JIOPAKI PEKEE KUSINI MWA JANGWA LA SAHARA KUANZISHWA NGORONGORO - MHE MCHENGERWA

May 26, 2023

 


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii - Mhe. Mohammed Mchengerwa amepokea timu ya wataalam saba kutoka nchini China ambao wamewasili nchini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa jiopaki ya Ngorongoro- Lengai, ambayo ndio jipaki pekee kusini kwa Jangwa la Sahara .

Pamoja na uimarishaji wa uhifadhi wa rasilimali za kijiolojia, mradi huu utaongeza vivutio vya utalii, ujenzi wa makumbusho ya kijiolojia, kuweka mitambo ya kufuatilia hatari za kijiolojia na kuwajengea uwezo wataalam wa kitanzania kuwezesha ukuaji utalii wa miamba na sura za nchi ( Geotourism and landscape tourism)


Mradi huu ambao utagharimu jumla ya dolla za kimarekani millioni 9.5 na kutarajiwa kukamilika baada ya miaka miwili na nusu, umefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.  

Makubaliano ya msaada huu yalisainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kitaifa nchini China Novemba, 2022.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuimarisha uhifadhi wa raslimali na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii kimataifa na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kikamili kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.


TAKUKURU DODOMA YAFUATILIA UTEKELEZAJI MIRADI 36 YA MAENDELEO

May 26, 2023
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma John Joseph.

Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU)Mkoa wa Dodoma katika utekelezaji wa majukumu yake imepokea jumla ya malalamiko 138 ambapo kati yake, malalamiko 81 yalihusu rushwa na mengine 7 taarifa zake kuhamishiwa Idara nyingine kwa hatua zaidi. 

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma John Joseph amesema hayo leo Mei 26,2023 wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu ufuatiliaji utekelezaji wa miradi 36 ya maendeleo ya zaidi ya bilioni 16.8 ikiwa ni sehemu ya  Utaratibu wake wa kutoa taarifa kwa kila kipindi cha miezi mitatu.

Amesema malalamiko 57 yalihusu rushwa ambapo yalipelekwa kufunguliwa majalada ya uchunguzi na kati ya hayo uchunguzi wa majalada 17 umekamilika ,mashauri mawili yamefunguliwa mahakamani na mengine 15 hatua mbalimbali za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Mkuu huyo wa TAKUKURU amefafanua kuwa Idara zinazo lalamikiwa Kutokana na taarifa 57 ni pamoja na Elimu (11), TAMISEMI (9),Sekta binafsi (9), Ardhi (7),Afya (7),Polisi(5),Kilimo(3),Manunuzi (2), Mahakama (1), Maji (1), Mazingira (1)na fedha (1).

"Mashauri mapya manne yametolewa maamuzi ambapo hadi sasa mawili tumeshinda na mawili tumeshindwa ,aidha jumla ya mashauri 31 yanaendelea kusikilizwa mkoani Dodoma na yako katika hatua mbalimbali,"amesema

Pamoja na hayo amesema katika kipindi cha miezi mitatu TAKUKURU Mkoa wa Dodoma wamefanya kazi za uzuiaji rushwa,uelimishaji wa jamii na uchunguzi.

Amefafanua kuwa katika jukumu la uzuiaji rushwa wamefanya tafiti 10 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma kwa Wilaya za Dodoma, Chamwino na Chemba na kufanya tafiti moja moja kwa kila Wilaya.

"Kwa Wilaya ya Bahi zilifanyika tafiti mbili na katika Wilaya ya Kongwa zilifanyika tafiti tano,tumeweza kufanya warsha tano ambazo zilitumika kuwasilisha matokeo ya chambuzi za mifumo zilizofanyika Kwa lengo la kushirikisha jamii kutafuta ufumbuzi dhidi ya mianya ya rushwa,"amefafanua.

Katika ufuatiliaji wa utejekezwaji miradi ya maendeleo, TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imefuatilia miradi 36 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 16 ambayo inatoka sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, Ardhi, Kilimo, ujenzi, barabara na fedha .  

