WAMILIKI WAAGIZWA KUHAKIKISHA USALAMA WA MIGODI YAO MKOANI SINGIDA

September 14, 2017
Wamiliki wote wa migodi inayofanya shughuli za uchimbaji wa madini Mkoani Singida wameagizwa kuhakikisha kuwa hakuna vifo wa majeruhi katika maeneo yao kutokana na uwepo wa miundombinu mibovu au uzembe wowote.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo alipotembelea mgodi wa madini katika Kijiji cha Konkilangi, Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui, Wilaya ya Iramba kuona shughuli za uokoaji mara baada ya mgodi huo kutitia huku watu wawili wakihofiwa kufariki.

Dkt Nchimbi amesema wamiliki wa migodi wanatakiwa kuwekeza katika kuboreha miundombinu ya migodi ili wachimbaji waweze kufanya kazi katika mazingira ambayo si hatarishi.“Madini yanatakiwa kuleta neema na kukuza uchumi wa taifa letu na sio kuangamiza nguvu kazi na kuleta majonzi, serikali haiwezi kukubali kupoteza vijana kutokana na uzembe wa baadhi ya watu”, amesema.

Ameongeza kwa kumtaka Kamishna Msaidizi wa madini kanda ya kati Sostenes Masolla kuweka ratiba ya kutoa mafunzo kila wiki huku akitakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili wachimbaji wapewe semina na mafunzo ya juu ya usalama wao wawapo migodini.

Dkt Nchimbi pia amemtaka Kamishna huyo wa madini kufuatilia taaluma na sifa zinazotumika kuchagua wakaguzi wa migodi maarufu kama ‘inspekta’ kwakuwa wao ndio hutakiwa kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kuwa shimo au duara liko salama kabla ya kuruhusu uchimbaji kufanyika.

“Hawa ma inspekta hawa wasituulie vijana kutokana na uzembe wao, unakuta hajakagua vizuri halafu anaruhusu watu walipue baruti matokeo yake ndio kama haya, hawa wakiwa makini ajali za kwenye migodi zitapungua sana”, amesisitiza.Aidha Dkt Nchimbi amewataka wachimbaji na wamiliki wa migodi kuachana na imani potofu kuwa endapo vifo vinatokea katika shimo la mgodi hapo panakuwa na madini mengi.

Amesema ikiwa atabaini kuwa imani hizo zinaendekezwa na kipa endapo patatokea tena kifo katika mgodi huo basi hatasita kufunga shughuli za uchimbaji katika mgodi huo.Kwa upande wao wachimbaji wameeleza kuwa ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa mgakuzi wa shimo hilo ambaye aliruhusu ulipuaji wa baruti wakati mazingira yakiwa hayaruhusu.

Wachimbaji hao wamemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa wamekosa amani kutokana na vifo hivyo ambavyo kwa kiwango kikubwa vimetokana na uzembe huku pia wakilalamikia utaratibu wa malipo yao.Mmoja wa wachimbaji hao Abuu Amiri amesema ma inspekta hao wamekuwa wakijali maslahi binafsi badala ya kuangalia usalama wa wachimbaji watakaoingia katika shimo hilo.

Mgodi ujulikanao kwa jina la Sekenke 1 katika kitalu namba 1, ambapo maduara matano yanayomilikiwa na Marijan Ramadhani na Jakobo Ntobi, yalititia mnamo tarehe tisa Septemba na kusababisha vifo kwa wachimbaji wawili huku mmoja tayari mwili wake ukiwa umepatikana na majeruhi watano.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na wachimbaji alipotembelea mgodi wa madini katika Kijiji cha Konkilangi, Wilayani Iramba kuona shughuli za uokoaji mara baada ya mgodi huo kutitia huku watu wawili wakihofiwa kufariki. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel Luhahula.
Wachimbaji wakiendelea na shughuli za uokoaji katika Kijiji cha Konkilangi, Wilayani Iramba mara baada ya mgodi huo kutitia huku watu wawili wakihofiwa kufariki.
Wachimbaji wakiwa wanatazama shughuli za uokoaji zikiendelea katika Kijiji cha Konkilangi, Wilayani Iramba mara baada ya mgodi huo kutitia huku watu wawili wakihofiwa kufariki.
Mmoja wa wachimbaji Abuu Amiri akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi alipowatembelea kuona shughuli za uokoaji katika mgodi wa madini wa Kijiji cha Konkilangi, Wilayani Iramba mara baada ya mgodi huo kutitia huku watu wawili wakihofiwa kufariki.
Umati wa Wachimbaji uliojitokeza kumsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi alipowatembelea kuona shughuli za uokoaji katika mgodi wa madini wa Kijiji cha Konkilangi, Wilayani Iramba mara baada ya mgodi huo kutitia huku watu wawili wakihofiwa kufariki.

MWANDISHI AANIKA SIRI MAUAJI YA ALBINO KWENYE KITABU, AHOAJIANA NA WAGANGA, WACHAWI NA MATAPELI

September 14, 2017
 Jalada la kitabu cha ‘MIFUPA YA ALBINO’.
Mwandishi Daniel Mbega, akiwa ameshikilia Karunguyeye waliokaushwa nyumbani kwa mganga wa jadi.

MWANDISHI wa habari mwandamizi nchini, Daniel Mbega, amekamilisha kuandika kitabu kinachofichua siri zilizo nyuma ya pazia kuhusiana na mauaji ya vikongwe na albino nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Mwandishi huyo, ambaye alifanya utafiti kwa kipindi cha miezi nane mfululizo katika mikoa 10 ya Kanda ya Maziwa Makuu, amesema kitabu hiyo alichokipa jina la ‘MIFUPA YA ALBINO’ kinatarajiwa kuwaingia kiwandani wakati wowote na kwa sasa anatafuta msaada wa fedha za kuchapia.
“Nimekamilisha, lakini nimekwama kidogo kuhusu fedha za uchapaji na kama kuna taasisi yoyote au mtu anayeweza kunisaidia nitashukuru sana,” amesema mwanahabari huyo.
“Yeyote mwenye nia njema na jamii ya Watanzania na anaguswa kusaidia uchapaji wa kitabu hiki, ninaomba awasiliane nami kwa namba hii 0656-331974, kwani naamini kitabu hiki kitakuwa msaada pia wa kiroho baada ya kujua mambo yanayofanywa hata na baadhi ya viongozi wa dini wanaotumia ushirikina,” aliongeza.
Bw. Mbega amesema kwamba, katika utafiti wake huo alifanikiwa kukutana na waganga wa jadi, wachawi na matapeli katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa, ambako alikaa kwa miezi miwili akifanya uchunguzi.
Aidha, amesema kwamba, katika uchunguzi wake huo alishiriki pia kikamilifu katika misako mbalimbali ya wahalifu walioshiriki kwenye matukio hayo na kushuhudia namna vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotenda kazi.
Kunusurika kifo kwa ajali ama kuzingirwa na baadhi ya wananchi ni moja ya hatari alizokumbana nazo wakati wa uchunguzi wake, huku akisafiri umbali wa zaidi ya kilometa 40,000 katika kipindi hicho.
“Wakati mwingine nilikosa usingizi hata kwa siku tano mfululizo, nililazimika kusafiri mchana na usiku katika mazingira mengi hatarishi nikikusanya habari,” alisema.