TASAC YATOA WITO KWA WASAFIRI WANAOTUMIA VYOMBO VYA MAJINI

May 31, 2023


Afisa Mfawidhi wa Shirika la TASAC Mkoani Tanga Kapten Christopher Shalua  (kushoto) akitoa maelezo kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara Conrad Millinga wa kwanza kulia ambaye alimwakilisha Waziri wa Viwanda wakati alipotembelea banda lao katika maoanyesho ya 10 ya biashara na Utalii yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwahako Jijini Tanga
Afisa Mfawidhi wa Shirika la TASAC Mkoani Tanga Kapten Christopher Shalua  akizungumza na vyombo vya habari katika Banda lao kwenye  maoanyesha ya 10 ya biashara na utalii yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwahako Jijini Tanga
Afisa Masoko Mwandamizi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Martha Kelvin (kushoto) akimkabidhi zawadi Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara Conrad Millinga kulia wakati alipotembelea Banda lao


Na Oscar Assenga,TANGA

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito kwa wasafiri wanaotumia vyombo vya Usafiri majini kuhakikisha wanatumia vyombo vilivyo ruhusiwa kisheria kubeba abiria na sio kupanda vyombo vya kusafirisha mizigo ikiwemo majahazi.

Wito huo ulitolewa leo na Afisa Mfawidhi wa Shirika hilo Mkoani Tanga Kapten Christopher Shalua wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya 10 ya biashara na utalii yanayoendelea katika viwanja vya Mwahako Jijini Tanga

Aidha, alisema kwa sababu viwango vya vyombo vipo kwenye madaraja tofauti ni vema kila chombo kikatumika kulingana na matumizi huzika yaliyothibitishwa na amewataka  wananchi wa Tanga kwa ujumla kutembelea Banda lao ili kupata elimu zaidi.

Alisema TASAC imeshiriki maonesho hayo kwa ajili ya kuwafikia wananchi hususani wanaoishi maeneo ya fukwe na kuwaelimisha kuhusu Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira Majini pamoja na majukumu yanayotekelezwa na Shirika hilo kwa Mujibu wa Sheria. 

Hata hivyo alisema kwamba jukumu lao pia ni kuhakikisha wanasimamia Bandari kuhakikisha wanatoa huduma katika viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuweza kuchochea ukuaji wa uchumi nchini .

Mwisho.

DKT. NCHEMBA AWAAGIZA WATAALAM WA UCHUMI WA KITAIFA NA KIMATAIFA KUTAFUTA SULUHU YA UPUNGUFU WA DOLA ZA MAREKANI KATIKA SOKO LA FEDHA

May 31, 2023
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akifungua kikao cha wataalamu wa Wizara hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu tathmini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), jijini Dodoma.

 

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akimsikiliza Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Harris Tsangaride wakati wa kikao cha wataalamu wa Wizara hiyo na IMF, waliokuja nchini kufanya tathmini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), Bw. Harris Tsangaride baada ya kufungua kikao cha wataalamu wa Wizara hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), waliofika nchini kwa ajili ya kufanya tathmini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM-Dodoma)





Na Farida Ramadhani-Dodoma


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango na ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kujadili namna ya kushughulikia athari za upungufu wa dola za Kimarekani katika mzunguko wa fedha ili kunusuru uchumi wa nchi zinazoendelea.

Mhe. Dkt. Nchemba (Mb) ametoa maagizo hayo wakati wa kufungua kikao kilichowashirikisha wataalam kutoka Shirika la Fedha na Kimataifa (IMF) waliowasili nchini kwa ajili ya kufanya tathimini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), kwa kushirikiana na wataalam wa ndani wa Serikali.

Alisema mabadiliko ya Sera za Fedha nchini Marekani ya kubana matumzi na kupunguza dola kwenye mzunguko wa fedha, yameleta athari zinazoonekana mpaka kwenye nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
“Tumekuwa tukirejea Uviko na vita baina ya Urusi na Ukraini kama moja ya vitu vinavyoathiri uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania lakini upungufu wa dola unaathiri uchumi kwa kiwango kikubwa ikiwemo uagizaji wa mafuta na uagizwaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumika katika shughuli za Sekta Binafsi”, alisema Dkt. Nchemba.