Kwa mujibu wa Mkuu wa TAKUKURU Dodoma jumla ya miradi 22 ya elimu imefanyiwa ufuatiliaji, Kilimo miradi 5,fedha 3 na afya miradi 4 hali iliyosaidia  kufikia fedha kiasi cha shilingi 1,050,000 katika Wilaya ya Chamwino.

"Miradi 21 imetolewa ushauri na elimu pia ufuatiliaji unaendelea, miradi 7 imekamilika ,miwili imetolewa maelekezo, chambuzi za mifumo ya warsha miradi miwili,miradi miwili inaendelea na ufuatiliaji nyaraka katika Wilaya ya Chamwino,"ameeleza 

 

KATAMBI:PENSHENI ZINALIPWA KWA WAKATI

May 26, 2023


Na Mwandishi Wetu, DODOMA

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi amesema serikali inalipa pensheni kwa wastaafu kwa wakati kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi.

Mhe.Katambi ameyasema hayo bungeni Mei 26, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe (CCM), Mhe. Nicodemus Maganga ambaye ametaka kujua serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pesheni za wastaafu zinalipwa kwa wakati.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Katambi amesema katika kuhakikisha wastaafu wanalipwa pensheni zao kwa wakati, Serikali kupitia mifuko ya pensheni ya PSSSF na NSSF imeweka utaratibu mahsusi wa kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki kupitia kwenye akaunti zao za Benki kabla au ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi.

Aidha, amesema hadi kufikia mwezi Machi 2023 idadi ya wastaafu wanaolipwa pensheni katika Mifuko ya PSSSF na NSSF imefikia 186,605 (ikijumuisha PSSSF wastaafu 158,735 na NSSF wastaafu 27,870).

Naibu Waziri Katambi amesema mifuko inaendelea kuimarisha mifumo ya ndani ya ulipaji wa mafao ili kuhakikisha maombi ya wastaafu wapya yanafanyiwa kazi kwa haraka na kuanza kulipwa pensheni ndani ya kipindi kisichozidi siku 60 kama Sheria inavyotaka.




 

MWENGE WA UHURU WASISITIZA UTUNZAJI VYANZO VYA MAJI

May 26, 2023

 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Ndugu Abdalla Shaibu Kaim amewaonya wananchi kutokufanya shughuli yoyote ikiwemo kilimo na ufungaji karibu na vyanzo vya maji kwani ni kinyume cha sheria na ni uharibifu wa Mazingira.


Ameongeza kwa kusema kuwa hairuhusiwi kwa mtu yeyote kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa ya kukagua utekelezaji wa mradi wa utunzaji Mazingira unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwenye mradi wa maji Kigamboni.

“Hatua hii ni muhimu kwa ajili ya kulinda na kuviendeleza vyanzo vya maji pamoja na uoto wa asili ikizingatiwa kuwa maji ni uhai. Sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za upandaji miti rafiki yenye kutunza mazingira katika vyanzo vyetu vya maji." amesisitiza Ndugu Kaim.

"Sheria, miongozo na kanuni zipo wazi kwani tunafanya hivyo kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji kwa kuwa maji ni uhai," ameeleza.

"Niwapongeze DAWASA kwa jitihada kubwa mnazozifanya za kulinda na kuendeleza Mazingira kwa kutunza vyanzo vya maji, mnafanya kazi nzuri, niwapongeze sana." ameeleza Ndugu Kaim.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa katika jitihada za kutunza na kuendelea vyanzo vya maji katika mradi wa maji Kigamboni, Mamlaka imefanikisha kupanda miti ya matunda na kivuli takribani miti 3,300.

"Huu ni mpango endelevu ambapo katika awamu ya kwanza tumeanza kupanda miti 1,800 kwenye eneo la tenki kubwa la maji." amesema.

Amebainisha kuwa mpango wa upandaji miti Kigamboni ulitekelezwa kwa kushirikisha wananchi wa maeneo jirani kwa kuwapa elimu ya umuhimu wa utunzaji wa Mazingira ili waweze kutunza na kunufaika na mazao ya miti hii.

