DK NCHIMBI ALAKIWA KWA SHANGWE NA MKUTANO MKUBWA UBARUKU, MBARALI

April 18, 2024

 Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amepokelewa kwa shangwe na nderemo na wananchi wa Mbarali, wakiongozwa na vijana waendesha bodaboda, baada ya kuwasili na msafara wake katika Kata ya Ubaruku, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, leo Aprili 18, 2024, akitokea Mbeya Mjini.


Dk Nchimbi alisimama kuwasalimia wananchi hao wa Ubaruku, akiwa njiani kuelekea Mkoani Njombe ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 6 ya Nyanda za Juu Kusini, ambapo ameambatana na Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa Ndg. Amos Makalla pamoja na Katibu wa NEC - Oganaizesheni Ndg. Issa Haji Gavu.







WAZIRI JERRY SILAA KUONGOZA KLINIKI YA ARDHI TANGA

April 18, 2024

Na Oscar Assenga,TANGA

WAZIRI wa Ardhi,Nyumba na Mendeleo ya Makazi Jerry Silaa anatarajiwa kuongoza Kliniki ya Ardhi kwa mkoa wa Tanga itakayofanyika kuanzia Aprili 22 mpaka 28 mwaka huu ikifanyika kwenye maeneo mawili Kijiji cha Miaka 21 Chumbageni Tanga na Korogwe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo,Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tanga Tumaini Gwakisa alisema zoezi hilo litafanyika kwenye maeneo mawili ambapo litaanzia Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Tanga eneo la Kijiji cha miaka 21 Chumbageni kuanzia Aprili 22 mpaka 25 mwaka huu.

Alisema baada ya kumaliza kwa Tanga wataelekea wilayani Korogwe ambapo litafanyika kuanzia Aprili 26 mpaka 28 mwaka hu na uendeshwaji wa program hiyo utasimaiwa na itaongozwa na Waziri wa Ardhi Jerry Silaa akiwa na wataalamu wa Wizara hiyo.

“Nichukue nafasi hii kwaalika wananchi wote wa mkoa wa Tanga kuhudhuria na kupata huduma mbalimbali za sekta ya ardhi katika maeneo ambayo kliniki hiyo itafanyika kwani kutakuwa na utatuzi wa migogoro ya ardhi ambapo Waziri atasikiliza kero mbalimbali za Migogoro hiyo”Alisema

Alisema pia kutakuwa na utolewaji wa elimu kuhusu usimamizi wa ardhi pamoja na uwepo wa kituo jumuishi kitakachotoa huduma ya kupokea maoni mbalimbali na utoaji hati miliki ,ukadiriaji wa kodi ya ardhi na ulipaji wa kodi ya ardhi.

Gwakisa aliwataka wananchi wa mkoa wa Tanga kuhudhuria na kushiriki ambapo Waziri atakuwepo na wataalamu kutoka Wizarani

MKUTANO WA 10 WA AFIIA WAFUNGULIWA JIJINI ARUSHA

April 18, 2024



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akiagana na Waziri wa Fedha, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango - Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum pamoja na viongozi wengine wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) mara baada ya kufungua Mkutano wa 10 wa Shirikisho hilo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akionesha tuzo aliyokabidhiwa na Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) wakati wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho hilo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Kushoto ni Waziri wa Fedha Ofisi ya Rais Fedha-Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum na kulia ni Rais wa Chama cha Wakaguzi wa Ndani Tanzania, Dkt. Zelia Njeza.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akikabidhiwa tuzo na Rais wa Chama cha Wakaguzi wa Ndani Tanzania, Dkt. Zelia Njeza iliyotolewa na Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) wakati wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho hilo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).


Waziri wa Fedha na Mipango Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Saada Mkuya akiteta jambo na pamoja Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG), Bw. Benjamini Magai na viongozi wengine wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) mara baada ya kufunguliwa kwa Mkutano wa 10 wa Shirikisho hilo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha na Kamati ya maandalizi ya Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) Pamoja na wajumbe wengine wa mkutano.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akiwa katika picha ya pamoja na watoa mada pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) mara baada ya kufungua mkutano.

Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Leornad Mkude (kushoto), akisikiliza hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Wizara ya Fedha, Bw. Moses Dulle (wa kwanza kiti cha pili) na Mkaguzi Mkuu wa Ndani Msaidizi Bw. Mwanika Semroki, wakisikiliza mada zilizokuwa zinatolewa wakati wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu Wizara ya Fedha Bw. Lisius Mwenda, (wa kwanza kulia), akifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 10 wa Shirikisho la Taasisi za Wakaguzi wa Ndani Afrika (AFIIA) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Fedha)

RAIS SAMIA ATUNUKIWA SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI (HONORIS CAUSA) YA UCHUMI NA CHUO KIKUU CHA ANKARA NCHINI UTURUKI

April 18, 2024

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubiawagenimbalimbali, viongozi na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ankara, mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) ya Uchumi kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki Profesa Necdet Unuvar kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo tarehe 18 Aprili, 2024. 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) ya Uchumi kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki Profesa Necdet Unuvar kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo tarehe 18 Aprili, 2024.  


NCHI ZA SADC ZAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MAONO YAKE KATIKA USIMAMIZI WA MISITU YA MIOMBO

April 18, 2024

 

Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe.Filipe Jaciton Nyusi akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo  jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.

******************

Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community-SADC) zimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake katika usimamizi na uhifadhi wa misitu miombo hasa katika kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kuelekea nishati safi ifikapo mwaka 2030.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 18,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika Mkutano wa Kimataifa unaohusu Misitu ya Miombo jijini Washington DC nchini Marekani.

“Kikubwa nchi zimeweza kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akitoa maelekezo mbalimbali kwetu sisi kama Wizara na Sekta katika kuhakikisha kwamba misitu ya miombo inalindwa kwa nguvu kubwa, na kwa namna ambavyo amechukua uamuzi thabiti wa kuhakikisha kwamba inapofika mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80 ya wananchi watakuwa wameachana na matumizi wa kuni na mkaa na watakuwa wamejielekeza katika nishati safi ya kupikia” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Amesema kuwa misitu ya miombo nchini Tanzania na katika ukanda wa kusini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa misitu ambao unasababishwa na ukataji wa miti usiozingatia sheria, taratibu na kanuni, moto, kilimo cha kuhamahama, uharibifu wa vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha, amefafanua kuwa kupitia mkutano huo, wadau mbalimbali wameanza kuonesha nia ya kusaidia mpango wa utekelezaji wa Azimio la Maputo la mwaka 2022 kuhusu ulinzi na uendelezaji wa misitu ya miombo.

Amesema lengo la Mkutano huo ni kuona namna ya kuendeleza Azimio la Maputo katika kulinda na kuendeleza Misitu ya Miombo ambapo takribani asilimia 93 ya misitu ya Tanzania ni miombo ambayo pamoja na mambo mengine, inatunza wanyamapori , vyanzo vya maji na huduma nyingine za kijamii.

Naye, Kamishna Uhifadhi wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema kuwa kupitia mkutano huo nchi za SADC zimekuwa na majadiliano kuhusu kutafuta namna ya kushirikiana baina ya nchi hizo na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kupata rasilimali fedha na kukuza ujuzi na utaalamu kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa misitu hiyo.

Ameongeza kuwa kongamano hilo limehitimishwa na hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi ambapo amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kushirikiana katika kubadilishana taarifa , kukabiliana na masuala ya uharibifu wa mifumo ya ikolojia ya miombo hususan biashara haramu za mazao ya misitu na wanyamapori katika ukanda wa SADC.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Deusdedith Bwoyo amesema kuwa mkutano huo umekuwa ni wa kipekee na muhimu ambapo nchi 11 zimebaini kuwa umoja ni nguvu na kwamba kila nchi haiwezi kusimamia kwa ufanisi mkubwa misitu yake na hivyo, zimekutana na kujadili kwa pamoja changamoto za misitu ya miombo na namna ya kuunganisha nguvu na kutafuta rasilimali fedha katika usimamizi na uendelezaji wake kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (kulia) akiwa na baadhi ya Mawaziri wa nchi za SADC katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo  jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jaciton Nyusi (katikati) akifuatilia mawasilisho kuhusu misitu ya miombo kutoka kwa wawakilishi wa nchi za SADC katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo  jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024. Kushoto kwake ni Waziri wa Ardhi na Mazingira wa Msumbiji, Mhe.Ivete Maibaze na Balozi wa Umoja wa Afrika nchini Marekani, Mhe. Hilda Suka-Mafdze (kulia).

Baadhi ya washiriki wa mkutano kutoka nchi mbalimbali wakipiga makofi baada ya kikundi cha burudani cha ngoma za asili kutumbuiza katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo uliofanyika jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) na baadhi ya washiriki wakifuatilia Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo uliofanyika jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.

