SERIKALI itaendelea kuunga mkono mikutano ya dini-DC Dendego

SERIKALI itaendelea kuunga mkono mikutano ya dini-DC Dendego

July 18, 2013
Na Nestory Ngwega,Tanga
MKUU wa wilaya ya Tanga Halima Dendego amesema,serikali itaendelea kuunga mkono mikutano ya dini inayohubiri amani na upendo ili kujenga maadili mema ya ndani ya jamii na kudumisha amani.

Aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akifungua mkutano wa neno la Mungu katika viwana vya Usagara jijini Tanga uliondaliwa na umoa wa makanisa ya kipentekoste.

Alisema kuwa amani ni kipaumbele cha kwanza katika nchi na kwamba serikali itashirikiana na wapenda amani wote.

Aliwapongeza waumini wa kikristo kwa kuonyesha mshikamano na kutunza amani iliyopo hivyo akawataka wananchi wote kwa ujumla waishi kwa upendo ili kudumisha amani.

Kwa upande wake muhubiri wa kimataifa Johannes Amritzer aliishukuru serikali na wananchi wa Tanga kwa ujumla kwa ushirikino na kuwapokea kwa upendo.

Alisema upendo aliouona ni ishara ya wazi kuwa wananchi wa Tanzania wanaishi kwa umoja na upendo na kwamba yeye ataendelea kuhubiri amani ya rohoni ambayo ndiyo inayozaa amani ya nje kwa kila mwanadamu.

Akimkaribisha mkuu wa wilaya,Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo Askofu Agostino Dedu alisema kuwa mkutano huo umekuwa wa baraka kubwa kiroho na kiuchumi pia ikizingatiwa kuwa wageni wapatao 150 kutoka Ulaya na Marekani wapo Jiini Tanga kuhudhuria mkutano huo na hivyo uongeza pato kwa wafanyabishara wa mahoteli,vyakula na bidhaa zingine.

Mwisho.

PICHA za matuki mbalimbali kwenye mkutano leo katika viwanja vya Usagara jijini Tanga.

July 18, 2013

Ashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kukutwa na Bunduki mbili kinyume cha Sheria

July 18, 2013
Na Hamisi Ramadhani,Handeni.
MKULIMA mmoja wa kijiji cha Sua Wilayani Handeni Mkoani Tanga, anashikiliwa na Polisi Wilayani hapa kwa tuhuma za kukutwa na Bunduki mbili aina ya magobole alizokuwa akizimiliki kinyume na sheria.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 11.30 jioni katika kijiji hicho baada ya raia wema kutoa taarifa polisi.
 
Alisema kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni baada ya wananchi kuwa na hofu na ndipo raia wema wakatoa taarifa polisi kwa kuhofia kuwa mtuhumiwa huyo anaweza kufanya uharifhu wakati wowote. 
 
Alilitaja jina la mtuhumiwa huyo kuwa ni Hamadi Ally Waziri (43) mkazi wa kijiji cha Sua ambaye alikamatwa nyumbani kwake baada ya polisi kufanyiwa upekuzi ndani kwake na ndipo wakazikuta bunduki mbili aina ya Magobole.
 
Kamanda Massawe aliwapongeza raia wema kwa kutoa taarifa hizo na kuwataka kuwa na ushirikiano na jeshi la polisi ili kuweza kutokomeza uhalifu ambayo mkoani hapa.
 
Mwisho
KIWANDA CHA CHOKAA CHAPUNGUZA UZALISHAJI

KIWANDA CHA CHOKAA CHAPUNGUZA UZALISHAJI

July 18, 2013

Na Pascal Mbunga,Tanga.

KIWANDA maarufu cha kutengeneza chokaa cha Kneelkant kilichopo nje kidogo ya jiji la Tanga kimewaachisha kazi idadi kubwa ya wafanyakazi wake baada ya kupunguza uzalishaji mali kiwandani hapo.
  
Akizungumza  na Blogi ya Tanga Raha Meneja wa Kiwanda, Rashid Hamoud alisema hali ya biashara imekuwa mbaya baada ya nchi zinazonunua bidhaa hizo kuingia katika machafuko ya kivita.
Meneja huyo ameyataja masoko ya bihaa zake kuwa ni nchi za maziwa makubwa ambazo ni pamoja na Kongo, Burundi, Zimbabwe, Zambia na Malawi.
Amesema kukosekana kwa hali  ya usalama katika baadhi ya nchi hizo kumesababisha usafirishaji wa bidhaa kuwa katika hatari ya kutekwa wakati na sehemu yeyote njiani.
Hamoud amefahahmisha kuwa kutokanana hali hiyo, uongozi wa kiwanda ulilazimika kuwaachisha kazi zaidi ya nusu ya idadi ya wafanyakazi wote kiwandani hapo.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kiwanda cha Kneelkanth kimeweza kuliingizia taifa pato la shs.bilioni 45 baada ya kuuza bidhaa tani 12,000 za chokaa katika nchi za maziwa makubwa.
Kiwanda cha Kneelkanth ni mradi ulioanzishwa mwaka 2009 na Mtanzania Rashid Hamoud akishirikiana na mwekezaji wa India , Kumar  Pajara na kuanza kazi rasmi mwaka 2010.
(Mwisho)
  

