SERIKALI ITAOKOA SH.BILIONI 900 KWA MWAKA ENDAPO IKIFANIKIWA KUTEKELEZA MKAKATI WA UWAZI KATIKA UJENZI NCHINI.

February 02, 2017


 Kaimu Mtendaji Mkuu Baraza la Taifa la Ujenzi,Elias Kissamo akizungumza katika ufunguzi wa  mkutano wa mchakato wa utoaji wa taarifa za miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umma katika ukumbi wa Holiday Inn jijini Dar es Salaam jana.
 Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Ikulu,Peter Ilomo,akifungua mkutano wa mchakato wa utoaji wa taarifa za miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umma katika ukumbi wa Holiday Inn jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Sekta ya Uwazi na Uwajibikaji katika Ujenzi (Cost Tanzania),Mhandisi Kazungu Magili na Kaimu Mtendaji Mkuu Baraza la Taifa la Ujenzi,Elias Kissamo. (PICHA NA ELISA SHUNDA)

 Wadau wa masuala ya ujenzi wakifuatilia kwa umakini wakati mkutano huo ukiendelea.
 
 Imeandaliwa na Mtandao wa www.elisashunda.blogspot.com mawasiliano elisashunda@gmail.com namba ya simu 0719976633.
  Mwenyekiti wa Baraza la Ujenzi la Taifa (Cost Tanzania),Mhandisi Kazungu Magili,akizungumza katika mkutano huo. 

Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Ikulu,Peter Ilomo akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Baraza la Taifa la Ujenzi Tanzania na wadau wa masuala ya ujenzi nchini.
 Imeandaliwa na Mtandao wa www.elisashunda.blogspot.com mawasiliano elisashunda@gmail.com namba ya simu 0719976633.



NA MWANDISHI WETU


SERIKALI itaokoa angalau Sh.bilioni 900 kwa mwaka endapo itafanikiwa katika utekelezaji wa Mkakati Uwazi katika  Ujenzi (CoST).

Aidha kupitia mkakati huo, miradi mbalimbali ya mashirika ya umma 10 inatarajiwa kufanyiwa tathmini itakayokamilika ifikapo Julai mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa mashauriano ya utoaji wa taarifa za miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umma wa baraza la wajenzi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Peter Ilomo alisema kuwa mkakati huo utapunguza rushwa na upotevu wa fedha za Serikali.

Ilomo alisema CoST itaisaidia Serikali na umma kujua fedha zinavyotumika katika ujenzi wa miundombinu, kuokoa fedha za umma kwa kupunguza rushwa na kuboresha usimamiaji wa utekelezaji wa miundombinu.

Mwenyekiti wa CoST, Kazungu Magili  alitaja mashirika yatakayofanyiwa tathmini na kuweka wazi miradi yake kuwa ni, Wakala wa Majengo (TBA), Wakala wa Barabara (Tanroads) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)/.

Mashirika mengine ni mifuko wa Taifa wa hifadhi ya jamii ya NSSF, GEPF, LAPF, Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii jinsia Wazee na Watoto na kutoa taarifa kwa umma ambapo utaweza kuitumia kufuatilia utekelezaji wa miradi husika.

Alisema kupitia tathmini hiyo, CoST itapata fursa ya kutambua majengo yaliyojengwa kwa mujibu wa vigezo ama chini ya kiwango  halisi cha fedha zilizotolewa na thamani ya jengo husika.

Magili alisema ikitokea kuna baadhi ya miradi imejengwa chini ya kiwango itafikishwa katika mamlaka mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ili hatua mbalimbali zichukuliwe.

Aidha alisema kuwa awali kabla ya kuanzishwa mkakati huo mambo mengi yalikuwa hayawekwi wazi hali ambayo imekuwa ikisababisha upotevu wa fedha. 


