MAALIMU SEIF ATEMBELEA UWANJA WA AMANI.

December 16, 2013
IMEWEKWA DESEMBA 17
 Na Masanja Mabula ,Zanzibar.
  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ametembelea uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar kukagua maendeleo ya zoezi la uwekaji wa nyasi bandia katika uwanja huo.

Meneja wa uwanja huo Khamis Ali Mzee, amesema zoezi hilo linaendelea vizuri, huku wakiendelea kukusanya vifaa zaidi kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo kwa wakati muafaka.

Amesema vifaa vinavyoendelea kukusanywa kwa sasa ni pamoja na mchanga maalum ambao unakwenda sambamba na uwekaji wa nyasi hizo ili kuweka umadhubuti zaidi wa uwanja huo.

Kwa upande wake mkandarasi wa uwekaji wa nyasi hizo bw. Ben Mushi kutoka kampuni ya EKIKA ya Dar es Salaam, amesema mvua zinazoendelea kunyesha  zinazorotesha zoezi hilo.

Hata hivyo amesema watafanya kila juhudi kuona kuwa zoezi hilo linakamilika kwa wakati, ili uwanja huo uweze kutumika kwa sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi, zinazotarajiwa kufika kilele chake tarehe 12 Januari, 2014.

Tamasha la Handeni Kwetu ni balaa, mambo yote burudani kabisa, chini ya Shirika la NSSF

December 16, 2013
MSIMU wa kwanza wa Tamasha la Utamaduni Handeni, lililokuwa  likisubiriwa kwa hamu hatimaye lilifanyika Juzi, wilayani Handeni  Tanga  ambapo kama ilivyokuwa ikitarajiwa, Shirika la Taifa la mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilijitokeza na kubeba tamasha hilo.
Meneja wa NSSF mkoani Tanga, Frank Maduga
Shirika hilo, likiwa limejitokeza dakika za mwisho katoa udhamini wake katika tamasha hilo kubwa na la kwanza kuwahi kufanyika katika Ardhi  ya wilaya ya Handeni linalojumuisha vijiji zaidi ya kumi, lilichangia fedha taslimu shilingi milioni mbili, fedha ambazo kwa kiasi kikubwa ukiacha mchango wa wahisani wengine zilichangia  kufanikiwa kwa Tamasha hilo.
Akizungumza wakati wa kutambulisha wadhamini na wahisani mbalimbali waliofanikisha kufanyika kwa Tamasha hilo, mratibu wa Tamasha la utamaduni Handeni 2013, Kambi Mbwana alisema kukiwa na dalili zote za tamasha kushindwa kufanyika kama ilivyotarajiwa, NSSF kupitia Ofisi ya kanda ya Tanga ilijitolea kunusuru Jahazi.
Mratibu wa Tanmasha la Utamaduni Handeni-Kambi Mbwana akitambulisha Wadhamini wa Tamasha hilo lililofanyika Juzi katika uwanja wa Azimio, wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga.
Mkuu wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu akimkaribisha mmoja wa wahudhuriaji wa Tamasha la Handeni Kwetu 2013.
Mkurugenzi wa Grace Products akitoa neno la Shukrani kwa Waandaji wa Tamasha


“Awali ya yote napenda kutanguliza shukurani zangu zote kwa wahisani wa Tamasha hili, Vodacom, Grace products pamoja a wadhamini wengine kwa kufanikisha Tamasha hili la kwanza kuwahi kuwakutanisha watu wa kadhia mbalimbali,
JKT walikuwepo wakafanya yao jukwaani ilikuwa ni noma saaaana
Utamu wa Ngoma uingie uicheze
DC Muhingo Rweyemamu

Shukurani kubwa ziende kwa NSSF, kwa kweli hawa watu wanajali utu, tunaomba watusamehe kwa mapungufu yetu lakini kwa kweli wanastahili kuitwa mfuko wa Hifadhi,” alisema Kambi
Awali akizungumza baada ya kuzindua Tamasha hilo ambalo lengo lake lilikuwa ni kuwakutanisha watu wa Handeni kusherekea utamaduni wao pamoja na kukumbusha umuhimu wa kujenga Handeni, Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema kwa kuwa na Matamasha kama hayo jamii inaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kupata Maendeleo wanayoyataka.