SERIKALI KUENDELEA KUDHIBITI ATHARI ZA MICHEZO YA KUBAHATISHA

April 18, 2024

 

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma.



(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha, Dodoma)


Na Farida Ramadhani, WF – Dodoma.

Serikali kupitia Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzuia na kudhibiti athari za michezo ya kubahatisha ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mlola, Mhe. Abdallah Shangazi aliyetaka kuwajua iwapo Serikali inatambua athari hasi kwa Jamii ya Watanzania zinazotokana na ongezeko kubwa la michezo ya kubahatisha.

Mhe. Chande alisema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 7(2)(i) cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41, mamlaka ya udhibiti ina jukumu la kuhakikisha kuwa jamii inalindwa ipasavyo dhidi ya athari hasi za michezo ya kubahatisha.

“Katika kutekeleza jukumu hilo, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuzuia na kudhibiti athari hasi zitokanazo na uwepo wa michezo ya kubahatisha, mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha udhibiti na uratibu wa sekta kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na matumizi ya mifumo ya TEHAMA,’’alisema Mhe. Chande.

Alifafanua kuwa Bodi inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za michezo ya kubahatisha, kufanya mapitio ya mara kwa mara ya mifumo ya usimamizi wa michezo ya kubahatisha pamoja na kufanya kazi ya udhibiti kwa kushirikisha wadau na mamlaka nyingine kama vile Jeshi la Polisi, TCRA na TRA.

Mhe. Chande alisema pamoja na faida za kiuchumi na kijamii zinazotokana na michezo ya kubahatisha, Serikali inatambua athari zake katika jamii endapo haitaendeshwa kwa weledi ikiwemo uraibu na kugeuza michezo ya kubahatisha kuwa mbadala wa ajira, ushiriki wa watoto katika michezo ya kubahatisha na uwepo wa michezo haramu isiyo na usajili wa mamlaka ya udhibiti.


 

WAZIRI MKUU AFUNGA MKUTANO WA SADCOPAC

WAZIRI MKUU AFUNGA MKUTANO WA SADCOPAC

April 18, 2024




Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Abeid Aman Karume Zanzibar ambako atafunga Mkutano wa Kujenga Uelewa wa Pamoja na Ufanyaji wa Kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge (SADCOPAC) kwenye hoteli ya Goilden Tulip, Aprili 18, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Mkutano wa Kujenga Uelewa wa Pamoja na Ufanyaji wa Kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge (SADCOPAC) kwenye hoteli ya Goilden Tulip, Zanzibar, Aprili 18, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kujenga Uelewa wa Pamoja na Ufanyaji wa Kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge (SADCOPAC) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofunga mkutano huo kwenye hotel ya Golden Tulip Zanzibar, Aprili 18, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
DKT. BITEKO ASEMA BWAWA LA UMEME JULIUS NYERERE LIKO SALAMA

DKT. BITEKO ASEMA BWAWA LA UMEME JULIUS NYERERE LIKO SALAMA

April 18, 2024

 



*Asema limepunguza athari za mafuriko

*Atoa pole kwa waathirika wa mafuriko Rufiji

*Aeleza jitihada za Serikali kwa waathirika

*Azungumzia umuhimu wa Nishati Safi ya Kupikia, Bei ya Gesi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Bwala la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lipo salama kutokana na kujengwa kisayansi na hivyo kuendelea kuzalisha umeme kupitia mtambo namba tisa huku mitambo mingine miwili ikiwa ukingoni kukamilika.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 18 Aprili 2024 jijini Dodoma katika mahojiano Mbashara kupitia kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC kuhusu Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.

“ Bwawa letu lipo salama kwani limejengwa kisayansi, ujazo wake wa maji ni mita za ujazo 183 na kwa takwimu za leo ni mita za ujazo 183.4, huko nyuma maji yalikuwa yakiingia mengi sana kwa kiasi cha mita za ujazo 8400 kwa sekunde hivyo yalipaswa kupunguzwa ili kuendana na ujazo wa bwawa.” Amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, bila ya kuwepo kwa Bwawa hilo athari za mvua zingeanza kuonekana tangu mwezi Oktoba mwaka jana lakini hali hiyo haikutokea mapema kwa sababu maji yalikuwa yakiijazwa katika bwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati na TANESCO ilishabaini uongezekaji wa maji katika mto Rufiji kuanzia mwezi Februari, mwaka huu na tahadhari ilianza kutolewa kuhusu kasi hiyo ya maji ili kuanza kuchukua hatua stahiki.