Alisema ni vema kutafuta namna ya kushughulikia jambo hilo kisera ili kunusuru nchi zinazoendelea kwa kuwa sekta ya nje ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.

Kwa upande wake Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Harris Tsangaride, alisema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha nchi inaendelea kupiga hatua kiuchumi na kijamii.
Aliipongeza Serikali kwa Sera zake nzuri ambazo zinaendelea kutekelezwa katika kukabiliana na athari za vita ya Ukraine na kuongeza kuwa ni matarajio yao kuwa zitaendelea kuchokea ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi.

Bw. Tsangaride alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache katika kanda ambazo zinafanya vizuri katika kutekeleza programu mbalimbali kwa kushirikiana na Shirika hilo na hivyo katika kikao hicho watajadiliana namna bora ya kuendelea kuiona nchi ikifanya vizuri zaidi. 

Mwisho.

BWAWA LA KIDUNDA KULETA AHUENI DAR NA PWANI KIPINDI CHA KIANGAZI

May 31, 2023

 Serikali kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi Bwawa la Kidunda litakalojengwa Mkoani Morogoro na kugharimu Tsh Bilioni 335 na litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji kwa yatakayotumika kwa miaka mitatu mfululizo.


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Morogoro, Kaimu Afisa Mtendaji DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema lengo la utekelezaji mradi huo ni kuwezesha mitambo ya maji ya Ruvu juu na Ruvu chini kuwa na maji ya kutosha ili kuzalisha maji kipindi cha kiangazi.

Aidha Kingu amebainisha kuwa bwawa hilo litakapokamilika litakuwa lina hifadhi maji kipindi cha masika ili maji hayo yaweze kutumika nyakati za kiangazi.

Mbali na upatikanaji wa maji kwa uhakika, Ndugu Kiula ameeleza faida za mradi huo na namna utakavyotoa fursa mbalimbali kwa Taifa ikiwemo Ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 101, uzalishaji wa umeme megawatt 20, uvuvi na utalii ambavyo kwa pamoja vitawanufaisha Wananchi kwa maeneo husika kwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi.

“Ujenzi wa mradi wa bwawa la Kidunda utaenda kuleta Uhakika wa upatikanaji wa maji kwa muda wote kwa mwaka mzima lakini pia Kuzalisha umeme katika bwawa la kidunda wa Megawati 20 zitakazoenda kuingia katika Gridi ya taifa pamoja na Kutunza hali ya mazingira kwa viumbe hai.” Aliongeza

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Isalama ya Wilaya ya Morogoro Mjini ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Rebeca Msemwa ameipongeza Serikali kwa udhubutu wa utekelezaji wa mradi na kutoa wito kwa DAWASA kuusimamia na kuutekeleza mradi kwa ukamilifu ili ulete manufaa kwa Watanzania.

“Tunajivunia utekelezaji wa mradi huu katika Mkoa wetu wa Morogoro, Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha kiangazi hivyo hatuna budi kuunga juhudi hizi kwa kuhakikisha DAWASA wanatekeleza mradi huu kwa ukamilifu kama ilivyo matarajio ya Watanzania “. Alisisitiza

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bonde la Wami Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi ameeleza mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha vyanzo vyote vinavyoingia katika bwawa la Kidunda linakuwa na maji ya kutosha kwa kuzuia shughuli zote za uharibifu zinazosababishwa na binadamu au mabadiliko ya tabia ya nchi.

"Tumejipanga kufanya uthamini na tathmini katika maeneo yote yanayozunguka chanzo cha mto Ruvu na kutangazwa kuwa maeneo ya uhifadhi kwa kutenga shilingi Bilioni Nne ili kuhakikisha bwawa la Kidunda linatoa suluhu ya upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani". Alisema Mhandisi Mmasi

Mradi wa Bwawa la Kidunda unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) unatarajia kuanza rasmi Juni 18, 2023 kwa kipindi cha miaka mitatu huku likitarajiwa kupunguza changamoto za huduma za maji kwa Wakazi wa Mikoa ya Dar es salaam na Pwani.