"Utunzaji wa Mazingira ni mojawapo ya kipaumbele cha Mamlaka kwa kuwa tunaelewa uendelevu wa huduma ya maji unategemea usalama wa vyanzo vya maji, hivyo DAWASA imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha vyanzo vya maji ikiwemo vya Mto Ruvu na visima virefu vinalindwa ipasavyo." ameeleza Ndugu Kingu.

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa zimeongozwa na kauli mbiu Tunza Mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa Ustawi wa viumbe hai kwa uchumi wa Taifa.



AFYA NA USTAWI WA VIJANA NI CHACHU YA MAFANIKIO YA ELIMU

May 26, 2023

 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kupitia mradi wake wa Haki Zetu, Maisha yetu, Mustakabali Wetu unaofahamika kama O3 Plus, likishirikiana na Chuo kishiriki cha elimu Dar es Salaam (DUCE) limekabidhi jengo la kituo cha ushauri nasihi na jengo maalum kwa ajili ya vijana katika kituo cha afya chuoni hapo ili kuboresha utoaji wa huduma rafiki kwa vijana.


Uboreshaji wa jengo maalum la vijana katika kituo cha afya na jengo la utoaji ushauri nasihi (council unit) umefadhiliwa na UNESCO kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya na ushauri nasihi zinazokidhi mahitaji ya vijana.

“UNESCO inaamini kwamba maboresho haya yataongeza hamasa kwa vijana katika kupata taarifa na huduma za afya hivyo kuwawezesha kutunza na kujali afya zao.Hii itasaidia vijana kuwa na afya bora na kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli zao za kielimu na zile za maendeleo kwa ujumla ” anasema Bw. Mathias Luhanya-Mkuu wa Programu ya Afya na Ustawi kutoka UNESCO

Maboresho haya katika utoaji wa huduma za afya yanafanyika pia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kampasi ya Mwalimu Nyerere) na Chuo Kikuu cha Dodoma na ni ishara kuwa Mradi umelenga katika kuacha alama ya kudumu inayogusa maisha ya vijana moja kwa moja.

Aidha, mbali na uboreshaji wa huduma hizi za afya, kupitia Mradi huu wa O3 Plus, zaidi ya wanafunzi 100,000 waliopo katika vyuo vikuu 17 hapa nchini wanategemewa kunufaika na afua mbalimbali zikiwemo zile za uanzishwaji wa madawati ya jinsia vyuoni, utoaji wa elimu ya kina ya stadi za maisha zinazozingatia VVU/UKIMWI, Afya ya uzazi na jinsia na matumii sahihi ya rasilimali (CSE) kupitia kozi mtandao na waelimisha rika, pamoja na utoaji wa mafunzo kwa watoa huduma za afya juu ya utoaji wa huduma rafiki za afya kwa vijana.

Mkuu wa Ofisi UNESCO, Bw.Michael Toto akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la Kituo cha Afya katika Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), uzinduzi ambao umefanyika Mei 25,2023 Jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Ofisi UNESCO, Bw.Michael Toto (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wawakilishi kutoka Wizara ya Elimu katika Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Ofisi UNESCO, Bw.Michael Toto (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Ofisi UNESCO, Bw.Michael Toto (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Waratibu wa Mradi wa O3 Puls katika Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Ofisi UNESCO, Bw.Michael Toto akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam

Mkuu wa Programu ya Afya na Ustawi kutoka UNESCO Bw.Mathias Luhanya akizungumza katikaMkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam
Msimamizi wa Mradi wa O3 Plus Dar es Salaam, Dkt.Alfred Msasu akiwasilisha Mada yake katika Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam

Msimamizi wa Mradi Mkoa wa Dodoma Bw.Faraja Msangi akiwasilisha Mada yake katika Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam

Bw.Clement Kihinga kutoka HISP akiwasilisha Mada yake katika
Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Kamati Tendaji ya Mradi wa O3 Plus uliofanyika Mei 25,2023 DUCE Jijini Dar es Salaam

WADAU SEKTA YA WANYAMAPORI NA MISITU WAONA MWANGA UTENDAJI WIZARA YA MALIASILI, WAMPONGEZA MHE. RAIS

May 26, 2023

 


Na John Mapepele

Wadau wa Sekta za Wanyamapori na Misitu nchini wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanywa hivi sasa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii hususan kasi ya utendaji wa viongozi wa wizara, ushirikishwaji wa wadau na kutangaza utalii kimataifa.