JAJI KORTI YA RUFANI KUONGOZA KAMATI TFF

July 18, 2013
Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda kuongoza Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kufuatia mabadiliko ya Katiba yaliyofanywa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) na kuingiza kamati nyingine mpya.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga ametangaza wajumbe wa kamati hizo leo (Julai 18 mwaka huu) mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema uteuzi wa wajumbe hao umezingatia maoni ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, lakini vilevile amewashukuru wajumbe walioteuliwa kwa kukubali kutoa mchango wao katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

Mbali ya Jaji Luanda ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, wajumbe ni Francis Kiwanga (Makamu Mwenyekiti), Anney Semu, Yohane Masalla na Allen Kasamala. Kamati ya Uchaguzi inaongozwa na Hamidu Mbwezeleni, Moses Kaluwa (Makamu Mwenyekiti), Mustafa Siyani, Hassan Dyamwale na Kitwana Manara.

Mwenyekiti Kamati ya Rufani ya Maadili ni Jaji Steven Ihema, Bi. Victoria Makani (Makamu Mwenyekiti), Mheshimiwa Mohamed Missanga, Henry Tandau na Mheshimiwa Murtaza Mangungu. Kamati ya Maadili inaundwa na Bi. Jesse Mguto (Mwenyekiti), Francis Kabwe (Makamu Mwenyekiti), Profesa Mtambo Madundo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Mohamed Mpinga na Evod Mmanda.

Profesa Mgongo Fimbo anaongoza Kamati ya Rufani ya Nidhamu wakati Makamu wake ni Ong’wanuhama Kibuta na wajumbe ni Kanali Mstaafu Idd Kipingu, Dk. Mshindo Msolla na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mstaafu Jamal Rwambow. Kamati ya Nidhamu inaongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) Mstaafu Alfred Tibaigana, Mustafa Kambona (Makamu Mwenyekiti), Mheshimiwa Azzan Zungu, Yusuf Nzowa na Mohamed Msomali.

Pia Kamati ya Utendaji imefanya mabadiliko katika Kamati ya Waamuzi ambapo Said Nassoro na Charles Ndagala kutoka Chama cha Waamuzi wanachukua nafasi za Joan Minja na Riziki Majala. Kamati hiyo inaendelea kuongozwa na Kapteni Mstaafu Stanley Lugenge, Omar Kasinde (Makamu Mwenyekiti) wakati mjumbe mwingine ni Mohamed Nyama.

Kamati ya Tiba inaongozwa na Dk. Paul Marealle wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti itajazwa baadaye na Rais Tenga. Wajumbe ni Mwanandi Mwankemwa, Anthony Ngome, Frank Mhonda, Kapteni Joakim Mshanga na Helen Semu.

Rais Tenga alisema mabadiliko mengine yamefanyika kutokana na waliokuwa wajumbe kuomba kupumzika. Wajumbe walioomba kupumzika ni Dk. Sylvester Faya, Idd Mtiginjola na Deo Lyatto

Jaji Ihema na Wakili mwandamizi Bi Jesse Mguyto kuongoza kamati za maadili TFF

July 18, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
JAJI Steven Ihema na wakili mwandamizi, Bi. Jesse Mguto wataongoza kamati muhimu za za maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoundwa baada ya kufanya mabadiliko kwenye katiba ya Shirikisho hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa TFF Leodegar  Tenga alitangaza jana.

