MCHANGO WA TAASISI YA ILTC YA JIJINI MWANZA KATIKA KUKUZA LUGHA MBALIMBALI.

January 07, 2017
Mwalimu Charles Mombeki ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi ya lugha ya International Training Centre (ILTC) iliyopo Isamilo, nyuma ya ofisi za Jiji la Mwanza, alipokuwa akizungumza na 102.5 Lake Fm.

Na BMG
Lugha ni alama muhimu katika jamii yoyote ile. Ni muhimu kwa ajili ya kuwaunganisha watu wa jamii mbalimbali. Bila lugha hakuna mafanikio wala maendeleo katika maisha ya mwanadamu. Inaelezwa kwamba kukanganyikana kwa lugha kulisababisha mafanikio ya ujenzi wa mnara wa Baberi kukwama.

Najua kila mmoja anayo lugha yake ya asili, iwe ya taifa ama kabila. Hoja yangu leo ni juu ya lugha za kukuunganisha na watu mbalimbali kote duniani, kwa ajili ya maendeleo yako. Piga ua, garagaza, hakikisha unajua kuandika na kuzungumza kwa ufasaha lugha ya kiingereza, kwani imekuwa lugha muhimu kote duniani, japo lugha nyingine kama Kiswahili, kifarasa, kichina, kireno, kiitariano, kiarabu na hata lugha yoyote ile, nazo zina umuhimu wake.

Kwa umuhimu huo, BMG inagonga hodi kwenye viunga vya taasisi ya lugha ijulikanayo kama International Language Training Centre (ILTC) iliyopo Isamilo karibu na ofisi za halmashauri ya Jiji la Mwanza. 

Ni baada ya kusikia sifa kede wa kede kuhusiana na taasisi hii, kwamba imekuwa kitovu cha lugha mbalimbali, kuanzia za asili hadi za kimataifa. Nakutana na Mwalimu Charles Mombeki ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi hii iliyojizolea sifa lukuki kwa zaidi ya miaka 20.

Mbali na lugha pamoja na masomo ya komputa, taasisi hii pia imeanza kugawa ujuzi kuanzia kwa watoto wadodo, ambapo sasa inatoa masomo ya chekechekea kwa ustadi wa hali ya juu.

Kama hiyo haitoshi, masomo ya ziada ya sayansi na hisabati yanafundishwa katika taasisi hii, ikizingatiwa kwamba hivi sasa wanafunzi wanaosoma masomo hayo, ni lulu kwa Taifa.

Mwalimu Mombeki anasema taasisi yake imejipanga vyema ili kuhakikisha inazalisha matunda bora ikiwa ni hatua za kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha taifa linakuwa na wasomi wengi wa masomo ya sayansi.

Inatosha kusema kwamba taasisi ya Internation Language Training Centre ni mkombozi wa lugha kwa watu wote, wawe wanafunzi na hata wasio wanafunzi. Hivyo kwa ukaribu wa Mwalimu Mombeki, fika Isamilo Jijini Mwanza, ili uwe mmoja wa wanufaika wa taasisi hii kwa mwaka huu wa mafanikio wa 2017.

Nami kwa ukaribu wangu, nasema, piga simu nambari 0754 66 49 33 ikiwa unatamani kujiunga na taasisi ya International Language Training Centre. Naitwa George Binagi-GB Pazzo, ahsante kwa kunisikiliza, mfikishie mwenzio ujumbe huu ili naye anufaike.
Bonyeza Hapa Au play hapo chini kusikiliza sauti.

Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar

January 07, 2017

 Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema adha ya mafuriko yanayotokea kila mwaka wakati wa msimu wa Mvua za Masika na kuwakumba Wananchi yataondoka au kupungua zaidi baada ya kukamilika kwa miradi tofauti iliyonzishwa na Serikali chini ya Mradi wa huduma za Jamii Mijini.
Alisema mafanikio ya mradi huo tayari yameanza kuonekana katika ujenzi wa michirizi ya maji ya mvua kwenye maeneo ya Daraja Bovu, Mnazi Mmoja, Kijangwani na baadhi ya maeneo ya Jang’ombe  na Wananchi wake tayari wanafaidika na matunda ya mradi huo.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani  Forodhani Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa harakati za shamra shamra za kusherehekea miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi imejipanga kuimarisha  miradi hiyo ikiwa sehemu ya Jududi za utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM  ya Mwaka 2015 ikilenga kuwaondoshea usumbufu unaowakumbwa wananchi walio wengi hasa wale wa maeneo ya Ng’ambo ya Mji.
Balozi Seif  alisema ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani  Forodhani Mjini Zanzibar ukiwa miongoni mwa miradi ya Jamii Mijini ni muhimu kwa maendeleo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliobahatika kuwemo kwenye  Miji ya urithi wa Dunia  ambao unategemewa kwa uchumi wa Taifa kwa upande wa Sekta ya Utalii.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Nd.  Khamis Mussa Omar alisema chimbuko la mradi wa ujenzi wa ukuta wa Mizingani umetokana na athari kubwa iliyojitokeza siku za nyuma ya kasi kubwa ya maji ya Bahari iliyoathiri eneo hilo.
Alisema Ujenzi  wa Ukuta huo ulioanza Tarehe 22 April 2015  ukiwa na urefu wa Mita 320, upana Mita sita na ongezeko na mita sita kuelekea usawa wa Bahari unatarajiwa kukamilika rasmi ndani ya Mwaka huu wa 2017.
Alieleza kwamba asilimia 65% ya ujenzi huo imekamilika kwa upande wa ukuta wenyewe na kazi iliyobaki na kuendelezwa kwa hivi sasa ni ujenzi wa bustani pamoja na bara bara ya watembeao kwa miguu.
Akimkaribisha Balozi Seif kuzindua ujenzi huo wa Ukuta, Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Khalid Salum Mohamed alisema uimarishaji wa Mji Mkongwe kupitia mradi wa Jamii Mijini utakuwa chachu ya kuimarika kwa Sekta ya Utalii Nchini.
Dr.  Khalid aliwaomba Wamiliki Binafsi wa majengo yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe kushirikiana na Serikali Kuu katika kuyaweka kwenye mazingira bora yatakayotoa haiba nzuri ya Mji wa Zanzibar unaotegemewa katika makusanyo ya Mapato ya Taifa kupitia sekta hiyo ya Utalii.
Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani  Forodhani Mjini Zanzibar  unasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mkono wenye masharti nafuu wa shilingi Bilioni 7,222,577,890 kutoka Benki ya Dunia.
Kampuni ya  Seyani Brothers ya Mjini Dar es salaam ndio iliyopewa jukumu la kujenga Ukuta huo chini ya Msimamizi  Mshauri muelekezi Kampuni ya Aurecon kutoka Nchini Afrika Kusini.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi, wahandisi wa ujenzi wa ukuta,  watendaji wa Wizara ya Fedha  pamoja na washauri walekeza wa ujenzi huo mara baada ya kukamilisha kwa hafla hiyo.
Kulia ya Balozi Seif waliokaa vitini ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulid, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Nd. Khamis Mussa, Kamishna wa Polisi Zanzibar Kamanda Hamdan Makame.
Kushoto ya Balozi Seif  ni Waziri wa Fedha Dr. Khalid Salum,  Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoud Mohamed Mahmoud na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Rashid  Ali Juma.
Makamu wa Pili a Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za kusherehekea miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ Dr. Khalid Salum Mohamed ambapo wa nyuma yake ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulid. Picha na OMPR – ZNZ.

BODI YA FILAMU NCHINI YAWAOMBA WATANZANIA KUZIPIGIA KURA FILAMU ZA KITANZANIA KWENYE TUZO ZA AMVA 2017

January 07, 2017
BMGHabari
Bodi ya Filamu nchini imewahamasisha watanzania kuongera ari ya kuzipigia kura filamu za kitanzania zinazowania tuzo za Africa Magic Viewers Awards (AMVA 2017) za nchini Nigeria.

Katibu Mtendaji wa bodi hiyo, Bi Joyce Fissoo (pichani juu) ametoa hamasa hiyo hii leo, wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Break Fast On Saturday kinachoendeshwa na watangazaji Philip Mwihava na Godfrey Kusolwa.