Wadau hao wametoa kauli hizo kwenye mkutano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa sekta za Wanyamapori na Misitu uliofanyika leo Mei 25, 2023 jijini Arusha.

Wamefafanua kuwa katika kipindi kifupi baada ya Rais Samia kuteua viongozi wapya wa Wizara, mwanga wa matumaini ya maendeleo na mapinduzi makubwa umeanza kuonekana.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji na Wauzaji wa Nyamapori Tanzania, Fransis Nade amesema katika kipindi hiki cha takribani miezi mitatu kumekuwa na ushirikishwaji mkubwa kwa wadau ambapo kumekuwa na mapitio makubwa ya maeneo mbalimbali ambayo yatasaidia kuboresha uhifadhi wa raslimali nchini.

Amesema njia pekee ya kuimarisha sekta hizo ni kuwashirikisha wadau kwa kufanya majadiliano ili waweze kutoa changamoto wanazokabiliana nazo hatimaye sekta iweze kutoa mchango mkubwa katika taifa ambapo mkutano wa leo umeshirikisha wadau wote.

“Ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutuletea mabadiliko haya katika kipindi hiki kwenye Wizara yetu, Mungu ambariki sana kwani kazi kubwa imefanywa na viongozi wa wizara tunaamini sekta zetu zinakwenda kuchangia kiasi kikubwa kwenye uchumi wetu." amefafanua mdau wa Wanyamapori Jackson Msome.


Mdau wa asali mwenye uzoefu wa miaka 53 katika sekta hiyo, Kimishua Yona amesema kiwango ambacho Waziri Mchengerwa alielekeza katika kilele cha siku ya Misitu na Asali cha kuzalisha tani 138000 kutoka tani 35000 kwa mwaka za sasa kinaweza kwenda mara mbili zaidi kama wananchi watatumia utaalam.

Akiongea na wadau hao, Mchengerwa amesema katika kipindi hiki kifupi amebaini changamoto kadhaa ambazo amesema zinakwenda kutatuliwa.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na Kampuni za Uwindaji wa Kitalii kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani, (Value Added Tax) kwa huduma zisizotozwa kodi (Non - taxable services).
Kumekuwa na ucheleweshaji wa migawo ya fedha kwa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii kutokana na kubadilishwa kwa mfumo wa ukusanyaji wa fedha na uhakiki wa viwango vinavyopaswa kutumwa.

Aidha, amesema kuwepo kwa tozo nyingi katika biashara ya mazao ya misitu na amefafanua kuwa Wizara imechukuwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na mamlaka zinazohusika ili kuona uwezekano kupunguza viwango vya tozo.


Mathalani Tozo ya CESS imepunguzwa hadi asilimia 3. Wizara inaendelea kulifanyia kazi suala hili.Pia kukosekana kwa wataalam wa kada ya misitu na ufugaji nyuki katika Halmashauri za Wilaya nyingi nchini hali inayosababisha mwitikio mdogo wa wananchi kushiriki katika shughuli za sekta za misitu pamoja ufugaji nyuki na kukosekana kwa soko la pamoja la mazao ya nyuki.

Amewataka watendaji wa Wizara kubadilika  na kuwa na uchungu wa nchi yao.

JUKWAA LA KIAFRIKA LA UONGOZI INSTITUTE LAOMBA VIONGOZI KUREKEBISHA HALI YA KILIMO ILI KUFUNGUA BIASHARA

May 26, 2023

 


Mlezi wa Africa Leaders Forum Rais mstaafu Dkt Jakaya Kikwete akihutubia mkutano huo ,Accra,Ghana Alhamis.Viongozi wengine wa Kiafrika waliohudhuria ni pamoja na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Tunisia Dr. Mohamed Moncef Marzouki, Rais wa zamani wa Nigeria Dr Goodluck Ebele Jonathan, Rais wa zamani wa Benin, Thomas Boni Yayi, Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn Boshe, na Rais wa zamani wa Sierra Leone Dr. Ernest Bai Koroma.Picha na Imani Nsamila



WAJUMBE katika mkutano  wa Uongozi wa Bara la Afrika wamezitaka nchi za Afrika kujenga mfumo imara wa ugavi wa thamani kwa kilimo kwasababu sekta hiyo inatoa fursa bora ya kuongezeka kwa biashara ndani ya Afrika.