Imeandaliwa na Mtandao wa www.elisashunda.blogspot.com mawasiliano elisashunda@gmail.com namba ya simu 0719976633.
Elisa Shunda

Photographer-Raia Tanzania Newspaper



KUSAFIRI KUSIKUNYIME FURSA YA KUFANYA MAZOEZI

February 02, 2017

Na Jumia Travel Tanzania

Je, unapenda mazoezi? Umeshawahi kujikuta ukiwa njia panda ukijiuliza aidha usafiri au la, kwa kuhofia kutopata fursa ya kufanya mazoezi? Basi ondoa shaka kwani Jumia Travel inakujulisha kuwa hoteli zifuatazo zina sehemu na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanyia mazoezi.    

Ledger Plaza Bahari Beach Hotel
Hii ni hoteli ya kisasa inayopatikana katika fukwe safi za mwambao wa bahari ya Hindi, Kunduchi jijini Dar es Salaam. Licha ya kuwa na huduma mbalimbali ambazo mteja atazihitaji akiwa pale, hoteli imezingatia uwepo wa sehemu ya kufanyia mazoezi iliyosheheni vifaa vya kisasa kabisa. Lengo ni kukidhi haja ya baadhi ya wateja ambao kwao mazoezi ni sehemu ya maisha yao. Hoteli ipo karibu na mji wa Bagamoyo ambapo ni mwendo wa takribani dakika 30 na pia itakuchukua dakika 10 kusafiri kwa kutumia boti kufika kisiwa cha Mbudya.   
Jangwani Sea Breeze Resort
Hoteli hii inapatikana Tanzania bara na inajivunia kuwa na mazingira rafiki kwa watoto. Hii ni kwa sababu wanaweza kwenda na wazazi wao huku wakipatiwa chumba chenye michezo mbalimbali kwa ajili yao. Ukiwa pale itakuchukua mwendo wa dakika 10 kwa boti kufika katika visiwa vya Mbudya na Bongoyo wakati kufika mji wa kihistoria wa Bagamoyo ni takribani dakika 40 tu. Hoteli hii nayo ina sehemu na vifaa vya kufanyia mazoezi, hivyo kuwatoa hofu wapenda mazoezi pindi wakiwa pale.   

Harbour View Suites
Kama unapenda kufurahia mandhari nzuri ya katikati ya jiji la Dar es Salaam, Harbour View Suites itakuwa ni chaguo sahihi kwako. Hoteli hii ya kifahari yenye nyota nne ina sehemu yenye vifaa vya kutosha kwa ajili ya mazoezi, sehemu ya kuogelea pamoja na ‘kasino.’ Ni sehemu nzuri kufikia na kupumzika kama una shughuli za kibiashara katikati ya mji kwa sababu ipo karibu na ofisi muhimu pamoja na kumbi za mikutano.

Mermaids Cove Beach Resort & Spa
Mbali na huduma nzuri utakazozikuta pale, hoteli hii inayopatikana katika fukwe safi za Pwani ya Mashariki mwa visiwa vya Zanzibar, inazo shughuli mbalimbali za kukufanya uburudike. Ikiwa na chumba kilichotengenezwa maalumu kwa michezo mbalimbali pia ina sehemu ya kufanyia mazoezi. Kwa kuongezea ina ukumbi wa mikutano, sehemu ya kupumzika pamoja na duka kwa ajili ya manunuzi madogo madogo ukiwa hotelini. 
Hii inaweza kuwa changamoto kwa wamiliki wa hoteli kutakiwa kuzingatia kutengeneza sehemu ya mazoezi pamoja na kuweka vifaa vya kisasa. Kutokuwa na huduma hii licha ya kuwa na nyinginezo inaweza ikawa ni sababu ya wateja kutochagua kufikia kwenye hoteli yako.
Tembelea dream deals ili kujionea ofa kabambe za namna ya kwenda kufurahia huduma kwenye hoteli zilizoorodheshwa hapo juu pamoja na zifuatazo: Hotel White Sands: The Beach Resort, Golden Tulip Hotel na Ramada Resort za Dar es Salaam; Paradise Beach Resort na Golden Tulip Zanzibar Boutique Hotel za Visiwani Zanzibar; Nashera Hotel (Morogoro), Kwetu Hotel (Tanga); na Ngare Sero Mountain Lodge (Arusha)  