“Filamu hizo ni Naomba Niseme, Aisha na Home Coming ambazo zinawania tuzo za filamu bora na Siri ya Mtungi ambayo inagombea filamu bora ya lugha ya Kiswahili. Niwaase Wanzania, ushindi wa filamu hizi ni sisi kuwapigia kura hawa vijana wetu ambao wameshika bendera yetu kwenda kutuwakilisha kule Nigeria, niwasihi waweze kuzipigia kura na wahakikishe wanahamasisha marafiki zao pia kuzipigia kura ili nafasi zote tuzo zije Tanzania”. Amesisitiza Fissoo.
Naye Mtayarishaji wa filamu nchini, Staphord Kihole (pichani) ambaye pia alikuwa kwenye kipindi hicho, ametumia fursa hiyo kuwaomba watanzania kuzipigia kura filamu za kitanzania ili zishinde tuzo za Africa Magic Viewers Choice Awards ikiwemo filamu yake ya "Naomba Niseme" inayowania vipengele viwili, kikiwemo kipendele cha Best East Africa na Best All Africa kinachoamuliwa na majaji.

Ili kuzipigia kura filamu za Tanzania ambazo ni Naomba Niseme, Aisha na Home Coming, unapakua Application ya We Chat, unajisajiri kwenye Africa Magic kwa kutumia nambari ya simu na kisha unatafuta kipengele cha AMVCA na utaweza kupiga kura kadri upendavyo ambapo mtu mmoja anaweza kupiga kura hadi 100 kwenye filamu tofauti tofauti.
Bonyeza Hapa  Au play hapo chini kusikiliza sauti  Credit: Clouds Fm
MUZIKI WA TANZANIA TUNAENDA MBELE?

MUZIKI WA TANZANIA TUNAENDA MBELE?

January 07, 2017

Januari 2013, niliandika makala kuhusu nilivyouona muziki mwaka 2012. Naona nirudie makala ile kama nilivyoiandika, na kukuachia msomaji kulinganisha na hali ilivyokuwa 2016.
Mwaka 2012 ndio huoo umetokomea, ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. Muziki wa nchi yetu ulitawaliwa na muziki wa Bongoflava, Taarab, muziki wa bendi, matarumbeta, muziki wa Enjili, na muziki wa kiasili. Si siri kuwa muziki wa Bongoflava ndio uliokuwa ukitawala katika vyombo vya habari na sehemu nyingi za maonyesho. Muziki huu ulikuwa  ukifuatiliwa na muziki wa Taarab na muziki wa enjili.  Katika muziki wote huu jambo lililokuwa wazi ni kuwa waimbaji ndio waliokuwa wakipewa kipaumbele katika tasnia hii.  Waimbaji katika aina zote za muziki uliotajwa hapo juu ndio waliotajwa sana na kupewa sifa kwa ubora wa muziki. Kumekuweko na mashindano kadhaa ambayo yote yamejikita katika kutafuta vipawa vya waimbaji japo mara nyingi yamejitambulisha kama mashindano ya kusaka vipaji mbalimbali.
Hakuna ubishi muziki wa dansi na muziki wa asili ndio muziki uliopewa muda mchache sana katika vyombo vya habari. Na hata katika muziki huo, bendi ambazo zimejikita kufuata mipigo ya Kikongo zilipewa nafasi zaidi kuliko bendi ambazo zimejichagulia njia nyingine za muziki wao.
Kuna sababu kadhaa ambazo zimefanya muziki wa bongoflava kuchukua nafasi zaidi katika vyombo vya habari, la kwanza ni uwingi wa kazi za bongoflava zinazorekodiwa. Karibu kila mji una studio ya kurekodi, na katika studio hizo kazi nyingi zaidi zinazorekodiwa ni aina hiyo ya muziki, hivyo kutokana na uwingi wa kazi hizo ni wazi kabisa ndizo ambazo zitaendelea kutawala anga la vyombo vya habari, na kutokana na mfumo wa vyombo vyetu vyote kujikita katika mfumo wa aina fulani tu za muziki.
Kwa mtizamo wangu heka heka za muziki wa Enjili zilipungua 2012. Yale matamasha makubwa ya muziki huo yalipungua sana, na hata nyimbo za kushtua jamii hazikuwa nyingi  kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Muziki wa Taarab haujaleta mabadiliko kimuziki, mengi yaliyofanywa katika 2012 ni marudio tu ya ubunifu uliofanyika nyuma. Kama vile uanzishwaji wa kucheza show katika taarab, upigaji wa gitaa na kuliachia pekee yake kama ilivyokuwa kwa bendi kuachia gitaa la rhythm miaka kabla ya tisini. Kumekuweko tu ubunifu wa misemo na mipasho, jambo jingine ambalo limesababisha kuenziwa zaidi kwa waimbaji tu katika fani hiyo.
Bendi ziko katika wakati mgumu, wakati wanamuziki wengi wa bendi wakilalamika kuwa muziki wa bendi haupigwi katika redio na TV, kumekuweko na jitihada ndogo za bendi kurekodi nyimbo mpya, maelezo mengi yamekuwa ni kuhadithia enzi ambapo muziki wa bendi ulitawala na kuona kama hiyo ni sababu tosha ya muziki huo kuendelea kurushwa hewani. Bendi chache zilizorekodi hazijaja na  nyimbo zilizoweza kuteka umma wa  Tanzania na hivyo kusababisha muziki huu kukosekana katika anga za muziki. Matangazo mengi ya muziki wa dansi yamekuwa ni kutangaza rap mpya au kupatikana kwa msanii mpya, lakini kiujumla hakujakuwa na kitu kipya katika muziki wa bendi.
Muziki asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa si vikundi vingi vya muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio. Pia studio nyingi zimejengwa kuruhusu wasanii wa Bongoflava tu kurekodi, studio za kuweza kuruhusu kundi la muziki wa asili kurekodi ni zenye gharama kubwa sana. Kundi la Makirikiri lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa Kiasili, kuwa na muziki wao ukifuata taratibu nzuri unauza, bahati mbaya kuna vikundi sasa vimeacha kuboresha muziki na ngoma zao, badala yake vinaiga uchezaji wa  Makirikiri.
Pengine watu watasema nimesahau muziki wa kwaya, sijausahau, kwa kweli muziki huu umebaki  hasa kwenye muziki wa Enjili. Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana mashuleni na kwenye siasa na kampeni , lakini kwa mwaka 2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu.
Pamoja na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele katika muziki, kwangu mimi naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza pesa nyingi zaidi, na hata kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini  kwangu hilo si kipimo cha maendeleo katika tasnia hii.
Kama nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndio alama ya muziki wa Tanzania. Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri ya muimbaji ni muhimu, na ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi sana, lakini  ule muziki unaomsindikiza muimbaji ni muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na ndio unaoweza kutufungulia mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana muziki wa kutoka Kongo, Nigeria, South Africa, pamoja na kuwa hatujui hata moja wanaloliongelea tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao. Kutokujali wapigaji katika mfumo wa nchi yetu ndio unatupelekea kuwa watu wa ‘copy and paste’ wa upigaji wa muziki wa nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo zote zilizotikisa nchi hii kwa mwaka 2012 utagundua asilimia kubwa ya muziki uliotumika ulikuwa ni wa kunakili mipigo kutoka muziki wa nchi nyingine, Nigeria, Congo na Afrika Kusini ndio wamekuwa waalimu wetu wakuu wa muziki. 
Na JOHN KITIME wa <www.johnkitime.co.tz>