Viongozi na washiriki wengine walibainisha kuwa Afrika ina ardhi ya kutosha kwa kilimo ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji na maendeleo ya bara hilo, ikishikilia zaidi ya nusu ya ardhi ya kilimo duniani na rasilimali kubwa za maji zenye uwezo wa kutosha kwa umwagiliaji.

Zaidi ya hayo, kwa idadi ya watu inayokadiriwa kuwa bilioni 1.3 ambapo wengi wao (angalau asilimia 70) wanaishi vijijini na wanajishughulisha na kilimo kama shughuli yao kuu ya kiuchumi inaonekana kuwa ni jambo la kushangaza kwamba bara hilo bado linachangia asilimia 4 tu ya uzalishaji wa kilimo ulimwenguni pote, walibainisha.

Akizungumza katika Mkutano huo wa Uongozi wa Afrika (ALF) ambao ulianza hapo Alhamisi, Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete alibainisha kuwa sekta hiyo ilichangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa na mapato ya fedha za kigeni kwa bara hilo na hivyo kutoa fursa ya kipekee kwa biashara ya ndani ya Afrika inayohitajika sana.

“Hakuna sekta inayowaajiri watu wengi kama kilimo, lakini bado haijafikia uwezo wake kamili, kwa hiyo kujadili jinsi ya kufungua uwezo wake ni jambo sahihi kufanya. Zaidi inahitajika kufanywa katika nchi za Afrika na kuunganisha na jinsi ya kuondoa umasikini, kuondoa upungufu wa chakula na njaa. Hii ni fursa kubwa kwa ushirikiano katika mnyororo wa biashara ya ndani ya Afrika,”alisema.

Taasisi ya UONGOZI imeandaa Mkutano wa 7 wa ALF mwaka huu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kwa kauli mbiu "Kukuza biashara ndani ya Afrika ili kufungua uwezo wa kulimo barani Afrika.

"Kama Mwenyeji na Mlezi wa ALF, Dkt. Kikwete, alibainisha kwamba kilimo ni nguzo kuu ya watu wengi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na utinwa mgongo wa uchumi, hakuna mahali bora pa kuanza katika kipaumbele cha kuzingatia na uvumbuzi ikiwa bara linataka kuongeza biashara kati yao," alisisitiza.

Alisema sekta hii muhimu haijafanikiwa kufanya kazi kikamilifu kwasababu ya vizuizi vingi vinavyozuia utumiaji kamili wa uwezo wake. Kwahivyo, kwa Jukwaa hili kujadili kufungua uwezo wa kilimo barani Afrika ni jambo sahihi kufanya.

Dkt. Kikwete alikiri kuwa juhudi zinafanywa na Serikali za Afrika kwa ajili ya wakulima wadogo wa Kiafrika na wadau wengine ili kubadilisha hali ya kilimo barani Afrika na kwamba tayari kuna maendeleo makubwa yaliyofikiwa na mafanikio mengi yamepatikana.

"Hatahivyo, kuna mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kilimo kiweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji na maendeleo ya mataifa ya Afrika na ustawi na utajiri wa watu wa Afrika," alisema.

"Mpaka sasa mambo yamekwenda vizuri lakini bado hayatoshi kama inavyothibitishwa na kiwango cha umasikini katika maeneo mengi ya vijijini ambap watu wetu wengi wanaishi na ripoti zisizoisha za watu kusumbuliwa na ukosefu wa chakula na njaa barani Afrika." alisema.

Alikuwa na mtazamo kwamba ripti za Afrika kuwa bado inatumia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni kununua chakula hazifurahishi kusikia. Vilevile, aliongeza kwamba ripoti za Afrika kuwa bado inauza malighafi za kilimo kwa nchi zilizoendelea na kununua bidhaa zilizotengenezwa kutokana na malighafi hizo ambazo Afrika ilizipeleka nje hazifurahishi.