TIMU YA WANAHABARI IRINGA YAPIGWA JEKI NA MBUNGE RITTA KABATI

February 02, 2017
Mbunge  wa  viti  maalum  mkoa  wa  Iringa Ritta Kabati (CCM) akimkabidhi mwenyekiti wa waandishi wa habari mkoani Iringa moja ya jezi alizotoa kwa waandishi wa habari kwa ajili ya mechi mbalimbali za timu hiyo
 Mbunge  wa  viti  maalum  mkoa  wa  Iringa Ritta Kabati (CCM) ameipiga jeki timu ya wandishi wa habari mkoa wa Iringa kwa kuwapatia   jezi  seti  moja ,mpira na pesa taslim kiasi cha Tsh  50O,000 ili viwasaidie katika malengo yao ya kukipiga ligi daraja la kwanza .
na fredy mgunda,Iringa

Mbunge  wa  viti  maalum  mkoa  wa  Iringa Ritta Kabati (CCM) ameipiga jeki timu ya wandishi wa habari mkoa wa Iringa kwa kuwapatia   jezi  seti  moja ,mpira na pesa taslim kiasi cha Tsh  50O,000 ili viwasaidie katika malengo yao ya kukipiga ligi daraja la kwanza .

 Akikabidhi  msaada  huo kwa mwenyekiti wa chama cha wandishi wa habari mkoa wa Iringa Frank Leonard juzi    mbunge huyo alisema kuwa  yeye kama mlezi  wa timu hiyo ameamu kujingiza kwa miguu yote kuisaidi timu hiyo ambayo inaonekana kufanya vema kwenye mchezo wa soka mkoani hapo .

Kabati alisema kuwa licha ya kuwa mpira ni ajira pia unamsaidia mtu kuwa na afya njema itakayomsaidia kujiepusha na magonjwa yanayoepukika ikiwemo presha .
“Niwatie moyo hichi mulichokianzisha ni kizuri na timu yenu ina fanya vizuri na juzi tu mumenyakua kombe la Spanest  kwa kuwanyuka kitisi huu ni ushahidi tosha mukiendelea hivi hivi mutakuja kuingia ligi daraja la kwanza na baadaye ligi kuu .

Kabati  aliwataka   wadau  wengine mkoa  Iringa na nje ya  Iringa  kuendelea  kujitolea  kuisaidia   timu   hiyo    ya wanahabari ili iendele kufanya vema ndani na nje ya mkoa wa iringa

Akipokea vifaa hivyo mwenyekiti wa wanahabari mkoa wa Iringa Frank Leonard alimshukuru mbunge huyo kwa vifaa na fedha alizotoa huku akimuahidi mbunge huyo kuwa timu hiyo itakipiga na timu mbalimbali ikiwemo timu ya bunge la jamuhuri wa muungano wa Tanzania

Frank alisema kuwa timu hiyo imekuwa ikifanya vema kutokana na kuwa na wandishi wazuri vijana waliona ari ya kusakata kambumbi hivyo ni vema timu ya bunge kujipanga kisawasa kwani hawata toka salama pindi watakapokipiga nao mjini dodoma