Muhingo alisema ili mafanikio yapatikane katika kila jambo ni lazima watu wa eneo Fulani wawe na utayari wa kukutana na kujadili mambo yao kwa sauti kama waratibu wa Tamasha hilo walivyofanya.
Vyakula vya Asili hapa palikuwa ni mahala pakee

“Tunajivunia kuwa na vijana wenye mawazo mapana kama haya, naambiwa tamasha hili ni matokeo ya mawazo ya kimaendeleo ya vijana wetu, Hongereni sana,” alisema Rweyemamu.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF, mkoani Tanga, Frank Maduga alisema shirika hilo limedhamiria kuendelea kushirikiana na waaandaaji wa Tamasha hilo kwa lengo la kuhakikisha Utamaduni wa Mtanzania unatumika kulitangaza Taifa.
Mamia ya Waandamanaji wakielekea katika Viwanja vya Azimio
Taem Tamasha la Utamaduni Handeni....chezea
Msanii kutoka katika kundi la Okalandima, akionesha uwezo wa kutafuna Moto, hii ni moja ya Vyakula vyetu huku Handeni hasa Kwamsisi, karibu Handeni Kwetu.....

Katika tamasha hilo,kulikuwa na vionjo mbalimbali vya Utamaduni wa Wanahandeni, ikiwa ni Pamoja na Ngoma za asili kutoka katika Vijiji vya wilaya ya Handeni kama vile, Kweingoma, Kwamatukutu, Kwediamba, Kwachaga pamoja na vikundi vingine vya Handeni Mjini.

Burudani kali na ya kuvutia iliyoonesha asili kamili ya Mtanzania ilitoka kwa Kundi la Sanaa la Jeshi la JKT Mgambo, Azimio Jazz band bila kusahau msanii wa kundi la Fataki, Machenja ambaye alipiga onesho
la kukata kiu akiwa na wana okalandima.

Tamasha la Utamaduni Handeni ambalo linafanyika kwa mara ya Kwanza lilidhaminiwa na NSSF, Clouds fm, Vodacom, Plan B, gazeti la Mwananchi, MICHUZI BlogKajunason Blog, Chichi Local Wear, Katomu Solar specialist, Dullah Tiles and Construction, Anesa Company Limited, Country Business directory, Jiachie Blog na TAIFA LETU.com.

MAKATIBU UVCCM TANGA WAASWA.

December 16, 2013
imewekwa desemba 16,2013 saa 11:56 asubuhi.
 Na Oscar Assenga, Korogwe.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga (UVCCM),Abdi Makange amewataka makatibu umoja huo ngazi ya wilaya na kata kuachana na makundi ya uchaguzi mwaka 2014-2015 kwani hali hiyo itawafanya kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo na kuleta mpasuko ndani ya umoja huo.


Kauli hiyo aliitoa  wakati wa kikao cha baraza la Vijana wilaya ya Korogwe ambacho kilihusisha wajumbe kutoka wilaya ya Korogwe mjini na Vijijini ikiwa ni ziara ya siku ya pili ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoa wa Tanga,Abdi Makange ya kukagua uhai wake na kusikiliza kero za wananchi maeneo mbalimbali mkoani Tanga.

“WAZEE WA NGWASUMA KUZINDUA "CHUKI YA NINI"MZALENDO PUB DESEMBA 21.

December 16, 2013


IMEWEKWA DESEMBA 16,2013.
Na Raisa Said, Tanga.
BENDI ya FM Academia “Wazee wa Ngwasuma” inatarajiwa kufanya uzinduzi wa Album yao ya 10 iitwayo “Chuki ya Nini”Desemba 21 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Tanga Raha Blog kwa njia ya simu, Rais wa Bendi hiyo, Nyoshi El Sadat alisema uzinduzi huo utaanza majira ya moja usiku ambalo Utakwenda sambamba na burudani toka kwa bendi mahiri hapa nchini ya Mashujaa.

Sadat alisema bendi hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatoa burudani ya aina yake kwa wapenzi na mashabiki wake hasa ukizingatia uzinduzi huo unafanyika siku chache kabla ya kuuaga mwaka 2013.


“Ninachoweza  kusema uzinduzi huo utakuwa sio mchezo kwa sababu tumejiandaa kikamilifu kuuaga mwaka kwa staili nyengine “Alisema El Sadat.

Aidha alisema uzinduzi wa Album hiyo umedhaminiwa na Kinywaji cha Wind Hoek Lager ambacho kitatoa bia moja kwa kila mshabikiwa wa bendi hiyo ambaye atahudhuria siku hiyo.

Katika uzunduzi huo viingilio vinatarajiwa kuwa kati y ash.20,000 kwa VIP n ash.15000 kwa viti vya kawaida lengo likiwa ni kuwapa fuksa wapenzi wa mziki wa dansi kujitokeza kwa wingi kushuhudia.