AWAMU YA TATU KUJA NA NGUZO ZA ZEGE

December 28, 2016


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani, akizungumza jambo wakati wa Mkutano wake na wananchi wa Kata ya Ngwanseri,wilaya ya Muleba, wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango,akizungumza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalema ni kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili.Wengine katika picha ni baadhi ya Viongozi wa Halmashauri hiyo,Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, REA,TANESCO, na Wakandarasi wanaotekeleza mradi husika.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani, akizungumza jambo wakati wa Mkutano wake na wananchi wa Kijiji cha Kishuro,Kata ya Ngenge Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera. Dkt.Kalemani amefanya ziara Wilayani humo ya kukagua Mradi utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili na kueleza mipango ya Serikali kutekeleza Awamu ya Tatu ya mradi husika.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani, (Wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Prof.Anna Tibaijuka (wa pili kushoto),Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango,(wan ne kushoto)pmoja na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, REA,TANESCO, na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mmoja wa Wananchi katika akiuliza jambo wakati wa mkutano wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kaleman
Wananchi wa Kata za Ngwanseri na Ngenge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt.Medard Kalemani na ujumbe wake wakati wa ziara yake a kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili wilayani Muleba.


Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini Prof.Anna Tibaijuka (kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt.Medard Kalemani ( katikati) mara baada ya kumaliza mkutano wake na wananchi wa Kijiji cha Kishuro. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango.


Wananchi wa Kijiji cha Kishuro Wilaya ya Muleba, wakisoma Jarida la Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakati wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt.Medard Kalemani (hayupo pichani) akieleza utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili na mipango ya Serikali ya kutekelza REA Awamu ya Tatu.


Na Asteria Muhozya, Muleba

Imeelezwa kuwa, Serikali imepanga kutumia Nguzo za Zege katika utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaotarajia kuanza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari, 2017 chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Pili katika Kata za Ngenge na Ngwanseri, Wilayani Muleba Mkoani Kagera, pamoja na kueleza mipango ya Serikali katika utekelezaji wa mradi husika Awamu ya Tatu.

Dkt. Kalemani amesema kuwa, lengo la kutumia nguzo hizo za zege ni kutokana na uimara wake utakaowezesha upatikanaji umeme wa uhakika na kuepuka kuchomwa na kuongeza kuwa, tayari nguzo hizo zimeanza kutumika katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumzia utekelezaji wa REA Awamu ya Pili, amesema Serikali imetekeleza mradi huo kwa kasi kubwa kutokana na dhamira yake ya kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2025 asilimia 75 ya Watanzania wawe wameunganishwa na nishati hiyo ambayo ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi.

“ REA awamu ya pili imekamilika kwa kiwango kikubwa. Vipo baadhi ya vijiji havijafikiwa kutokana na dosari ndogo ndogo lakini tutavikamilisha kuwezesha utekelezaji wa Awamu ya Tatu. Hata katika Wilaya hii vipo na tayari nimemwelekeza Mkandarasi kukamilisha kazi hiyo haraka,”amesisitiza Dkt. Kalemani.

Akielezea mipango kwa Awamu ya Tatu, amesema kuwa, Serikali imelenga kuhakikisha kuwa, awamu hiyo inavifikia vijiji vyote ambavyo havikuunganishwa katika Awamu ya Pili, visiwa vyote, Taasisi mbalimbali, Sehemu zinazotoa Huduma za Kijamii zikiwemo za Afya, shule na visima vya maji.

Aidha, alisema kuwa, kukamilika kwa utekelezaji wa Miradi Ujenzi wa njia za Kusafirisha umeme wa Msongo Mkubwa wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na Singida kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na kuchochea uchumi wa viwanda hususan katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Wakati huo huo, Dkt. Kalemani ametumia fursa hiyo kuzitaka Halmashauri zote nchini kushirikiana na TANESCO kuweka utaratibu shirikishi ambao utawawezesha wananchi kupata huduma za kuunganishiwa nishati hiyo kupitia utaratibu wa kuanzisha madawati ya TANESCO katika maeneo yatakayotambuliwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi.

“TANESCO na Halmashauri, pangeni namna ya kuwawezesha wananchi kufikiwa kwa urahisi na huduma za kunganishwa nishati ya umeme. Mkubaliane kupanga siku maalum ambayo wananchi watahudumiwa. Serikali inataka kila mwananchi apate umeme, hivyo tuweke utaratibu ambao utarahisisha na kuwezesha azma hiyo kufikiwa kwa haraka,” amesisitiza Dkt. Kalemani.

Pia, Dkt. Kalemani amewataka Wakandarasi wote wakati wa utekelezaji wa miradi ya Awamu ya Tatu kuhakikisha kuwa, wanajitambulisha katika Halmashauri na Mamlaka nyingine ili waweze kutambulika ili kuepusha udanganyifu.