MGODI WA BUZWAGI WALIPA KODI ZAIDI YA MIL 700 KWA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA

February 02, 2017
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo(wa pili kutoka kulia) na Meneja Uendelevu wa Mgodi wa Buzwagi ,George Mkanza wakikabidhi hundi ya kodi ya huduma ya zaidi ya Sh Mil 740 kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Fadhili Nkurlu(wa pili toka kushoto) tukio lililofanyika juzi mjini Kahama ,Wa kwanza kushoto ni makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Kahama Bi Marry Manyambo.
Mkuu wa Wilaya Kahama,Fadhili Nkurlu na akimkabidhi hundi iliyotolewa na Mgodi wa Buzwagi kama Kodi ya Huduma yenye thamani ya zaidi ya Sh Mil 740 , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hospitali kubwa ya wilaya ya Kahama, mradi ambao ujenzi wake utategemea fedha zinazotokana na kodi za ushuru wa huduma unaolipwa na Mgodi huo.
 Baadhi ya waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kahama wakifuatilia hafla ya kukabidhi hundi kwa halmashauri ya mji wa Kahama.
 Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo akiwahutubia waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Kahama pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla ya kukabidhi hundi kwa halmashauri ya Mji wa Kahama
 Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu (aliyesimama) akihutubia wageni waalikwa wakati wa hafla ya kupokea hundi ya ushuru wa huduma kutoka Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi. Kutokea kushoto waliokaa ni Katibu tawala wa wilaya Kahama Timothy Ndanya na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo.
 Mkuu wa wilaya Kahama na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi wakiteta jambo.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii ,Kanda ya Kaskazini.


HALMASHAURI ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga imepokea kiasi cha Sh Mil 700,040,000  kutoka kwa kampuni ya Acacia inayomiliki mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi ikiwa ni sehemu ya kodi ya huduma (service levy) ya kipindi cha mwezi Julai na Desemba 2016.

Kiasi hiki ni zaidi ya kilichotolewa kipindi cha Julai na Desemba mwaka 2015 ambapo mgodi huo uliikabidhi halmashauri ya mji wa Kahama hundi yenye thamani ya kiasi cha sh Mil 500,088,000 kama kodi ya huduma ikiwa ni utekelezaji wa sheria kwa kulipa kodi zilizopo kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Hundi ,Meneja mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo alisema Buzwagi inamatumaini makubwa kuwa katika siku za karibuni halmashauri itaanza kutekeleza mradi huo na hivyo kutoa matumaini kwa wananchi wa Kahama kupata huduma nzuri za afya ndani ya wilaya.

“Mpaka sasa kama Kampuni tumekwisha kabidhi kwenu takribani kiasi cha bilioni 1.4 hii ikiwa na maana ya kodi yote ya ushuru wa huduma katika kipindi cha mwaka 2016, wananchi wangetamani kuona mradi huu unaanza maana kiasi hicho kilichopo kama kitatumika kinaweza kutekeleza sehemu kubwa ya mradi huu kwa kuanzia wakati tukisubiri awamu zingine” alisema Mwaipopo.

Katika hafla hiyo ya makabidhiano iliyofanyika katika viwanja vya makazi ya viongozi katika wilaya hiyo,Mwaipopo alisema licha ya Kampuni yake kulipa kodi mbalimbali bado imekuwa ikijishughulisha katika kuhakikisha inakuwa mdau muhimu wa maendeleo kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yanayozunguka Mgodi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Fadhili Nkurlu aliyepokea hundi hiyo kutoka kwa uongozi wa Buzwagi na baadae kuikabidhi kwa mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama ameupongeza uongozi wa Mgodi wa Buzwagi kwa jitihada ambazo wamekuwa wakizifanya katika kuhakikisha wanalipa kodi mbalimbali pamoja na jushirikiana na Jamii katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Alisema Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi umeekua mstari wa mbele katika kulipa kodi mbalimbali ambako mpaka kufikia sasa zimefikia zaidi ya shilingi bilioni 197 ambazo zimetolewa katika vipindi tofauti.

Akizungumzia matumizi ya pesa hizo katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kahama Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama Anderson Msumba alisema halmashauri iko katika hatua za mwisho za utekelezwaji wa ujenzi huo.

