewa wa Kanuni na Mwongozo wa biashara ya kaboni kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini Juni 19, 2023 kwenye ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), sehemu ya Mlimani.

Alisema biashara hiyo hufanyika miongoni mwa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi Mwanachama wa Mikataba hii. hivyo, pamoja na sera na mikakati iliyopo na kwa kuzingatia umuhimu wa biashara hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa Kanuni na Mwongozo wa Taifa wa Usimamizi wa Biashara ya Kaboni nchini.” Alifafanua Bw. Mitawi.

Akizungumzia Malengo makuu ya Kanuni na Mwongozo huu alisema,  nipamoja na kuweka utaratibu na masharti ambayo wadau na wawekezaji wa biashara ya kaboni watapaswa kuzingatia wakati wa utekelezaji wa miradi mipya na miradi inayoendelea ya biashara ya kaboni katika sehemu mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kanuni na Mwongozo zilishatangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 636 la tarehe 28 Oktoba, 2002. hivyo, kuwa tayari kwa matumizi.” Alibainisha.

Nyenzo hizi zimejikita katika kuimarisha mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesijoto na hivyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa ajili ya maendeleo endelevu, alisema.

“Mtakubaliana nasi kuwa sote kwa pamoja tunapaswa kuchukua hatua mahususi ili kuimarisha hifadhi ya mazingira nchini kwa maendeleo endelevu, hivyo basi, kupitia warsha hii  ni matumaini yetu kuwa sote kwa pamoja kupitia taasisi zetu tutashirikina katika kusimamia utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa biashara ya kaboni nchini ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi.” Alisisitiza Bw. Mitawi.

Tayari Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesaini makubaliano ya awali (MoU) ya kufanya biashara ya Hewa Ukaa (Carbon dioxide -CO2) na Kampuni ya Kigeni ya GreenCop Development PTE LTD Mei 18, 2023 jijini Dar es Salaam.

Awali Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA  Mabula Misungwi Nyanda alisema kuna makampuni mengi yameleta maombi ya kuwekeza kwenye eneo hili, na matatu yako kwenye hatua za mwisho. 

“Kampuni ya GreenCop PET Ltd inahusisha maeneo matatu ambayo ni pori la Akiba la Selous, Kilombero na Msanjesi.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano Bw. Abdallah Hassan Mitawi, akizungumza na Wahariri kwenye ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), sehemu ya Mlimani Juni 19, 2023.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde akizungumza mwanzoni mwa warsha hiyo.

Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt.Andrew Komba akizungumza mbele ya wahariri Juni 19, 2023
Baadhi ya washiriki
Bw. Abdallah Hassan Mitawi
Baadhi ya washiriki
Mgeni rasmi na washiriki