Vilevile, Dkt. Kalemani ameitaka TANESCO kuwaidhinisha Wakandarasi wote watakaofanya kazi ya ‘wiring’ katika nyumba za wananchi katika utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu ikiwemo kutoa orodha zao ili kuwapunguzia wananchi kero ikiwemo kuwaepusha na utapeli unaofanywa na baadhi ya wasiowaaminifu.

Akizungumzia Sekta ya Madini, Dkt. Kalemani amewahamasisha wachimbaji wadogo wadogo kujiunga katika vikundi ikiwemo kujisajiri katika Ofisi za Madini zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwawezesha wachimbaji hao kuomba ruzuku kupitia vikundi pindi zinapotolewa na Serikali.

Katika ziara ya kutembelea Kata hizo, Dkt. Kalemani ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyango, Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, REA, TANESCO na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA Awamu ya Pili Wilayani humo.

VAZI LA KHANGA KUTUFUNGIA MWAKA 2016 PALE REGENCY PARK HOTEL DON’T MISS!

December 28, 2016

MAAMBUKIZO YA VVU NA UKIMWI YASHUKA KWA ASILIMIA 20 NCHIN

December 28, 2016
 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko (katikati), akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo, wakati akitoa taarifa kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi katika mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka huu. Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Muitikio ya Kitaifa, Dk.Hafidhi Amri, Mkuu wa Kitengo cha Sheria Tacaids, Elizabeth Kaganda na Mkurugenzi wa Habari na Ulaghibishi, Jumanne Issango.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko (kushoto), akisisitiza jambo kwenye mkutano huo. Kulia ni Mkurugenzi wa Habari na Ulaghibishi, Jumanne Issango.
 Mkutano na wanahabari ukiendelea.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 Wapiga picha wakichukua taarifa hiyo.
Wanahabari wakiwa kazini.

Na Dotto Mwaibale

MAAMBUKIZO Mapya ya VVU na Ukimwi yameshuka nchini  kwa zaidi ya asilimia 20 kati ya mwaka 2010 na 2015 imefahamika.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari katika mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka huu.

Alisema maambukizo mapya ya VVU yaliyokadiriwa kuwa watu milioni 2.1 kwa mwaka 2015 Duniani kote wakati maambukizo mapya yameshuka kwa asilimia 50 miongoni mwa watoto duniani.

Alisema watoto 290,000 wapya waliambukizwa mwaka 2010 na watoto 150,000 waliambukizwa mwaka 2015 ambapo maambukizo mapya kwa watu wazima hayajashuka tangu 2010 duniani.

Katika hatua nyingine Dk. Maboko alisema Tafiti  zimeonesha kuwa wanawake ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya VVU kwa upande wa Tanzania Bara ukilinganisha na wanaume.

Alisema maambukizo VVU kwa upande wa Tanzania Bara ni asilimia 5.3 wanawake wakionesha kuathirika zaidi kwa asilimia 6.2 ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 3.8.

"Katika utafiti huo wa mwaka 2011 na 2012 ulionyesha kuwa Mkoa wa Njombe ulikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizo ukiwa na asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mbeya kwa asilimia 9" alisema Dk.Maboko.

Dk.Maboko alisema Mkoa wa Manyara ulikuwa na kiwango kidogo cha maambukizo ya asilimia 1.5 lakini takwimu za ndani ya mkoa huo eneo la Mirelani kwenye mgodi wa Tanzanite maambukizo ya VVU yalikuwa ni asilimia 16 kiwango ambacho ni cha juu ya Mkoa wa Njombe.

Dk. Maboko aliwaomba wananchi kote walipo kutobweteka kwa mafanikio yaliyo ya mapambano dhidhi ya VVU na ukimwi na kuwa yawe endelevu hata katika maeneo au mikoa ambako kuna maambukizo kidogo ya VVU.

Alisema kama nchi tunatakiwa kuweka nguvu nyingi kifedha na kimkakati katika maeneo na makundi yenye kiwango kikubwa cha maambukizo ya VVU ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa takwimu za VVU na Ukimwi ili tuendelee kubaini na kupanga mipango dhidi ya ugonjwa huo inayoongozwa na takwimu.

Aliongeza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi (UNAIDS) limeweka malengo ya muda wa kati ya tisini tatu (90-90-90). 90 ya kwanza ikimaanisha asilimia tisini ya watu wote wanaokisiwa kuwa na VVU kujua hali zao na 90 ya pili ikimaanisha kuwa asilimia tisini ya waliobainika kuwa na VVU kuanza kutumia dawa za kupunguza makali 
ya VVU (ARV) mara moja na 90 ya tatu ya walioanza dawa waweze kuwa na ufubazo endelevu wa virusi vya ukimwi mwilini mwao.

Dk. Maboko alitoa mwito kwa wananchi, Taasisi za kijamii, Serikali, watu binafsi na makampuni ya kibiashara kuchangia mfuko wa udhamini wa masuala ya ukimwi (AIDS TRUST FUND-ATF) ulioanzishwa na serikali ili kuondokana na utegemezi kwa wafadhili.