Miloni 700,040,000  zilizotolewa zinafanya juma ya pesa zote zilizotolewa katika vipindi vya miaka miwili kufikia Bil 1.2 fedha ambazo zitasaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa Afya.

WANA USALAMA WA CUF YA PROFESA LIPUMBA WATOA ONYO KALI KWA WANAOTAKA KUKIHUJUMU CHAMA HICHO

February 02, 2017
 Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Wananchi (CUF), Masoud Mhina, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, kuhusu madai ya hujuma zinazopangwa kufanywa dhidi ya chama hicho. Kushoto ni Ofisa  Dawati wa CUF, Awadhi Mdoe.(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
 Ofisa  Dawati wa CUF, Awadhi Mdoe, akizungumza katika mkutano huo. Kutoka kulia ni Naibu Kamanda wa Blue Gurd, Wilaya ya Kinondoni,  Mohamed Kiotola, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Zainabu Mdolwa, Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Wananchi (CUF), Masoud Mhina na Mkurugenzi wa Blue Gurd wa Wilaya ya Temeke, Saidi Mtumbwe.
Wafuasi wa chama hicho wakiwa kwenye mkutano huo.

TAARIFA KWA UMMA

Wahe,Waandishi wa Habari,nimewaiteni hapa leo kwa ajili ya kuwapa Taarifa za hujuma zinazopangwa kufanywa dhidi ya chama chetu.

Kama mnavyofahamu kwamba,Chama chetu kiko katika sintofahamu ya Mgogoro wa Kiuongozi.

Hata hivyo pampja na hali hiyo kuwepo,tunaimani kwamba,sintofahamu hii ya Kiuongozi tutaumaliza wana CUF wenyewe.

Mara nyingi huwa siyo kawaida yangu kusimama hadharani kuzungumzia hali ya chama kupitia Vyombo vyenu vya habari,lakini kwa hali ilivyo nimewajibika kutokeza hadharani kuzungumza nanyi.

Kwa mujibu wa Katiba ya CUF Ibara ya 88 (2)   Nanukuu.Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama atakuwa na wajibu Ufuatao,Mwisho wa kunukuu.

Ibara ya  88 (2) (a) Atakuwa Mtendaji Mkuu wa Kamati ya Ulinzi na      Usalama ya Chama Ibara ya 87 (1)Wajibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Taifa ni kuhakikisha Usalama wa Chama Nchini kote

Nimeona ninukuu vifungu hivi vya Katiba ya CUF ili kuweka sawa uhalali wangu katika kutoa Taarifa hii kwenu ninyi Waandishi wa Habari.

Tunazo Taarifa kwamba,Katibu Mkuu wetu anafanya Vikao mbalimbali na Viongozi wa Chadema vyenye muelekeo wa kuhujumu harakati za chama chetu  pamoja na baadhi ya Viongozi wa CUF upande wa Tanzania Bara.

Napenda kuchukua fursa hii kumsihi Katibu Mkuu wa Chama changu,Mhe,Maalim Seif,kwamba aache kufanya hivyo kwani vikao hivyo havina tija kwake ziadi ya kujenga Uhasama dhidi ya Wanachama na Viongozi wa CUF wa Bara na Zanzibar.

Nimshauri Katibu Mkuu wangu kwamba,Viongozi wa Chadema anaowatumainia kama ndiyo wataweza kumsaidia katika dhamira zake,atakuwa anapoteza muda wake bure.

Tunazo Taarifa kwamba kuna Vijana wanaandaliwa kuja kuvamia Ofisi Kuu za CUF Buguruni  kwa ajili ya kufanya Uharibifu wa Mali za Chama.

Nichukue fursa hii pia kutoa ONYO KALI kwamba Vijana hao wasithubutu wala kujaribu kufanya kitu kama hicho kwani Ulinzi wa Chama umejipanga vyema kukabiliana vikali na Kikundi chochote ambacho kina dhamira ya kufanya hujuma yeyote dhidi ya chama chetu cha CUF.