Dkt. Biteko ameeleza kusikitishwa kwake na athari zilizotokea kutokana na mafuriko ambayo yamesababisha athari katika maisha ya watu na mali zao na kueleza kuwa Serikali inafanya kila jitihada kurejesha hali ya kawaida kwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo.

Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini, Dkt. Biteko amesema kuwa, watu wengi bado wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia kama vile mkaa na kuni na wananchi wachache wanatumia gesi na nishati nyingine kama vile umeme.

Ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na kwamba Serikali imepitisha Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni moja ya njia za utekelezaji wa ajenda hiyo ambayo inanadiwa na Kinara wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameongeza kuwa, katika kutekeleza mpango huo wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeshatoa waraka wa kutotumia kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu kuanzia 100 na zaidi kama vile Shule na Magereza.

Kuhusu upatikanaji wa umeme wa uhakika Dkt. Biteko amesema kuwa kwa sasa uzalishaji umezidi mahitaji hivyo kinachofanyika sasa ni kuboresha miundombinu ya umeme ikiwemo ya kusafirisha umeme kwani baadhi ya sehemu laini za umeme ni ndefu sana hivyo vitajengwa vituo vya kupoza umeme takriban 83 nchini ili kuondoa athari za watu wengi kutopata umeme pale laini inapopata hitilafu.

Kuhusu Bei ya Gesi amekiri kuwa bei ni kubwa na kueleza kuwa, Serikali inaangalia kwa karibu sana suala hilo ili kuweza kupunguza gharama na hii haiishii kwenye gesi pekee bali kwenye majiko banifu na katika mwaka huu wa fedha Serikali itaanza kutengeneza majiko ya bayogesi kwenye nyumba za wananchi wanaofuga mifugo ili watumie nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.

RAIS DKT SAMIA SULUH APOKELEWA NA MWENYEJI WAKE RAIS WA UTURUKI MHE RECEP TAYYIP ERDOGAN,IKULU YA KULLIYE ANKARA NCHINI UTURUKI

April 18, 2024
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwenyeji wake Rais wa Uturuki Mhe. Recep Tayyip Erdogan mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya KulliyeAnkara nchini Uturuki tarehe 18 Aprili, 2024. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama pamoja na Mwenyeji wake Rais wa Uturuki Mhe. Recep Tayyip Erdoganwakati wa Wimbo wa Taifa wa Tanzania ukiimbwa mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Ikulu ya KulliyeAnkara nchini Uturuki tarehe 18 Aprili, 2024. 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride la Heshima mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu ya KulliyeAnkara nchini Uturuki tarehe 18 Aprili, 2024. Kushoto ni Mwenyeji wake Rais wa Uturuki Mhe. Recep Tayyip Erdogan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mwenyeji wake Rais wa Uturuki Mhe. Recep Tayyip Erdogan kabla ya kuanza mazungumzo katika Ikulu ya KulliyeAnkara nchini Uturuki tarehe 18 Aprili, 2024. 












VICTORIA GWARA: SHUJAA WA HEDHI SALAMA ANAYEIPIGANIA JAMII YAKE

April 18, 2024

Mohammed Hammie Rajab.

Hedhi salama si jambo linalozungumzwa kwa kiasi kikubwa hususani katika jamii nyingi za kitanzania, hii ni kutokana na imani za kidini, mila pamoja na tamaduni.

Licha ya kuwepo kwa kampeni na harakati nyingi zenye lengo la kuelimisha wanawake na wasichana juu ya hedhi salama hapa nchini, lakini bado kumekuwa na changamoto ya ufikaji wa elimu hiyo hasa maeneo ya vijijini.

Jitihada zinazofanywa na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya hedhi salama ni kielelezo tosha cha kuisaidia serikali pale ambapo kumekuwa na ufinyu wa ufikiwaji wa maeneo hayo kwa ajili ya kutoa elimu.

Victoria Gwera kutokea kijiji cha Mgudeni wilayani Kilombero mkoani Morogoro ni miongoni mwa wanawake waliowahi kufikiwa na elimu ya hedhi salama, mafunzo aliyoyapata kutokea shirika la CEMDO lililopo Ifakara mkoani humo.


Bi Victoria Gwera akiwa kwenye tabasamu. Moja ya picha iliyopigwa akiwa kijijini kwake Mgudeni anapoishi.