Wananchi wasaidia kuzima moto uliotokea kituo cha Data cha Tigo Morogoro

January 07, 2017
Afisa mkuu wa ufundi na miundombinu kutoka Tigo, Jerome Albou, akimuonyesha mbunge wa mjimbo la Morogoro mjini, Aziz Abood juzi,mtambo wa 4G mkoani Morogoro, mara baada ya kukabidhi vyeti kwa wananchi kata ya Mji Mwema waliosaidia kuokoa mtambo huo usiteketee na moto mwishoni mwa mwaka jana.



Mbunge wa mjimbo la Morogoro mjini, Aziz Abood akihutubia 

wananchi kata ya Mji Mwema waliosaidia kuokoa mtambo huo usiteketee na moto mwishoni mwa mwaka jana.

Mkurungezi wa Tigo Kanda ya Pwani akihutubia wananchi kata ya Mji Mwema waliosaidia kuokoa mtambo huo usiteketee na moto mwishoni mwa mwaka jana.

Afisa mkuu wa ufundi na miundombinu kutoka Tigo, Jerome Albou akikabidhi cheti kwa mmoja kati ya wananchi 49 kata ya Mji Mwema waliosaidia kuzima moto uliotokea kwenye kituo cha kurushia mawasiiano cha Tigo(Data Centre) kata ya Mjima Mkoani humo mwishoni mwa mwaka jana.


Wananchi 49 wa kata ya Mji Mwema waliosaidia kuzima moto uliotokea kwenye kituo cha kurushia mawasiiano cha Tigo(Data Centre) kata ya Mjima Mkoani humo mwishoni mwa mwaka jana
 Kituo cha kurushia mawasiiano cha Tigo(Data Centre) kata ya Mjimwema  Mkoani humo kilichonsurika kuungua kwa moto mwishoni mwa mwaka jana