"Uwekezaji katika watu wetu hasa wakulima wadogo na vijana wetu; uwekezaji katika taasisi na miundombinu yetu ili kuhakikisha mazingira mazuri ya kufanya biashara yanahitajika; na zaidi ya yote kujitolea kwetu kuwekeza katika ajenda ya muda mrefu ya Afrika kuliko vipaumbele vya ndani vya muda mfupi.

"Akifungua Mkutano mapema Rais wa Ghana, Nana Addo Dankwa Akufo-Addo, alisema biashara ndani ya Afrika ni moja ya chini kabisa katika eneo hilo na bado imegawanyika na uwezo mdogo wa uzalishaji.

"Kuna nguvu katika umoja. Ikiwa nchi zote 54 zenye watu bilioni 1.3 na Pato la Taifa la dola trilioni 3 zitashirikiana, hii ni fursa kubwa ya ukuaji na kukabiliana na ongezeko la bei na kutokuwa na uhakika wa kimataifa." alisema.

Alisema kuwa kwa kuwa hii inatoa fursa sekta binafsi, serikali lazima iwe na ujasiri kupitia hatua zenye mkakati wa kujenga thamani na lengo kubwa zaidi.

Katibu Mkuu wa AfCFTA, Wamkele Mene, pia alibainisha kuwa Afrika bado ni bara linalonunua chakula kutoka nje kwa kiwango kikubwa, na gharama ya kununua chakula kutoka nje ilifika dola bilioni 80 kati ya mwaka 2015 na 2017.

"Tunahitaji kufungua uwezo wa jamii zetu za vijijini ili kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani wa kimataifa na kuwezesha wakulima wadogo kuwa sehemu ya biashara ya kimataifa. Kwa kutambua jukumu la sekta binafsi na biashara zinazomilikiwa na wanawake, AfCFTA imetoa kipaumbele kwa kilimo na usindikaji." alisema

Akitoa muktadha wa kikao cha jumla, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekele alisema soko la kilimo la Afrika bado limegawanyika na kusambaa, ambayo inafanya hali ya ujumuishaji kama njia ya kuongeza soko na kufanya bara kuwa mchezaji wa kimataifa.

Aliomba taasisi za kifedha kushirikiana katika soko kama sehemu ya suluhisho la kupata fedha za kusaidia mifumo ya kilimo barani Afrika. 

Viongozi wengine wa Kiafrika waliohudhuria ni pamoja na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Tunisia Dr. Mohamed Moncef Marzouki, Rais wa zamani wa Nigeria Dr Goodluck Ebele Jonathan, Rais wa zamani wa Benin, Thomas Boni Yayi, Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn Boshe, na Rais wa zamani wa Sierra Leone Dr. Ernest Bai Koroma.

Pia walihudhuria  sekta binafsi kutoka kote barani Afrika, wakitafuta kutoa nafasi ya kushiriki uzoefu na ufahamu wao katika kufanikisha biashara ya kilimo kati ya nchi za Afrika. Kupitia kipindi cha ukimya na kikao cha kuonyesha video zake zenye nguvu kuhusu mageuzi ya Afrika, wajumbe walitoa heshima fupi kwa Mpatanishi wa ALF na Rais wa zamani Benjamin Mkapa.

Tukio hili la siku 2 limeangazia uwezo wa kilimo barani Afrika na fursa zinazojitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kushiriki uzoefu na masomo kuhusu vikwazo (ndani na kimataifa) katika kufikia uwezo wa kilimo barani Afrika, kujadili uwezo na vikwazo, pamoja na mahitaji halisi na ya vitendo ya kutekeleza AfCFTA ndani ya muktadha wa kilimo barani Afrika na kutambua vipaumbele na ramani ya barabara kwa utekelezaji wa mtazamo wa biashara ya kilimo chini ya AfCFTA ili kufikia lengo lake la kiuchumi la kubadilisha.

Wadhamini wa tukio walikuwa ni AfCFTA, Benki ya NMB, Benki ya CRDB, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, NBC Bank Tanzania, ASAS CommNet na RAHISI, DTB Tanzania, Karibu Travel, Jarida la Uongozi wa Kiafrika na wengine kadhaa.