Kuhusu kuwafanyia hujuma baadhi ya Viongozi wa Chama chetu,tunawaambia kwamba,wote wanaotaka kufanya Vitendo hivyo tunawajua mmoja mmoja na anapoishi,ila kwa sababu maalum,sitoweza kuwataja kwa sasa,lakini kwa kuwa,chama chetu kinafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Nchi,Tayari tumevitaarifu Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Serikali juu ya Vitisho ya vitendo dhalimu vinavyokusudiwa kufanywa na Wasaliti wa Chama chetu dhidi ya Viongozi wetu wa Chama upande wa Tanzania Bara.

Lakini pia napenda kuchukua fursa hii kutoa Onyo pia kwa wale wanaojiita ni Viongozi wa CUF halafu wanazungumzia Uchochoroni na kuwatukana Viongozi halali wa Chama cha CUF,kwamba waache mara moja,tumewavumilia sana kiasi cha kutosha sasa dawa yao iko jikoni mmoja mmoja baada ya mwingine tutawajibika nao.

Waheshimiwa Wanahabari nawashukuru,asanteni sana kwa kunisikiliza.


HAKI SAWA KWA WOTE

Masoud Omar Mhina


MKURUGENZI WA ULINZI NA USALAMA CUF TAIFA.

TIGO YAONGEZA KASI YA KILLI MARATHON

February 02, 2017

Mkurugenzi wa Mawasiliano kampuni ya Tigo Kanda ya Kaskazini George Lugata Akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Udhamini wa Mashindano ya Kilimanjaro International Marathon
 Wateja wakifurahia huduma za Tigo zilizoboreshwa katika Ofisi za Tigo zilizoko Blue Rock jijini Arusha



Na Woinde Shizza,Arusha.

Kampuni ya Simu za mkononi ya TIGO imejipanga kunogesha mashindano ya Kilimanjaro International Marathon kupitia udhamini mnono ya mashindano hayo kwa upande wa kilomita 21 ambapo licha ya udhamini huo watahakikisha huduma zote muhimu za kifedha zinapatikana katika mashindano hayo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano kampuni ya Tigo Kanda ya Kaskazini,George Lugata  amesema kuwa zaidi ya nchi 45 zinatarajia kushiriki katika mashindano hayo ya kimataifa yanayotarajia kufanyika Februari 26 mwaka huu mjini Moshi mkoa wa Kilimanjaro.

George alisema kuwa kampuni ya Tigo imejipanga kuhakikisha kuwa huduma za Tigo Pesa zinapatikana kwa kipindi chote kwani wameongeza idadi kubwa ya mawakala  wataotoa huduma hizo.

“Ni vyema tukatambua kuwa wateja kutoka mitandao yote nchini wanaweza pia kulipia huduma na bidhaa kutoka katika maduka ya wafanyabiashara wowote jijini Moshi kwenye mabango yaliyoandikwa Lipa kwa Tigopesa” Alisema George

Alisema kuwa katika kipindi chote hicho watatoa huduma zenye ubora wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wa Washiriki na Watakaohudhuria wanafurahia huduma hizo.

Mkurugenzi huyo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kushiriki mbio hizo zenye hadhi kubwa kitaifa na kimataifa .





WAZIRI MAKAMBA AZINDUA BODI YA MFUKO WA TAIFA WA DHAMANA YA HIFADHI YA MAZINGIRA

February 02, 2017
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiongea katika uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya Mazingira. Bodi hiyo iko chini ya Uenyekiti wa Bw Ali A. Mafuruki. Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiwakaribisha wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya Mazingira (hawapo pichani), kulia ni Bw. Ali Mufuruki Mwenyekiti wa Bodi.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Eng. Ngosi Mwihava (kushoto) akiwa na Bw. Ali Mufuruki Mwenyekiti wa Bodi, wakati wa halfa ya uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya Maizngira jiini Dar es Salaam.