Mbali na elimu hiyo, Victoria na washiriki wengine walipatiwa pia mafunzo ya kutengeneza tauli za kike (pedi) kwa kutumia vitenge pamoja na sabuni ambazo kwa mujibu wa lengo la mafunzo hayo zingewasaidia kwenye usafi wakati wote wa hedhi.

Baada ya mafunzo hayo Victoria aliamua kufanya kitu cha kipekee kwa jamii yake ambacho mpaka sasa kinaendelea kuacha alama.

“Niliporudi kijijini baada ya kupata mafunzo, niliamua kuanza kutengeza pedi na sabuni kwa ajili ya matumuzi yangu na jamii kwa kuuza kwa bei rahisi” anasema Victoria wakati wa mazungumzo maalumu na mwandishi wa makala hii.

Anasema ilimchukua muda wa miezi miwili tu kufanyia kazi mafunzo ya utengenezaji wa pedi hizo na sabuni, kuzijaribu, kuzitumia yeye mwenyewe kwanza kabla ya kupata wazo la kuanza kusaidia wanawake na wasichana wanaokumbana na changamaoto ya gharama za pedi wakati wa hedhi.

(Bi Victoria Gwera akiwa kwenye shughili zake za utengenezaji wa tauli za kike nyumbani kwake Mgudeni.

Victoria angeweza kuyapiga teke maarifa aliyoyapata na kusingekuwa na mtu wa kumuuliza, huenda pia ilikuwa hivyo kwa washiriki wingine, lakini yeye kuna kilichomsukuma mpaka akaamua kufanya kitu cha pekee.

“Wakati nipo msichana mdogo niliwahi kupatwa na changamoto ya kukosa pedi, gharama zilikuwa kubwa kulinganisha na hali ya familia yetu, hivyo kila nikikumbuka hali hiyo huwa naumia. Sitaki wasichana na wanawake wengine hapa kijijini wapitie yale niliyowahi kupitia mimi na ndio maana nikaamua kutengeza hizi pedi na sabuni na kuuza kwa bei rahisi” anasema Victoria.

Inaelezwa kuwa moja kati ya nyenzo za msingi ili kufanikisha hedhi salama ni elimu sahihi, upatikanaji wa taulo za kike (pedi), sabuni pamoja na maji safi na salama, vitu ambavyo Victoria mbali na kuvikamilisha, pia anawasaida wanawake wenzake kukamilisha.

“Mimi nimepata mafunzo ya hedhi salama, kwa hiyo ninapokwenda kuuza hizi pedi huko maeneo ya kijijini huwa natoa na elimu pia. Inawasaidia sana wasichana wanaoingia kwenye hedhi kwa mara ya kwanza” anasisitiza Victoria.

Kwa kutumia baiskeli, Victoria husafiri zaidi ya kilomita tano kwa siku ili kuwafikia wateja wake, wengi kutokea kijiji alichopo na vijiji jirani ambavyo anaamini bado elimu ya hedhi salama haijafika kwa kiwango kikubwa. Pedi tatu akiuza kwa kiasi cha shilingi za kitanzania elfu moja.


Bi Victoria Gwera akielekea kwenye biashara yake ya kuuza tauli za kike na sabuni

Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Tanzania wanawake Milioni 13,750,122 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 hupata hedhi kila Mwaka. Ikielezwa kuwa idadi hiyo ni kubwa na hivyo jamii ina kila sababu ya kuhakikisha kuwa kundi hilo linapata huduma bora wakati wa hedhi ikiwemo kuhakikisha uwepo wa maji, sabuni na taulo za kike ili kufanya hedhi iwe salama kwao.

Hivi karibuni Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye maadhimisho ya wiki ya hedhi salama duniani alitoa wito kwa jamii kuwa na uelewa kuwa hedhi sio balaa, ugonjwa wala sio laana bali ni mabadiliko ya hali ya kawaida yanayomtokea mwanamke au msichana mara baada ya kubalehe kama ishara kwenye mfumo wa maumbile yake ya uzazi.

Victoria Gwera anawakilisha wanawake wengine wengi nchini Tanzania ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kuikomboa jamii yao na changamoto ya hedhi salama kwa kuonekana ama kutoonekana. Hivyo ni vyema serikali na wadau wengine kuenzi na kuendeleza jitihada hizi ili kuwanusuru wanawake na wasichana.

Mwisho

Mohammed Hammie Rajab
A Human Rights to Water Journalist
(Equal Water Voice To All)
Phone: +255719000010