Shirikisho hilo pia limemteua Jaji Bernard Luanda kuongoza Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wakati Profesa Mgongo Fimbo ataendelea kuongoza Kamati ya Rufaa za Nidhamu na Kamanda Mstaafu, Alfred Tibaigana akiendelea kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu.
Rais Tenga alisema hayo wakati alipoongea na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho kikatiba kina jukumu la kuunda Kamati Ndogo za TFF na vyombo vya maamuzi.
“Tulitaka tuwe na watu solid (imara) na makini ambao watatuhakikishia tunakwenda vyema,” alisema Tenga akizungumzia uteuzi huo ambao unahitimisha mchakato wa mageuzi kwenye Shirikisho baada ya Uchaguzi Mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika mwezi Februari kusimamishwa kutokana na baadhi ya wagombea kupinga kuenguliwa na baadaye kwenda FIFA.
Katika kumaliza tatizo hilo, FIFA ilituma ujumbe wake kusikiliza walalamikaji na watu wengine na baadaye kuagiza kuundwa kwa Kamati za Maadili na kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa TFF kwa ajili ya kuingiza vyombo hivyo kwenye katiba kabla ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa TFF.
“Tumezingatia pia maoni ya wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao walitaka kamati ziwe na majaji... lakini si rahisi kupata seating judges (majaji walio kazini) ndio maana tunawashukuru wale waliotuambia kuwa wako tayari kutusaidia.
“Tumetafuta majaji na mawakili waandamizi ambao tunaamini watatuhakikishia haki inatendeka na inaonekana inatendeka,” alisema Tenga na kuongeza kuwa pia walizingatia maombi ya wajumbe wengine watatu ambao walitaka kupumzika, akiwataja kuwa ni Deo Lyatto, Sylvester Faya na Idd Mtiginjollah.
Alisema kutokana na mfumo huo mpya, mambo yote yanayohusu masuala ya ndani ya uwanja sasa yatashughulikiwa na Kamati ya Nidhamu, wakati yale ya nje ya uwanja, ambayo yanawahusu viongozi na wanafamilia ya mpira wa miguu kwa ujumla, yatashughulikiwa na Kamati za Maadili.
Tenga alisema mabadiliko hayo pia yamegusa kamati nyingine mbili, yaani Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Uchaguzi ambayo sasa itaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamidu Mbwezeleni
Jaji Ihema ataongoza Kamati ya Rufaa za Maadili akisaidiwa na mwanasheria mwingine mwandamizi, Victoria Makani, huku Bi. Mguto, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza vyombo vya vya maamuzi ataongoza Kamati ya Maadili akisaidiwa na makamu wake Francis Kabwe, ambaye Msajili wa Mahakama Kuu.
Katika uteuzi huo, baadhi ya wajumbe wamehamishwa kutoka kamati moja hadi nyingine. Mhe. Murtaza Mangungu, ambaye awali alikuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi, sasa ataingia kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili; Kamanda Mohamed Mpinga na Prof Madundo Mtambo wamehamishwa kutoka Kamati ya Rufaa za Uchaguzi kwenda Kamati ya Maadili.
Wajumbe wapya kwenye Kamati hizo ni pamoja na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Mshindo Msolla na Kamanda Mstaafu Jamal Rwambow wanaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; mwanasheria maarufu Evodi Mmanda anaingia kwenye Kamati ya Maadili; mwanasheria mwandamizi Mustapha Kambona ambaye anaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; Mhe. Mohamed Misanga ambaye anaingia kwenye Kamati ya Maadili na Kanali Iddi Kipingu, ambaye anasifika kwa kuendesha soka la vijana, anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za Nidhamu.
Pia Mwanasheria Anne Steven Marealle anakuwa mjumbe kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi; Yohane Masale (Rufaa za Uchaguzi), Allen Kasamala (Rufaa za Uchaguzi);  Francis Kiwanga ambaye pia aningia kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi na mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau ambaye anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili.
Kamati ya Utendaji pia imefanya mabadiliko kwenye Kamati ya Waamuzi ambako mwenyekiti Said Nassoro na katibu Charles Ndagala wa Chama cha Waamuzi wanaingia kwenye kamati hiyo kushika nafasi ya Joan Minja na Riziki Majala.
Wajumbe wa Kamati hizo ni kama ifuatavyo:
Kamati ya Rufaa za Maadili ni Jaji Steven Ihema (mwenyekiti), Victoria Makani (m/mwenyekiti), Mhe. Mohamed Misanga, Henry Tandau na Mhe. Murtaza Mangungu.
Kamati ya Maadili: Bi Jesse Mguto (mwenyekiti), Francis Kabwe (m/mwenyekiti), ACP Mohamed Mpinga, Prof. Madundo Mtambo, na Evod mmanda.
Kamati ya Rufaa za Nidhamu: Prof. Mgongo Fimbo, Ong’wanuhama Kibuta (m/mwenyekiti), Kanali Mstaafu Idd Kipingu, Dk. Mshindo Msolla, ACP Jamal Rwambow.
Kamati ya Nidhamu: Kamanda Mstaafu Alfred Tibaigana (mwenyekiti), Mustafa Kambona (m/mwenyekiti), Azzan Zungu, Yussu Nzowa na Mohamed Msomali.
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi: Jaji Bernard Luanda (mwenyekiti), Francis Kiwanga (m/mwenyekiti), A. Steven Semu, Yohane Masalla na Allen Kasamala.
Kamati ya Uchaguzi: Hamidu Mbwezeleni (mwenyekiti), Moses Kaluwa (m/mwenyekiti), Mustafa Siani, Hassan Dyamwale na Kitwana Manara.
Kamati ya Waamuzi: Kapteni Mstaafu Stanley Lugenge (mwenyekiti), Omar Kasinde (m/mwenyekiti), Said Nassoro, Charles Ndagala na Mohamed Nyama.
Kamanda Mstaafu Jamal Rwambow anaingia kwenye Kamati hiyo.