Sehemu ya Wajumbe wa Bodi (mstari wa mbele) wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba katika hafla ya uzinduzi wa Bodi na Mfuko wa Dhamana ya Mazingira.






Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya Mazingira, mara baada ya kuizindua hii leo, Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam.



Na Lulu Mussa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Muungano na Mazingira Mh. January Makamba hii leo amezindua Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya Mazingira Nchini iliyo chini ya Mwenyekiti Ali Mufuruki.
Waziri Makamba amesema Uzinduzi wa Mfuko  na Bodi hiyo utasaidia  upatikanani wa fedha za usimamizi wa Mazingira Nchini. “Ni matarajio yangu tutafanya kazi pamoja kuhakikisha mfuko unakuwa na fedha ya kutosha na unafanya kazi ili kukidhi malengo yaliyodhamiriwa hususan uboreshaji wa mazingira nchini” Alisisitiza Waziri Makamba
Waziri Makamba amesema  uteuzi wao una maana kubwa na kuwataka wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa kujituma na kuhakikisha kuwa Hifadhi ya Mazingira inakuwa ni ajenga ya kitaifa.
Waziri Makamba amewafahamisha wajumbe kuwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 Kifungu cha 213 imeanzisha Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo fedha za kutosha za kulinda na kusimamia hifadhi ya mazingira nchini.
Aidha, tangu kuanzishwa kwa Mfuko huu kisheria, kumekuwepo na maandalizi mbalimbali ya kuhakikisha kwamba mfuko unaanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo. Baadhi ya maandalizi hayo ni: Kufanya utafiti kuhusu vyanzo vya fedha kwa ajili ya Mfuko; kuandaa mwongozo wa kusimamia fedha za Mfuko; kuandaa kanuni za uendeshaji Mfuko; na kuwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango mapendekezo ya vyanzo vya mfuko ili kupata utaratibu muafaka kwa kupata fedha hizo kwa ajili ya Mfuko.
Waziri Makamba amefanunua kuwa Malengo ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira kama yalivyobainishwa kwenye Sheria ya Mazingira ni pamoja na: Kusaidia utafiti unaolenga kuboresha hifadhi ya mazingira; Kujenga uwezo wa taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC na nyinginezo katika hifadhi ya mazingira; Kutoa tuzo zinazolenga uhamasishaji wa hifadhi ya mazingira; Kutoa majarida yanayohusu hifadhi ya mazingira.

Malengo mengine ni pamoja na kutoa ufadhili kwa ajili ya mafunzo yanayohusu shughuli za    mazingira; Kusaidia jamii kwa kutoa misaada kwa ajili ya kutekeleza prgramu za hifadhi ya  mazingira; na Kulipia gharama za mikutano ya Kamati ya Mazingira ya Ushauri ya Taifa (National Environmental Advisory Committee - NEAC) na Bodi ya Wadhamini wa Mfuko, Waziri Makamba alisisitiza.
Waziri Makamba amesema kuwa juhudi za Serikali katika hifadhi ya mazingira zitakuwa endelevu na kuhakikisha kuwa Bodi itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha hifadhi ya mazingira inasimamiwa na kuendeshwa kwa mujibu wa Sheria kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira Bw. Ali Mufuruki amemuhakikishia Mhe. Waziri Makamba kuwa yeye na wajumbe wa bodi yake wako tayari kufanya kazi hiyo kwa heshima kubwa na kuhakikisha kuwa hifadhi na usimamizi wa mazingira unakua endelevu.
Bodi hiyo inaongozwa na Bw Ali Mufuruki ambaye Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Kampuni ya Infotech, Mwajuma Mbogoyo, Imelda Teikwa, Profesa Razak Bakari Lokina na Hatibu Senkoro. Wengine ni Alesia Mbuya, Baraka Juma Kalangahe, Dkt. Andrew Komba na Profesa Yunus Mgaya.